Cambodia ni kiini cha kuongezeka kwa biashara ya meno ya tembo na pembe za faru kutoka katika bara la Afrika. (Cambodia’s increasing role in the African ivory and rhinoceros horn trade).
Kati ya mambo yanayogonga vichwa vya habari kwenye magazeti na kurasa nyingi za mashirika mmbali mbali ya uhifadhi hapa duniani ni kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo na pembe za faru. Tafiti nyingi zimefanyika na mengi yameandikwa kuhusiana na mada hii ya ujangili na biashara ya meno ya tembo. Ukweli ni kwamba tatizo limekuwa kubwa sana kwa nchi moja na hata kwa dunia kulitatua kwa njia rahisi, sasa limekuwa ni janga kubwa kwa dunia.
Pamoja na hali hiyo kuendelea duniani, bado kuna nchi ambazo kwa mujibu wa tafiti na majarida yaliyoandikwa katika ripoti hii inaonyesha kushamiri na kuenea kwa biashara hii, nchi ya Cambodia ni nchi inayotajwa sana kuwa kinara katika kusaidia sana kukua na kuenea kwa biashara ya meno ya tembo na pembe za faru, ngoja tuangalia uchambuzi wa makala moja iliyoandikwa na Thomas Gray na wenzake kuhusiana na nchi ya Cambodia kujihusisha na biashara hii haramu.
Ili kupambana na usafirishaji, biashara ya meno ya tembo na pembe za faru kunahitajika juhudi za makusudi ili kukabiliana na changamoto hii, pia utekelezaji wa sheria zilizopo ni njia muhimu ya kupambana na hali hii inayoendelea kumaliza wanyamapori wetu kutoka katika bara la Asia na Afika.
Tangu mwaka 2011 kumekuwa na matukio mbali mbali ya ukamataji wa nyara za meno ya tembo, Loxodonta Africana zaidi ya 15 na pia matukio sita ya ukamataji wa pembe za faru katika nchi ya Cambodia, pia inaonyesha kuwa nyara 24 za tembo na faru zilizokamatwa zimeripotiwa kutoka katika nchi mbali mbali na kufika Cambodia kama kituo na sehemu ya usafirishaji haramu wa nyara hizo.
Kwa mantiki hii ni kwamba nchi ya Cambodia imekuwa ndio sehemu muhimu ya kupokea nyara kutoka katika nchi za Afrika na Asia na huzisafirisha kwenda nchi nyingne ambazo zina uhitaji wa baidhaa hzio, nchi kama China, na miji yake maarufu hupokea kiasi kikubwa cha shehena ya nyara za meno ya tembo na pembe za faru kwa ajili ya shughuli mbali mbali walizonazo. Hivyo bandari na viwanja vya ndege vya Cambodia hutumika kama sehemu muhimu ya kupokea na kusafirisha bidhaa na nyara za wanyamapori hasa tembo na faru.
Kasi cha tani 1.35 kilishikiliwa huko Ho chi Mnh moja ya jiji ma arufu nchini Vietnam, taarifa zinaonyesha kuwa shehena hiyo ya meno ya tembo ilitoka Afrika magharibi kupitia Cambodia na kufika Vietnam, pia mwaka huo huo 2017 Oktoba kiasi cha sehena ya pembe 8 na meno ya tembo yenye uzito usiojulikana ilikamatwa katika uwanja wa ndege wa Bankok, ikiwa inatoka Zambia lakini ilipitia Cambodia.
Taarifa za utafiti zinaonyesha kiasi cha tani 13 za meno ya tembo na pembe za faru zenye uzito wa kilogramu 124 ambacho kwa mujibu wa taarifa hizi ni kiasi kikubwa sana kuwahi kukamatwa kwa mwaka 2016. Hali hii ndio inayopelekea nchi ya Cambodia kuwa nchi ya pili duniani kutiliwa shaka katika kujihusisha na biashara ya pembe za faru na meno ya tembo. Hii ni kwa mujibu wa Mfumo wa Taarifa ya Biashara ya Tembo (Elephant Trade Information System, ETIS).
Kiasi kikubwa cha shehena inayokamatwa na mamlaka za usimamizi huko Cambodia zinatokea kwenye viwanja vikubwa viwili ya ndege kwenye miji miwili, mji mkuu wa kibiashara wa Phnon Penh na Siem Reap ambao ni mji maarufu na pia ni njia kubwa ambayo hutumiwa zaidi na watalii wanaokuja kutalii nchini Cambodia. Pia inaonyesha kiasi kikubwa zaidi cha shehena ya pembe za faru kukamatwa nchini Cambodia hivi karibuni Novemba 2016, zenye uzani wa kilogramu 35.
Taarifa za kina zinaeleza kuwa pembe na meno haya zinatoka katika nchi sita za Afrika. Nchi hizo ambazo zimetajwa kuwa ni sehemu ambazo nyara hizi zimetoka ni Angola, Kenya, Msumbiji, Namibia, Afrika ya Kusini na Uganda. Hadi shehena hiyo kufikia Cambodia zilipita kwenye viwanja vya ndege vya nchi mbali mbali na baadhi ya bandari na viwanja vya ndege vilivyotumika zaidi ni Addis Ababa, Bangkok, Doha, Dubai, Singapure, Seoul, hivyo ni viwanja vya ndege na vituo ambavyo hutumika katika usafirishaji haramu wa meno ye tembo na pembe za faru kabla ya kufika Cambodia.
Aidha katika bandari kuu ya Preah Sihanoukivile nchini Cambodia shehena zenye uzani wa kilogramu 600 ambazo ni meno ghafi ya tembo zilishikiliwa na taarifa zinasema kuwa zimetoka katika nchi ya Msumbiji zikiwa zimefichwa kwenye shehena ya mahindi, na pia kiasi cha uzani wa kilogramu 3000 za meno ya tembo zilishikiliwa zikiwa zinatoka nchini Kenya, zilipitia Malasia zikiwa zimesafirishwa pamoja na maharage hadi kufika katika bandari kuu ya Cambodia hii ni kwa mujibu wa taarifa za Agasti 2016 na Mai 2014.
Katika bandari hii ya Cambodia, matukio mengi sana ya usafirishaji wa nyara kutoka nchi za Kenya hupitia hapa. Kuna taarifa za mwaka 2016, zinazoeleza namna bandari ya Kenya na bandari ya Cambodia zinavyojihusisha na usafirishaji wa nyara za wanyamapori. Kwa mfano Disemba mwaka 2016 zaidi ya kilo 1300 za meno ya tembo, mfuvu 10 ya paka wakubwa, mifupa yenye uzani wa kilo 82 na magmba (scales) ya Kakakuona yenye uzani wa kilo 137, yalishikiliwa huko Phnon Phenh huko Cambodia yakiwa yemefichwa kwenye uwazi ulio katika magogo ya mbao yakitokea Msumbiji.
Hali hii inaonyesha ni kwa namna gani nchi ya Cambodia ilivyo kitovu cha biashara hii ya nyara za tembo na faru, inasemekana pia hata wavietnamu na Wachina huja kufanya shughuli zao Cambodia kwa ajili ya urahisi na ni sehemu ambayo hupokea shehena za nyara kutoka katika nchi mbali mbali duniani, Afrika ndio ikiwa kinara mkuu, kwasababu nyara nyingi za wanyamapori zilizopo kwenye mizunguko ya kibiashara huko Cambodia hutokea katika nchi za Afrika.
Mwandishi wa makala hii katika jarida la TRAFFIC Bulletin, anamalizia makala yake kwa kuwa na wasi wasi kuwa endapo hali ya mambo itabakia kama ilivyo sasa, nchi ya Cambodia itakuwa zaidi ya hapo na itatumika kama sehemu kuu inayohusika na usambazaji wa nyara za tembo na faru kwenda sehemu nyingine zenye mahitaji ya nyara hizo kwa njia rahisi. Mfumo wa usimamizi na ukaguzi katika maeneo nyeti ya usafirishaji kama vile viwanja vya ndege na bandari uko dhaifu sana na unatoa mwanya kwa biashara hii haramu kushamiri nchini humo.
Hali ya mambo inaweza kubadilika endapo Cambodia itahitaji msaada wa kupambana na ujangili huu uliokithiri kwenye nchi yao. Mashirika mengi ya uhifadhi yapo tayari kusaidia hali hii isiendelee kuwa mbaya, maana kadri siku zinavyoenda mtumizi ya nyara hizi yanazidi kuongezeka hali ambayo inapelekea kupungua kwa wanyamapori hawa katika maeneo yao. Tushirikiane katika kupambana na ujangili ili kuokoa wanyama hawa wenye thamani kubwa kwa kizazi chetu na vizazi vingi vijavyo.
Nakushukuru sana Rafiki kwa kusoma makala hii hadi mwisho, naamini umepata mwanga kwenye masuala haya ya uhifadhi wa maliasili zetu. Karibu tuendelee kujifunza zaidi kwenye makala ijayo hapa hapa kwenye mtandao wako wa Wildlife Tanzania. Pia usiache kuwashirikisha wengingi haya uliyojifunza hapa.
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaam.net/wildlifetanzania