Habari za siku kidogo kwani tumepotezana kwa muda sasa na hasa kutokana na changamoto zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Lakini kwa sasa nadhani nimerudi rasmi na tutakuwa pamoja katika kulisongesha gurudumu letu la uhifadhi wa wanyamapori kama kawaida yetu. Ukweli ni kwamba niliwakumbuka sana hasa katika kujuzana machache kuhusu wanyamapori na nilikuwa nikipokea jumbe nyingi kwamba mbona nipo kimya, lakini sikuwa kimya kwa kupenda zilikuwa ni changamoto za hapa na pale.
Kama kawaida leo tutaingia tena darasani ili kujuzana mambo machache lakini yenye faida kubwa sana kuhusu wanyamapori. Tunaendelea na mtiririko wetu wa kuwaelezea wanyama jamii ya swala kama tulivoanza hapo mwanzoni. Leo katika Makala hii tutamzungumzia mnyama jamii ya swala ajulikanae kwa jina la “TAYA” ambae kwa lugha ya kiingereza hufahamika kama “ORIBI”. Na sasa bila kupoteza muda kabisa twende moja kwa moja kumjua huyu Taya ni nani na ana sifa zipi ambazo ni tofauti na swala wengine.
Kabla hatujaanza kumuelezea mnyama taya ningependa tufahamu kwamba kuna takribani spishi kumi na tatu za taya hapa barani Afrika. Na ifahamike kuwa wanyama hawa wanapatikana barani Afrika tu na si kwingineko hapa duniani. Ukimuona taya nje ya bara la Afrika basi ujue alisafirishwa kwa madhumuni maalum huko alipo.
SIFA NA TABIA ZA TAYA
Miili yao ina rangi ya manjano au wekundu unao shabihiana na manjano kwa upande wa juu mgongoni.
Maeneo ya shingoni, kifuani, tumboni na nyuma wanyama hawa huwa na rangi nyeupe.
Tofauti na wanyama wengine jamii ya swala, taya ukiwachunguza vizuri utaona wana alama ya manyoya meupe juu ya macho yao iliyo kaa umbo la nusu duara au mwezi mwandamo.
Miili yao ina umbo la yai, wana mashingi yaliyo nyooka, miguu myembamba na mifupi huku mikia yao mifupi ikiwa imejaa manyoya yenye rangi nyeusi nchani.
Madume huwa na pembe ndogo, zilizo chongoka kuelekea juu na zenye miduara sehemu ya chini ambazo hurefuka na kufikia hadi urefu wa sentimita 19 wakati majike huwa hawana pembe kabisa.
Tofauti na jamii nyingi za swala, sehemu za magoti taya wana manyoya mengi.
Ukiwachunguza vizuri chini ya macho utaona kuna alama nyeusi mfano wa machozi, haya ni matezi ambayo mara nyingi madume hutumia wakati wa kuweka mipaka katika himaya zao.
Taya ni miongoni mwa swala wadogo katika kundi hili la wanyama jamii ya swala. Kimaumbo taya hujumuishwa pamoja na ngurunguru (mbuzi mawe) na digi digi.
Ni wanyama ambao huishi kwa kujitenga, hii inamaana kuwa ni mara chache sana kuwakuta taya katika kundi kubwa labda tu pale utakapo wakuta ndama wakiwa pamoja hasa kipindi cha kuzaliana.
Dume na jike huishi kwa uaminifu, dume hudumu na jike wake mmoja mpaka pale mmoja wapo atakapofariki au kuliwa na maadui zao.
Hufanya shughuli zao hasa kula na michezo mingine majira ya asubuhi na alasiri lakini pia majira ya usiku hasa kipindi ambacho mwezi unatoa nuru, kipindi cha joto kali hasa wakati wa mchana wanyama hawa hupendelea kupumzika kivulini.
Wanapo hisi kuna adui hujificha kwenye majani marefu na pale adui anapo karibia zaidi huchomoka kama mshale kwa mwendo wa kuruka ruka juu na chini.
Wanyama hawa pia hujulishana kwa kutumia sauti mithili ya filimbi pale wanapo hisi kuna hatari.
Taya ni miongoni mwa swala wakimbiao kwa kasi sana, kwani wana uwezo wa kukimbia hadi kilometa hamsini kwa saa (km50/saa)
KIMO, UREFU NA UZITO WA TAYA
Kimo: Taya hufikia kimo cha sentimeta 66
Urefu: Kuanzia kichwani hadi mkiani wanyama hawa hufikia urefu wa hadi inchi 45.4
Uzito: Huwa na uzito wa wastani wa kilogramu 22 (kg22)
MAZINGIRA
Taya hupendelea maeneo yenye majani mengi na sehemu yenye vichaka kidogo. Mara nying wanyama hawa huishi karibu na vyanzo vya maji kwani hupendelea kunywa maji karibu kila siku.
Miongoni mwa nchi ambazo wanyama hawa wanapatikana sana na huonekana kwa urahisi ni Tanzania, Zambia, Afrika Kusini, Sierra Leone kuja mpaka maeneo ya Ethiopia.
CHAKULA
Taya ni miongoni mwa wanyama walao majani kama walivyo swala wengine na hupendelea kula nyasi hasa kipindi cha unyevunyevu na majani kipindi cha majira ya kiangazi.
KUZALIANA
Taya hupandana majira yoyote ya mwaka japo mara nyingi huwa kipindi cha mwezi Novemba na Disemba. Mara baada ya kupandana na jike kufanikiwa kubeba mimba, jike hukaa na mimba kwa takribani siku 200 – 210 (sawa na miezi saba) na baada ya hapo huzaa mtoto mmoja tu. Mtoto hubaki mafichoni na hasa sehemu yenye nyasi ndefu kwa takribani wiki 8 -10 tangu kuzaliwa.
Baada ya kipindi cha wiki hizi nane mpaka kumi mtoto huwa tayari kujiunga na kuongozana na baba na mama. Kwa kipindi chote hiki mtoto huwa chini ya uangalizi wa mama kwani mtoto wa taya hutegemea maziwa ya mama kwa takribani miezi 4 – 5.
Watoto wa kike hufikia hatua ya kuzaa mapema kuliko madume. Majike huwa na uwezo wa kubeba mimba wafikishapo miezi kumi wakati madume huanza kupanda pale wafikishapo miezi kumi na nne (sawa na mwaka na miezi miwili). Japo mara baada tu ya miezi 6 na kuendelea watoto wote hufukuzwa kwenye himaya na hapo ndipo dume na jike hujiandaa kwa ajili ya kupandana ili kupata mtoto mwingine.
Umri wa taya wa kuishi hasa katika mazingira yao asilia huwa ni miaka 13 japo katika mazingira ya kufugwa hususani katika bustani za wanyamapori, taya huweza kufikisha mpaka myaka 14.
UHIFADHI
Kutokana na taarifa ya shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na masuala uhifadhi wa maumbile asili (International Union for Conservation of Nature- IUCN) wanyama hawa bado hawajawa hatarini kutoweka duniani. Hii ni kutokana na uwepo wa wanyama hawa katika maeneo mbali mbali hasa hapa barani Afrika. Takwimu za mwaka 1999 zinaonesha idadi ya wanyama hawa ni 750,000.
Katika idadi hiyo, asilimia 50% wapo katika maeneo tengefu ya wanyamapori huku 50% iliyo baki wapo nje ya maeneo hayo. Idadi inazidi kupungua hasa kwa wale walio nje ya hifadhi za wanyamapori na hali hii ikiendelea wanyama hawa watatoweka kabisa baadhi ya maeneo yaliyopo nje ya hifadhi za wanyamapori.
Ukifanya hesabu za haraka haraka utaona kuwa tangu tafiti zifanyike kuhusu idadi ya wanyama hawa mpaka sasa ni miaka 17 sasa, hivyo bado kuna wasiwasi sana juu ya idadi hiyo kama imebaki vile vile au imepungua zaidi.
Hatutakiwi kuridhishwa na idadi hiyo kwani zamani wanyama hawa walikuwa wanapatikana kwa wingi nchi nyingi hapa Afrika lakini kwa sasa wanapatikana zaidi katika nchi nilizo orodhesha hapo juu huku nchini Kenya baadhi ya maeneo wamekuwa wakubahatisha kidogo. Nchi kama Burundi wanyama hawa wametoweka hata uzunguke vipi huwezi waona tena japo zamani walikuwepo nchini humo. Nchini Tunisia wanyama hawa wameanza kutoweka baadhi ya maeneo na hali ikiendelea kama ilivo sasa kuna hatari ya kutoweka nchi nzima.
CHANGAMOTO NA MAADUI KWA TAYA
Katika kipengele hiki huwa napenda sana kukizungumzia kwa namna mbili tofauti ili tuweze kupata mwanga na hatari itokanayo na changamoto na maadui kwa wanyama hawa iko upande gani. Hapa huwa tunaangalia matishio asilia na yale yatokanayo na shughuli za kibinaadamu.
Nikianza na maadui asilia, maadui wakuu wa taya katika mazingira yao asilia ni simba, chui, duma, fisi, mbweha na mamba. Maadui hawa kwa taya ni lazima wawepo ili kuweka usawa wa kiikolojia katika mazingira husika kwani wanyama wanaishi kwa kutegemeana. Ni lazima idadi ya taya iwe sawa au iendane na ukubwa wa mazingura husika wanayoishi hivyo ni lazima waliwe na wanyama wengine.
Sasa nikirudi kwa upande wa shughuli za kibinaadamu hapa ndo kwenye tatizo kubwa sana ambalo linahitaji umakini wa hali ya juu ili kukabiliana na upungufu wa wanyama hawa. Matatizo au changamoto asababishazo mwanadamu kwa wanyama hawa ni kama ifuatavyo;
1.Ujangili unaokithiri, wanyama hawa wanakumbwa na tatizo la ujangili kama walivo swala wengine. Hali hii inapelekea idadi yao kupungua sana kwani biashara haramu ya wanyamapori na malighafi zao imeshamiri kwa kasi sana hasa hapa nchini kwetu Tanzania. Tusipokuwa makini nasisi tutawapoteza wanyama hawa kama wenzetu Burundi. Mfano mzuri ni nchini Ivory Coast kati ya mwaka 1978 – 1998 taya walipungua kwa asilimia 92 (92%), hii ni hatari kubwa sana kwani kwa miaka 20 tu idadi kubwa ya taya ilitoweka nchini humo kutokana na tatizo la ujangili tu.
2.Shughuli za kilimo hasa karibu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori, watu wamekuwa wakivamia sana maeneo ya wanyamapori na kuanzisha shughuli za kilimo kitu ambacho kinapelekea sana uharibifu wa mazingira. Si uharibufu wa mazingira tu bali pia uharibifu wa mahitaji ya kiikolojia ya taya nakufanya wanyama hawa kuhama maeneo hayo kutokana na ukosefu wa chakula na mahitaji mengine ya kiikolojia. Lakini hali hii pia husababisha migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu kwa taya wanpokwenya kula mazao wakulima hulazimika kuwauwa kwa sumu au mishale na kusababisha kupungua kwa idadi ya wanyama hawa.
3.Ufugaji holela, jamii nyingi za wafugaji zimekuwa zikivamia maeneo ya hifadhi za wanyamapori nakuingiza mifugo katika maeneo hayo. Hii inasababisha uwepo wa changamoto na kugombea chakula baina ya mifugo na taya kitu ambacho husababisha taya kuhama katika mazingira yao. Lakini hali hii pia husababisha kuenea kwa magonjwa baina ya mifugo na wanyamapori hali ambayo ni hatari sana kwa upande wa wanyama wote kwa ujumla.
4.Uanzishaji wa makazi katika maeneo ya wanyamapori, mbali na shughuli za kilimo na ufugaji ipo pia changamoto kubwa ya watu kuvamia maeneo tengefu ya wanyamapori na kuanzisha makazi. Hali hii inapelekea kuziba kwa varanda za wanyamapori lakini pia huchochea kuongezeka kwa biashara haramu ya wanyamapori na ujangili kwa wayama hawa. Mfano mzuri ni eneo lijulikanalo kama kwakuchinja ambalo linunganisha hifadhi ya taifa ya Tarangire na hifadhi ya taifa ya Ziwa Manyara, varanda hii ilikuwa kubwa sana na wanyama walitegemea sana varanda hii kama mapitio yao. Lakini kwa sasa varanda hii imezibwa kabisa kutikana na uvamizi wa watu na kuanzishwa kwa makazi.
NINI KIFANYIKE KUWANUSURU TAYA HASA HAPA KWETU TANZANIA
Njia za kisasa za kupambana na majangili mfano matumizi ya kamera na GPS ili kugundua makazi ya majangili itasaidia sana kupunguza ujangili dhidi ya taya. Lakini pia kupambana na kutokomeza kabisa biashara haramu ya wanyamapori na malighafi zao kwani hii ndio sababu kubwa sana inayo pelekea kuongezeka kwa tatizo la ujangili hapa nchini.
Sheria za matumizi ya ardhi zifuatiliwe sana ili kutatua tatizo la uvamizi wa ardhi tengefu kwa ajili ya wanyamapori kwa shughuli za kilimo. Watu wamekuwa wakikaidi sana sheria za ardhi kitu ambacho kinaleta uhasama mkubwa sana kwa wakulima na mamlaka mbali mbali zinazo simamia uhifadhi wa wanyamapori.
Katika kuongezea hili, hapa kuna suala la siasa ambalo limekuwa kama mwiba wa sumu na kurudisha nyuma sana shughuli za uhifadhi. Wapo wanasiasa kwa tamaa tu za kupata kura kutoka kwa wananchi wamekuwa wakitetea suala la watu kulima maeneo mbalimbali hata yale ambayo yametengwa kwa shughuli maalumu mfano uhifadhi wa wanyamapori. Hali hii inasababisha shughuli za uhifadhi kuwa ngumu kwani mkono wa siasa ukishaingia katika uhifadhi huwa ni vigumu sana kuleta maendeleo chanya.
Suala la uingizaji wa mifugo katika maeneo ya wanyamapori litafutiwe ufumbuzi wa haraka zaidi kwani linazidi kukuza uhasama kati ya mamlaka za wanyamapori na wafugaji hasa pale mifugo inapokamatwa. Huwa siachi kulisema hili kwani kuna maeneo mengi sana hapa nchini ambayo yanafaa kwa shughuli za ufugaji, hivyo serikali iwatengee wafugaji ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima baina ya mamlaka za wanyamapori na wafugaji.
Wizara ya ardhi na makazi kupitia sera yake ya mipango miji na makazi ihakikishe inatatua suala la uvamizi wa watu katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Jitihada zinafanyika sana kweli tunaona lakini bado hazijagusa katika maeneo haya kwani yana migogoro mikubwa sana ambayo ipo siku itazua tafrani kubwa sana hapa nchini. Hivyo waziri mwenye dhamana husika ajitahidi kuitatua migogoro hii kwani wanyama hawa wanakuwa wanakosa maeneo ya kutawanyikia hasa kutokana na maeneo yao kumegwa kidogo kidogo kutokana na uanzishwaji wa makazi holela.
Jamii zishirikishwe katika masuala mazima ya uhifadhi wa wanyamapori kwa kuelezewa faida zitokanazo na uhifadhi wa wanyamahawa kwa ngazi ya pato la taifa na pia kwa ngazi ya hifadhi za jamii. Tukiweza kuishirikisha jamii kwa ufasaha basi wanajamii watakuwa mabalozi wakubwa katika kuwafichua majangili. Ni wazi kwamba majangilai tunaishinao kwenye jamii zetu, lakini kutokana na muamko na ushirikishwaji hafifu wa jamii katika suala la uhifadhi inakuwa ni ngumu kwa wanajamii kufichua makazi ya ajangili kwani nao wanapata kidogo kitu kutoka kwa majangili hawa.
HITIMISHO
Uhifadhi wa wanyamapori ni jukumu la kila mtanzania na si mamlaka husika pekee. Kupungua kwa idadi ya taya kutapelekea athari kubwa sana hasa katika suala la utalii kwani utalii unaingiza kiasi kikubwa cha mapato hapa nchini. Wapo wageni wanatoka nje ya nchi ili kuja kuwaona taya tu na wengine huja kwa ajili ya shughuli za utafiti kwa wanyama hawa. Mbali na taya tu hata kwa wanyama wengine pia tunahitaji nguvu moja ili kunusuru wanyama hawa.
Napenda kuzipongeza mamlaka mbali mbali zinazosimamia uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini kama TANAPA hasa kwa jitihada kubwa sana wanazo fanya kuhakikisha wanyama hawa wanaendelea kuwepo. Ukweli kupitia televisheni ya taifa TBC watu wameanza kuwa na muamko mkubwa sana wa kutaka kujua nini kinaendelea katika hifadhi zetu lakini pia hamasa yakutaka kutembelea hifadhi mbalimbali kitu ambacho kitasaidia sana kukuza utalii wa ndani. Bila kuwasahau mamlakaya hifadhi ya eneo la ngorongoro-NCAA na TAWA kwa kazi kubwa sana wanayoifanya kuwatunza wanyamapori hapa nchini inaleta hamasa pia kwa watu na kuzidi kupata moyo wa kushirikiana nanyi katika suala zima la uhifadhi.
Pongezi nyingine pia ziende kwa waziri wa maliasili na utalii Dr. Kingwangalla kwa kazi kubwa sana anayoifanya kwani jitihada zake zinaonekana. Nasi kama wazalendo wenye uchungu na maliasili zetu hatuna budi kuzisaidia mamlaka mbalimbali ili kuhakikisha tunaendelea kuwa na wanyamapori wetu wakiwa katika hali nzuri.
MWISHO…
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamaopi, maswali na ushauri kuhusu makala hizi usisite kuwasiliana na mwandishi wa Makala hii kupitia.
Sadick Omary
Simu: 0714116963/0765057969/0785813286
Email: swideeq.so@gmail.com
Instagram: @sadicqlegendary
……” I’m The Metallic Legend” ….