Plans to protect air and water, wilderness and wildlife are in fact plans to protect man. Stewart Udall

Habari za leo muhifadhi, karibu kwenye tafakari ya leo ambayo inatusaidia kuyaangalia maisha yetu na nafasi yetu kama binadamu hapa duniani. Maelezo ya makala nzima yatajikita kwenye nukuu ya Stewart Udall. Ambayo inaelezea juhudi ya dunia kuhifadhi hewa, maji na maeneo ya wanyamapori na wanyamapori wenyewe. Ukiangalia vitu vyote ambavyo ni muhimu kwa maisha ya binadamu basi ni hewa safi, hewa ya oksijeni, halafu kuna maji, lakini pia kikubwa zaidi ni kile kinachotunza na kufanya maji yawepo kwenye maeneo husika ambayo ni maeneo ya asili na maeneo ya wanyamapori. Uhifadhi wa maeneo haya umeleta sio tu kuwa na wanyamapori wengi wa kuvutia hali ya hewa bali hata afya ya maisha ya binadamu hapa duniani.

Katika nukuu ya leo ambayo nataka tuitafakari na kuchukua maamuzi mazuri na ya busara kwenye uhifadhi wa wnyamapori na maliasili zetu. Nikiyatafsiri maneno ya nukuu hii ya leo tunaweza kuayaelewa kwa Kiswahili kwa namana hii, mipango ya kuhifadhi/kutunza hewa na maji, mapori na wanyamapori kwa hakika ni mipano ya kumtunza binadamu. Kwa hiyo kwa maneno ya Kiswahili kisicho sanifu hivyo ndivyo Stewart anavyomaanisha. Na mimi nimeamua kuielezea nukuu hii kama tafakari yetu kwenye mambo ya uhifadhi wa maliasili zetu kwa manufaa yetu wenyewe. Tunapoweka juhudi kulinda na kutunza maliasili za nchi yetu au kwenye jamii yetu, sio kwamba tunataka kuona maliasili zikiwa nyingi pekee na lakini ni uwekezaji bora kabisa  wa kuja kuokoa maisha ya vizazi vijavyo.

Kwa namna ambavyo Mungu amaetuumba amehakikisha anaunganisha sehemu ya maisha yetu na udongo, maji, hewa na mazingira tunayoishi, ili kwamba unapoharibu kimoja wapo uwe unajiharibu mwenyewe. Hii ni kanuni muhimu sana kwenye mfumo wa maisha tunayoishi hapa duniani. Yani matendo na maamuzi yetu tunayoyafanya kwenye misitu, maji na vyanzo vya maji, wanyamapori, ndege, na hata wanyama na samaki wa baharini inaamua ubora  wa maisha yetu na vizazi vya baadaye. Hii ndio sababu kuu Mungu aliona ni muhimu akatupa ufahamu na akili ili tujue na kutambua na kuamua kwa busara kwenye maliasili zetu. Unajua Mungu angeweza kutuumba na kutuacha tu bila kutupa akili na ufahamu, lakini aliamua kutupa akili na ufahamu ili tujue, tifikiri na kuchukua hatua muhimu kwa uhifadhi wa mazingira yetu.

Hivyo tunapoambiwa tutunze mazingira yetu sio kwa faida ya wale wanaotuambia tutunze mazingira yetu, ila ni kwa faida yetu wenyewe na watoto wetu wengi ambao hawajazaliwa bado. Hivyo tunatakiwa kuwa wakali kwa watu ambao hawatumii akili na ufahamu wao pale wanapoharibu na kuchafua vyanzo vya maji, hewa,kuchoma misitu na maeneo muhimu ya uhifadhi wa wanyamapori bila utaratibu maalumu. Sheria kali zifuatwe na wanaofanya mambo ya uharibifu wa mazingira wajue wanaharibu maisha yao wenyewe na maisha ya watu wengine kwa matendo yao. Tutambue kuwa maji yakiwepo yatasaidia miti na mimea kuwepo na mimiea ikiwepo itasaidia kutoa hewa safi ya oksijeni, na kuondoa hewa chafu ya kaboni diyoksaidi kwenye mazingira yetu, pia uwepo wa miti unasiaidia kuwepo kwa viumbe hai wengine kama wanyamapori.

Naamini umeielewa vizuri tafakari ya leo, na pia utaamua kwa busara kwenye mazingira yanayokuzunguka. Ukweli ni kwamba hakuna sehemu ambapo utaisha usema hakuna mazingira, mazingira yapo kila mahali na yanahitaji kutunzwa dhidi ya watu wanaoendesha maisha yao bila kutumia akili na busara. Naamini utakuwa mjumbe mzuri sehemu yoyote ile ulipo, utawaelimisha wengine kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Kwa maoni, maswali na ushauri wasiliana nami kwa mawasiliano yaliyopo hapa chini mwisho wa makala hii.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania