Habari msomaji wa makala za kila siku za wanyamapori, karibu kwenye makala ya leo ambayo ni uchambuzi wa ripoti maalumu inayohusisha jinsi bandari ya Mombasa Kenya inavyojihusisha na usafirishaji haramu wa meno ya tembo na bidhaa nyingine kinyume na sheria za nchi, na sheria za wanyamapori. Katika ripoti hii ya utafiti uliofanywa na mashrika makubwa yanayojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori, lakini yanayofanya kazi kubwa sana ya kufuatilia nyendo na kila kinachofanyika kuhusiana na wanyamapori kuanzia sehemu za ujangili, watu wanaotumiwa, watu wa kati wanaopokea mzigo na kusafirisha, njia za usafirishaji, hadi kufikia watumiaji wakuu na matumizi ya bidhaa hizo kwa wateja wake.

Mashirika haya ni ya kimataifa na yameanzishwa kwa lengo hilo la kupambana na ujangili kwa njia zote na kuhakikisha njia za kufanya ujangili zinajulikana na jinsi ambavyo wahifadhi na wadau wengine wa maliasili wanavyoweza kubuni mbinu mbadala za kutatua changamoto hiyo ili kuhakikisha wanyamapori wanatunzwa na kuhifadhiwa kwa ushirikiano mkubwa. Mashrika haya yaliyofanya utafiti na kuandika ripoti hii ni Wildleaks, Elephant Action League (EAL) pamoja na ushirikiano wa karibu na watu kutoka katika serikali ya Kenya na wadau wengine.

Ripoti hii inaanza kwa kutaja kuwa bandari ya Mombasa ni moja ya bandari muhimu sana kwa ajili ya usafirishaji katika bara la Afrika. Licha ya kuwa bandari hii ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi ya Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki, pia imekuwa ni bandari inayosafirisha meno ya tembo kwa kiasi kikubwa sana ukilinganisha na bandari nyingine, inakadiriwa kiasi cha zaidi ya tani 43 za bidhaa haramu za vitu mbali mbali zimesafirishwa kupitia bandari hii kwa miaka mingi tangu mwaka 2009 hadi ripoti hii inakamilika mwaka 2015.

Bandari ya Mombasa ni moja ya bandari kubwa na ya kisasa kuliko bandari zote za Afrika mashariki, ambayo ina uwezo wa kuchukua zaidi ya makontena milioni moja kwa mwaka. Kwa mujibu wa ripoti hii muhimu inaonyesha kwamba kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara bandari ya Mombasa ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya makontena kwa mwaka baada ya bandari ya Durbani iliyopo nchini Afrika Kusini ambayo inapokea zaidi ya makontena milioni moja kwa mwaka jambo ambalo linawapa fursa serikali ya Kenya kupanua na kuongeza bandari yao hadi. Bandari ya Mombasa huwa inasimamiwa na Mamlaka ya bandari ya Kenya na Mamlaka ya mapato ya Kenya. Hivi ndio vyombo vikuu vya serikali ya Kenya ambavyo husimamia kwa karibu kila kitu kwenye bandari ya Kenya, pia vyombo vingine vinavyojihusha na kufanya kazi na mamlaka ya bandari ya Kenya ni Jeshi la polisi na huduma za wanyamapori za Kenya.

Bandari hii imekuwa ndio mhusika mkuu wa usafirishaji wa meno ya tembo kutoka bara la Afrika hadi kwa watumiaji wakuu kwenye bara la Asia, kwa mujibu wa katibu mkuu wa CITES anasema usafirishaji mkubwa wa meno ya tembo kuanzia mwaka 2009 hadi 2011 ulikuwa unatokea Kenya au Tanzania ambapo ilikuwa imehifadhiwa kwenye makontena makubwa ambayo yalipakiwa na kusafirishwa kupitia bandari kuu ya Mombasa na Dar es salaam Tanzania. Pia ripoti hii inaonyesha kuwa taarifa za umoja wa mataifa zinaelezea kuhusu biashara haramu za dawa za kulevya zinatokea sehemu mbali mbali duniani, lakini inasema bandari ya Mombasa imekuwa ndio kiini na sehemu kuu ya kusafirishia kwenda nchi nyingine duniani.

Katika kufanya uchunguzi wa siri na wa kina kuhusiana na bandari ya Mombasa timu ya watafiti kutoka kwenye mashirika ya Wildleak na Elephant Action League, waliingia kwenye bandari hiyo kwa mbinu ya aina yake kama wafanyakazi wa kampuni ya madini, jambo ambalo liliwafanya waweze kujua na kuchunguza kwa kina kila hatua za ukaguzi, upakiaji na usafirishaji wa makontena hapo bandarini, kwa muda wa kufanya ukaguzi huu waligundua mapungufu makubwa sana sio tu kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa haramu lakini pia masuala ya kiusalama hayakuwa sawa.

Kwenye ukaguzi wa bandarini kuna mashine ambazo hutumiwa na mamlaka za bandari kwa ajili ya ukaguzi wa makontena, na mamlaka hayo ndio huamua ni kontena gani la kukagua kulingana na wingi wa makontena, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi inaonyesha kuwa mamlaka za bandari, maafisa wa polisi, na mamlaka ya mapato ya Kenya wanazozana sana kuhusu ukaguzi wa kontena, lipi la kufanyia ukaguzi na lipi sio la kukagua. Hivyo kumekuwa na mambo ya kuangalia maslahi binafsi na mambo ya rushwa. Pamoja na hayo kuna maafisa wa inteligensia ambao pia huamua kontena gani lichunguzwe. Pia ukaguzi wa makontena unategemea sana ni nani anafanya biashara kwa muda mrefu na kuwa ana makontena mengi anaweza asifanyiwe ukaguzi kwenye makontena hayo.

Aidha usafirishaji wa makontena na bidhaa kupitia bandari ya Mombasa unatoa msamaha kwa baadhi ya bidhaa kutochunguzwa au kupekuliwa, bidhaa kama majani ya chai ambayo husafirishwa kwa kiasi kikubwa kwenda nchi nyingine. Hii ni kutokana na makubaliano yaliyokubaliwa na nchi wanachama wa Afrika Mashariki miaka mitano iliyopita kuhusu makontena yaliyobeba majani ya chai yasipekuliwe au kuchunguzwa. Kutochunguzwa kwa makontena yaliyopakia majani ya chai yanapofika bandarini ni mwanya mkubwa sana kwa wasafirishaji wa bidhaa haramu kama vile meno ya tembo, pembe za faru au bidhaa nyingine za wanyamapori.

Kama tunavyojua sehemu yoyote ile ambapo vitu haramu vinafanyika basi suala la rushwa halikosekani, rushwa imetajwa sana na inaonekana inasaidia sana kurahisisha usafirishaji haramu wa meno ya tembo na bidhaa nyingine haramu. Takwimu zinaonyesha kuwa nchi ya Kenya inashika nafasi ya 145 kati ya 175 kwa rushwa duniani. Kwenye ripoti hii inaonyesha kabisa kuwa zaidi ya tani 640 za rosewood zilisafirishwa kutoka Madagasca mwaka 2014 kupitia bandari ya Mombasa.

Kwenye ripoti hii mambo mengi yameandikwa kuhusu bandari ya Kenya inavyotumika kama kitovu cha usafirishaji wa mweno ya tembo na bidhaa nyingine haramu amabazo zimekatazwa kusafirishwa kwa mujibu wa sheria. Hii ni ripoti ambayo ina taarifa za ndani na za siri ambazo watu wenye nia mbaya na maliasili zetu hutumia kwa ajili ya kuendeleza bishara hii haramu za ujangili wa wanyamapori na mimea.

Uchambuzi wa ripoti hii utasaidia sana kujua maeneo ambayo majingili na watu wanaofanya bishara haramu za maeno ya tembo na pembe za faru hutumia ili kuwafikia walengwa. Naamini kabisa sehemu hizi za bandari hutumiwa na watu wenye uwezo na wenye nafasi za juu serikalini, usafirishaji wa madawa ya kulevya, meno ya tembo, pembe za faru na hata bidhaa au nyara za serikali bila kufuata taratibu na sheria za nchi na sheria za kimataifa ni kosa la jinai na hukumu yake ni kubwa sana.

Nchi zote zenye bandari zinatakiwa kuwa macho na kuhakikisha ulinzi wa uhakika pamoja na ukaguzi wa kina unafanyika mara kwa mara ili kukomesha biashara na usafirishaji huu haramu. Bandari ya Mombasa ni mfano mzuri jinsi watu wanavyotumia bandari hizi kusafirishia magendo na vitu haramu. Urahisi wa kusafirisha unapokuwepo hata ujangili hauwezi kuisha kwenye hifadhi na maliasili zetu. Kunapokosekana usafirishaji hata ujangili utapungua. Hivyo ili kuongeza na kudhibiti ujangili kwenye hifadhi na kwenye mapori yetu haitoshi tu kuwa na askari kwenye mapori na hifadhi zetu, bali tunatakiwa kuwa na ulinzi na usimamizi kwenye vituo vyote vya usafirishaji kama vile bandari, vituo vya mabasi, viwanja vya ndege na sehemu nyingine za usafirishaji.

Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu kwa makala nyingine.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania