Umewahi kusikia kuhusu “Tembo wa kale” au kwa lugha ya kingereza wanaitwa “Mammoth” walikuwa ni tembo ambao waliishi duniani miaka 10,000 iliyopita, hii ni kwa mujibu tafiti za wagunduzi wa sayansi ya mambo ya kale. Hawa walikuwa ni tembo wa kubwa sana ambao kwa mujibu wa vyanzo mbali mbali vya habari za utafiti inaonyesha tembo hawa walikuwa na urefu wa au kimo cha mita 4.3, wakiwa na mengo makubwa sana yenye urefu wa mita 4. Hawa ndio wanaitwa tembo wa kale au mammoth. Kwa sasa hatuna tembo wakubwa namna hii hapa duniani, walishatoweka na kupotea kabisa, lakini tumebakiwa na meno yake kwenye makumbusho mbali ya nchi za China, na Russia.
Picha ya mammoth
Nimeanza makala hii kwa kujenga ufahamu huu kwanza ili tuweze kwenda sambamba kwenye uchambuzi wa ripoti hii muhimu iliyoandaliwa na timu ya watafiti na wataalamu wa masuala ya upeleleze kuhusu wanyamapori na mimea, kwa upande wa wanyamapori watafiti hawa ambao hufanya kazi na shirika lisilo la kiserikali linalojuliakana kama Elephant Action League (EAL), wamekuwa wanafanya kazi kubwa na ya hatari katika uhifadhi wa wanyamapori. Lakini wamejikita kufanya utafiti na uchunguzi wa kina ili kubaini ujangili kwenye hifadhi zetu, miji yetu na kwenye sehemu muhimu za usafirishaji. Pia wanajikita katika kufuatilia kwa karibu kujua mtandao unaohusika na uuzaji wa pembe za faru na meno ya tembo ili kuwakamata na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria na kuharibu kabisa mtandao hou haramu.
Baada ya kujiridhisha kuwa taifa la China ndio muhusika mkuu wa meno ye tembo na biashara nyingi za meno ya tembo hufanyika katika taifa hili kubwa duniani linaloongoza kuwa na idadi kubwa ya watu, timu ya wataalamu katika masuala ya uchunguzi na utafiti iliingia nchini China na kufanya uchunguzi wa kina kwenye miji yote mikuu ya nchi hii ambapo biashara ya meno ya tembo na pembe za faru hufanyika na kutumiwa zaidi na wachina wenyewe. Baada ya kufanya uchunguzi na utafiti wa kina kwa muda usiopungua miezi kumi kuanzia mwishoni mwa mwaka 2014 hadi kufikia ukingoni mwa mwaka 2015 ripoti hii ilikuwa imeshakamilika na kupewa kichwa cha habari kinachojulikana kama “Blending Ivory, China Old Loopholes, New Hope”. www.elephantleague.org
Ripoti hii iliyosheheni kila aina ya taarifa ambazo sisi kama wahifadhi tunahitaji kuzijua kwa ajili ya kujipanga na kupanga mikakati ya kuua au kutokomeza kabisa mtandao huo na kuhakikisha biashara hii haramu haiendelei sehemu yoyote duniani. Sambamba na hilo kuweka mbinu na mipango ya kuhakikisha wanyamapori, hasa tembo na faru ambao wanawindwa na kuuliwa sana na majangili, wanalindwa sana kwa mbinu bora za kisasa, hivyo basi maarifa na taarifa zilizomo ndani ya ripoti hii ni muhimu kuzifahamu na kuzielewa na kila mtu, hivyo nawapa rai wasomaji wa makala hii kutafuta ripoti hii na kuisoma kwa makini ina mambo mengi ambyo tunapaswa kuyafahamu mapema ili kuwa na ufanisi kwenye uhifadhi wa maliasili zetu.
Kama nilivyoanza na utangulizi wa kuelezea kuhusu aina ya tembo ambao walisha wahi kuishi hapa duniani miaka zaidi ya elfu kumi iliyopita, tembo hawa wanajulikana kama tembo wa kale, au kwa lugha ya kingereza wanaitwa Mammoth. Tembo hawa wa kale waligundulika huko Kaskazini Mashariki mwa Rashia (Russia), baada ya barafu kuyeyuka ndipo walipoona mabaki ya tembo hawa ambao walikuwa na meno makubwa sana. Meno haya yaliuzwa kwa nchi ya China bila hata kuwa na kibali chochote, na hata usafirishaji wa meno ya tembo hawa wa kale hauitaji kibali cha CITES, hivyo kwa kuwa hakuna kibali cha kusafirisha meno kwenda sehemu yoyote nchi ya China ilikuwa na hazina kubwa ya meno ya tembo hawa wa kale.
Wafanyabiashara ambao walimiliki mizigo mikubwa ya meno ya mammoth hawakusumbuliwa wala kuwa na usumbufu wa vibali kama ilivyo kwa wamiliki wa meno ya tembo wa kawaida ambao umiliki, usafirishaji na hata biashara ya meno yake unahitaji mlolongo mrefu sana unaojumuisha kuwa na kibali kutoka kwa CITES na nchi wanachama,
Kwa kuwa kulikuwa na unafuu kufanya biashara ya meno ya tembo wa kale au mammoth, wafanyabishara wengi walitumia njia hii kuendesha biashara haramu ya meno ya tembo ambao sio mammoth. Ukweli kutoka kwenye ripoti hii unaonyesha wazi kuwa meno ya mammoth na meno ya tembo wa kawaida hayana tofauti yoyote ingawa meno ya mammoth ni ya miaka mingi iliyopita. Kwasababu hiyo wafanya biashara wakubwa nchini china walitumia mwanya huo kuchanganya meno na bidhaa za mammoth na za tembo wa kawaida na kuuza kwa wateja wao bila shida yoyote.
Biashara ya meno ya tembo wa kale au mammoth ilianza kushamiri kwenye miaka ya 2000. Jambo ambalo lilipelekea kuanzishwa kwa viwanda na vinu vya kufulia na kutengeneza vitu na bidhaa nyingi kutokana na meno ya mammoth. kwa mujibu wa ripoti hii inaonyesha kuwa walioanzisha viwanda kwa jina la mammoth, hawakuwa na lengo la kuuza au kutengeneza vifaa au bidhaa kwa kutumia meno ya mammoth pekee bali kwa ajili ya kuficha biashara haramu za meno ya tembo ambayo sio mammoth. Na kwa kuwa hakuna anayejali kama mfanyabiashara au mtu anamiliki bidhaa za mammoth, wafanyabiashara waliamua kutumia mwanya huo kuimarisha biashara zao kwa njia zisizo halali. Hii ni moja kati ya kampuni kubwa sana zinazojihusisha na meno ya tembo huko China inaitwa. Beijing Mammoth Art Co LTD.
Hii ni kampuni kubwa sana na inayojulikana sana kutokana na biashara kubwa inazofanya na kumiliki kiasi kikubwa cha meno na bidhaa za meno ya tembo. Kampuni hii ambayo ni kubwa sana ina matawi mengine katika jiji la Hong Kong ambapo husambaza bidhaa zake na kuuza sehemu mbali mbali ndani ya nchi ya China. Kuhusiana na suala la kuwa na vibali vya kuendesha biashara hii, mmoja kati ya watu waliohojiwa na timu ya wataalamu hawa alisema kuwa, kinachohitajika hapa China ili kuendesha biashara hii ya meno ya tembo ni kupata kibali tu kutoka kwa mamalaka husika. Taarifa zinaonyesha kwamba haijalishi meno ya tembo unayomiliki umeyaotoa wapi au yametoka sehemu gani duniani, kinachotakiwa ni kupata leseni au kibali ili kuendelea na biashara zako kama kawaida.
Kwa mantiki hii ni kwamba China haikuwa inajishughulisha kwa dhati katika kampeni za kupinga ujangili wa tembo na pia kukiuka makubaliano ya CITES kwamba hawakuruhusiwa kununua meno ya tembo kutoka nje ya nchi hasa Afrika kutokana na idadi ya tembo kwenye hifadhi za wanyamapori kupungua kwa kasi na kusababisha kukosekana kwa utulivu kwenye hifadhi za wanyamapori, pia kwa kutokufuatilia meno yametoka wapi au yametokea sehemu gani hii inaonyesha kuwa hakuna juhudi za dhati kuzuia na kupambana na majangili ambao wanzidi kumaliza tembo wa Afrika.
Aidha, taarifa za kitafiti kwenye ripoti hii zinaonyesha wazi kuwa wamiliki wa kampuni ya Beijing Mammoth Art Co LTD, wanamiliki pia kampuni za uwindaji kwenye nchi za Afrika ya Kusini na Zimbwabwe, hivyo kwa kuwa na kampuni za uwindaji na kuwa na washirika wanaojihusisha na uwindaji wa wanyamapori na kuwasafirisha wakiwa wamekufa au kusafirisha nyara zao ndivyo wanavyofanya wafanyabiashara hii ya meno ya tembo ili kuhakikisha malighafi hazikosekani kwenye viwanda na kwenye masoko yao.
Pia taarifa zinasema kuwa kuna idadi kubwa ya makreti ambayo hubeba nyara za wanyama na bidhaa nyingine ambayo husafirishwa hadi kuwafikia walengwa. Hakuna mtu anayewza kujua ndani ya makreti hayo kuna kitu gani, sio rahisi kufahamu, hivyo njia hii ndio inayochochea kuongezeka kwa ujangili katika bara la Afrika.
Kwa hali hii hatuwezi kukaa chini na kushangaa, kila kukicha watu wanaamka na mbinu mpya ya kuendelea kuangamiza na kuhakikisha wanyamapori hasa tembo na faru wanapotea na kutoweka katika uso wa dunia. Ripoti hii ningeshauri isomwe na wahifadhi na watu wote wanaosimamia wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Usipojua adui yako anafanya nini huwezi kujiandaa na kuchukua tahadhari. Macho ya dunia sasa yapo Afrika unapozungumzia masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na misitu.
Cha kusikitisha zaidi ni kwamba waafrika wenyewe ndio wanaotumika katika ujangili wa kuwauwa wanyama wao wenyewe, na wakikamatwa wanaishia kufia jela wakati wahusika wakubwa ambao wapo kwenye mataifa makubwa hakuna hatua zozote za kisheria wanazochukuliwa, wao wanaendelea kutamba mtaani na familia zao. Lakini wale waliofanya kazi ya hatari za kuingia porini na kuua tembo, hakuna kikibwa wanachoweza kunufaika nacho na hakuna ulinzi wowote endapo atakamatwa anafanya ujangili. Hivyo ndugu zangu waafrika na wale mnaoshawishiwa kufanya vitendo hivyo vya kijangili chonde chonde rafiki, ukisikia mtu anakwambia habari hizo kimbia na usikubali kamwe, kamwe usikubali hata kama umeahidiwa kiasi gani cha fedha.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255683 862 481/+255742 092 569
www.mtalaam.net/wildlifetanzania