Habari Rafiki, karibu katika makala zetu za kila siku kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, maliasili na utalii tunazojifunza hapa katika mtandao wetu wa wildlife Tanzania. Kadri siku zinavyokwenda mambo yanabadilika kwa kasi sana na hivyo hata hatua tunazochukua zinatakiwa kwenda sambamba na kasi ya dunia.

Katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine ili ziendelee kuwepo njia nyingi mbali mbali zimebuniwa na kutumika ili kujua kama zinaweza kusaidia kuleta matokeo chanya katika uhifadhi wa wanyamapori, lakini pia kusababisha maisha ya watu ambao wanaishi karibu na wanyama hawa wanaona faida na sio hasara mara kwa mara.

Kama wote tunavyofahamu kuwa jamii zinazoishi kando kando ya maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori zinakabiliwa na changamoto nyingi sana kwenye maisha yao, hasa eneo la uzalishaji mali na chakula. Kwa kiasi kikubwa jamii hizi ni wakulima na wafugaji ambao huishi kando ya maeneo haya yaliyohifadhiwa kwa ajili ya kuendesha shughuli mbali mbali za kujipatia kipato kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi nk.

Hivyo kwa kuwa kuishi kwenye maeneo hayo ni changamoto kubwa kutokana na uharibifu unaosababishwa na wanyamapori kama vile tembo, tandala, nyani na wanyama wengine wanaokula majani huaribu kabisa mazao ya wakulima ambao hulima pembezoni mwa maeneo ya hifadhi ya wanyamapori.

Kwa upande mwingine wafugaji nao hapata hasara ya kuliwa mifugo yao na wanyama wanaokula nyama kama vile simba, fisi, chui, duma, mbwa mwitu nk. Wanavamia mifugo ya wafugaji wakiwa malishoni wakati wa mchana na pia wakati wa usiku wakiwa nyumbani.

Hali hii ndio imefanya serikali za nchi mbali mbali na mashirika binafsi kubuni mpango wa kusaidia kupunguza changamoto hizi kwa kuanzisha programu ya kutoa fidia kwa walioharibiwa malizao na wanyamapori. Jambo ambalo ni jema na linaonekana kuwa la kiungwana kwa kiasi kikubwa.

Tafiti zilizofanyika na watalaamu wa masuala ya wanyamapori zimebaini udhaifu katika mfumo wa kulipa fidia jamii ambazo huharibiwa mali zao na wanyamapori. Kwenye maeneo mbali mbali duniani mfumo huu hutumika sana kwa jamii ambazo zimo pembezoni mwa hifadhi za wanyamapori, nchi kama India na Kenya hutumia mfumo huu wa kutoa fidia kwa walioharibiwa mali zao na wanyamapori.

Tafiti zinatilia shaka mfumo huu kwa kuwa unaonekana hautaweza kudumu kwa muda mrefu kutokana na ukweli kwamba, kwa sehemu fedha za kufidia uharibifu hutolewa na serikali za nchi husika au misaada kutoka kwa wahisani ambayo nayo sio ya uhakika. Fikiria mwenyewe hali ya mambo ilivyo kila siku, kama unadhani kutoa fidia ni suluhisho kwa jamii kuishi vizuri na wanyamapori, au jamii itaacha kufanya vitendo vya kijangili kuwinda wanyamapori.

Ukweli ni kwamba fidia imelenga kusaidia jamii kutolipiza kisasi kutokana na uharibifu wa mali zao, kama vile mifugo na mazao; hivyo fidia ilikuwa ni kwa ajili ya kuifanya jamii kuona kuwa nayo inafikiriwa na changamoto wanayopata serikali inaijua na inawajali hivyo kupooza hali ya mambo na kufanya kwa kiasi fulani jamii kuwa na uvumilivu na uwepo wa wanyamapori kwenye maeneo yao, tafiti zinasema suala la kutoa fidia haliwezi kutatua tatizo la msingi dhidi ya migogoro kati ya watu na wanyamapori.

Katika moja ya makala iliyoeleza vizuri jambo hili, inasema kuwa kutoa fidia kwa pande zote mbili ambazo zinaathirika na wanyama waharibifu inaweza kuoneka ni suluhisho, likini ni la muda mfupi na inaeleza kuwa endapo fidia itaendelea kutolewa basi hatutakuwa na matokeo mazuri sana kwenye uhifadhi endelevu. Mfano chukulia mkulima ameheribiwa mazao yake na tembo, sawa ataumia na kupata hasara, lakini kama hatapata fidia inamaanisha mkulima huyo hatalima tena kwenye maeneo karibu na makazi ya tembo, lakini pia hatakuwa na shauku ya kufanya upanuzi wowote wa shamba lake hivyo ataacha makazi ya wanyamapori na misitu kuwa salama, pia kutolipa fidia kutamfanya atafute namna nyingine ya kupata kipato na kuishi maisha yake, pia kutokutoa fidia kutazuia wale ambao wana nia ya kuja kufanya kilimo kwenye maeneo karibu na hifadhi wa wanyamapori kuacha kuja kufanya kilimo maeneo hayo. Lakini kama suala la fidia litakuwepo itakuwa ni kinyume chake kabisa.

Kwa upande wa wafugaji, suala la kutoa fidia limeelezwa vizuri sana kwenye makala hii ya utafiti niliyoichambua, inasema kuwa endapo wafugaji watalipwa fidia kutokana na kuliwa mifugo yao na wanyama wanaokula nyama itakuwa ni kuongeza tatizo juu ya tatizo kwenye uhifadhi wa maliasili kwa namna ambayo itasaidia wafugaji kuwa na mifugo mingi ambayo italeta usumbufu sana na kwa kuwa wana eneo dogo la malisho kitakachofuata hapo ni wafugaji kukiuka sharia na kuanza kulisha mifugo yao kwenye maeneo ya wanyamapori na hivyo kusababisha chakula cha wanyamapori wanaokula majani kupungua. Jambo ambalo litasababisha mogogoro isiyoisha kati ya wafugaji na wanyama wanao kula nyama. Na endapo majani yatapungua kutokana na mifugo kula majani hayo matokeo yake wanyamapori wanaokula nyasi ambao huliwa na simba watakufa au kuondaoka, nahapo ndipo simba watakapokuja kula mifugo ya wafugaji na kusababisha vita na ugomvi.

Kwa hiyo kutoa fidia kutakuwa hakujaleta matokeo yoyote chanya kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Hivi ndivyo watafiti wa masuala haya wanavyoona hali ya mambo endepo kutakuwa  na utaratibu wa kutoa fidia hata kama ni kidogo, hali ya mambo haitakuwa nzuri endapo itaendelea kutolewa.

Watafiti wanapendekeza kuwepo na njia mbadala za kukabiliana na changamoto hizi, na sio kutumia utaratibu wa kutoa faidia. Ushauri umekuwa kuwasaidia wafugaji na wakulima ambao wanachukua tahathari za kuzuia mifugo yao na mazao yao yasiliwe ana wanyamapori. Na hapa ni kuhakikisha wanashiriki katika uhifadhi na pia wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na wanyamapori kwenye maeneo yao.

Kwa kuwa watu watakuwa wanaogopa kulima na kupanua maeneo ya mashamba kwenye maeneo yenye wanyamapori watasaidia sana katika uhifadhi wa maeneo mhimu na mfumo mzima wa ikolojia utabaki salama bila kuharibiwa kwa kilimo. Pia hali hii inatakiwa kwenda sambamba na kuzuia uwindaji wa kiholela unaofanywa na jamii, jamii ijifunze kuwa wavumilivu na wanyamapori na pia wawapende.

Makala hii ni uchambuzi wa jarida iliyokuwa inahusu Why compensating wildlife damages may be bad for conservation” iliyoandikwa na Erwin H. Bulte na Daniel Rondeau. Ni jarida lililosheheni mambo mengi yatakayotusaidia sana katika kufikiri na kuweka mipango mizuri ya uhifadhi kwa faida ya sasa na baadaye.

Nakushukuru sana Rafiki kwa kusoma makala hii hadi mwisho, naamini umepata mwanga kwenye masuala haya ya uhifadhi wa maliasili zetu. Karibu tuendelee kujifunza zaidi kwenye makala ijayo hapa hapa kwenye mtandao wako wa Wildlife Tanzania. Pia usiache kuwashirikisha wengingi haya uliyojifunza hapa.

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania