Kutokana na wingi wa rasilimali tulizo nazo katika nchi ya Tanzania inawezekana kabisa imechangia maendeleo kwenye upande mmoja tu na kuacha maeneo mengine yakiwa hayajaguswa kabisa. Katika uhalisia wake Tanzania ni nchi yenye fursa nyingi sana kwenye kila sekta, hii ni kutokana na jografia yake katika uso wa dunia. Wingi wa fursa na rasilimali unaweza kuwa ndio sababu kubwa ya kuweka vipaumbele kwenye kukuza na kuzitumia fursa hizo. Kwa miongo kadhaa iliyopita ukiangalia vipaumbele vya kukuza uchumi na maendeleo vimekuwa kwenye kilimo, na madini nk. Lakini kuna upande mwingne ambao umeachwa ambako kuna fursa nyingi sana za kukuza uchumi na kuitangaza Tanzania. Hii ndio sababu kubwa kumekuwa hakuna mapato ya kuridhisha yatokanayo na uwepo wa rasilimali hizi za utalii. Sababu kubwa ni uwekezaji kidogo tulioweka kwenye sekta hii ya utalii. Ukifahamu Jambo Hili Utaishi Kwa Busara Na Kuwajibika Siku Zote
Kwa jinsi siku zinavyokwenda sekta ya utalii inazidi kukua na kuwa na ushindani mkubwa sana hapa duniani, kila nchi yenye rasilimali za kuvutia wageni na wawekezaji kwenye utalii wametumia mbinu na kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sehemu hii ili kuwavutia wawekezaji na wageni kutalii kwenye nchi yao. Ingawa nyingi ya nchi ambazo zinafanya uwekezaji mkubwa kwenye utalii hazina maeneo wala rasilimali nyingi kuliko Tanzani, wanaonekena kupata mapato makubwa kutokana na uwekezaji wao kwenye sekta ya utalii.
Aidha, ninapoandika haya simaanishi kwamba Tanzania haifanyi uwekezaji kwenye sekta ya utalii, wala simaanishi hakuna juhudi za zinazofanyika kuwekeza kwenye sekta hii, juhudi zipo na uwekezaji upo, lakini kwa kiasi gani? Unajitosheleza? Unakidhi viwango vya kisasa vya ushindani kwenye soko la utalii. Ingawa tuna kila kivutio kwenye nchi yetu, nimejifunza kwamba haitoshi tu kuwa na rasilimali nyingi zenye mvuto wa kitaifa na kimataifa kama rasilimali hizo hazisaidii kuboresha maisha ya watu kutokana na uwepo wake, manufaa yanatakiwa kuonekana na kuwasaidia watu ili wote watambue kwamba ni muhimu kuendelea kutunza na kuhifadhi kwa ajili ya manufaa zaidi ya baadaye.
Kuchelewa kwetu kuwekeza kisasa kuendana na kasi na teknologia inachangiwa na mambo mengi na moja ikiwa ni bajeti ya kufanya hivyo, nchi yetu inakabiliwa na changamoto nyingi kwenye kila sekta, kwa mfano sekta ya miundombinu, sekta ya afya, sekta ya kilimo, sekta ya elimu nk. Ni sekta zenye changamoto kubwa sana na hivyo hata kama kutakuwa na bujeti za kufanya maendeleo moja kwa moja inabidi ziende kulenga maeneo muhimu yanayohitaji suluhisho la haraka na pia kulingana na vipaumbele vya serikali na pia wanaangalia kutimuza malengo ya milenia. Hivyo kwa sababu chache hizi, fedha nyingi hutawanywa sana na kusambabisha sehemu ndogo ya fedha kwenda kwenye uwekezaji kwenye sekta hii ya utalii.
Licha ya kwamba sekta ya utaii Tanzania inazalisha fedha nyingi kulinganisha na sekta nyingine bado fedha zinazorudi kwenye maendeleo ya sekta ya utalii ni ndogo, na hii inasababishwa na changamoto tulizo nazo kama taifa. Pamoja na hayo yote bado tunahitaji kwenda mbele na kuwa na mafanikio kwenye sekta hii, kuna kila sababu ya kuwa na mapato mengi, kuna kila sababu ya sekta hii kuongoza kwa kuwa na mapato ya juu kabisa kuliko sekta nyingine hapa Tanzania sababu ni nyingi na inawezekana kabisa kufanikiwa kwenye sekta hii.
Serikali, wadau wa utalii na wadau wengine wa maliasili wanatakiwa kuweka mfumo bora kabisa unaowavutia wawekezaji kwenye sekta hii, na sio tu wawekezaji kutoka nje ya nchi bali kutoka hata Tanzania, yaani wawekezaji wa ndani. Kama biashara ya ushindani, sekta ya utalii Tanzania inatakiwa kufanyiwa ufuatiliaji makini na tafiti nyingi zinahitajika ili kuhakikisha hakuna kinachoturudisha nyuma na kama kuna sehemu inachangamoto itatuliwe mapema. Kwenye ufanyaji wa kazi hii inahitaji sio tu mtu anayeweza kuifanya, bali mtu mwenye shauku na pia nidhamu ya hali ya juu, uadilifu na kujituma. Maana inahitaji ufuatiliaji makini, kujua tabia za watu, kujua maeneo muhimu ya kuweka nguvu zaidi, kujua mienendo ya soko la utalii duniani, kujua majira na hali ya hewa, hali za kisiasa za nchi, tamaduni za watu, hali ya miundombinu ya utalii, hali ya kiuchumi na bei za bidhaa, sheria za fedha na kila kitu kinachogusa sekta hii kinatakiwa kueleweka kwake na kukiweka kwenye msitari mzuri ili mazingira ya kuwavutia watalii yawe bora zaidi.
Naamini kabisa hakuna sehemu bora hapa duniani kuwekeza kama Tanzania hasa kwenye sekta ya utalii. Kwa sababu kuna kila kinachotakiwa kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta hii, amani ipo, maeneo yapo, watu wapo tena wakarimu kweli kweli. Kwa miaka ya nchi yetu tangu tupate uhuru ni miaka 56 tu, hivyo kulinganisha na nchi nyingie utaona sisi bado wachanga, hivyo hatuna budi kujifunza kwa wenzetu waliotutangulia kwenye sekta hii, wenzetu wana miaka 100, wengine 200 wengine 80 na wengine 40 na 50, tunahitaji kujifunza kwa kila mtu ili kuweka ubora kwenye utalii wetu. Kuna nchi nyingine ambazo ni change zaidi yetu lakini wamepiga hatua kubwa sana kwenye utalii na wanaendelea kufanya vizuri, tujifunze kwao pia. Mfano mzuri ni majirani zetu Kenya, tuna mengi ya kujifunza kwa mafanikio na makosa yao kwenye utalii.
Jambo jingine zuri, ambalo huwa napenda nguvu kubwa iwekwe ni kwenye kuinua na kukuza utalii wa ndani hakuna kitu kizuri kama kuona watanzania wao wenyewe wanahamasika na kuwa wakwanza kwenye kutembelea maeneo ya vivutio vya nchi yao. Hapa panahitaji kazi kubwa sana, na tafiti zinaonyesha kadri siku zinavyokwenda mitazamo na hali ya watanzania inabadilika sana, ukienda hifadhini utakutana na watanzania na familia zao wanatembelea hifadhi na kupiga picha wanyamapori, hii ni hatua kubwa sana hivyo endapo tutawekeza zaidi hapa tutakuwa na watalii wa kutosha kwenye maliasili na vivutio vyetu.
Kuna mengi ya kuandika kwenye makala hii, lakini kwa kadri siku zinavyokwenda tutaendelea kujifunza na kushirikishana maarifa haya kwenye blogu hii ya wildlife Tanzania, naamini tutajifunza na kuyafanyia kazi, lakini pia kwa wadau na serikali wanaweza kutumia kusaidia kufanya baadhi ya maamuzi ya kukuza sekta hii. Makala ifutatayo nitafafanua maeneo muhimu ambayo yanahitaji uwekezaji kwenye sekta hii ya utalii. Hivyo endelea kijifunza na kufuatilia makala hizi. Ukiwa na ushauri, maswali au mapendekezo usisite kuwasiliana nami kwa mawasiliano yaliyopo chini ya makala hii.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania