Vichocheo na mwenendo wa usafirishaji haramu wa wanyamapori nje ya nchi katika nchi ya Kenya na nafasi yake kama kiini cha kusafirisha biashara haramu ya spishi za wawanyama na mimea mwitu katika Afrika mashariki. (Drivers and trends of transnational wildlife crime in Kenya and its role as a transit point for trafficked species in East Africa).

TRAFFIC ni shirika lisilo la kiserikali ambalo limejitoa kufanya kazi kubwa sana kuhakikisha kunakuwa na udhibiti na usimamizi mzuri unaozingatia weledi katika biashara za wanyamapori. Ripoti tunayoichambua leo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na watalaamu na watu wenye weledi kwenye masuala mbali mbali yanayogusa wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Ripoti hii iliyotoka Mei 2016 imeandikwa na Sam Weru, imesheheni mambo mengi mazuri sana ambayo ni msaada kwa uhifadhi wa maliasili zetu.

Ingawa ripoti hii inaielezea sana nchi ya Kenya kwenye masuala mengi sana ya ujangili na njia za kusafirisha bidhaa na nyara za wanyamapori nchi za nje. Ni muhimu sana sisi tulio majirani tukafahamu yanayoendelea kwa wenzetu ambao tunashirikiana mambo mengi linapokuja suala la uhifadhi wa mazingira na wanyamapori. Hivyo basi leo tutachambua vipengele vifuatavyo katika ripoti hii, karibu twende pamoja tujifunze mambo haya muhimu.

1.Historia fupi ya uhifadhi wa wanyamapori na hapa tutagusia mambo yote muhimu kuhusu hali halisi nchini Kenya ili itupe mwanga tumetoka wapi na tunaelekea wapi, hivyo ni kipengele muhimu sana kukisoma.

2.Tembo, hapa tutaenda moja kwa moja kujifunza kuhusu historia ya tembo tangu kipindi cha ukoloni hadi sasa, hapa ndio tutajua baadhi ya takwimu muhimu za wanyama hawa kwa nchi ya Kenya.

3.Faru, tutajua mambo ya msingi sana kuhusu wanyama hawa katika nchi ya Kenya, lakini pia mwandishi atatupa historia ya wanyama hawa ilivyokuwa hapa barani Afrika, pia tutajua nafasi ya nchi ya Kenya kwenye uhifadhi wa wanyama hawa muhimu sana hapa duniani.

4.Kakakuona wa Afrika, ukweli kuhusu wanyama hawa wa ajabu na jinsi wanavyopukutika kutokana na sababu kadha wa kadha, tutaona hali halisi ya wanyama hawa kwa nchi ya Kenya.

5.Ujangili na biashara haramu katika nchi ya Kenya, hapa tutaona kwanini nchi ya Kenya inanyooshewa kidole na jumuiya ya kimataifa pamoja na mashirika mengine kuhusu ujangili na biashara haramu.

6.Ujangili, mwelekeo na vitu vinavyopelekea kushamiri kwa biashara haramu, hapa tutajifunza kujua kwa undani kuhusu mambo yanavyokwenda

7.Mwelekeo wa ujangili, ripoti hii imeonyesha yote yaliyo muhimu sana kwenye biashara hii na pia itataja hatima ya haya yote.

8.Vichocheo vikuuu, ujangili na kushamiri kwa ujangili, kwenye makala hii ya uchambuzi tutaona vyote hivyo na tutaelewa sababu inayowasukuma watu kuua wanyamapori hawa.

9.Muundo wa ujangili na mitandao ya biashara haramu. Tutaeleza kila kitu kuhusu mtandao wa ujangili sawa na mwandishi wa ripoti hii anavyoweka wazi mambo haya.

10.Njia kuu za biashara haramu na watumiaji wa kuu wa nyara hizi, tutaeleza na kwa pamoja tutajifunza na kujua njia wanazotumia majangili kufanikisha azma yao.

  1. Ukamataji na ufilisi, hapa inaeleza hatua muhimu zinazochukuliwa kwa wale waliokamatwa na nyara za serikali kinyume na sheria za uhifadhi na sheria za nchi.
  2. Mtandao uhalifu unavyofanya kazi kwa ushirikiano na baadhi ya makundi ya kigaidi, tutaona ushiriki wa vikundi vya kigaidi kwenye ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo na pembe za faru.

13.Sera ya wanyamapori na sheria ya mazingira ya Kenya, tutaanalia baadhi ya mambo ya kisheria na kisera kwenye makala hii. Na hapa tutagusia vitu mbali mbali vya kisheria, mahakama na majaji

14.Hitimisho na mapendekezo, hapa tutaona mikakati waliyoiweka na pia mapekezo ya kufanyia kazi ili kuwe na matokeo mazuri kwenye kazi kubwa wanayoifanya.

Hivi ndivyo tutakavyojifunza na kuichamubua ripoti hii muhimu sana kwa kupata maarifa na taarifa za kusaidia kuwa na uwanja mpana wa kufanya maamuzi muhimu kwenye kuboresha sekta ya maliasili na utalii hapa Tanzania. Hivyo nakukaribisha twende pamoja tukachambue moja baada ya jingine mambo muhimu ya uhifadhi wa wanyamapori na faida ambazo tuanatakiwa kuzipata kenye uhifadhi wa maliasili.

1.Historia ya jumla

Kenya ni nchi yenye eneo kubwa la ardhi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 582, 646 ikiwa na utajiri mkubwa wa bioanuwai kuanzia katika pwani yote ya Kenya hadi katika kilele cha mlima Kenya ambao ni mlima wa pili kwa urefu barani Afrika. Kenya ni moja ya nchi za jumuiya ya afrika mashariki zinazokuwa kwa kasi kiuchumi na pia ni nchi yenye ukuaji mkubwa wa idadi ya watu, inakadiriwa kuwa na watu milioni 43.

Ukuaji wa teknolojia za mawasiliano, miundombinu ikiwa na wafanyakazi wengi wenye elimu. Kuligana na taarifa za benki ya dunia Kenya ni nchi ya 9 kwa ukuaji mkubwa na ya 5 kwa nchi zilizo na ukuaji mkubwa wa uchumi kwa nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara. Inakadiriwa kuwa na mapato ya dola za kimarekani bilioni 55. Kilimo ndio kinaongoza kwa kuingiza mapato makubwa zaidi ya asilimia 27, kilimo cha chai, kahawa, na kilimo cha maua.

Sekta ya maliasili na utalii ndio inashika nafasi ya pili kwa mapato kwa nchi ya Kenya zaidi ya asilimia 21. Kwa kutambua hilo nchi ya Kenya katika malengo yake ya muda mrefu kabla ya kufikia mwaka 2030, wameiweka sekta ya utalii kuwa moja ya sekta muhimu sita zinazotakiwa kuongezeka kwa kipato kwa asilimia 10 kila mwaka.

Nchi ya Kenya ni sehemu muhimu sana duniani kwa uhifadhi wa wanyamapori adimu sana. Uoto wa asili na mfumo mzuri wa ikolojia unaojumuisha mahitaji yote muhimu ya viumbe hai kama vile wanyamapori na mimiea vinapatikana katika nchi ya Kenya, makazi ya wanyamapori yamehifadhiwa kuanzia maeneo yote muhimu ya bahari, maziwa, mito na hata sehemu muhimu za milima. Uwepo wa bonde la ufa kuanzia Kaskazini hadi Kusini mwa Kenya kumechangia sana uwepo wa uoto na makazi asilia ya wanyamapori.

Nchi ya Kenya inajivunia uwepo wa idadi kubwa ya nyumbu wanaohama ambao wamekuwa kivutio kikubwa sana hapa duniani, uwepo wa makundi makubwa ya tembo, bila kusahau uwepo wa faru, wanyamapori ambao wapo katika hatari kubwa ya kutoweka. Uwepo wa wanyamapori wengine wanaokula nyama, kama vila simba, chui, duma na mbwa mwitu kumechangia sana kuifanya nchi ya Kenya kujulikana kimataifa na kuwa sehemu yenye mvuto wa kipekee katika nchi za Afrika mashariki.

Kipindi kabla ya ukoloni, maliasili za wanyamapori zilihifadhiwa na kusimamiwa kwa mfumo wa asili wa kitamaduni na imani walizokuwa nazo kwanya maliasili. Lakini mambo hayakuendelea kuwa hivyo baada ya kuingia kwa ukoloni na kuigawa bara la Afrika, ilisababisha kuanza kwa mahitaji ya meno ya tembo na pembe za faru kushika hatamu katika nchi nyingi za Afrika.

Hata baada ya kupata uhuru bado kulikuwa na uhitaji wa nyara hizi za wanyamapori kutoka katika nchi ya Kenya kwenda katika nchi za mashariki ya mbali, jambo ambalo lilisababisha hali mbaya sana kwenye hifadhi za wanyamapori hawa hasa tembo ambao idadi yao iliporomoka sana. Ndipo ilipohitajika juhudi za kimataifa kufunga na kudhibiti biashara ya meno ya tembo mwaka 1989. Licha ya sheria kali za kusimamisha biashara hiyo, bado tunashuhudia hali ya mambo ikizidi kuwa mbaya kutokana na nchi za Asia kuendelea kuhitaji meno ya tembo na pembe za faru, jambo ambalo linachochea sana ujangili katika nchi ya Kenya.

Methodology (Njia za kupata taarifa zilizotumika kuandaa ripoti hii)

Maandalizi ya ripoti hii tunayoichambua leo, ni matokeo ya juhudi kubwa sana za wadau mbali mbali ambao walihusika kwa namna moja ama nyingine. Mwandishi wa ripoti hii anaeleza vyanzo vya taarifa alizoweka katika ripoti hii muhimu, baada ya kufanya utafiti wa kina na kupata maoni ya wadau mbali mbali kama vile viongozi wa serikali, mashirika binafsi na pia kupitia majarida na makala za kitaaluma, intaneti na pia kufika sehemu hifadhi ya jamii ili kuona na kupata maoni ya wanajamii kuhusu uhifadhi na changamoto zake.

Pia ripoti hii ina badhi ya mambo muhimu yaliyojadiliwa na wadau wa maliasili katika mkutano uliowakutanisha watalaamu wa masuala haya kutoka sehemu mbali mbali za nchi ya Kenya na sehemu nyingine duniani, sekta zote na idara za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori. Waliofanikisha kufanyika kwa mkutano huo ni shirika la TRAFFIC wakishirikiana na wadau wengine kama vile USAID na IUCN. Wote walikua na lengo la kufanya tathimini ya hali ya biashara haramu ya wanyamapori na nini kifanyike kuweka mambo sawa.

Hali ya kibaiolojia ya spishi kuu za wanyamapori ambazo zimeonekana katika biashara

Kwa mujibu wa ripoti hii, Kenya ina idadi ya wanyamapori na mimea 9152 amabayo imeandikwa au inayojulikana na kuandikwa kwenye vitabu kwa mujibu wa tafiti. Kati ya idadi hiyo 2148 ni wanyama. Kutokana na ongezeko la watu na makazi, kilimo na majanga ya asili imesababisha maeneo na makazi ya wanyamapori kuendelea kupngua kila siku. Idadi ya wanyamapori ambao wapo katika hatari ya kutoweka ni 325. Na idadi hiyo inaongezeka kila siku kutokana kukithiri kwa ujangili.

Tembo

Mpango wa 2011 – 2020 wa uhifadhi na usimamizi wa tembo nchini Kenya unasema kuwa idadi ya tembo imeporomoka sana kwa kipindi cha miaka 100 iliyopita sababu kubwa ikiwa ni biashara ya meno ya tembo. Idadi ya tembo imepungua sana kutoka makadirio ya tembo 167,000 mwaka 1973 hadi 20,000 mwaka 1990. Ingawa kunaweza kukawa na ugumu wa kulinganisha ubora wa taarifa za miongo iliyopita na taarifa zinazopatikana sasa. Lakini taarifa za hivi karibuni mwaka 2014 zinaonyesha kuwa idadi ya tembo katika nchi ya Kenya inakadiriwa kufikia 32,000 zikionyesha zilikuwa zinapungua kwa miaka mitatu iliyopita.

Aidha, kutokana na tathimini iliyofanywa na ripoti hii inaonyesha kuwa licha ya kwamba tembo ni wanyama ambao wametafitiwa sana nchini Kenya, lakini kumekuwa na ukosefu wa taarifa za kitafiti za zaidi ya miaka 8 maka 20 za tembo ambao wanaishi kwenye misitu. Taarifa zilizopo kwenye machapisho mengi ni taarifa za utafiti wa tembo wa savanna pekee. Hivyo kuna idadi kubwa ya taarifa ambazo zinahitajika ili kukadiria vizuri idadi ya tembo katika nchi ya Kenya.

Hata hivyo, ujangili, kubadilika kwa maeneo ya malisho ya tembo imekuwa ni moja kati ya sababu kuu za kuporomoka kwa idadi ya tembo nchini Kenya. Kwa miaka zaidi ya 25 taasisi inayoshughulika na huduma za wanyamapori Kenya (Kenya Wildlife Services, KWS) na watafiti wengine wa tembo wameandika kuwa kubadilika kwa maeneo ya tembo nchini Kenya ni kwasababu ya uuaji, kuharibika kwa makazi yao kutokana na ukame, na kupotea kwa maeneo mtawanyiko na njia za tembo ni kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya watu na mifugo.

Pia kuna sababu nyingine ziliyopelekea kupungua kwa idadi ya tembo, kama ilivyoainishwa kwene ripoti hii ni shughuli nyingi za kimaendeleo na kujipatia kipato kama vile upanuzi wa mashamba, ujenzi wa makazi ya binadamu, upanuzi wa miundombinu ya barabara, uchimbaji wa madini, ukataji wa misitu na miti ya asili, kuongezeka kwa idadi ya mifugo, kuharibika na kukauka kwa maeneo ya ardhioevu nk.

Faru

Miaka ya 1960, idadi ya faru katika bara la Afrika ilikadiriwa kuwa ni zaidi ya 100,000 lakini idadi hiyo haikuendlea kuongezeka kama ilivyotarajiwa bali ilipungua kwa kasi sana na kufikia idadi ndogo sana ya faru 2410 mwaka 1995. Sababu kubwa iliyopelekea kupungua kwa faru kiasi hiki ni biashara ya uwindaji wa wanyamapori hawa kushindwa kusimamiwa ipasavyo na kutoa mwanya kwa majangili kuanza uharibifu kwa wanyamapori hawa muhimu.

Baada ya utekelezaji wa maagizo ya CITES idadi ya faru weusi imeongezeka kidogo sana na kufikia faru 5081 mwaka 2013. Leo asilimia 96 ya faru weusi wanapatikana katika nchi nne pekee hapa barani Afrika, nchi hizo ni Afrika ya Kusini, Namibia, Kenya na Zimbabwe. Hii inaifanya Kenya kuwa nchi ya kipekee duniani kuwahifadhi wanyama hawa ambao wapo katika hatari kubwa ya kutoweka.

Historia ya faru nchini Kenya inamulika hali ya mambo ilivyo katika sehemu nyingine barani Afrika. Mwaka 1970 Kenya ilikuwa na idadi kubwa ya faru inayofikia 20,000 lakini idadi hiyo iliendelea kupungua zaidi kutokana na ujangili uliokithiri kati ya miaka ya 1970 na 1980.

Kutokana na hali hiyo mamlaka ya serikali ya Kenya kwa mara ya kwanza ilanzisha bustani ya kuwahifadhi wanyama hawa iliyoitwa Rhino Santuary, katika hifadhi ya taifa ya ziwa Nakuru mwaka 1987, bustani hiyo iliyoanzishwa ilikuwa chini ya uangalizi mkali sana wa serikali ya Kenya, juhudi hizo za serikali ya Kenya zilizaa matunda baada ya spishi ya faru weusi wa Mashariki kuongezeka kutoka 381 mwaka 1987 na kufikia faru 648 mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimia 70 kwa miaka 27.

Halikadhalika ongezeko la faru weupe walioingizwa nchini Kenya kutoka Afrika Kusini ambapo idadi yao imeongezeka kutoka faru 74 mwaka 1992 na kufikia faru 399 mwaka 2014. Kwa hali hiyo nchi ya Kenya kwa sasa inashika nafasi ya tatu duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya faru weusi na weupe ambao idadi yao ilifikia 1047 mwaka 2014. Faru nchini Kenya wanalindwa na kuhifadhiwa kwenye bustani (sanctuaries) 16 za serikali na za binafsi moja ipo katika ukanda wa ulinzi wa hali ya juu (Intensive Protection Zone) katika hifadhi ya taifa ya Tsavo na sehemu nyingine zinazohifadhi wanyama hawa ni maeneo ya mtawanyiko na maeneo ya asasi za kijamii au maeneo ya hifadhi ya jamii.

Mpango mkakati wa faru nchini Kenya wa mwaka 2012 – 2016 umekusudia ongezeko la asilimia 5 ya faru kwa mwaka, lakini hali halisi inaonyesha kukithiri kwa vitendo vya kijangili vinakwamisha kufikia malengo hayo. Kwa sasa kiwango cha ujangili wa faru nchini Kenya kimekuwa na kufikia asilimia 6 kwa mwaka. Kiwango hicho ni kikubwa sana na kimezidi kabisa kiwango cha faru wanachozaliwa, hiyo ndio changamoto kubwa sana inayoikabili nchi ya Kenya kwa sasa kwenye masula haya ya uhifadhi wa spishi za wanyama hawa.

Faru weupe wa Kaskazini (Northen white rhino) ni spishi ya faru ambayo inaaminika kutoweka kabisa katika mwitu, kutoweka kwa spishi ya faru huyu aliyekuwa amesalia katika hifadhi ya taifa ya Garamba katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo mwaka 2006. Kwa kuwa spishi nne za faru hawa zilihamishiwa nchini Kenya kwa ajili ya kuzaliana ili baadaye wawarudishe kwenye maeneo yao ya mwanzo, kwa bahati mbaya mpango wa kufanya hivyo haukufanikiwa kwasababu faru wote walikufa bila hata kuzaliana, chanzo cha kifo ni kutokana na sababu za kiasili.

Makazi na maeneo ya faru weusi na weupe yamepungua sana kwa kadri siku zinavyokwenda. Ripoti inaonyesha kulikuwepo wa faru kwenye maeneo ya nchi ya Kaskazini mwa Chadi na katika nchi ya Sudani. Hali halisi sivyo ilivyo sasa, meneo ya faru yamekuwa madogo sana na yapakatika nchi chache za Kusini na Mashariki mwa bara la Afrika.

Watumiaji wa mwisho wa meno ya tembo na pembe za faru Kusini mwa Asia na Mashariki ya Kati imebadilika kabisa kwa sasa. Kwenye miaka ya 1970 na 1990 nchi za Yemeni, Japani, Korea Kusini, Taiwani na China walikuwa ndio watumiaji wakuu na ndio waliokuwa na mahitaji makubwa ya pembe za faru.

Matumizi makubwa ya pembe za faru Kusini mwa Asia ilikuwa ni kwa ajili ya dawa za asili (dawa za kienyeji) wakati kwa nchi ya Yemeni walihitaji sana pembe za faru kwasababu ya kutengeneza hala za kuwekea au kubebea visu na majambia. Lakini katika miaka ya 2000 kumekuwa na mlipuko mkubwa zaidi wa uhitaji wa pembe za faru katika nchi ya Vietnam ambao wamekuwa wakitumia pembe za faru kama sehemu ya kuonyesha utajiri au heshima fulani kwenye jamii pamoja na matumizi ya dawa za asili.

Kabla sijamalizia kipengele hiki kuhusu faru nchini Kenya, nataka tuone mpango mkakati wa nchi ya Kenya katika kuhakikisha faru wanahifadhiwa kwa vizazi vjiavyo. Mpaka kufikia mwaka 2014 nchi ya Kenya ilikuwa na idadi ya faru 1047, na kwa mwaka huo faru waliouwawa kwa ujangili ilifikia faru 35.

Kuna malengo na mkakati wa uhifadhi na usimamizi wa faru weusi nchini Kenya wa mwaka 2012 – 2016 mkakati huo ulieleza dhamira na malengo makubwa waliyonayo kuhusu uhifadhi wa faru weusi kwa kusema kuhifadhi angalau faru weusi wapatao 750 kabla ya kufikia mwishoni mwa mwaka 2016, na kufikia kiwango cha ongezeko la asilimia 5 cha ukuaji, na kiasi chini ya asilimia 1 ya mauaji yanayosababishwa na binadamu na magojwa. Mpango huo ulilenga kuwa na maono ya kufikia faru 2000 kwenye hifadhi zao.

Na ili kufikia malengo na maono hayo, mikakati ifuatayo iliazimiwa;

  1. kupunguza uuaji haramu wa faru ili uwe chini ya asilimia 1 kwa mwaka na pia kupunguza kabisa biashara ya pembe za faru na nyara nyingine za faru.
  2. kuendelea kusimamia na kutoa taarifa za kitaalamu zitakazosaidia katika uhifadhi, idadi yao na katika kuweka programu za kiutekelezaji.
  3. kufikia na kuendeleza kiwango cha ukuaji wa asilimia 6 wa faru weusi katika bustani zilizoanzishwa kwa ajili ya uhifadhi wa faru na kiasi cha chini kiwe kukua kwa asilimia 5 ili kufikia malengo ya kuwa na faru weusi 750 kabla ya mwaka 2016.
  4. kuandaa maeneo salama kwa ajili ya kupanua maeneo ya uhifadhi wa ongezeko la faru.
  5. Kukuza ufahamu na uelewa kwa umma kuhusu faru ilikwa pamoja kupata ushirikiano kimataifa katika kuwahifadhi wanyama hawa.
  6. Kutengeneza mfumo na ushirikiano ili kujenga uwezo wa utekelezaji wa mikakati hiyo.

Ujangili na biashara haramu Kenya

Wanyamapori na mazingira yao asili ni uti wa mgongo wa sekta ya utalii nchini Kenya, na pamoja na ukweli huo bado nchi ya Kenya inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa rasilimali hizo kwa sababu mali mbali kama vile ujangili, biashara haramu ya wanyama na mimea mwitu. Wahifadhi na watalamu wa masuala haya ya wanyamapori wanakiri kuwa licha ya kuwa nchi ya Kenya imefunga kabisa biashara ya pembe za faru na meno ya tembo, bado uhalifu wa wanyamapori umekuwa ndio tishio kubwa linalopelekea kupungua na kupotea kwa wanyamapori tangu miaka ya 1970 hadi sasa.

Spishi nyingi za wanyamapori zinazohusishwa sana kwenye biashara hii haramu ni meno ya tembo husafirishwa yakiwa ghafi au yakiwa yameshatengenezwa husafirishwa hadi Asia, ngozi za wanyama pori wanaokula nyama jamii ya paka (cat family) kama vile simba, duma, chui husafirishwa kama viungo au wakiwa hai kwenda nchi za Ulaya, Mashariki ya kati, na Marekani. Reptilia kama vile mijusi, nyoka, vinyonga na kobe husafirishwa sana wakiwa hai, sumu zao au sehemu za viungo vyao kwenda nchi za Ulaya, Marekani na Mashariki ya Kati. Kakakuona nao ni wanyama wanaosafirishwa sana wakiwa hai au magamba yao kwenda nchi za Mashariki na Kusini mwa Asia. Magogo au miti ya (Sandalwood) husafirishwa kama magogo na kufikia nchi za Mashariki ya Asia. Mimea ya Alovera nayo piani miongoni mwa spishi zinazosafirishwa kwa njia haramu kwenda Ulaya na Asia.

Mwelekeo wa ujangili

Nchi ya Kenya ilifuta vibali vyote halali ya uwindaji binafsi mwaka 1973, lakini udhaifu bado ulibakia kwenye sheria ambayo iliwaruhusu viongozi wabadhirifu wa serikali kuuza kwa mnada meno ya tembo yaliyokuwa kwenye chumba huko Mombasa, jambo ambalo lilitoa mwanya kwa biashara haramu ya meno ya tembo kushika hatamu. Kenya ilitangaza kufunga kabisa biashara ya meno ya tembo kutokana na mahitaji ya biashara hiyo kuwa makubwa katika nchi za Asia na Japani. Miaka ya 1970 na 1988 baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini walishutumiwa kwa kuuza meno ya tembo.

Nchi ya Kenya iliunda tena uongozi wake uliokuwa unasimamia masuala ya uhifadhi wa wanyamapori mnamo mwaka 1989 na kusababisha kuundwa kwa shirika la kiserikali la huduma za wanyamapori lililojulikana kama Kenya Wildlife Servce (KWS) ambapo pamoja na mambo mengine liliwajibika katika kusimamia na kuangalia kwa karibu wanyamapori, shirika hili kwa mara ya kwanza liliongozwa na mkurugenzi ambaye alikuwa ni mtafiti wa mambo ya kale na pia alikuwa ni muhifadhi wa wanyamapori Richard Leakey.

Chini ya uongozi wa Leakey waliamua kuunda kikosi cha migambo ambao watakuwa na jukumu la ulinzi wa wanyamapori, haikuishia hapo baada tu ya kuunda kikosi hicho cha mgambo kilianza kampeni ya kupinga ujangili iliyopelekea nchi ya Kenya kuchoma shehena yake yote ya meno ya tembo iliyokuwa stoo, yenye thamani ya dola za kimarekani million 3. Kwa kufanya hiyo nchi ya Kenya ilipeleka ujumbe kwa dunia kuwa hawako tayari kuvumilia vitendo vya kijangili dhidi ya wanyamapori. Kampeni hiyo ilikuwa na matunda mazuri kwa sababu iliamsha uelewa kwa ngazi zote serikalini na kwa jamii ili kupambana na ujangili.

Kwa kadri dunia inavyoendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwenye mambo mbali mbali hasa kwenye karne ya 21, njia nyingi za kufanya ujangili ziliingia na kuanza kuzamisha juhudi zote zilizopatikana katika kipindi cha nyuma, kutokana na hali ya watu kuwa masikini, kiwango cha juu cha rushwa na udhaifu uliokuwepo kwenye sheria za wanyamapori halikadhalika mahitaji ya meno ya tembo katika masoko ya nchi za Vietnam na China yalikuwa makubwa sana hivyo mambo hayo yalifungua milango kwa majangili kushamiri sana katika nchi ya Kenya.

Kwa ujumla wake hivi ndio vitu vinavyopelekea ujangili wa meno ya tembo na pembe za faru katika nchi ya Kenya.

  1. Rushwa kwa baadhi ya viongozi wa serikali na wale wa sekta binafsi hasa maeneo ya usafirishaji;
  2. Kuongezeka kwa bei ya meno ya tembo na pembe za faru kwenye masoko haramu inayochochewa na mahitaji kutoka nchi za Mashariki ya Asia.
  3. Kupitisha silaha isivyo halali katika maeneo ya mipaka ya nchi ya Kenya na pia kukosekana kwa amani eneo la Kaskazini mwa Kenya;
  4. Urahisi wa usafirishaji wa nyara za wanyamapori na pia urahisi wa majangili kutembea kokote wanakotaka katika mipaka ya Kenya ambayo haina usimamizi makini;
  5. Kupanuka kwa makazi ya watu kwenye maeneo muhimu ya faru na tembo; na
  6. Udhaifu ulipo kwenye sheria za wanyamapori, hasa mtuhumiwa anapokamatwa na nyara.

Kama ripoti hii inavyoonyesha kuwa rushwa kwa viongozi wa serikali na wale wa sekta binafsi ndio kichocheo kikuu cha ujangili na kushamiri kwa biashara haramu ya pembe za faru na meno ya tembo. Jambo hili pia limeonyeshwa kwenye ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu madawa ya kulevya na uhalifu. Kazi kubwa inahitajika sana ili kupambana na hali hii inayomaliza wanyamapori hawa wenye thamani kubwa kwenye mfum wa maisha na ikolojia nzima ya viumbe hai.

Mfumo wa ujangili na mitandao ya biashara haramu

Mfumo mzima wa ujangili katika nchi ya Kenya unahusisha watu wa aina mbali mbali kuanzia watu wa chini kabisa wanaoishi karibu na maeneo yenye hifadhi za wanyamapori, maaskari wanyamapori, mtu wa katikati wasafirishaji na pia kiongozi mkuu anayeagiza meno ya tembo au pembe za faru. Kutokana na kuwa na mtandao makini na wenye akili huwa wanafanya kazi zao kwa weledi sana huku wakiwatumia viongozi wa serikali na viongozi wa maaskari kwa kuwapa rushwa ili waonyeshe maeneo yenye tembo, lakini pia waonyeshe maeneo ambayo askari wa wanyamapori hawapo ili kufanya ujangili huo. Kwa nchi ya Kenya ujangili wa wanyama hawa hufanywa pia na watu kutoka nchi jirani za Tanzania au Uganda hivyo kusafirisha hadi Kenya.

Pia ujangili kwa nchi ya Kenya umekithiri kutokana na urahisi wa kupata silaha kali kama vile G-3, AK -47, rifles na nyingine nyingi ambazo zimesadia sana katika ujangili wa wanyamapori. Silaha hizo huingia nchini Kenya kwa njia haramu kutoka katika nchi za Ethiopia, Sudani Kusini, Somalia na Uganda ambapo migogoro ya kutumia silaha inatumika sana na kuzoeleka kwa muda mrefu.

Njia kuu za biashara hii haramu na maeneo sehemu za watumiaji wakuu

Kenya imekuwa ni sehemu kuu ya kusafirishia bidhaa haramu kutokana na maendeleo yake kwenye sekta ya usafirishaji. Kuna bandari, viwanja vikubwa vya ndege na pia teknolojia yake inakua kwa kasi sana, hivyo ni sehemu nyeti sana kwa usafirishaji katika bara la Afrika na Afrika mashariki.

Lakini bidhaa, nyara ambazo husafirishwa kwenda kwa watumiaji wakuu huwa zina sehemu zinatoka, sehemu hizo ni kama ifuatavyo;

  1. Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa husafirisha meno ya tembo;
  2. Msumbiji ambayo husafirisha zaidi meno ya tembo na pembe za faru;
  3. Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ambayo kwa kiasi kikubwa husafirisha meno ya tembo;
  4. Kutoka katika mapori ya kawaida kiasi kikubwa husafirisha meno ya tembo, pembe za faru, ngozi za paka wakubwa, na magamba ya kakakuona;
  5. Uganda ambao kwa kiasi kikubwa husafirisha meno ya tembo, magamba ya kakakuona, na mbao;
  6. Zambia husafirisha zaidi meno ya tembo;
  7. Sudani Kusini nao husafirisha zaidi meno ya tembo.

Bandari ya Kilindini iliyopo Mombasa na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata International Airport, uwanja wa taifa wa ndege wa Kenya uliopo Nairobi, vimekuwa vikitambulikana kama sehemu inayoongoza kwa usafirishaji haramu wa nyara za wanyamapori kwenda sehemu nyingine duniani.

Taarifa zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2009 kiasi kikubwa cha meno ya tembo kimesafirishwa kupitia bandari ya Mombasa kuliko njia nyingine yoyote katika bara la Afrika zikiwa zinaelekea katika nchi za China na Vietnam. Uwanja wa ndege wa taifa wa Kenya na shirika la usafiri wa anga la Kenya limekuwa likifanya safari za moja kwa moja kutoka Nairobi Kenya kwenda Mashariki mwa Asia zikiwa zimebeba abiria wenye nyara za wanyamapori kwenye mizigo yao.

Kwa mujibu wa shirika la huduma za wanyamapori Kenya, sehemu nyingine inayoongoza kwa usafirishaji wa nyara za wanyamapori ni kupitia kwenye mipaka ya (border) Busia na Malaba zote zimekuwa zikitumika kupitisha meno ya tembo kutoka DRC, Sudani Kusini na Uganda kwenda Kenya na baadaye hupelekwa katika bandari ya Kilindini iliyopo Mombasa. Pia kwa nchi za Ethipia, Somalia na Tanzania hutumia mpaka au boda ya Namanga, Tarakea, Tsavo Lunga Lunga, Liboi na Moyale.

Ukamataji na utaifishaji

Kwa kuwa sehemu za usafirishaji wa nyara za wanyamapori ni bandari ya Mombasa na sehemu nyingine za viwanja vya ndege, mamlaka ya usimamizi nchini Kenya zinakiri kuwa katika bandari ya Mombasa ndio muhusika mkuu wa kusafirisha meno ya tembo na nyara nyingine kutoka nchi jirani kama Tanzani na Ruwanda. Mamlaka za bandari zinakiri kukamata kiasi kikubwa sana cha meno ya tembo katika bandari hiyo chenye thamani ya dola za Kimarekani million 1.5 ikiwa ni kiasi kikubwa sana kuwahi kukamatwa na mamlaka hizo tangu mwaka 2009. Kiasi hicho cha meno ya tembo kilichokamatwa kilikuwa kinatoka nchi za Tanzania na Rwanda na zilikuwa tayari kusafirishwa kwenda Indonesia kama mapambo na majani ya chai.

Mwezi Aprili mwaka 2015 jumla ya meno ya tembo 511 yalifichwa pamoja na majani ya chai yaliyokuwa na uzani wa tani 11 yanakadiriwa kuwa na uzito usiopungua tani 3, na thamani yake ni kama dola za kimarekani million 6, shehena hiyo ilikuwa tayari kusafirishwa kwenda Thailand. Hii inaonyesha kabisa Mombasa ilivyo kitovu kikuu cha biashara haramu za wanyamapori katika bara la Afrika.

Ukamataji uliendelea kufanyika katika mipaka ya maeneo ya hifadhi na ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori, pia ripoti inaonyesha wahusika wa ujangili kukamatwa maeneo ya sokoni, mijini wakiwa katika harakati za kusafirisha meno ya tembo. Miaka ya 2010 na 2014 ukamataji na utaifishaji wa meno ya tembo na pembe za faru ulifikia kilele cha tani zaidi ya 18 zikiwa na uzani wa kg 42 za pembe za faru na ndio mwaka huo ambao ukamataji wa majangili hao ulikuwa mkubwa sana kufikia watuhumiwa 318.

Pia kwa mujibu wa ripoti hii inaonyesha kuwa taarifa za hivi karibuni kuhusiana na ukamataji wa viungo au sehemu za wanyamapori wanaokula nyama jamii ya paka wakubwa imeshuka hii inaweza kuwa ni kutokana na sababu zifuatazo

  1. juhudi za sasa za mamlaka za kisheria kuendeleza ukamataji wa meno ya tembo na pembe za faru kwenye kipindi hiki chenye changamoto nyingi;
  2. kuongezeka kwa vitendo vingi sana vya biashara haramu ya paka hawa wakubwa hivyo kuepuka kugundulika;
  3. kushuka kwa idadi ya wanyama wanaokula nyama;
  4. kupungua kwa biashara haramu ya wanyama hawa.

Utafiti wa kina unahitajika ili kubaini nini kinaendelea kuhusiana na wanyama hawa kwa sababu kwa kiasi kikubwa wanaokamatwa na nyara za wanyama hawa ni maeneo ya kijijini jambo ambalo linatupa wakati mgumu kubaini ni wapi nyara za wanyama hawa zimeazimiwa kupelekwa au kusafirishwa.

Mahusiano ya uhalifu na vikundi vya wapiganaji (waasi)

Kwa siku za hivi karibuni ujangili na biashara haramu ya wanyamapori limekuwa ni jambo ambalo linaangaliwa sana na dunia, kwa mujibu wa Umoja wa mataifa ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na mimea mwitu inaleta matishio makubwa sana kutokana na ukuaji wake ambao unakaribia biashara haramu ya madawa ya kulevya, usafirishaji haramu wa silaha na usafirishaji haramu wa binadamu; kuna ushahidi wa taarifa kuwa vikundi vya kihalifu vinatumia njia hizi ambazo hutumiwa na majangili na pia hutumia mianya yote ya udhaifu kwenye usimamizi wa sheria za wanyamapori na sheria za usafirishaji kusafirishia vitu haramu au bidhaa haramu za wanyamapori (UNODC,2015).

SOMA: UCHAMBUZI WA RIPOTI; (Flash Mission Report Port of Mombasa, Kenya), Bandari Ya Mombasa Na Usafirishaji Wa Nyara Na Bidhaa Haramu.

Uhusiano kati ya biashara haramu ya wanyamapori na biashara nyingine haramu unafahamika, lakini kuna sintofahamu inayowafanya watafiti na waandishi kushindwa kuandika moja kwa moja kuhusu mtandao wa ujangili na ufanyaji wa biashara haramu za wanyamapori na vikundi vya uasi na vikundi vya kigaidi kama vile Al- shabaab. Taarifa za kimataifa zinaonyesha kwenye ripoti ya Umoja wa mataifa kuwa kikundi cha kigaidi cha Al-shabab kinajuhusisha na biashara haramu ya kuuza mkaa, ili wapate fedha za kuendeshe shghuli zao za kijangili, ingawa bado kuna mashaka na vikundi vya kigaidi kuhusishwa na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori, waandishi wengi kwa kiasi kikubwa wanakubali hali inaweza kuwa hivyo.

Kwa upande mwingine kuna taarifa zikionyesha vikundi vya kipiganaji vya nchi za Afrika ya Kati vinaweza kuwa vinanufaika na usafirishaji haramu wa meno ya tembo kutoka Sudani Kusini kwenda Kenya. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira linahusisha kwa karibu zaidi kuwa kuna biashara haramu za meno ya tembo zenye thamani ya dola za kimarekani miloni 12 hutumiwa na kikundi cha Janjaweed wanaofanya kazi zao katika nchi za Sudani, Chadi na Niger. Pia utafiti huu unakwenda mbali zaidi kuelezea namna ujangili na biashara haramu ya tembo wanaoishi katika misitu ya Kongo wanavyotengeneza fedha ambazo husaidia vikundi hivyo vya kipiganaji vya DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati kama vile Lord’s Resistant Army (LRA).

Sera ya wanyamapori ya Kenya na sheria za mazingira

Sera ya uhifadhi wa wanyamapori ya Kenya inaenda mbali sana hadi kufikia kipindi cha ukoloni wakati wa uanzishwaji wa hifadhi ya taifa ya Nairobi mwaka 1946 kama eneo la kwanza la uhifadhi wa wanyamapori nchini Kenya, kuanzishwa kwa hifadhi hii ya wanyamapori kuliifanya Kenya kuwa msitari wa mbele katika juhudi za uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori.

Baada ya uhuru serikali ya Kenya katika kikao chake mwaka 1975 ilipitisha sera ya uhifadhi wa wanyamapori ambayo ndio msingi wa sheria ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori ya mwaka 1976.  Katika sheria hiyo ilielezea kwa mapana sana kuhusu wanyamapori na ikijumuisha masula yote ya vivutio, utamaduni, kisayansi kama sehemu muhimu ya kuinua maisha ya watu kiuchumi. Hata hivyo kama ilivyoelezewa vizuri kabisa kuwa pamoja na uwepo wa sharia za uhifadhi nchini Kenya, sheria hizo zilikuwa na mapungufu na udhaifu katika uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori.

Sheria ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori ya Kenya ya mwaka 1976 ndio ilikuwa chombo kikuu cha kusimamia wanyamapori kilichoanzishwa baadaya kipindi cha ujangili miaka ya 1970 na 1980, badaye ikaja kufanyiwa maboresho mwaka 2010 baada ya nchi ya Kenya kuboresha katiba yao ya nchi. Pia serikali ya Kenya ilipitia tena sheria ya usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori na kuifanya kuwa mpya mwaka 2013.

Mabadiliko hayo kwenye sheria yalikuwa kuweka adhabu kali sana kwa yeyote anayejihusisha na vitendo vya kijangili. Hata hivo mabadiliko hayo yalilenga kuipa nguvu taasisi ya Kenya inayojihusisha na huduma za wanyamapori (Kenya Wildlife Services) kulinda, kuhifadhi kwa matumizi endelevu na usimamizi wa wanyamapori wa Kenya. Pia mabadiliko hayo kwenye sheria yakaenda sawa na moja ya maono yao ya 2030 yaliyosimamia kwenye utalii, mazingira na usalama.

Aidha, kipengele muhimu kwenye sheria ya uhifadhi hakikusahauliwa, katika sheria hiyo walitambua mchango wa jamii katika masuala ya uhifadhi, pia wadau binafsi kwenye masuala haya ya uhifadhi wa wanyamapori walitambuliwa ipasavyo. Mabadiliko hayo yalienda sambamba na kutoa adhabu kali kwa wahalifu wa sheria hii pia kuongeza kiwango cha adhabu kwa watakaobainika kwa namna yoyote kufanya ujangili wa wanamapori, hata hivo nimeona adhabu ya kifungo cha maisha kwa atakayepatikana na hatia ya kuua moja wapo wa wanyama ambao wapo hatarini kutoweka, mfano faru. Hii ndio hatua kubwa wanayojisifia wakenya kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili zao, kuwa kwa sasa wana chombo imara kinacholinda na kutetea maslahi ya wanyamapori na rasilimali nyingine za taifa lao.

Nikiwa naelekea ukingoni mwa makala hii, napenda ufahamu kuwa ripoti hii ina mambo mengi sana ya kina kuhusu uhifadhi, ulinzi, usimamizi na biashara haramu ya wanyamapori nchini Kenya, haya niliyochambua hapa ni machache na sio yote. Hivyo nakushauri ikiwa unataka kusoma ripoti hii yote usisite kuwasiliana nami, nitakutumia kwa njia ya email popote pale ulipo. Lengo langu kushirikishana mambo haya ili kwa pamoja tupate ufahamu na uelewa kwenye mambo haya, na pia itusaidie katika juhudi zetu za kuhifadhi na kusimamia rasilimali tulizonazo za wanyama na mimea pori.

Hitimisho na mapendekezo

Wanyamapori wa nchi kavu na majini nchini Kenya wanakabiliwa na hatari kubwa sana kwenye mustakabali wa maisha yao ya baadaye, hii ni kutokana na sababu za kibinadamu na sababu za kiasili ambazo kwa pamoja vinasababisha wanyamapori kuendelea kupungua na wengi kuwa katika hatari ya kutoweka kabisa. Ukuaji wa ongezeko la idadi ya watu, upanuzi wa maeneo ya kilimo, viwanda, ujangili na biashara haramu za wanyamapori vimetajwa sana kama vyanzo vikuu vya kuendelea kupungua kwa idadi ya wanyamapori kama tembo na faru kwenye makazi yao, hata hivyo hakuna usalama kwenye makazi ya viumbe hawa kutokana na ardhi kuwa ndogo na idadi ya watu inaongezeka kila siku.

Wanyamapori kama vile tembo na faru ni wanyama ambao wapo katika hatari kubwa sana ya kutoweka, hii ni kwa mujibu wa shirika la IUCN ambalo limewaweka wanyama hawa katika kipengele cha mstari mwekundu ikimaanisha wapo katika hatari kubwa ya kutoweka na wengine wapo katika hatari kubwa zaidi. Haya yote yanasababishwa na sababu kuu tulizotaja hapo juu, lakini pia ongezeko la mahitaji yake kwenye nchi za Asia na Ulaya ambao huitaji meno ya tembo na pembe za faru kwa ajili ya mambo ya ufahari na kwa matumizi ya dawa za asili.

Katika mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hii ni kuhakikisha nchi ya Kenya ina fanya kila linalowezekana kupunguza ujangili kwenye maeneo ya wanyamapori na hiyo inatakiwa kwenda sambamba na kuwapotezea hamu wateja wa meno ya tembo na pembe za faru kwenye nchi za Mashariki na Kusini mwa Asia. Hili ndio jambo muhimu sana tunaloweza kufanya kwa sasa. Kwa upande mwingine serikali ya Kenya na taasisi inayojihusisha na huduma za wanyamapori katika nchi ya Kenya wanatakiwa kushirikiana na kutafuta wadau wa kushirikiana nao kwenye mapambano haya ya ujangili.

Eneo lingine la kuangaliwa zaidi ni jamii, kwa sababu kiasi kikubwa cha wanyamapori nchini Kenya kipo nje ya maeneo yaliyohifadhiwa, hivyo basi serikali na taasisi zinazotoa na kusimamia huduma za wanyamapori zinatakiwa kufahamu siku zote jamii inayozunguka maeneo ya hifadhi ni muhimu sana kwenye uhifadhi, na wao ndio wa kwanza kuathiriwa na changamoto za wanyama waharibifu kwenye mifugo na mazao yao. Kinachoshauriwa kwenye ripoti hii ni kuhakikisha jamii hii inanufaika ipasavyo kutokana na uwepo wa wanyamapori kwenye maeneo yao. Hii itapunguza migogoro na chuki dhidi ya wanyamapori na pia kwa kutoa manufaa kwa jamii hizi, itasaidia sana kukuza ushirikiano katika uhifadhi na kufanikiwa kufikia malengo ya jumla ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori.

Aidha, mapendekezo na hatua za kuchukua ili kutekeleza mambo yote ambayo baada ya tathmini kufanyika na kuandaliwa kwa ripoti hii yameorotheshwa kwenye jedwali kwa kuzingatia vipaumbele. Nitakwenda kukushirikisha maafikiano na makubaliano ya hatua za pamoja walifikia baada ya tathimini ya ujangili na biashra haramu ya wanyamapori katika nchi ya Kenya. Yafuatayo ni mapendekezo hayo. Na ndio yanayohitimisha kabisa uchambuzi wa ripoti hii.

Hatua za kuchukua kwa hali ya kibailojia ya spishi kuu za wanyamapori ambao wamehusishwa katika biashara.

  1. Kutambua meneo kijografia na kufanya utafiti ili kutoa taarifa muhimu kwa wakati kuhusu hali ya kibiolojia ya spishi za wanyamapori muhimu, mkazo ukizingatiwa kwa tembo, kakakuona na paka wakubwa (big cats).
  2. Kumalizia utafiti na tathmini ya biashara ya nyama pori nchini Kenya
  3. Kuendeleza na kuinua programu ya kitaifa ya utambuzi, uchunguzi na utatafiti waspishi za wanyamapori.
  4. Kutekeleza mapendekezo yote muhimu yaliyopo kwenye ripoti ya “Mapping Corridors and Conectivity for Conservation Task Force” kwa kufokasi kwenye ekosistimu (ecosystem) ya Mara.
  5. Kufanya utafiti wa kitafa kuhusu matumizi ya ardhi na kuweka mkazo wa kuelewa kilicho nyuma ya kuendelea kupungua kwa maeneo ya uhifadhi.

Kw upande wa utekelezaji wa sheria na usimamizi wake, mapendekezo kadhaa yalitolewa ambayo ni;

  1. Kufanya uchunguzi na tathimini ili kutoa data au aarifa zinazokosekana kwenye ujangili na biashara haramu ya wanyamapori kama vile tembo, kakakuona, paka wakubwa, reptilia, ndege na spishi za majini.
  2. Kuanzisha maabara ya kitafiti katika jiji la Nairobi kwa huduma za wanyamapori za Kenya na kuhusisha taasisi nyingine za kimataifa katika utafiti wa wanyamapori.
  3. Kushirikishana kwa mapana kuhusu masuala ya kitalaamu na ushahidi wa kidigitali na kutoa taarifa za mara kwa mara endapo kuna mabadiliko yametokea kwa siku za karibuni, ili kuwasaidia wachunguzi, majaji na waendesha mashtaka.
  4. Kuimarisha uwezo wa kufanya tafiti za kichunguzi kwenye masuala ya uhalifu wa wanyamapori na kuwasaidia wasimamizi wa sheria kupitia mafunzo na tathimini, na mambo mengine ya kitalaamu yanayoendana na sheria za usimamizi wa wanyamapori
  5. Kuendeleza taasisi ya huduma za wanyamapori ya Kenya kwa kuwa na mkakati wa kupambana na rushwa na kukabiliana na tatizo la sasa katika usimamizi na ulinzi wa maliasili na kuboresha.
  6. Kutengeneza mfumo salama wa kiintelijensia wa kukusanya na kupeana taarifa kwa wadau wote wa uhifadhi kuhusiana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.
  7. Kusaidia na kupanua wigo kwa taasisi ya huduma za wanyamapori ya Kenya, KWC, na kuwapa uwzo mkubwa wa kuendesha mashtaka na mambo mengine ya kisheria, na pia hata watafiti wanatakiwa kufahamu na kujua na kujengewa uwezo huo wa kisheria.
  8. Kukuza na kuwezesha matumizi ya teknolojia kwenye masuala ya usimamizi wa wanyamapori na usimamizi wa sheria.
  9. Kufafanua na kutekeleza taratibu za kimashirikiano na mahusiano katika masuala yanayovuka mipaka katika ukanda, na kidunia ili kwa pamoja kushirikiana katika vita dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori.
  10. Kuendelea kuwajengea uwezo mamlaka za bandari na mamlaka za mipakani na viwanja vya ndege kuhusiana na uwezo wa kubaini uhalifu. Hasa kupitia utaratibu wote wa kusafirisha vitu nje ya nchi na kusafirisha vitu kuleta ndani ya nchi, kuangalia maeneo yote ya mipakani na kuzipa nguvu sehemu zote zenye udhaifu ili kuwakamata watu wote wanaojihusisha katika biashara hizi haramu na kuwafungulia mashtaka, bila kuwasahau watu wa kati ambao ndio wanaofanikisha uhalifu huo.
  11. Kutengeneza mfumo wa kuwasajili wakosaji wote wa masuala ya wanyamapori na kuwashirikisha wadau na mawakala wengine waliopo katika nchi na kanda mbali mbali.
  12. Kufanya kazi na makampuni binafsi ya fedha, mawasiliano na usafirishaji ili kujua hali ya mambo ilivyo.
  13. Sheria ya uhifadhi na usimamzi wa wanyamapori ya Kenya inafanya kazi pia kwa wanyamapori waishio majini, lakini taarifa za kitafiti kwenye eneo hili ni kidogo sana. Hivyo basi ni wakati wa mamlaka zinazofanya kazi kwenye maeneo haya ya majini kupata msaada na nguvu za kutafiti.

Katika eneo la kuwapa watu elimu na ufahamu kwa jamii, mapendekezo na hatua za kufanyia kazi zilipendekezwa zifuatazo;

  1. Kumalizia taratibu za kusimamia kutoa motisha kwa wamiliki binafsi wa ardhi na jamii ili waanzishe hifadhi, ushoroba (corridor) na maeneo ya mtawanyiko kwa ajili ya kuwa na ardhi ya kutosha kwa wanyamapori.
  2. Kumalizia na kutoa kanuni zitakazosimamia ufanyaji kazi kwenye hifadhi za wanyamapori.
  3. Kuendeleza na kutekeleza mipango ya usimamizi wa hifadhi kwa kushirikiana na jamii kama ilivyoainishwa kwenye sheria kuu ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori ya Kenya.
  4. Kuendeleza maadili ya taifa katika uhifadhi kupitia kampeni za kielimu na ufahamu ili kulinda asili na uchumi wa wanyamapori na kupunguza migogoro ya watu na wanyamapori.
  5. Kufundisha na kuajiri maaskari wa wanyamapori kutoka katika jamii ili kusimia utekelezaji wa sheria za uhifadhi kulingana na mahitaji ya tathimini iliyofanywa na mtalaamu wa kujitegemea.
  6. Kuendeleza na kutekeleza kanuni za kugawana manufaa au faida kwa utaratibu ulioanzishwa na sheria ya usimamizi na uhifadhi wa wayamapori ya Kenya.
  7. Kuboresha uelewa na ufahamu wa jamii kuhusu sheria zilizopo, kwa kuweka mkazo kwenye sheria ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na sheria ya usimamizi wa mazingira na uratibu.
  8. Kuimarisha uwezo kwa vyama vya uhifadhi wa wanyamapori vya Kenya na vyama vya uhifadhi wanaymapori vya kikanda kama chombo muhimu cha usafiri kufikia mikakati ya ushiriki wa serikali, wahisani na wawekezaji.
  9. Kuvijengea uwezo vyama vya usimamizi wa wanyamapori vya Kenya, ili viwe na viwango vizuri vya uongozi na ufanyaji kazi.
  10. Kubadilishana uzoefu kwa kutembeleana baina yao kwenye vyama hivi vya uhifadhi wa wanyamapori.

Pia ripoti hii katika mapendekezo yake imegusia hatua za kuchukua kwenye masula mtambuka yanayogusa uhifadhi wa wanyamapori kama ifuatavyo;

  1. Kutumia na kuimarisha muungano wa uhifadhi Kenya (Kenya Consrvation Allience, KCA) kama chombo muhimu cha kimkakati kushirikiana na serikali, kupeana taarifa na data, uratibu na utatuzi wa migogoro au mizozo.
  2. Kuoanisha mipango ya matumizi bora ya ardhi na maendeleo sawa na sheria ya usimamizi wa mazingira na sheria nyingine zinazohusika.
  3. Kutathimini thamani ya kiuchumi ya spishi kuu ambazo zimeathiriwa na biashara ili kusaidia uhifadhi, utekelezaji na hatua nyingine muhimu za mchakato wa kisheria.

Nakushukuru sana Rafiki yangu kwa kusoma makala hii muhimu, karibu tuendelee kuwa pamoja kujifunza na kufanyia kazi haya muhimu tuliojifunza hapa. Nakuahidi mambo mazuri zaidi endelea kufuatilia makala hizi kila siku na pia washirikishe wengine maarifa haya.

Ahsante sana!

Mchambuzi wa ripoti hii ni;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania