Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunatafakari kidogo kuhusu baadhi ya mambo muhimu kwenye rasilimali hizi. Ni jambo la kisheria na la msingi kwa watanzania wote kufahamu kuwa uwepo wa rasilimali katika nchi yetu ni kwa ajili yetu na kwa ajili ya vizazi vijavyo. Hivyo basi kwa kutambua hilo sheria na katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania imeanisha na kuweka wazi jambo hili ili kuhakikisha haki za msingi na za kikatiba zinafuatwa katika utoaji wa huduma hizi kwa jamii.

Pamoja na kuwa maliasili na rasilimali zote za nchi ya Tanzania ni mali ya watanzania, usimamizi na utoaji wa huduma zitokanazo na rasilimali hizi haujakabidhiwa moja kwa moja kwa watanzania. Bali ungalizi na utoaji wa faida na manufaa mengine umekabithiwa au upo chini ya serikali ya Jamhuri ya Tanzania. Hivyo basi kwa kufanya hivi na sheria imetamka wazi kuwa Rais ndiye atakayekuwa na mamlaka ya mwisho kwenye namna ya utumiaji wa rasilimali hizi, au kwa namna nyingine ni kwamba dhamana kuu ya kuhakikisha maliasili na rasilimali zote za nchi ya Tanzania zipo chini ya Rais kwa niamba ya watanzania wote.

Lakini hapo hapo sheria inataka wananchi ndo wawe walinzi na wasimamizi wa rasilimali hizi kwenye maeneo yao. Hii ni kwasababu wananchi ndio waliopo karibu zaidi na rasilimali hizi na wao ndio wahanga wa changamoto za uhifadhi wa rasilimali hizi. Na ili kuendana na njia nzuri ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine ilikuwa ni lazima jamii ishirikishwe kwa kila hatua, ili serikali na wanajamii washirikiane kwenye uhifadhi wa maliasili hizi.

Ingawa changamoto kubwa ni namna gani nzuri ya kuisaidia jamii kuona na kuthamini maliasili hizi, kwa asilimia kubwa kazi kubwa imefanyika kuhakikisha jamii inaelewa na kufahamu nia ya serikali ya kuhifadhi wanyamapori misitu na rasilimali nyingine muhimu. Pamoja na haya yote mwitikio kutoka kwa wananchi unaendelea kuwa mzuri kuhusu uhifadhi na njia nzuri ya kusherikiana na serikali na wadau wengine wa uhifadhi na mazingira katika kutimiza adhma yao.

Kazi kubwa inaendelea kubaki kwa viongozi na wadau wengie wanaotoa huduma kwa jamii kuhakikisha jamii inapata taarifa zote sahihi na za wazi kuhusu jinsi ambavyo rasilimali zao zinavyo simamiwa na serikali na watu wengine. Kusipokuwa na uwazi mara nyingi hakuna uwajibikaji, hivyo jamii inatakiwa kufahamu kwa kina na kushirikishwa kwenye hatua za kupanga mikakati na mipango ya uhifadhi, utumiaji na uwekezaji wowote kwenye sekta hii.

Naamini kabisa endapo jamii itapata taarifa sahihi mara kwa mara kuhusiana na uhifadhi, matumizi na usimamizi wa rsilimali zao kwenye kila ngazi basi dhna pana ya uhifadhi itawaingia wananchi na wengi wataelewa na kuwa walimu wazuri kwa wengine. Na pia taarifa, uwazi na uwajibikaji unapokuwepo hata jamii itakuwa na shauku ya kushirika hatua zote muhimu za uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za nchi.

Naamini katika kufanya kazi kwa pamoja kutaleta matokeo makuba na bora kwenye sekta hii ya uhifadhi wa wanyamapori. Hivyo ni jukumu la wadau wote ikiwemo na viongozi wanaosimamia maliasili hizi kufanya kazi kwa uwazi na weledi ili jamii itambue mchango wao na kuwa tayari kushiriki katika uhifadhi.

Asante sana kwa kusoma makala hii, tukutane kwenye makala ijayo hapa hapa.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania