Habari msomaji wa makala za kila siku kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, misitu na pia utalii. Karibu katika makala ya leo tuendelee na uchambuzi wa ripoti iliyotoka hivi karibuni inayoitwa “EUROPE DEADLY IVORY TRADE”. Hii ni moja ripoti iliyoweka mambo mengi wazi hasa ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo na bidhaa zake inayofanyika na nchi nyingi za Umoja wa Ulaya. Karibu tuendelee na uchambuzi wa ripoti hii.

SOMA: Mambo Usiyoyajua Kuhusu Nchi Za Umoja Wa Ulaya Zilivyochangia Kushamiri Kwa Ujangili Wa Tembo Barani Afrika

Biashara ya meno ya tembo kwa Umoja wa Ulaya ilizuiwa kabisa baada ya tembo kupewa ulinzi wa hali ya juu sana na baada ya makubaliano ya mkataba wa CITES, makubaliano ambayo serikali zilikubaliana kudhibiti biashara za bidhaa za wanyamapori (Julai mosi 1975 kwa tembo wa Asia na Januari 18, 1990 kwa tembo wa Afrika). Kwa sheria za umoja wa Ulaya ni kwamba meno yote ya tembo ambayo yamepatikana baada ya mwaka 1947 na kabla ya mwaka 1990 hayataruhusiwa kuingia katika biashara bila cheti cha kibali kutoka kwa serikali za nchi husika, bali bidhaa za meno ya tembo ambazo zimetokana na tembo walioishi kabla ya mwaka 1947 yanaweza kuuza au kuingia katika biashara bila kuwepo kwa cheti au kibali chochote na hii ndio mwanya wa kushamiri kwa biashara haramu na kukua kwa ujangili ulipoanzia.

Hakuna kipande chochote cha meno ya tembo kilichonunuliwa kwa ajili ya utafiti huu wa (kutumia Radiocarbon) kiliuzwa kwa cheti maalumu au kibali, na utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa meno ya tembo yaliyopo katika mzunguko yametokana na tembo waliouwawa miaka michache ya hivi karibuni.

Kasi ya kusitisha biashara ya meno ya tembo

Biashara ya kimataifa ya meno ya tembo ilishasitishwa na CITES tangu mwaka 1989, lakini bado kuna nchi ambazo ziliendelea na biashara hiyo ndani ya nchi zao wenyewe. Lakini kuna ushahidi wa kila namna unaoonyesha jinsi ambavyo biashara ya meno ya tembo kwenye masoko ya ndani ya nchi inavyosababisha na kuchochea janga la ujangili wa tembo wa Afrika, tunantakiwa kufanya kila linalowezekana kusitisha biashara ya masoko ya ndani ya meno ya tembo kwenye nchi zinazofanya biashara hizo.

Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia uhifadhi na maumbo asilia (ICUN), lilipitisha maazimio mwaka 2016, ya kutaka kufungwa kwa masoko yote ya ndani yanayojihusisha na meno ya tembo, jambo ambalo limeungwa mkono na shirika la umoja uwa mataifa la udhibiti wa biashara ya wanyama na mimea mwitu iliyopo hatarini kutoweka (CITES), CITES wametoa wito kwa nchi zote ambazo zinajiuhusisha na biashara ya meno ya tembo kwenye nchi zao, kuyafunga masoko hayo kwani ndio kichocheo kikuu cha ujangili wa tembo katka bara la  Afrika.

SOMA: Masoko Ya Meno Ya Tembo Yaliyopo Ulaya Ambayo Hujawahi Kuyasikia Kabisa

Sasa nchi nyingi duniani zipo katika harakati za kufanyia kazi mapendekezo hayo ya kufunga na kusitisha biashara ya meno ya tembo kwenye nchi zao, au kwenye masoko ya ndani.

Hong Kong ambayo ndio inaongoza duniani kwa kuwa na masoko makubwa ya meno ya tembo, mwezi januari mwaka 2018 wametamka kufuta na kusitisha kabisa biashara ya meno ya tembo kwa miaka mitatu ijayo.

China ilisitisha biashara ya meno ya tembo na bidhaa za meno ya tembo Desemba mwaka 2017, ikimaanisha biashara zote za meno ya tembo sasa ni haramu au ni kinyume na sheria kabisa, isipokuwa kwa kile walichokiita “mapambo halisi” au “genine antique”, tayari hadi hapa juhudi za nchi ya China zimeonekana, na taarifa zinasema baada ya kufikia uamuzi huo biashara ya meno ya tembo iliporomoka kwa 65% mwishoni mwa mwaka 2017.

SOMA:Teknolojia Ya Kutumia RADIOCARBON Ilivyosaidia Katika Vita Dhidhi Ya Ujangili Na Biashara Haramu Katika Nchi Za Umoja wa Ulaya

Marekani nayo imechukua hatua za kusitisha biashara za meno ya tembo chini ya sheria ya spishi zilizopo katika hatari ya kutoweka, kwa kuipa sheria nguvu ili kuzuia kuuza, kununua na kusafirisha meno ya tembo sehemu yoyote ile.

Ulaya nao katika harakati za kusitisha kabisa biashara ya meno ya tembo kwenye masoko ya ndani ya nchi wanachama wa umoja huo, wamedhamiria kusitisha kabisa biashara hiyo ya meno ya tembo, hakuna kununua, kuuza au kusafirisha kwenda kwenye nchi nyingine ikiwa ni pamoja na nchi za umoja huo. Ikiwa imetoa msamaha kwa masharti makali sana kwenye vifaa vya miziki ambavyo vina meno ya tembo, lakini pia kwa kuuzia makubusho meno ya tembo.

Nchi mbalimbali duniani sio tu zinasitisha masoko ya meno ya tembo kwenye nchi zao, bali wanazitaka nchi za umoja wa Ulaya kufanya hivyo pia. Nchi mbali mbali duniani kote wameridhia na kutia saini kusitisha baishara za meno ya tembo, katika ripoti hii zaidi ya watu milioni moja wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau wa uhifadhi wa wanyamapori kuzitaka nchi zinazoendesha biashara hizi kusitisha mara moja.

Asante sana msomaji wangu kwa kusoma makala hii hadi mwisho, naamini umepata mambo mengi mazuri ya kujifunza ili kwa pamoja tuwe na uelewa mzuri kuhusu sekta hii mihimu hapa Tanzania na sehemu nyingine. Jifunze pia mshirikishe na Rafiki yako maarifa haya.

Mchambuzi wa ripoti hii ni;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania