Moja ya vitu ambavyo navipenda kwenye maisha yangu ni kusafiri na kwenda sehemu tofauti kabisa ambayo nilikuwa siijui wala sikuwahi kufika, napenda sana kwenda maeneo ambayo ni mageni kwangu napenda kuonana na watu ambao sijawahi kuwaona, napenda kuona vitu ambavyo sijawahi kuviona, napenda kuona mazingira ambayo sijawahi kuyaona. Hii ndio sababu napenda sana kusafiri napenda kwenda sehemu ambazo ni mpya kwangu. Kwenye sehemu hizi mpya sio kwamba nazifurahia na kuona mambo mapya na kuanza kushangaa, huwa najifunza sana maisha na huwa naona kama ni vipande vya maisha ambavyo sivijui. Hivyo nakuwa na hamasa sana ya kutaka kuona na kujua kwa undani historia ya sehemu au kitu fulani.
Naamini kabisa asilimia kubwa ya watu wanatamani kusafiri na kutembelea sehemu tofauti tofauti kwa ajili ya kujifunza, kufurahi na kuona mambo mapya. Hivyo ni vizuri sana tukawa sehemu ya kukuza utalii wetu kwa kuwa mabalozi kwa wenzetu, hasa watanzania wenzetu.
Rafiki katika barua ya leo, nataka kukukumbusha jambo moja ambalo wengi wetu hatulifanyi wala kulipanga kama sehemu muhimu ya maisha yetu. Nimekwisha kuandika makala kuhusu kutembelea hifadhi na pia nimeandika makala ambayo inahusu malengo ambayo watu wengi wanasahau kujiwekea kwenye uandaaji wa malengo na mipango yao ya mwaka mzima. Kwenye makala ile nilielezea kwa kina na nafikiri ni makala nzuri na muhimu sana kwa kila moja wetu kuisoma, nitaweka link ya makala hiyo hapa…Hili Ndio Lengo Muhimu Ambalo Watu Wengi Wamesahau Kuliandika Kwa Mwaka Huu 2018
Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inajiandaa kwa mipango mingi kuinua sekta ya utalii na kuhakikisha utalii wa Tanzania unatangazwa ipasavyo inafikiwa, siku za karibuni waziri wa maliasili na utalii aliunda kamati ya wajumbe 21 kwa ajili ya kufanya kazi moja ya kuitangaza Tanzania na maliasili zake. Hili ni jambo muhimu na zuri sana kutangaza maliasili za Tanzania ambazo ni kiutio kkikubwa sana, pia idadi ya wageni au watalii ambao wanatembelea Tanzania haiendani wala hairidhishi. Kwa vivutio tulivyo navyo hapa Tanzania na idadi wa wageni tunaowapata ni ndogo, hivyo kwa kuwa wageni ni wachache basi hata mapato ni machache sana.
Najua kwa asilimia kubwa tunapoandaa mipango ya kutangaza utalii wetu huwa akili na mawazo yetu yanaenda kwa wazungu, hivyo tunafanya kila kinachowezekana kwa wazungu kupata taarifa muhmiu na namna ya kufanikiwa kufika Tanzania na kutembelea vivutio vilivyopo. Mipango mizima na mbinu za kuongeza wageni zinakuwa za kuwavutia sana wazungu, hili sio jambo baya wala sio vibaya kuanza namna hiyo. Lakini nataka tutumia nguvu kubwa zaidi kuwasaidia watanzania wenzenzetu ili na wao waanze kutengeneza shauku na mitazamo ya kutembelea hifadhi za wanyamapori na vivutio vingine.
Pia tafiti zinaonyesha kabisa kwamba watanzania wamebadilika na wanatembelea hifadhi za wanyama, ingawa idadi yao ni ndogo kulinganisha na wingi wa watanzania wote lakini hata hatua ndogo hizo ni muhimu na bora zaidi. Tutumia nguvu kubwa zaidi kuwekeza kwa waanzania kutembelea vivutio vyao wenyewe, ili hata kama hao wazungu wakiamua kuja au wasipo kuja sisi tutakua na shehemu yetu ya kufanya na tutaifanya kwa ubora.
Na sisi watanzania, tunatakiwa kuwa msitari wa mbele kuonoza kwenye jambo hili, tunatakiwa kushiriki kuitangaza Tanzania kwa kutembelea vivutio vyake na ukipata muda washirikishe wengine vitu vizuri ulivyojifunza.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania