1.Historia ya jumla
Kenya ni nchi yenye eneo kubwa la ardhi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 582, 646 ikiwa na utajiri mkubwa wa bioanuwai kuanzia katika pwani yote ya Kenya hadi katika kilele cha mlima Kenya ambao ni mlima wa pili kwa urefu barani Afrika. Kenya ni moja ya nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki zinazokua kwa kasi kiuchumi na pia ni nchi yenye ukuaji mkubwa wa idadi ya watu, ikiwa inakadiriwa kuwa watu milioni 43 hii ni kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2015. Ukuaji wa teknolojia za mawasiliano, miundombinu ikiwa na wafanyakazi wengi wenye elimu.
Kuligana na taarifa za benki ya dunia za mwaka 2014, Kenya ni nchi ya 9 kwa ukuaji mkubwa na ya 5 kwa nchi zilizo na ukuaji mkubwa wa uchumi kwa nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara. Inakadiriwa kuwa na mapato ya dola za Kimarekani bilioni 55. Kilimo ndio kinaongoza kwa kuingiza mapato makubwa zaidi ya asilimia 27, kilimo cha chai, kahawa, na kilimo cha maua. Sekta ya maliasili na utalii ndio inashika nafasi ya pili kwa mapato kwa nchi ya Kenya zaidi ya asilimia 12. Kwa kutambua hilo nchi ya Kenya katika malengo yake ya muda mrefu kabla ya kufikia mwaka 2030, wameiweka sekta ya utalii kuwa moja ya sekta muhimu sita zinazotakiwa kuongezeka kwa kipato kwa asilimia 10 kila mwaka.
Nchi ya Kenya ni sehemu muhimu sana duniani kwa uhifadhi wa wanyamapori adimu sana. Uoto wa asili na mfumo mzuuri wa ikolojia unaojumuisha mahitaji yote muhimu ya viumbe hai kama vile wanyamapori na mimiea vinapatikana katika nchi ya Kenya, makazi ya wanyamapori yamehifadhiwa kuanzia maeneo yote muhimu ya bahari, maziwa, mito na hata sehemu muhimu za milima. Uwepo wa bonde la ufa kuanzia Kaskazini hadi Kusini mwa Kenya kumechangia sana uwepo wa uoto na makazi asilia ya wanyamapori.
Nchi ya Kenya inajivunia uwepo wa idadi kubwa ya nyumbu wanaohama ambao wamekuwa kivutio kikubwa sana hapa duniani, uwepo wa makundi makubwa ya tembo, bila kusahau uwepo wa faru, wanyamapori ambao wapo katika hatari kubwa ya kutoweka. Uwepo wa wanyamapori wengine wanaokula nyama, kama vila simba, chui, duma na mbwa mwitu kumechangia sana kuifanya nchi ya Kenya kujulikana kimataifa na kuwa sehemu yenye mvuto wa kipekee katika nchi za Afrika mashariki.
Kipindi kabla ya ukoloni, maliasili za wanyamapori zilihifadhiwa na kusimamiwa kwa mfumo wa asili wa kitamaduni na imani walizokuwa nazo kwanya maliasili. Lakini mambo hayakuendelea kuwa hivyo baada ya kuingia kwa ukoloni na kuigawa bara la Afrika, ilisababisha kuanza kwa mahitaji ya meno ya tembo na pembe za faru kushika hatamu katika nchi nyingi za Afrika. Hata baada ya kupata uhuru bado kulikuwa na uhitaji wa nyara hizi za wanyamapori kutoka katika nchi ya Kenya kwenda katika nchi za mashariki ya mbali, jambo ambalo lilisababisha hali mbaya sana kwenye hifadhi za wanyamapori hawa hasa tembo ambao idadi yao iliporomoka sana.
Ndipo ilipohitajika juhudi za kimataifa kufunga na kudhibiti biashara ya meno ya tembo mwaka 1989. Licha ya sheria kali za kusimamisha biashara hiyo, bado tunashuhudia hali ya mambo ikizidi kuwa mbaya kutokana nan chi za Asia kuendelea kuhitaji meno ya tembo na pembe za faru, jambo ambalo linachochea sana ujangili katika nchi ya Kenya.
Methodology (Njia za kupata taarifa zilizotumika kuandaa ripoti hii)
Maandalizi ya ripoti hii tunayoichambua leo, ni matokeo ya juhudi kubwa sana za wadau mbali mbali ambao walihusika kwa namna moja ama nyingine. Mwandishi wa ripoti hii anaeleza vyanzo vya taarifa alizoweka katika ripoti hii muhimu, baada ya kufanya utafiti wa kina na kupata maoni ya wadau mbali mbali kama vile viongozi wa serikali, mashirika binafsi. Na pia kupitia majarida na makala za kitaaluma, intaneti na pia kufika sehemu hifadhi ya jamii ili kuona na kupata maoni ya wanajamii kuhusu uhifadhi na changamoto zake.
Pia ripoti hii ina badhi ya mambo muhimu yaliyojadiliwa na wadau wa maliasili katika mkutano uliowakutanisha watalaamu wa masuala haya kutoka sehemu mbali mbali za nchi ya Kenya na sehemu nyingine duniani, sekta zote na idara za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori. Waliofanikisha kufanyika kwa mkutano huo ni shirika la TRAFFIC wakishirikiana na wadau wengine kama vile USAID na IUCN. Wote walikua na lengo la kufanya tathimini ya hali ya biashara haramu ya wanyamapori na nini kifanyike kuweka mambo sawa.
Hali ya kibaiolojia ya spishi kuu za wanyamapori ambazo zimeonekana katika biashara
Kwa mujibu wa ripoti hii, Kenya ina idadi ya wanyamapori na mimea 9152 amabayo imeandikwa au inayojulikana na kuandikwa kwenye vitabu kwa mujibu wa tafiti. Kati ya idadi hiyo 2148 ni wanyama. Kutokana na ongezeko la watu na makazi, kilimo na majanga ya asili imesababisha maeneo na makazi ya wanyamapori kuendelea kupngua kila siku. Idadi ya wanyamapori ambao wapo katika hatari ya kutoweka ni 325. Na idadi hiyo inaongezeka kila siku kutokana kukithiri kwa ujangili.
Asante sana kwa kusoma makala hii, nakukaribisha kwenye mfululizo mwingine wa makala ijayo ya uchambuzi wa ripoti hii iliyosheheni mambo mengi ya kujifunza na kufanyia kazi.
Mchambuzi wa ripoti hii ni;
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania