Habari msomaji wa makala za mtandao huu, karibu kwenye makala hii muhimu niliyoandika kutoa ujumbe kwenye siku ya wanyamapori duniani. Sisi kama wadau wakubwa wa maliasili hii tuna wajibu wa kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana na nchi nyingine katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine. Katika ardhi ya Tanzania tumebarikiwa kuwa na spishi nyingi sana za wanyama na mimea, tumebarikiwa kuwa na sehemu nyingi ambazo ni kivutio kwa watalii, tuna mandhari zenye hadhi za kimtaifa, tuna kila aina ya vivutio na mazingira mazuri ya asili.

Katika makala hii nataka kuangazia mambo kadhaa ambayo tunapaswa kuyaangalia kwa jicho la tatu ili kuhakikisha uhifadhi una tija kwa jamii yetu, mambo haya sio mapya sana, ni mambo ambayo tumekuwa tunajifunza na kuyasoma kwenye makala mbali mbali za kila siku. Nimemua kutumia siku hii ya wanyamapori duniani tujikumbushe baadhi ya mambo muhimu ili tuwe na hamasa kubwa ya uhifadhi wa maliasili zetu na kuhakikisha maliasili hizi zinamanufaa ya kudumu kwa kizazi cha sasa na cha baadaye. mambo haya ndio yanayoshika kasi kwenye masuala mazima ya uhifadhi.

1.Ujangili na biashara haramu za wanyamapori

Katika harakati za mapambano ya kutokomeza ujangili na biashara haramu za wanyamapori na bidhaa zao ndipo tunapojua kwa kina ujangili ulivyojikita na kuweka mizizi mirefu kwenye kila maeneo muhimu kwenye jamii yetu na kwenye nchi kubwa duniani. Kwa miaka 5 ya nyuma takwimu zinaonyesha mauaji makubwa ya tembo kwa ajili ya biashara ya meno ya tembo kwenye nchi za Aisa Ulaya na Marekani. Kwa tafiti nyingi na za kina zinazofanywa kila siku zinaonyesha jinsi ambavyo ujangili na biashara haramu za viumbe hai kama wanyamapori zinavyofanyika na kuhusisha watu wakuu na viongozi wakubwa serikalini. Kwa hiyo ni mtandao ambao unaanzia chini kabisa ambapo wanajamii wanatumwa kwenda kuua tembo, wakati mwingine au mara nyingi askari wa wanyamapori wanatumika kwa kufanya ujangili huu, baadaye meno au pembe hizo husafirishwa hadi nchi kubwa za China, Japani, Vietnam na baadhi ya nchi ya Ulaya na Marekani.

2.Shughuli za kibinadamu kando kando ya hifadhi za maliasili

Tunashuhudia kila siku idadi ya watu ikiongezeka kwa kasi hasa kwenye nchi zetu za Afrika, kwa mika 20 iliyopita hii haikuwa tishio, lakini sasa idadi ya watu inakuwa tishio kwa wanyamapori na misitu ya asili, na vyanzo vya maji. Tumeshuhudia upanuzi wa mashamba, tumeshuhudia upanuzi wa maeneo ya makazi ya watu, tumeona watu wakiharibu misitu ya asili kwa ajili ya kupata maeneo ya kilimo na ufugaji. Jambo hili ndilo linaloleta migogoro ya ardhi isiyoisha kwenye jamii yetu. Mambo haya yamekuwa na athari kubwa sana kwenye maeneo ya wanyamapori kwani yamepunguza maeneo ya makazi na malisho kwa wanyamapori na kusababisha wanyamapori na mifugo kuwa na mwingiliano ambao unaweza kusababisha kuambukizana magonjwa yatokanayo na wanyama hivyo kusababisha uharibifu mkubwa.

3.Maeneo, migogoro na hifadhi za misitu na wanyamapori

Maliasili za nchi yoyote zinalindwa na sheria na kanuni, hivyo endapo kutakuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni zilizowekwa kwa ajili ya uhifadhi na usimamizi wa maliasili hizi, bila shaka hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaovunja sheria hizo, wafugaji wamekuwa na adha hii kwa muda mrefu kwenye maeneo yao, wamekuwa wakikabiliwa na adha hii kwa sababu ya kulisha mifugo yao kwenye hifadhi za wanyamapori na misitu. Kwa kuwa hatua kali  zinachukuliwa dhidi yao wamejiona kuwa kama wanaonewa na kupelekea kuwa na mtazamo mbaya kwa wanyamapori, au kuwachukia wanyamapori, jambo ambalo linaweza kusababisha jambo jingine baya zaidi kama kulipiza kisasi endapo mifugo yao imeliwa na wanyama wanaokula nyama. Pia hata wakulima wamekuwa wahanga wa wanyamapori pale ambapo wanyamapori wamekuja na kuharibu au kula mazao yao, hali hii imesababisha jamii kuwa na mtazamo hasi kuhusiana na wanyamapori. Hivyo tunapoadhimisha siku ya wanyamapori duniani, haya ni mambo ambayo tunatakiwa kuyafikiri kwa kina ili tuone tunayatatuaje.

4.Faida ambayo jamii inaipata kutokana na wanyamapori kwenye maeneo yao

Nguvu kubwa ya kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelevu ni kuishirikisha jamii kwenye masuala ya uhifadhi wa maliasili, jamii ina haki kwa mujibu wa katiba na kwa mujibu wa sheria za nchi kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine muhimu. Jamii hii sio tu wana wajibu wa kuhifadhi maliasili hizi, lakini pia wana haki ya kunufaika na maliasili hizo. Serikali na wadau wengine kwenye sekta hii ya uhifadhi wa maliasili tunatakiwa tujitafakari sana kwenye eneo hili ili kuhakikisaha maliasili na jukumu la uhifadhi lisiwe mzigo kwa jamii yetu, bali liwe ni jambo ambalo jamii inapenda kulifanya na inafurahia kulifanya, na hapa ndio tunapaswa kuangalia kwa kina faida na maslahi ya jamii kutokana na wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Hatua kubwa zinatakiwa kupigwa kwenye kipengele hiki.

  1. Uanzishwaji wa mradi ya maendeleo kwenye maeneo ya hifadhi ya maliasili

Maeneo ya maliasili yamekuwa na rasilimali nyingi muhimu, sio tu uwepo wa wanyama na mimea lakini pia kuna madini na rasilimali nyingine muhimu kama vile gesi nk. Hivyo kwa kuwa serikali ndio wanajukumu na ndio mwamuzi wa mwisho kwenye rasilimali hizi, wawekezaji na hata washauri wa uchumi na maendeleo wanatakiwa kuzingatia sana maisha na makazi ya miaka mingi ya wanyama na mimea ya eneo hilo. Tumeona barabara zikipitishwa kwenye maeneo ya wanyamapori, tumeona mitambo na uwekezaji mkubwa kwenye maeneo ya wanyamapori, pia tumeona kilimo kikubwa cha mpunga kinachotishia sana maeneo ya wanyamapori. Kuna miradi mingi ambayo pande zote mbili zinatakiwa kuelewa na kufanya maamuzi sahihi na yenye tija kwa muda mrefu.

6.Utalii

Utalii ni njia nzuri sana ya kuongeza thamani kwenye maliasili zetu, hatuwezi kuwa wahifadhi tu, tunatakiwa pia kuwa na utalii kwenye hifadhi zetu, kuna utalii wa aina mbili utalii wa picha na utalii wa uwindaji. Katika nchi yetu sehemu pekee ambazo utalii wa uwindaji hufanyika ni kwenye maeneo yote ya hifadhi ya wanyamapori isipokuwa hifadhi za taifa na hifadhi ya eneo la Ngorongoro. Maeneo yote yanaruhusu utalii wa picha. Kwa vyovyote vile utalii umekuwa ni nguzo muhimu katika uhifadhi na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uhifadhi na maendeleo katika sekta nyingine.

7.Rushwa

Kama kuna ugonjwa mbaya sana unaomaliza maliasili zetu ni rushwa, rushwa imekuwa ikitajwa kwenye ripoti zote za ujangili, biashara haramu, hadi kwenye usimamizi wa maliasili hizi. Rushwa imeabomoa kabisa maadili na kusababisha maelfu ya tembo na wanyama wenine kutoweka, rushwa imechangia sana kutokea kwa majangwa kutokana na uharibifu wa mazingira. Rushwa imechangia kuteketezwa kwa hekta za mamia kwa maelfu ya misitu ya asili. Uhifadhi ni zaidi ya kujua wanyama na mazingira yao asilia, ni kazi inayohitaji nidhamu kwenye usimamiaji na utunzaji wa mapato yatokanayo na rasilimali. Pia kujua madhara ya rushwa kwenye mfumo wa ikolojia na usimamizi wa wanyamapori na mistu.

Kuna mengi naweza kuyaandika hapa kuhusiana na siku hii, lakini nataka leo tupitie maeneo haya saba na kuyatafakari kwa kina ili tuwe na uhifadhi endelevu. Changamoto zetu ni kubwa na zinahitaji zaidi ya elimu kwenye utatuzi wake, nyingine zinahitaji nidhamu na uadilifu kwenye maamuzi, usimamizi na kujifunza.

Nakutakia siku njema katika maadhimisho haya ya siku ya wanyamapori duniani ambayo hufanyika kila tarehe 3 ya mwezi March ya kila mwaka. Tuchukue hatua!

Ahsante sana

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania