Kila mtu anaweza kuongea sana na kuelezea mipango yake, kila mtu anaweza kujisifia mikakati yake na mipango yake aliyojiwekea. Kwa kweli kupanga na kutenda ni vitu viwili tofauti kabisa, unaweza kupanga kitu ukakaanacho kwa miaka hata kumi bila hata kukitekeleza, kila mwaka unaahirisha kila mwezi unaairisha, unasema utaanza mwakani au utaanza mwezi ujao. Hii ndio hali ilivyo kwa watu wengi ambayo inapelekea halii hii kuingia kwenye biashara na kwenye makampuni na hata kwenye sekta za uzalishaji. Ukifuatilia kwa ukaribu kila sekta na kila wizara hapa Tanzania ina mipango na mikakati yake mizuri sana imeandikwa kwenye makaratasi bila kuwa na utekelezaji wowote.

Nimesoma ripoti nyingi kwenye sekta ya maliasili na utalii hapa Tanzania, nimegundua kwenye ripoti hizo kuna maelekezo na uchambuzi wa kitaalamu ambao kama ungefuatwa na kutekelezwa tungekuwa kwenye hatua nzuri sana kwenye utalii wetu. Mambo mengi mazuri yapo kwenye makaratasi, tunayaongea kila siku, yanashauriwa kila siku na watalamu na wadau wa utalii na uhifadhi wa wanyamapori. Kwa kweli kuna faida kubwa sana ya kuingia kwenye utekelezaji wa mipango na mikakati ya kukuza na kuinua utalii wetu, tuachane na habari za kuongea tu bila utekelezaji. Kama kuna kitu tunachoweza kukifanya sasa ni kuingia kwenye utekelezaji wa mipango na mikakati tuliyojiwekea ya kukuza utalii hapa Tanzania.

Moja ya ripoti nilizosoma zinaeleza kwa kina kuhusu ukuaji wa utalii katika kanda ya Kaskazini, inaeleza kwa kina utalii wa aina mbili ule wa picha na ule wa uwindaji, ikionyesaha namna kila utalii unavyoweza kuongeza na kuleta mapinduzi makubwa kwa nchi yetu kwenye upande wa pato la taifa. Kama inavyofahamika na katika uhalisia wake utalii kwa upande wa Kaskazini mwa Tanzania umekua na kufahamika kuliko kanda nyingine za Kusini na Magharibi.

Ukuaji wa utalii kwa uapnde wa Kaskazini mwa Tanzania inatoakana na mipango mingi ya kuinua utalii kutekelezwa, vile vile uwepo wa miundombinu mbali mbali imechangia sana ukuaji wa utalii kwenye ukanda huu. Utalii wa picha unashika kasi sana na unakadiriwa kutoa mapato makubwa sana kwa siku zijazo kuliko utalii wa uwindaji. Hivyo nguvu kubwa inatazamiwa kuwekezwa kwenye utalii wa picha kuliko ule utalii wa uwindaji.

Tanzania ina zaidi ya Hifadhi ya taifa ya Serengeti na Kilimanjaro, ambazo huingizia mapato makubwa nchi yetu kwa njia ya utalii. Tanzania ina Hifadhi za Taifa 16, ina mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngororongoro ambayo ni moja ya maajabu saba ya dunia na ni sehemu inayoheshimika sana duniani na shirika la kimataifa la UNESCO limeitaja mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro kuwa sehemu ya urithi wa dunia. Mapori ya akiba 28, mapori tengefu 44 na maeneo ya hifadhi ya jamii au WMAs 38. Haya yote ni maeneo muhimu sana kwa uwekezaji wa utalii wa picha na utalii wa uwindaji. Tunaweza kuapaga vizuri ili kuwe na uwiano mzuri wa uzalishaji kwenye sekta hii. Kwa mfano ukanda wa kusini ambako kuna maeneo mengi sana ambayo hayajulikani sana kwa utalii wa picha kutokana na miundombinu mibovu na sababu nyininge maeneo haya yanaweza yakatumika vizuri chini ya usimamizi makini kuwa maeneo ya uwindaji wa kitalii, jambo hili litaweka usawa wa uzalishaji kwenye sekta hii.

Pia kwa kuwa ukanda wa kskazini kuna maendeleo makubwa ya utalii wa picha, utalii wa uwindaji usingeendelea kufanyika tena maeneo haya, badala yake ungehamia kusini ili kujaribu kuweka usawa na kupunguza gharama kubwa za maandalizi ya kuwekeza kwenye utalii wa picha. Utalii wa picha unahitaji uwekezaji mkubwa sana na wa gharama kubwa kuliko ule wa uwindaji ambao ni rahisi kufanyika sehemu yoyote. Kabla ya kuwa tayari tuanze utekelezaji wa mipango yetu ya kuinua utalii hadi kufikia na kupita malengo tuliyojiwekea kwa mwaka.

Jinsi ambavyo tunachelewa kutekeleza mipango yetu, ndio tunavyochelewa kufikia mafanikio tunayoyatarajia kwenye sekta hii. Hakuna njia nyingine rahisi ya kufanikiwa kwenye hili bila kuchukua hatu na kutekeleza mipango yetu. Tukumbuke sio sisi pekee ndio tuna maliasili na vivutio vya utalii, utalii umekuwa biashara ya ushindani sasa, kuna majirani zetu wanatumia nguvu kubwa sana kutangaza utalii wao, sisi pia tunaweza kuanza kufanyia kazi kwa kasi ili kujiweka kwenye nafsi tunayostahili. Hakuna faida yoyote ya kuandika mipango na mikakati mizuri ambayo hatuitekelezi, hakuna faida yoyote ya kutumia fedha nyingi kufanya utafiti na uchambuzi kwenye sekta ya utalii kama hatutachukua hatua kufanyia kazi mapendekezo na ushauri wa watalaamu wenye tija.

Kuna nafasi na fursa kubwa sana ya kufanikiwa zaidi kwenye sekta ya utalii hapa Tanzania kuliko sekta nyingine yoyote, tujipange na tuchukua hatua za utekelezaji mara moja. Napenda kuishi kuona maliasili zetu za wanyamapori na misitu zinatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania na kuboresha maisha wa wananchi wote hasa wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hizi.

 

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania