Maisha siku zote yamekua ni kujifunza kutokana na wengine na kujifunza kutokana na vitu mbali mbali ambavyo vimetokea na vinavyotokea kila kona ya dunia. Ukweli ni kwamba katika kujifunza vitu mbali mbali hakuna anayeweza kupata vitu vyote kwa wakati mmoja na kujifunza na kufahamu kila kitu. Maisha yamekuwa na maana nyingi sana kutokana na maeneo ambayo watu wanaishi, utamaduni na hata Imani. Dunia ina kila aina ya watu ambao wana aina yao ya maisha ambayo ni tofauti na maisha tunayoyaishi sisi au tulioyazoea kuyaona mara kwa mara. Dunia bado ina mambo na vitu vizuri na vya kushangaza vinavyofanywa na watu mbali mbali kutokana na tamaduni, sehemu wanazoishi na mfumo wa maisha yao.
Tangu dunia iumbwe na watu waumbwe kumekuwa na mtawanyiko mkubwa sana ambao umesababisha watu kuwa na mifomo tofauti tofauti ya maisha, mifumo hiyo tofauti ndio imetufnya kuwa tofauti. Kuna sehemu hapa duniani watu wanakula vitu ambavyo wewe huwezi kula, kuna sehemu hapa duniani watu wanafanya vitu ambavyo wewe huwezi kufanya wala hujawahi kufikiri kama kinaweza kufanyika. Kuna watu hapa duniani wanaishi maisha ambayo wengine hawawezi kuyaishi kabisa. Hivyo ndivyo binadamu alivyoumbwa na uwezo mkubwa wa kuishi vyovyote na wa kufanya vitu tofauti tofauti. Hapo bado sijaweka maswala ya Imani, kuna watu wanaamini vitu ambavyo wengine hawawezi kuamini kabisa, wana Imani tofauti kabisa na wengine.
Tofauti hizi ndio zinafanya maisha kuwa na mvuto wa kipekee, sisi binadamu huwa tunapenda sana vitu vya kushangaza na kuvutia, hiyo ndio asili yetu, tunapenda kuona na kusikia vitu visivyo vya kawaida hasa kama vimefanywa na wanadamu wenzetu. Kwa asili tunapenda miujiza na kuona vitu vikubwa vinavyofanyika hata nje ya upeo wa maisha yetu, binadamu tunapenda kushangazwa, tunapenda kuona vitu vipya vikitokea.
Hii ndio maana Mungu alituweka sehemu tofauti tofauti na tuishi maisha tofauti tofauti yasiyofanana na mtu mwingine, ndio maana kuna watanzania, wakenya, waitalia, waisraeli, wachina , wajapani, wamarekani wahispania, wabarazili nk. Hawa wote wapo sehemu tofauti tofauti na wana maisha tofauti na wengine. Utofauti huu ndio unafanya maisha kuwa ya kipekee na yenye mvuto mkubwa.
Kama hiyo haitoshi, kwenye nchi yaani ndani ya nchi husika sio watu wote wanafanana na sio wote ni weupe na sio wote ni weusi. Kwa mfano nchi ya Tanzania ina zaidi ya makabila 120, haya makabila yote yasingekuwepo kama hakuna utofauti kati yao, kuna utofauti mkubwa sana kwenye masuala mengi sana hasa ya utamaduni, mila na desturi, mfumo wa maisha na hata lugha zao za asili zinatofautiana, hata vyanzo vya kipato na njia za kujipatia chakula zinatofautiana ndio maana sehemu nyingine ni wafugaji na sehemu nyingine ni wakulima, sehemu nyingine wanalima mahindi pekee sehemu nyingine wanalima mpunga, sehemu nyingine ni wavuvi, sehemu nyingine wanalima kahawa na sehemu nyingine hawalimi kabisa kahawa tena wanaweza wasijue chochote kuhusu kahawa labda kama wamesoma shuleni au sehemu nyingine.
Kwanini naandika haya yote, ni kwasababu nataka kuweka mambo kwenye msitari mmoja ya kuwa maisha yana maana mbali mbali kwa watu tofauti tofauti, usiyafikiri na kuyaamulia maisha kwa tafsiri yako mwenyewe kwenye eneo dogo unalojua la Kijiji au nchi yako. Kumbuka kuna maisha ambayo hujayajua na hujayaishi hivyo fikra na mawazo yako yasihitimishe kuwa maisha yana rangi ya moja pekee. Maisha yana rangi nyingi sana ambazo umeziona wewe kuna wengine wameziona nyingi zaidi ya hizo rangi, na kuna wengine hawajaona rangi yoyote, hivyo kwa mantiki hii ndipo linapokuja suala la elimu kuwa haina mwisho na kujifunza hakuna mwisho. Ni mjinga pekee ndiye anaye weza kufkiri na kujiaminisha kuwa ameshajifunza na kufahamu kila kitu kwenye maisha.
Aidha kwa kutambua jambo hili, nchi mbali mbali zimekuwa makini sana kuhakikisha zinatumia njia mbali mbali kwa ajili ya kuhifadhi na kutunza utamaduni na vitu mbali mbali vinavyoonyesha utamaduni na maisha ya watu wa kale walioishi aina fulani ya maisha tofauti na sisi wa leo. Utamaduni una nafasi yake kubwa sana kwenye nchi yoyote, utamaduni umekuwa ndio kitambulisho kikubwa kwa nchi na mataifa mbali mbali hapa duniani. Na kwasababu watu wapo tofauti hivyo na utamaduni ni tofauti na hapa ndipo maisha yanakuwa na mvuto wa kipekee. Kila nchi ina utamaduni ambao inakubali na inautunza kwa gharama zote.
Moja kati ya faida kubwa ya kuwa na utamaduni ni sifa ambayo nchi inapata na kufahamika kwa jambo hilo duniani kote. Kama tunavyojua utamaduni sio jambo moja tu, bali unajumuisha na kuonyesha mfumo mzima wa maisha ya watu au wahusika. Utamaduni ni maisha ya watu, na kama ni maisha ya watu lazima yatahusisha, aina ya vyakula, mavazi, vitu mbali mbali wanavyotumia, Imani zao, makazi, mapokeo yao na hata mahisiano na malezi ya watoto. Hivyo utofauti huu ndio unaowavuta watu kutoka sehemu mbali mbali duniani kuja kuona aina na upekee wa watu ambao wanaishi maisha tofauti na waliyoyazoea. Hii ndio maana sekta ya maliasili na utalii imepewa dhamana kwa mujibu wa sheria za nchi kusimamia utamaduni na kuufanya kuwa sehemu muhimu ya utalii Tanzania.
Utalii wa utamaduni sio maarufu sana na wala haufahamiki sana na wakati mwingine unakosa mvuto kwa wenyeji, hasa watanzania kwa sababu wanajua aina moja tu ya utalii ambao unatangazwa kwa nguvu kupitia njia mbali mbali za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Watanzania wengi unapozungumzia utalii wanajua kuhusu kwenda kutembelea hifadhi za taifa za Mikumi, Ruaha,Serengeti, Manyara, Kilimanjaro nk, kwa ajili ya kuona wanyamapori.
Lakini ni wachache wanaofahamu kuhusu utalii wa kitamaduni ambao una nafasi kubwa sana ya kukuza uchumi na maisha ya watu. Uzuri wa Tanzania kuna kila kitu, yaani utalii wa kitamaduni, utalii wa kutalii hifadhi za wanyama na utalii wa kutembelea fukwe za bahari nk. Tumejitosheleza kwenye hilo. Kuna nchi nyingine duniani hawana wanyama wana utalii tu wa kitamaduni, na wengine hawana fukwe za bahari wana utalii tu wa wanyama, lakini sisi tumebahatika kuwa navyo vyote.
Pamoja na kwamba tuna sehemu nyingi na za kila aina kwa ajili ya utalii, tumekuwa wazito sana kufuatilia na kutembelea sehemu hizi muhimu zenye urithi na kuonyesha jinsi ambavyo wahenga na watu wengine waliishi na wanavyoishi. Kwa mfano hapa Tanzania kuna sehemu nyingi sana za utalii wa kitamaduni kama mabanda ya wamasai amabo hutengeneza vitu mbali mbali kwa ajili ya kuonyesha ubunifu wao kwa jamii na watu wengine kama wazungu.
Lakini ni watanzania wachache sana wanaopenda kwenda sehemu kama hizi kwa ajili ya kuona ubunifu huo na kujifunza aina ya maisha waliyonayo wenzetu. Pamoja na hayo kuna sehemu nyingi sana hapa Tanzania kuna historia za kuvutia za mambo ya kale na vitu vya kale, lakini watanzania wanaopenda kwenda sehemu hizi ni wachache mno. Hii inafanya kutojali utamaduni wetu ambao tunautunza na kuuenzi kwa gharama kubwa.
Kuna sehemu nyingi ambazo tunaweza kwenda kwa ajili ya utalii wa kitamaduni na mambo ya kale. Hii ndio njia nzuri ya kukuza utamaduni wetu kujifunza na kutoa elimu ya uhifadhi na mazingira kwenye jamii yetu. Kuwa mtalii haihitaji uwe na fedha nyingi au uwe tajiri au uwe mzungu au aina yoyote ile, kuwa mtalii unaweza kuwa na mtu yeyote anaweza kuwa mtalii, unaweza kupanga siku zako za mwisho wa wiki ukaamua kwenda sehemu moja kujifunza na kuona mambo ya kale na mambo ya utamaduni ya watu wengine. Hutakosa cha kujifunza endapo utachukua hatua hizo. Jiamulie na jiwekee ka utaratibu kako anza na sehemu za historia zilizopo karibu na maeneo ulipo au unapoishi,nenda pale kafurahie, kajifunze na uulize maswali unayotaka utafurahia hakika.
Sehemu hizi hazina hata gharama kubwa kama wengi wanavyofikiria, sehemu hizi ni gharama nafuu sana kutembelea na kuona. Hivyo fedha isiwe kikwazo cha kutotembelea sehemu hizi muhimu. Kwa uchache napenda niorotheshe baadhi ya sehemu muhimu za kitamaduni na mambo ya kale ambapo unaweza kwenda kutembelea na kujifunza kwa muda wowote.
Makumbusho ya taifa Dar es salam
Sehemu ya Kihistoria ya Bagamoyo
Sehemu ya kihistoria ya Isimila iringa
Mji mkongwe wa Kilwa
Sehemu ya utamaduni na urithi ya Ruaha
Mchoro ya mapangoni huko Kondoa Irangi
Mji mkongwe huko Zanzibar
Msitu wa maajabu wa nyumba Nitu huko Njombe
Hizi ni baadhi tu ya sehemu ambazo unaweza kwenda kutembelea na kujifunza kuhusu tamaduni na mambo ya kale. Uzuri karibu kila mkoa wa Tanzania kuna sehemu ambayo imetengwa kama makumbusho kwa ajili ya kujifunza na kujua tamaduni za wahenga. Ni jukumu letu kuchukua hatua na kujifunza mambo haya ili kuwa watu wenye misingi na wasiofuta kila kitu. Utamaduni wowote ulio mzuri serikali ipo tayari kwa ajili ya kuutunza na kuuridhisha kwa vizazi vingine, lakini tamaduni ambazo sio nzuri zinazoharibu maadili na zisizo na msaada wa kuboresha maisha ya watu hazina faida na zinatakiwa kuondolewa kwenye jamii.
Kuna mambo mengi ya kujifunza sehemu hii ya utamaduni kwenye utalii wetu. Utalii ili uwe na nguvu kubwa lazima sekta husika, sekta ya maliasili na utalii wajifunze namna bora zaidi ya kuunganisha vivutio vyote vya kitamaduni na vile visivyo vya kitamaduni ili kwa pamoja viwe na ushawishi na upekee ambao utawavutia sio wageni na wazungu pekee, bali hata kwa watanzania wenyewe. Hivyo kwa namna yoyote ile tunatakiwa kuelewa na kuja kuwa utamaduni una nafasi kubwa sana kuinua uchumi wa nchi na pia maisha ya jamii husika yanaimarika kutokana na kipato wanachopata kupitia utalii wa utamaduni kwenye maeneo yao. Napia serikali itengeneze mazingira mazuri kwa jamii na watu wanaojihusisha na utalii wa aina hii, maana una faida kwa taifa.
Naamini umejifunza jambo hapa, karibu tukutane kwenye makala nyingine nzuri hapa hapa, pia mshirikishee na mwenzako maarifa haya. Ukiwa na maswali, maoni, ushauri usisite kuwasilia nami.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania