Habari msomaji wa mtandao wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo tujifunze jambo ambalo ni muhimu kuhusu maliasili zetu. Katika msimu huu wa sikukuu za Pasaka watu wengi wapo kwenye mapumziko ya kazi na wanaweza kutumia muda huu kutembelea sehemu mbali mbali za vivutio vya wanyamapori, misitu, mambo ya kale au makumbusho, mambo ya utamaduni au kwenda sehemu za fukwe za bahari kwa mapumziko. Huu ndio msimu mzuri sana kwa watu wenye shauku ya kutembelea vivutio vilivyopo hapa Tanzania.

Ikumbukwe pia hapa Tanzania kuna kila kitu unachotaka kukiona, hasa kwenye masuala ya utalii na vivutio, kama nilivyoainisha hapo juu, kuna watu wanapenda kuona wanyamapori, kuna wengine wanapenda kuona misitu minene, kuna wengine wanapenda sehemu zenye miteremko na maporomoko ya maji, kuna wengine wanapenda sehemu zenye mambo ya kihistoria, au mambo ya kale na wengine watapenda kutalii sehemu za fukwe na sehemu za mambo ya kitamaduni. Mambo haya yote yapo hapa Tanzania.

Maeneo haya yote yaliyopo hapa Tanzania yamesheheni mambo mengi ya kusisimua na kufurahisha. Utakapotembelea maeneo haya utajifunza na kujua mambo mapya kabisa ambayo ulikuwa huyajui kwenye maisha yako. Waswahili wanasema tembea uone, hivyo na mimi nakwambia sio tu tembea uone bali tembea ujifunze, ushangae na maisha yako yatakuwa na mtazamo mpya kwasababu utakutana na  vitu vipya na vya kuvutia sana.

Hivyo ni wewe mwenyewe kuamua sehemu gani itakuwa rahisi kwako kutembelea kwenye msimu huu wa sikuku za pasaka. Na kama hujui shemu ya kwenda msimu huu wa pasaka usisite kuwasiliana nami. Pengine unataka kwenda kutalii sehemu za wanyamapori au sehemu za kihistoria zenye mambo ya kale, usisite kuwasiliana nami kwenye jambo hilo. Nitakupa utaratibu wote ambao unatakiwa kwa ajili ya kufika eneo husika na kutalii.

Tumepewa maisha yaha tuyafurahie na kuwa na amani, hivyo unapopata nafasi wakati huu, itumia kwa ajili ya kuboresha maisha yako na kuyafanya maisha yako kuwa na furaha wakati wote. Kuna vitu ukivigundua kwenye maisha yako unakuwa na furaha na vinaongeza thamani kwenye maisha yako. Hivyo jipe nafasi hiyo, wape watoto wako nafasi hiyo, na pia mpe mwenzi wako nafasi hiyo, maisha hayatabaki kama yalivyo.

Nimeandika makala hii kukumbusha na kukuhamasisha kuchukua hatua na kutalii hapa nyumbani Tanzania. Amua na chukua hatua kwa ajili ya maisha yako na nchi yako.

Asante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255683 862 481/+255742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania