Habari msomaji wa makala za mtandao huu, karibu kwenye makala ya leo, leo tunatakiwa tujiulize swali moja muhimu sana kuhusiana na uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine muhimu. Uwepo wa wanyamapori na rasilimali nyingine muhimu kama vile misitu, madini na vitu vingine unategemea sana maamuzi yetu na matendo yetu ili viweze kuendelea kuwepo kwa miaka mingi na kuwanufaisha vizazi vingi vijavyo.
Afrika imbarikiwa kuwa na rasilimali nyingi muhimu na adimu sana duniani, kuna kiasi kikubwa cha mamilioni ya hekta za misitu ya asili, kuna idadi kubwa ya wanyamapoari na maeneo muhimu ya kuwahifadhi, kuna hali ya hewa nzuri na pia kuna uwepo rasilimali nyingine muhmu kama vile ardhi yenye rutuba, mito, madini, mafuta na gesi. Hivi ni vitu ambavyo kwa kiasi kikubwa vipo katika ardhi ya Afrika na Tanzania. Ukweli ni kwamba ili tunufaike na uwepo wa rasilimali hizi kwenye maeneo yetu, inahitajika maamuzi mamzuri pamoja na usimamizi mzuri wa rasilimali hizi.
Kadhalika Afrika imebarikiwa kuwa na idadi kubwa ya wanyamapori na mimea mingi mizuri na adimu ambayo haipatikani sehemu nyingine hapa duniani. Wanyamapori wana historia ndefu sana katika bara la Afrika na hususana katika pembe ya afrika Mashariki, kwa miaka mingi Afrika imekuwa ikitumiwa na mataifa mengine kama sehemu ya kupata malighafi kwa ajili ya viwanda ambavyo vipo kwenye mataifa ya Ulaya, Asia, na Marekani. Malighafi hizi zimekua za aina nyingi, kama vile pamba, katani, kahawa, madini, pembe za faru, meno ya tembo na hata Ngozi za wanyamapori.
Kwa miaka mingi nchi za Asia kama vile China, Japani, Vietnamu na nchi nyingine za Ulaya zimekuwa zinatumia njia mbali mbali kupata malighafi kwa ajili ya nchi zao, kwa karne hii moja kati ya malighafi kubwa iliyosababisha uharibifu mkubwa kenye maliasili zetu na meno ya tembo, pembe za faru, na biashara za wanyamapori na sehemu za miili yao. Kwa mfano uhitaji wa meno ya tembo umekuwa wa juu sana kwa nchi kama China, Japani na Vietnam kutokana na matumizi yao yasiyo na msigi kwenye nchi zao.
Katika kufanikisha adhma yao ya kupata meno ya tembo na pembe za faru au wanyamapori wengine huwa wanawatumia watu wetu, wasimamizi waliopewa dhamana na serikali zetu kwa ajili ya kuhakikisha ulinzi wa wanyamapori hawa. Taarifa nyingi za ujangili na biashara haramu ya usafirishaji wa bidhaa za wanyamapori na meno inaonyesha kabisa jinsi ambavyo wasimamizi wetu ambao wapo kwenye sehemu za uhifadhi wa maliasili zetu wanavyotuangusha na kuwa sehemu ya kufanya uharamia na ubadhirifu kwenye maliasili zetu.
Kwa mujibu wa taarifa za kina kutoka katika ripoti za uhifadhi wa wanyamapori na ujangili inaonyesha kabisa jinsi ambavyo rushwa inaharibu maliasili zetu. Watu ambao wanawatumia askari au wasimamizi wa maliasili kwenye hifadhi zetu, huwa wanauwezo wa kutumia hadi watu wa juu serikalini kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya ujangili kwenye hifadhi za wanyamapori.
Swali langu litabakia kuwa ni hili, je, tutaendelea kutumiwa kama vibarua na wasio na faida kwa mataifa na watu ambao wanatushawishi kuwaua wanyamapori wetu wenyewe kwa faida yao binafsi?
Fikiria jinsi ambavyo wanyamapori wanapukutika, angalia jinsia ambaovyo tembo wanaisha kila wakati, kuna taarifa fulani niliona juzi BBC, kuna mtu alikuwa anaelezea jinsi ambavyo tunawapoteza tembo wetu kila saa na kila dakika. Alisema kwa siku idadi ya tembo 100 wana uwawa na majangili. Hii ni idadi ubwa sana, na takwimu zinaonyesha kuwa tumebakiwa na idadi ndogo sana ya tembo hapa duniani, yani idadi ya tembo wanaouwawa na wale wanaozaliwa ni kwamba idadi ya wale wanaouwawa ni kubwa kuliko ya wale wanaozaliwa.
Tupende maliasili zetu, tuwe wazalendo, na kukataa kutumika kwa namna yoyote ile kwenye masuala ya ujangili na rushwa. Jambo hili linawezekana na linaanza na sisi wenyewe.
Ahsante sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania