Habari msomaji wa makala za kila siku za maliasili na wanyamapori, karibu kwenye makala ya leo tujifunze na kufikiri kwa pamoja njia bora ya kutatua changamoto ambazo zipo kwenye jamii yetu. Kwa kiasi kikubwa matatizo tuliyonayo kwenye maisha yetu ni kutokana na kutojua nini hasa cha kufanya, tumekosa ufahamu sahihi na maarifa sahihi ya kutusaidia kutatua changamoto zetu na pia kutoingia kwenye changamoto za mara kwa mara.

Kwa kiasi kikubwa changamoto na migogoro inaasababishwa na ukosefu wa njia mbadala za kuishi maisha, tunaamini kwenye njia moja na hatuna maarifa ya kutosha kutufungua kuona njia nyingine bora zaidi za kuishi. Hali ipo sehemu zote za jamii, ukiwa mjini hali ni ile ile ukienda kijijini hali ni ile ile. Mfumo wa maisha unafana sana kiasi kwamba unafanya maisha yanakuwa magumu kuishi.

Mfano mzuri ni jamii zetu zinazoishi kando kando ya maeneo ya hifadhi ya wanyamapori, jamii hizi hukabiliwa na changamoto kubwa sana za kuishi maisha yao kutokana na wanyamapori kuharibu mazao ya wakulima na pia kwa upande wa wafugaji wanyama wanaokula nyama wanavamia na kula mifugo ya wafugaji jambo ambalo ni hasara sana kwa jamii hizi.

Kwa sababu asilimia kubwa ya jamii hizi hujishughulisha na kilimo na ufugaji, njia nyingine za kuishi maisha zimekuwa ndogo sana na jamii hizi tangu enzi na enzi hutegemea njia hizo katika kupata chakula na kipato kwa ajili ya kuishi maisha yao. Na kwasababu ya utegemezi huu wa njia moja ya kujipatia kipato  ambayo inakumbwa na changamoto kubwa kiasi hicho, hapo ndipo migogoro huanzaia, na ndipo hali za maisha ya watu zinazidi kuwa chini kabisa.

Miaka na miaka maisha yamekuwa yanazunguka kwenye mfumo huo, na kutokana na ukweli kwamba kiasi kikubwa cha wakulima na wafugaji hawa hawana elimu na maarifa zaidi ya kuwafanya wabadili au wafikiri kuna njia nyingine ya kuish maisha yao.

Katika hali kama hii, tunweza kuwa na uhifadhi endelevu wa maliasili zetu? Tunaweza kuwa na uvumilivu wa kuendelea kuishi na wanyamapori na kuwafurahia, kwa hakika wengine wanaweza kuona umuhimu na fahari ya wanyamapori, lakini wale walio karibu na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori wanaweza wakawa na mtazamo tofauti.

Tunatakiwa kuchukua hatua mathubuti za kuwa na suluhisho la kudumu kwa changamoto hizi. Kuna njia nyingi nzuri za kukabiliana na hali hii ambazo zinatumiwa na serikali na mashirika binafsi ili kuwafanya watu waone thamani ya wanyamapori na maliasili nyingine. Njia hizi kama za ujenzi wa huduma za afya, barabara, shule na nyingine nyingi ambazo zinapunguza makali ya maisha kwa jamii hizi ni muhimu sana zikaendelea kuboreshwa na kufanyika kwa awamu mbali mbali kulingana na vipaumbele na changamoto walizonazo jamii hizi.

Ukifuatilia historia utaona mambo yaliyowafanya watu wakabadilika na kubadili mfumo wao wa maishi ni kupata elimu na maarifa sahihi ya kuishi maisha yao. Mtu akipata elimu na maarifa sahihi uwezekano wa kuishi maisha yanayoleta madhara mabaya hasa kwenye uhifadhi wa wanyamapori na mazingira kwa ujumla ni ndogo.

Hivyo naamini endapo tutakazana kutoa elimu bora na maarifa sahihi kwa jamii zetu tunaweza kuleta matokeo chanya sana hasa kwa jamii hizi ambazo zinaishi kwenye maeneo haya ya vijijini na yana changamoto kubwa hasa ya umasikini.

Pia kutokana na hali hiyo, hata utatuaji wa changamoto utakuwa mkubwa na wa ufanisi zaidi kuliko mwanzo, pia kutakuwa na njia mbadala za kuishi na kupata kipato. Hali hii itapunguza presha ambayo ipo kwa watu kutaka kuvamia maeneo ya wanyamapori ili kulima na kuishi na wanyamapori.

Naamini umejifunza kupitia makala hii, karibu kwenye makala nyingine hapa hapa.

Asante sana!

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania