“Only when the last tree is cut, only when the last river is polluted, only when the last fish is caught, will Men realize that they can’t eat money.” Native American proverb

Habari za leo raafiki, karibu kwenye makala ya leo, katika makala hii nimeandaa kama tafakari ya kutusaidia kujiangalia na kujitathimini jinsi tunavyoishi na kufanya shughuli zetu za kila siku. Ni vizuri kila mmoja wetu akawa na uwelewa na ufahamu wa kutosha kuhusu mazingira yake jinsi yalivyo muhimu kwenye utendaji wa kazi na kusababisha maisha kwenye dunia hii yaende.

Katika nchi zetu za Afrika tumejaiwa kuwa na maeneo mengi ambayo hadi leo karne ya 21 bado maeneo haya yapo katika uasili wake. Tofauti na sehemu nyingine duniani ambako wamemaliza maeneo yote muhimu ya asili kwa mipango mibaya ya maendeleo ya miji na viwanda. Baada ya hayo ndio wanakuja kushtuka hawana maeneo ambayo ni ya asili kwa ajili ya hifadhi ya wanyama na misitu. Hata kama wanayo ni ndogo sana nazo zinakabiliwa na changamoto kubwa na wanyamapori wanaoishi humo wamekosa nafasi ya kutosha kwa ajili ya kutembea kutafuta chakula na makazi mazuri ya aina mbali mbali.

Hivyo basi kwa kuwa tuna rasilimali nyingi asilia za wanyama na misitu, tunatakiwa tuzichukulie kwa uangalifu mkubwa na umakini wa kutosha ili rasilimali hizi ziendelee kuwepo wa vizazi vingi vijavyo. Katika maneno aliyopo kwenye nukuu hii yanatufanya kufikiri sana kwa kina kuhusu maliasili zetu na kuchukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kuhakikisha zinaendelea kuwepo na kufanya maisha ya wanyamapori kuendelea.

Kwa tafsiri isiyo sahahi sana kuhusiana na maneno ya nukuu hii ni kwamba anasema, “Ni pale tu mti wa mwisho unapokatwa, ni pale tu mto wa mwisho unapochafuliwa, ni pale tu samaki wa mwisho anapokamatwa, ndipo watu watakapojua na kutambua kwamba hawawezi kula fedha”. Huu ni ukweli kabisa kwenye umamkini na uangalizi wa rasilimali zetu, rasilimali ambazo binadamu anaongoza kwa kuzitumia vibaya, kwa mfano watu wanakata miti hovyo bila mpangilio wala utarati na wakati mwingine bila sababu za msingi na wakati mwingine wanafanya hivyo bila kufikiria kupanda miti mingine, kwa kufanya hivi ni kuharibu kabisa mfumo wa ikolojia ya maisha ya viumbe hai ikiwa ni pamoja na binadamu. Hapo hapo watu wanapochafua mito ya maji na vyanzo vyake kwa taka na kemikali zenye sumu ni hatari sana kwa viumbe wa majini na wengine wote wanaotumia maji kwa ajili ya maisha yao.

Hivyo kwenye maisha yetu ya kila siku tunatakiwa kwa na umakini mkubwa kwenye matumizi ya maliasili zetu. Tunatakiwa kuwa na usimamizi mzuri kwenye misitu yetu, wanyama wetu, mito ya maji na vyanzo vingine vya maji ambavyo ni msaada mkubwa kwa viumbe hai wote.

Naamini kwa tafakari hii kila mmoja wetu atachukua hatua stahiki na kufanya maamuzi ya busara kwenye mazingira na maisha yetu ya kila siku.

Asante kwa kusoma makala hii ukutane kwenye makala ijayo.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania