Habari msomaji wa mtandao wetu wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala hii tushirikishane yale ya msingi ambayo yanatupasa kuyaua ili kuweka uelewa mzuri kwenye maliasili zetu na namna tunavyoweza kuwaridhisha watoto wetu taarifa nzuri kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na maliasili zetu kwa ujumla.
Haina maana kuwa na vitu ambavyo hatuvielewi, kila kitu kwenye maisha kinaweza kueleweka endapo kila mtu atajali na kufanyia kazi ili kueleweka. Tanzania ina utajiri mkubwa sana wa maliasili za aina mbali mbali, lakini maliasili hizi hazijajulikana ipasavyo kwa watanzania, bado kuna watu hawana uelewa wa kutosha kuhusu maliasili hizi muhimu hasa zinazohusisha vivutio vya wanyamapori, mambo ya kihistoria, misitu na fukwezwe za bahari.
Kuna sehemu nyingi sana hapa Tanzania ambazo watanzania hawajawahi hata kuzisikia, kuna maeneo yenye historia ya kuvutia na ni hazina inayotambulika kimataifa, lakini ni watanzania wachache sana wanafahamu sehemu hizi. Kazi yetu kubwa sisi ambao tunajifunza na kufahamu sehemu hizi ni kuhakikisha sehemu hizi zinafahamika na kuwa kivutio kwa watanzania.
Inashangaza sana kuona wageni wanafahamu zaidi sehemu hizi kuliko sisi mwenyewe, watalii wanapokuja kutalii au akutembelea sehemu hizi huwa wanashauku sana ya kujua sehemu zenye upekee na historia, wanapenda kuona wanyama, makumbusho na hata kuona mambo ya kale kwenye nchi yetu. Hivyo huwa wanajifunza mengi kutoka kwetu kuliko sisi wenyewe.
Miaka ya nyuma, ukizungumza utalii na kutembelea wanyamapori au vivutio watu wanakushangaa na wanaona kama sio jambo linalowahusu wao. Hivyo wanaona uhifadhi wa vivutio ni kwa ajili ya wageni. Hivyo watu wamekua na utamaduni ambao sio wa kuthamini maliasili zao wenyewe.
Tunatakiwa kuelewa kuwa jamii na watanzania wote tuna haki na wajibu wa kufurahia uwepo wa rasilimali hizi katika nchi yetu wenyewe, tunatakiwa kuzitumia na kuzitanzangaza kwa wenzetu ili iwe sehemu ya utamaduni wetu kufanya hivyo; hii ndio njia nzuri ya kuwarithisha watoto wetu na vizazi vijavyo utamaduni wa kupenda kutalii nyumbani na pia kuwa wazalendo kwa vitu vyao.
Asante sana kwa kusoma makala hii.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania