Siku zote changamoto zinapotokea katika maisha tunatakaiwa kuzielewa na baada ya kuzielewa ndio hatua za utatuzi wake zinaanza kufanyika, hatutakiwi kukimbia changamoto kwenye maisha, tunatakiwa kuzitatua na kuweka mipango na mikakati mipya ya changamoto hiyo kutojirudia tena. Hivi ndivyo walivyofanya wakenya ili kukabiliana na changamoto ya ujangili na biashara haramu za wanyamapori.
Ripoti niliyoichambua ina mambo mengi sana ambayo nikiyaandika kwenye makala moja pekee makala hiyo itakuwa kubwa sana, hivyo nimeamua kuweka vipengele baada ya kipengele ili tunapovisoma viwe na mtiririko na kuleta maana na uelewa kwa msomaji. Ripoti hii tunayoichambua ilitoka Mei mwaka 2016 na mwandishi wake ni Sam Weru. Ripoti hii iliyotolewa na shirika la TRAFFIC ina kichwa cha habari “WILDLIFE PROTECTION AND TRAFFICKING ASSESSMENT IN KENYA”.
Baada ya tathimini na utafiti wa mwenendo wa ujangili na biashara haramu ya wanyamapori. Ripoti hii kupitia maoni ya wadau mbali mbali wa wanyamapori na mazingira walipendekeza hatua na vipaumbele vya kuchukua ili kunusuru wanyamapori katika nchi ya Kenya. Yafuatayo ni mapendekezo na vipaumbele vya utekelezaji vilivyopendekezwa, hivyo msomaji karibu tujifunze pamoja.
Hatua za kuchukua kwa hali ya kibailojia ya spishi kuu za wanyamapori ambao wanahusika sana katika biashara.
- Kutambua meneo kijografia na kufanya utafiti ili kutoa taarifa muhimu kwa wakati kuhusu hali ya kibiolojia ya spishi za wanyamapori muhimu, mkazo ukizingatiwa kwa tembo, kakakuona na paka wakubwa (big cats).
- Kumalizia utafiti na tathmini ya biashara ya nyama pori nchini Kenya
- Kuendeleza na kuinua programu ya kitaifa ya utambuzi, uchunguzi na utatafiti waspishi za wanyamapori.
- Kutekeleza mapendekezo yote muhimu yaliyopo kwenye ripoti ya “Mapping Corridors and Conectivity for Conservation Task Force” kwa kufokasi kwenye ekosistimu (ecosystem) ya Mara.
- Kufanya utafiti wa kitafa kuhusu matumizi ya ardhi na kuweka mkazo wa kuelewa kilicho nyuma ya kuendelea kupungua kwa maeneo ya uhifadhi.
Kw upande wa utekelezaji wa sheria na usimamizi wake, mapendekezo kadhaa yalitolewa ambayo ni;
- Kufanya uchunguzi na tathimini ili kutoa data au aarifa zinazokosekana kwenye ujangili biashara haramu ya wanyamapori kama vile tembo, kakakuona, paka wakubwa, reptilia, ndege na spishi za majini.
- Kuanzisha maabara ya kitafiti katika jiji la Nairobi kwa huduma za wanyamapori za Kenya na kuhusisha taasisi nyingine za kimataifa katika utafiti wa wanyamapori.
- Kushirikishana kwa mapana kuhusu masuala ya kitalaamu na ushahidi wa kidigitali na kutoa taarifa za mara kwa mara endapo kuna mabadiliko yametokea kwa siku za karibuni, ili kuwasaidia wachunguzi, majaji na waendesha mashtaka.
- Kuimarisha uwezo wa kufanya tafiti za kichunguzi kwenye masuala ya uhalifu wa wanyamapori na kuwasaidia wasimamizi wa sheria kupitia mafunzo na tathimini, na mambo mengine ya kitalaamu yanayoendana na sheria za usimamizi wa wanyamapori
- Kuendeleza taasisi ya huduma za wanyamapori ya Kenya kwa kuwa na mkakati wa kupambana na rushwa na kukabiliana na tatizo la sasa katika usimamizi na ulinzi wa maliasili na kuboresha.
- Kutengeneza mfumo salama wa kiintelijensia wa kukusanya na kupeana taarifa kwa wadau wote wa uhifadhi kuhusiana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.
- Kusaidia na kupanua wigo kwa taasisi ya huduma za wanyamapori ya Kenya, KWC, na kuwapa uwzo mkubwa wa kuendesha mashtaka na mambo mengine ya kisheria, na pia hata watafiti wanatakiwa kufahamu na kujua na kujengewa uwezo huo wa kisheria.
- Kukuza na kuwezesha matumizi ya teknolojia kwenye masuala ya usimamizi wa wanyamapori na usimamizi wa sheria.
- Kufafanua na kutekeleza taratibu za kimashirikiano na mahusiano katika masuala yanayovuka mipaka katika ukanda, na kidunia ili kwa pamoja kushirikiana katika vita dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori.
- Kuendelea kuwajengea uwezo mamlaka za bandari na mamlaka za mipakani na viwanja vya ndege kuhusiana na uwezo wa kubaini uhalifu. Hasa kupitia utaratibu wote wa kusafirisha vitu nje ya nchi na kusafirisha vitu kuleta ndani ya nchi, kuangalia maeneo yote ya mipakani na kuzipa nguvu sehemu zote zenye udhaifu ili kuwakamata watu wote wanaojihusisha katika biashara hizi haramu na kuwafungulia mashtaka, bila kuwasahau watu wa kati ambao ndio wanaofanikisha uhalifu huo.
- Kutengeneza mfumo wa kuwasajili wakosaji wote wa masuala ya wanyamapori na kuwashirikisha wadau na mawakala wengine waliopo katika nchi na kanda mbali mbali.
- Kufanya kazi na makampuni binafsi ya fedha, mawasiliano na usafirishaji ili kujua hali ya mambo ilivyo.
- Sheria ya uhifadhi na usimamzi wa wanyamapori ya Kenya inafanya kazi pia kwa wanyamapori waishio majini, lakini taarifa za kitafiti kwenye eneo hili ni kidogo sana. Hivyo basi ni wakati wa mamlaka zinazofanya kazi kwenye maeneo haya ya majini kupata msaada na nguvu za kutafiti.
Katika eneo la kuwapa watu elimu na ufahamu kwa jamii, mapendekezo na hatua za kufanyia kazi zilipendekezwa zifuatazo;
- Kumalizia taratibu za kusimamia kutoa motisha kwa wamiliki binafsi wa ardhi na jamii ili waanzishe hifadhi, ushoroba (corridor) na maeneo ya mtawanyiko kwa ajili ya kuwa na ardhi ya kutosha kwa wanyamapori.
- Kumalizia na kutoa kanuni zitakazosimamia ufanyaji kazi kwenye hifadhi za wanyamapori.
- Kuendeleza na kutekeleza mipango ya usimamizi wa hifadhi kwa kushirikiana na jamii kama ilivyoainishwa kwenye sheria kuu ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori ya Kenya.
- Kuendeleza maadili ya taifa katika uhifadhi kupitia kampeni za kielimu na ufahamu ili kulinda asili na uchumi wa wanyamapori na kupunguza migogoro ya watu na wanyamapori.
- Kufundisha na kuajiri maaskari wa wanyamapori kutoka katika jamii ili kusimia utekelezaji wa sheria za uhifadhi kulingana na mahitaji ya tathimini iliyofanywa na mtalaamu wa kujitegemea.
- Kuendeleza na kutekeleza kanuni za kugawana manufaa au faida kwa utaratibu ulioanzishwa na sheria ya usimamizi na uhifadhi wa wayamapori ya Kenya.
- Kuboresha uelewa na ufahamu wa jamii kuhusu sheria zilizopo, kwa kuweka mkazo kwenye sheria ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na sheria ya usimamizi wa mazingira na uratibu.
- Kuimarisha uwezo kwa vyama vya uhifadhi wa wanyamapori vya Kenya na vyama vya uhifadhi wanaymapori vya kikanda kama chombo muhimu cha usafiri kufikia mikakati ya ushiriki wa serikali, wahisani na wawekezaji.
- Kuvijengea uwezo vyama vya usimamizi wa wanyamapori vya Kenya, ili viwe na viwango vizuri vya uongozi na ufanyaji kazi.
- Kubadilishana uzoefu kwa kutembeleana baina yao kwenye vyama hivi vya uhifadhi wa wanyamapori.
Pia ripoti hii katika mapendekezo yake imegusia hatua za kuchukua kwenye masula mtambuka yanayogusa uhifadhi wa wanyamapori kama ifuatavyo;
- Kutumia na kuimarisha muungano wa uhifadhi Kenya (Kenya Consrvation Allience, KCA) kama chombo muhimu cha kimkakati kushirikiana na serikali, kupeana taarifa na data, uratibu na utatuzi wa migogoro au mizozo.
- Kuoanisha mipango ya matumizi bora ya ardhi na maendeleo sawa na sheria ya usimamizi wa mazingira na sheria nyingine zinazohusika.
- Kutathimini thamani ya kiuchumi ya spishi kuu ambazo zimeathiriwa na biashara ili kusaidia uhifadhi, utekelezaji na hatua nyingine muhimu za mchakato wa kisheria.
Asante kwa kusoma mapendekezo haya yaliyoainishwa kwenye ripoti ya utafiti na tathimini ya ujangili na biashara haramu za wanyamapori. Karibu tuendelee kujifunza pamoja mambo haya kila siku.
Mchambuzi wa ripoti hii ni;
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania