Nimekua narudia kusoma dhima (ujumbe) wa siku ya wanyamapori duniani wa mwaka 2018 na kuona jinsi ambavyo dunia inazidi kuteketea kwa kuendelea kupoteza maelfu ya wanyamapori ambao ni muhimu sana kwenye mfumo mzima wa ikolojia ya hifadhi na maisha ya viumbe hai wengine. Katika kusoma katika ukurasa mbali mbali na tovuti ya UN, taarifa na ujumbe ulioandaliwa na shirika la umoja wa mataifa kwa siku ya wanyamapori duiani ni Big Cats” kwa Kiswahili chake ni “Paka wakubwa”.  Paka wakubwa wapo katika hatari ya kutoweka duniani, elimu, nguvu, na ushirikiano unahitajika katika uhifadhi wake.

Katika ujumbe mfupi uliotolewa kwenye siku hii ya wanyamapori duniani, umeonyesha jinsi ambayo dunia inavyoendelea kushuhudia kuporomoka kwa idadi ya wanyama hawa wanaokula nyama maarufu kama paka wakubwa. Big cats’ au paka wakubwa ni wanyama jamii ya paka mfano simba, chui, duma, na tiger wanyama hawa ambao wanakabiliwa na majanga mbali mbali yanayopelekea kuendelea kupungua kwenye makazi na maeneo yao. Kwa mujibu wa taarifa ya siku ya wanyamapori duniani iliyotolewa na shirika la umoja wa mataifa inaonyesha hatari kubwa sana inayowakabili wanyama hawa kwa mfano kwa miaka mia moja iliyopita idadi ya tiger imeporomoka kwa asilimia 95. Huku idadi ya simba ikiporomoka kwa asilimia 40. Hii ni hali ya kutisha sana kutokea kwenye wanyamapori muhimu kama hawa.

Siku ya wanyamapori duniani iliundwa mwaka 2013, baada ya nchi wanachama na wadau wengine wa masuala ya uhifadhi wa maliasili na wanyamapori kuamua kuitangaza kuwa siku ya tarehe 3 Machi kila mwaka itakuwa ni siku ya wanyamapori duniani. Siku hii huambatana na jumbe na dhima kuu zenye lengo la kuhamasisha jamii kufuatilia na kuelewa kuhusu wanyamapori. Lengo la siku hii kutoa elimu na ufahamu kwa jamii na pia kuhakikisha uelewa wa wanyamapori unawaelea wanajamii na dunia nzima. Hivyo nchi wanachama, serikali za nchi na wadau wengine wa sekta hii ya wanayamapori wanatakiwa kuitumia siku hii kuhakikisha umma unafahamu kuhusu wanyamapori, athari wanazokabiliwa nazo, na faida kuu wanayoweza kutoa kwa jamii endapo watatunzwa na kuhifadhiwa.

Wanyamapori wanafaida kubwa sana kwa jamii na kwenye ikolojia ya mazingira, watu wana shauku kubwa ya kuwaona wanyama kama simba, chui na hata duma. Wanyama hawa wanaovuta sana hisia za watu na kufanya waonekane wa kipekee sana kwenye mazingira yao wamesaidia sana kukuza utalii na kuinua uchumi wan chi mbali mbali kupitia shughuli za utalii. Katika ujumbe uliotolewa na umoja wa mataifa kwenye siku hii ya wanyamapori duiani, inawaomba watu wote wakubwa kwa wadogo kushirikiana katika uhifadhi wa paka hawa.

Tanzania tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutupa ardhi yenye utajiri wa wanyamapori. Na naamini kabisa tunatakiwa kuuelewa zaidi ujumbe ulotolewa kwenye siku ya wanyamapori duniani. Wakati dunia ikishuhudia kupungua na kuporomoka kwa wanyama hawa jamii ya paka idadi ya wanyama hawa jamii ya paka kama vile simba , chui na duma sio mbaya kwa hapa Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine duniani. Hii ni kwa sababu tuna maeneo mengi makubwa ya kutosha na pia kazi nzuri inayofanywa na serikali na wadau wengine kwenye usimamizi wa rasilimali hizi. Ingawa kuna changamoto za hapa na pale zinazowakabili wanyama hawa hapa Tanzania, ni changamoto ambazo zinatatulika na zinaweza kuisha endapo tutashirikiana kwa pamoja.

Wanyama kama tiger, hawapatikani kabisa katika nchi ya Tanzania, jamii kubwa ya wanyama aina ya tiger wapo kwenye nchi za Asia na Marekani. Tiger ni wanyama waliopo kwenye msitari mwekundu ikiashiria wapo hatarini kutoweka duniani. Kwa taarifa zilizotolewa kwenye siku ya wanyamapori duniani inaonyesha idadi ndogo sana ya tiger duniani ikiwa ni 4000 pekee. Licha ya kuwa tiger wapo hatarini kutoweka bado kuna ujangili na biashara haramu zinazosababisha kupungua kwa tiger kila siku. Watu wemekuwa wanatumia bidhaa za tiger kama vile meno, kucha, Ngozi na mifupa kwa ajili ya mapambo na urembo. Hivyo biashara haramu imeshamiri sana kuwakabili wanyama hawa. Ni jukumu la kila mmoja kwa sehemu alipo kuwajibika  na kufanya kazi na mamlaka husika ili kutokomeza ujangili kwenye maeneo yao. Nguvu na juhudi za kila moja zinahitajika ili kukomesha mauaji na biashara haramu za wanyama hawa.

Kwa Tanzania na maeneo mengi ya Afrika ambao wana paka jamii ya simba, duma na chui changamoto kubwa ipo kwetu wenyewe na jamii yetu. Changamoto kubwa zinazotishia sana idadi ya paka hawa kwa hapa Tanzania ni uwindaji usiozingatia sheria na weledi, uwindaji unaosababishwa na jamii kulipiza kisasi kutokana na mauaji ya mifugo yao, kuweka sumu kwenye mizoga na kusambabisha wanyama hawa kufa baada ya kula mzoga wenye sumu, pia kuna sababu za kitamaduni ambazo husababishwa na baadhi ya makabila kuendeleza mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati na hazina tija kwa taifa na jamii kwa ujumla. Hizi ndio baadhi changamoto kuu zinazowakabili wanyama hawa kwa hapa Tanzania na sehemu nyingine Afrika.

Ili kuendelea kutoa uelewa kwa jamii kuhusu hali ilivyo kwa wanyama hawa, siku ya wanyamapori duniani haitakiwi kuishia tarehe 3 Machi, inatakiwa iendelee na kila siku iwe siku ya wanyamapori duniani, tukiwa na nia na lengo moja tu la kuhifadhi wanyamapori wetu kwa manufaa ya sasa na ya baadaye. Wanyama hawa wakitoweka au kupungua kwenye maeneo yao sio kwamba wataharibu mfumo wa ikolojia yao na ya wanyama wengine tu, bali hata mfumo wa maisha ya binadamu utaathirika pia. Hivyo tunapokazana kuwahifadhi wanyama hawa na wanyamapori wengine pamoja na mazingira yao tunatengeneza nafasi nzuri sana ya sisi kuwa na maisha bora na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.

Hivo naamini kwa dhima kuu ya mwaka 2018 kuhusu big cat, itakuwa na matokeo makubwa kwenye hifadhi na mapori yetu ya wanyamapori. Tutaendelea kuelimisha na kujifunza mambo haya ili tuwe na kitu bora cha kuwarithisha watoto wetu na vizazi vijavyo.

Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu kwa makala nyingine.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania