The continued existence of wildlife and wilderness is important to the quality of life of humans.Jim Fowler

Namna nzuri ya kufupisha maisha yetu hapa duniani ni kufupisha maisha ya viumbe hai wengine kama vile wanyamapori na mimea. Mimea na wanyama hasa wanyamapori wanahitaji mazingira ya asili kabisa ili waweze kuishi na kuzaliana, na endapo wanyamapori watafugwa basi, itahitajika mazingira ya asili yanayoshabihiana na yale ya mwituni. Kanuni za asili zitabakia kuwa za asili hakuna namna tunaweza kuzibadili kuwa kitu kingine, kufanya tofauti na asili ndio mwanzo wa matatizo na mwishowe kupelekea matatizo makubwa tusiyoweza kuyatatua.

Kwenye tafakari ya leo, ambayo mwandishi Jim Fowler anatuambia ni kwamba kuendelea kuwepo kwa wanyamapori na maeneo yao ni muhimu kwa ubora wa maisha ya binadamu. Hii ni kauli ya kweli kabisa ambayo nataka na sisi tuitafakari na kuwa na kufanya kwa hekima kwenye maliasili zetu. Hakuna anayefanya juhudi kubwa ya kuhifadhi wanyamapori kwa ajili ya wanyamapori pekee, kuhifadhi wanyamapori na mazingira yao au makazi yao ni muhimu sana kwasababu sio tu wanyama wataendelea kuwepo bali hata maisha ya binadamu yataendelea kuwepo na yatakuwa bora.

Gharama kubwa ya maisha itakuwa pale ambapo tumeharibu makazi ya wanyamapori na kuwaua wanyamapori kwa kutimiza mahitaji ya muda mfupi. Gharama kubwa ya maisha itakuwa pale ambapo tutachafua na kuua kabisa vyanzo vya maji. Tunatakiwa kufikiri kwa kina zaidi inapofika wakati wa kutumia maliasili muhimu zenye kugusa mamilioni ya maisha ya viumbe hai.

Suala la uwepo wa wanyamapori na makazi yao sio swala la kundi fulani la watu wanaojisikia na kuwa na mapenzi ya kuhifadhi na kuwafurahia uwpo wao. Hili ni jambo ambalo linamuhusu kila mtu ambaye yupo katika uso wa dunia, iwe unapenda au huwapendi wanyamapori, iwe unapenda au hupendi makazi yao, suala la kuhakikisha uwepo wao unaendelea kuwepo hapa duniani ni la kila mmoja wetu, sio swala la kujisikia au la kupenda ni suala la mfumo wa maisha, ni suala la kutengeneza mfumo mzima wa maisha yetu na maisha ya viumbe hai wengine.

Ndio maana uhifdhi wa wanyamapori na mazingira kwa ujumla sio suala la nchi husika pekee ni suala linalohitaji ushirikiano wa dunia nzima, ni upo hapo kijijini kwenu au kwenye mji wenu hakuna sehemu ambayo itawavuta watu wengi na hisia za nchi mbali mbali kama mazingira na utunzaji wake.

Popote pale ulipo simama kama balozi, simama kama kiongozi kutunza na kulinda mazingira, maana kwa kufanya hivyo unaokoa si tu maisha ya viumbe hai wanaotegemea mazingira hayo moja kwa moja bali unaokoa maisha ya vizazi vingi vya sasa na baadaye.

 

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania