- Yamenifika shingoni, hii sasa imetosha,
Ubaya wa tamaduni, nyingine zinapotosha,
Kutembea hifadhini, twaona ni kujichosha,
Tujenge utamaduni, kutembelea mbugani.
2.Leo naweka mezani, ikibidi badilisha,
Tamaduni wa gizani, hautatufanikisha,
Tumewachia wageni, hatutaki jihusisha,
Tujenge utamaduni, kutembelea mbugani.
3.Nasema najiamini, msiseme ninajikosha,
Utalii si wageni, wala wazungu la hasha!
Vivutio jifunzeni, mali yakufaidisha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
4.Nilikuwa safarini, niliona vya kustusha,
Nilik’a naye kitini, kuwa mtalii kabisha,
Anasema masikini, utali’ bei yatisha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
5.Tanzania fikirini, lini tajitambulisha,
Kilimo nayo madini, bado hayajatuvusha,
Utalii naamini, hakika watupaisha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
6.Tukatalii mbugani, mbona twajichelewesha,
Tuondoke majumbani, tukatalii Arusha,
Sitaki tuwe tabuni, kwa hili ntawajulisha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
7.Tamaduni badilini, kitabuni ntachapisha,
Kwanza twende Saadani, hakika taing’arisha
Tusianze ushindani, tabaki kughairisha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
8.Tuna sifa duniani, utalii siokwisha,
Watoka ujerumani, kuona kujiridhisha,
Sisi tulio jirani, tutaki jishughulisha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
9.Tusishie vitabuni, twende kujielimisha,
Tusikae sana mjini, tembea ona maisha,
Utajifunza njiani, utalii tadumisha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
10.Tujenge utamaduni, mengi nimewajulisha,
Mbona twenda mikoani, utalii sije shusha,
Siwe kama wakoloni, ujinga watupofusha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
11.Waungwana ahsanteni, shairi nahitimisha,
Mengi mewajulisheni, kalamu naidondosha,
Shairi hili someni, hakika la kufundisha,
Tujenge utamaduni, tutembelea mbugani.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255683 862 481/+255742 092 569
www.mtalaam.net/wildlifetanzania