Kwa mara nyingine tena nakualika katika ule mfululizo wetu wa darasa huru kuhusu wanyamapori. Leo tunakuja na mnyama mwingine tena ambae kwa hakika utahamasika kumjua kwa undani zaidi. Nacho amini kupitia darasa hili utajifunza mengi zaidi juu ya mnyama huyu. Nae ni “DUMA”.

UTANGULIZI

Duma ni mnyama jamii ya paka ambae watu wengi sana humfananisha na chui na hatimae wanapomuona humuita chui. Laahasha kumbe ni tofauti kabisa na chui. Hivyo basi ni matumaini yangu kupitia darasa hili utaweza kumjua duma lakini pia kuweza kumtofautisha duma na chui kwa haraka zaidi hata pale unapomuona mmoja wapo.

SIFA ZA DUMA

  1. Duma ndio mnyama anaye ongoza kwa kukimbia kwa kasi zaidi kuliko wanyama wote waishio aridhini.
  2. Duma ana miguu myembamba na mirefu, mwili ulio chongoka ambapo sifa zote hizi humuongezea uwezo wa kukimbia kwa kasi.
  3. Dumja ana rangi ya mng’ao yenye mabaka meusi mwili mzima.
  4. Tofauti ya duma na wanyama wengine jamii ya paka ni kwamba duma ana mwili mdogo, kichwa kidogo na hata masikio yake ni madogo pia.
  5. Kubwa zaidi ambalo kwa haraka haraka unaweza mtofautisha duma na wanyama wengine jamii ya paka ni “Duma wana alama ya machozi yenye rangi nyeusi inayo anzia sehemu ya upande wa ndani wa jicho mpaka pembeni ya pua pande zote mbili.

TABIA ZA DUMA

  1. Hupenda kujificha kwenye majani marefu kwa ajili ya kuwinda.
  2. Duma ni wanyama wenye uwezo wa kuona zaidi kipindi cha mchana kuliko usiku. Hii ni tofauti na wanyama wengine jamii ya paka.
  3. Muda mzuri ambao duma hupenda kuwinda ni asubuhi mapema na alasiri pale jua linapoanza kupungua ukali.
  4. Kutokana na uwezo wake wa kukimbia, huwa ni nusu tu ya wanyama awakimbizao hufika sekunde 20-60, na hawa hupona na kubahatika kukimbia.
  5. Anapo mkamata mnyama humuuma shingoni na kubaki hapo mpaka mnyama atakapo kufa kutokana na kushindwa kupumua.
  6. Mara tu anapopata kitoweo hulazimika kula haraka haraka kabla ya wnyama wengine walao nyama hawajamuona na kumnyang’anya, mfano simba, fisi au mbwa mwitu.
  7. Duma ni wanyama ambao huishi kwa kujitenga.
  8. Hutokea marachache sana dume kukaa na ndugu zake wadogo kwa muda mfupi, lakini mama hulea watoto akiwa pekeake kwa takribani mwaka na nusu au zaidi.

MUHIMU KUJUA

Duma anapo kimbiahutumia mkia wake kuongeza kasi lakini pia kugeuka na kuelekea upande anaotaka kwenda na hasa wakati anapokuwa anakimbiza mnyama.

UREFU,KIMO NA UZITO

UREFU=futi 3.5-4.5 na mkia hufika inchi 25.5-31.5.

KIMO=futi 2.5-3

UZITO=hufikia uzito wa kilogramu 35kg-65kg.

UMRI WA KUISHI

Duma wanapokuwa maeneo ya hiufadhi huishi kiasi cha myaka 12-14 ila endapo atakuwa anafugwa basi hufikia mpaka umri wa myaka 17.

MAZINGIRA

Duma hupendelea maeneo yalio wazi yenye majani marefu kidogo. Majani haya humsaidia duma kujificha wakati wa kuwinda. Mara nyingi maeneo haya huwa tambarare ambayo pia humsaidia duma kuona mbali zaidi na kuweza kukadiria umbali aliopo mnyama.

CHAKULA

Duma ni jamii ya wanyama walao nyama. Miongoni mwa wanyama ambao duma hupendelea sana kuwawinda ni swalatomi, swalapala, watoto wa nyumbu na wanyama wengine wadogo wadogo wenye kwato.

SEHEMU WAPATIKANAZO DUMA NA IDADI YAO

Historia inaonyesha kuwa duma walikuwa wanapatikana maeneo yote barani Afrika na sehemu kubwa ya bara la Asia, yaani kuanzia Afrika Kusini mpaka maeneo ya India. Lakini kwa takwimu za sasa duma wanasemekana kusalia maeneo ya Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Kusini magharibi mwa Afrika na sehemu ndogo sana ya Iran.

Mpaka kufikia miaka ya 1900, bara la Afrika lilikuwa na duma zaidi ya laki moja. Lakini kwa sasa takwimu zinaonesha kuwa bara la Afrika wamebaki duma kati ya 9,000-12,000. Huku Iran wakiwa wamesalia duma takibani 200 tu.

KUZALIANA

Duma hawana kipindi maalumu cha kuzaliana hivyo huzaa wakati wowote wa majira ya mwaka. Duma jike hubeba mimba kwa muda wa siku 90-100 (mkadirio ya miez 3) na huzaa watoto kati ya 4-6. Watoto wa duma huzaliwa wakiwa na rangi ya kijivu wakiwa na manyoya marefu kama yafananayo na sufu yalio lala upande wa mgongoni. Manyoa hayo huwasaidia pia kujificha kwenye majani kutokana na maadui mfano simba na fisi. Mama huwa na jukumu la kuwahamisha watoto kila baada ya muda siku chache na kutafuta maficho mengine ambayo ni salama. Wiki ya 5-6 watoto huanza kuongozana na mama yao na kula chakula ambacho mama anakuwa amewinda kwa muda huo.

Mama hukaa na watoto kwa muda wa miezi 16-18 na baada ya hapo familia hii husambaratika na kisha mama kutafuta dume mwingine kwa ajili ya kuzaa tena.

Watoto wa duma hufikia umri wa kuzaa kuanzia miezi 20-24 (takribani myaka 2). Watoto wengi wa duma huwa wanakufa wakiwa na umri mdogo na hii ni kwasababu mama hulazimika kuwaacha peke yao anapokwenda kutafuta chakula na hapo ndipo fisi, simba, mbwa mwitu au nyati wanapo wakuta huwauwa.

UHIFADHI

Duma ni wanyama ambao wamepungua kwa kasi kubwa sana kutokana na changamoto mbali mbali. Hali hii imepelekea wanyama hawa kuingizwa kwenye sheria muhimu za nchi husika katika uhifadhi. Shirika la umoja wa mataifa linalo jihusisha na uhifadhi wa maumbile asili (IUCN-International Union for Conservation of Nature) limewaweka duma katika kundi la wanyama ambao endapo idadi yao itashindwa kuongezeka basi watakuwa ni wanyama waliopo hatarini kutoweka duniani.

Ni jambo la kuskitisha sana kuona Afrika Mashariki kwa ujumla tuna duma wapatao 2,572 tu,hii ni hatari sana kwakweli.

CHANGAMOTO ZINAZO WAKUMBA DUMA

  1. Migogoro kati ya binadamu na wanyama hasa jamii za wafugaji kwa duma wanao ishi nje ya maeneo ya hifadhi wamekua wakiuliwa sana pale wanapo shambulia mifugo ya watu.
  2. Shughuli za uwindaji ambazo hupunguza idadi ya wanyama tegemezi kwa duma hivyo kufanya wanyama hawa kuwa na njaa kwa muda mrefu.
  3. Duma wana naswa sana na wanya ambazo hutegwa na majangili kwa ajili ya kukamata wanyamapori hivyo kufia mitegoni bila msaada.
  4. Ajali za barabarani hasa kwa barabara zilizo pita ndani ya hifadhi mfano Hifadhi ya Taifa Mikumi na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na hata zile zilizopo karibu na maeneo ya hifadhi. Magari yamekua ya kigonga sana wanyama hawa kutokana na mwendokasi wa mabasi usababishwao na maderva wazembe.
  5. Idadi kubwa ya magari ya watalii hifadhini. Duma ni wanyama ambao wanavutia sana kuwaangalia hivyo anapoonekana sehemu watalii huitana na kujaa sehemu moja hivyo kuwafanya duma kukimbia kwa hofu.
  6. Uchimbaji rasilimali asili mfano madini na mafuta vimepelekea sana kuharibu mazingira na hivyo kuwafanya duma kutoweka baadhi ya maeneo.
  7. Ujangili ulio kithiri ambapo duma huwindwa kwa ajili ya ngozi na sehemu nyingine za mwili kama kucha na meno. Hii yote husababishwa na biashara haramu ya wanyamapori na malighafi zao.
  8. SIASA- huu ni ugonjwa mkubwa sana katika uhifadhi wanyamapori na mfano mzuri ni hapa nchini kwetu. Mbunge anadiriki kusema kuwa Tanzania tuna maeneo mengi yalio tengwa kwa ajili ya uhifadhi na kudai kwamba kwanini wananchi wasipewe maeneo hayo wakalima. Aibu kubwa hii kwa msomi pia mbunge tegemezi kwa jamii za watanzania.

NINI KIFANYIKE KUWANUSURU DUMA HASA HAPA TANZANIA

  1. Viongozi waepuke kuleta siasa kwenye uhifadhi kwani wakumbuke kua wao ni wakupita tu ipo siku wataondoka ila wanyamapori watabaki tu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
  2. Kutafuta njia sahihi ya uvunaji rasilimali asili bila kuharibu mazingira ya wanyama maeneo ya hifadhi.
  3. Kuwep kwa elimu ya uhifadhi mashuleni, uzalendo na kuongeza idadi ya askari wanyamapori ili kutokomeza tatizo la ujangili.
  4. Sheria kali zenye kuumiza zichukuliwe kwa madereva wazembe wanaogonga wanyama hifadhini ili kupunguza ajali hizi. Maana baadhi ya madereva wamekua viburi na hivyo kupuuzia alama za hifadhini zilizopo barabarani.
  5. Kusimamia idadi maalumu ya watalii na magari kwani tumeona duma wamekua wakipata hofu sana kutokana na idadi kubwa ya watalii na magari mengi eneo moja.
  6. Migogoro ya binadamu na wanyama hususani jamii za wafugaji itafutiwe ufumbuzi ili kupunguza mauaji ya wanyamapori.

HITIMISHO

Duma ni wanyama wanao vutia sana kuwaangalia kutokana na maumbile yao pia michezo yao na kubwa zaidi ni pale unapo shuhudia wakimkimbiza mnyama. Tuwe na uzalendo wakutembelea Hifadhi za Taifa hapa Nchini ili tuweze kujionea wenyewe kuhusu mnyama duma awapo hifadhini na mbwebwe zake.

Natamani vitukuu wa vitukuu wangu nao waje kumuona duma na kufurahi kama ninavyo furahi mimi zama hizi. Pongezi kwa sana kwa shirika linalo simamia uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini (TANAPA) kwa kazi kubwa na nzito wanao ifanya ili kusaidia uwepo wa wanyamapori hapa nchini.

…………. MWISHO……….

Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori wasiliana nami kupitia

SIMU=0714-116963/ 0765-057969/ 0785-813286

Email = swideeq.so@gmail.com

 

“I’M THE METALLIC LEGEND”.

you might also like