Hakuna sayari nyingine mbadala ya kuishi zaidi ya dunia hii, maisha tunayoishi hapa duniani ni kama vile tunataka kuikimbia dunia na tunafikiria kuna sayari nyingine bora zaidi ya kuishi. Ukweli ni kwamba Mungu aliichangua dunia hii kwa kuwa ndio inayofaa sisi kuishi na viumbe hai wengine. Hakuna sayari nyingine bora ya kuishi zaidi ya dunia hii. Hivyo basi kwa ufahamu huu, kila ambacho kinaifanya dunia hii iendelee kuwa sehemu salama ya kuishi kinatakiwa kulindwa na kusimamiwa gharama zote.

Maisha yetu hapa duniani yemefungwa katika mzunguko wa kitegemeana katika kuishi na viumbe wengine, na katika viumbe wote, binadamu pekee ndiye aliyepewa utashi wa kuelewa mfumo mzima unavyofanya kazi, na sio tu anaelewa namna mfumo unavyofanya kazi lakini pia anaelewa kuwa endapo kutatokea hitilafu kwenye mfumo huo viumbe wote watakuwa katika hatari kubwa.

Tofauti na mategemeo, binadamu angetumia utashi wake kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi kwa viumbe hai wote, mambo sasa yamekuwa tofauti na ni ishara mbaya inayoashiria jinsi tulivyoshindwa kusimamia rasilimali hizi muhimu tulizopewa na Mwenyezi Mungu.

Angalia jinsi ambavyo tulivyoharibu mazingira, tumekata miti mingi kuliko tuliyopanda na kusababisha maeneo mengi ya dunia kuwa jangwa, hivyo kupelekea vifo vya mamilioni ya viumbe hai wakubwa kwa wadogo. Utupaji wa taka hovyo umechangia kuharibika kwa udongo na kusababisha milipuko ya magojwa ambayo imeua maelfu ya watu na pia kusababisha ardhi kutofaa kwa kilimo na uzalishaji.

Usimamizi mbovu wa taka za viwandani na uchafuzi wa vyanzo vya maji umesababisha hali mbaya kwenye uso wa dunia. Samaki na viumbe wengine wa majini wamekufa na wengine kubadilika kabisa na kuwa kitu ambacho hakikutegemewa. Moshi wa viwandani na hali nyingine nyingi imesababisha uchafuzi wa hewa na pia uharibifu katika mabadiliko ya tabia nchi, hivyo kusababisha joto kuongezeka, mafuriko, ukame na majanga mengine makubwa.

Katika hali ya kukatisha tamaa namna hii, unaweza kujiuliza ni nani anahusika na kusababisha dunia kuwa kwenye hali ya majanga ya namna hii, bila shaka ni yule aliyepewa usimamizi, yaani binadamu. Kwa sababu ya kuangalia mambo kwa jicho bovu lisiloona miaka mingi ya vizazi vijavyo, tumetumia na kuharibu rasilimali tulizonazo kwa maslahi yetu binafsi na yasiyozingatia usawa na kutojali wengine, au viumbe wengine.

Leo tarehe 12 Agusti, tunapoadhimisha siku ya tembo duniani, kuna mengi yemetokea kwa tembo na ni mambo ambayo yanatuonyesha jinsi tulivyojisahau na kusababisha uharibifu mkubwa kwa viumbe hawa. Leo hii sio sawa  na miaka 50 iliyopita tukizungumzia idadi ya tembo kwenye hifadhi zetu, leo hii wanyama hawa wanazungumzwa duniani kote kuhusu haki yao ya kuishi tena, leo hii wanyama hawa wanajadiliwa kila kona ya dunia kuhusu kama kutokuwepo kwao porini kunaweza kuleta madhara yoyote; kwa kweli hapa ndipo tulikofika katika juhudi za usimamizi wa wanyamapori.

Kwa miongo michache hadi hapa tulipofikia tumeshuhudia mauaji mabaya sana ya tembo kuwahi kutokea katika historia ya dunia. Tembo wanawindwa, wanauwawa, kwa sababu ya tamaa ya pesa, utajiri, anasa, ufahari, na sababu nyingine za kitamaduni, kama dawa nk. Meno ya tembo yemekuwa na matumizi makubwa kwenye nchi za Ulaya, Asia na Marekani. Hali hii ndio imesababisha na kuchochea ujangili uliopitiliza kwenye mapori ya wanyamapori hawa.

Kutokana na utafiti uliofanyika kuhusu wanyama hawa inaonyesha idadi yao inazidi kupungua badala ya kuongezeka, viumbe hai wote wenye uwezo wa kuzaa wanatakiwa kuongezeka pale wanapoachwa wakiwa kwenye mazingira yao, lakini hali imekuwa kinyume kabisa kwa tembo, wanapungua kila siku. Ingekuwa ni jambo la busara na kujisifia kuwa tunasimamia rasilimali hizi kwa weledi pale ambapo tembo wangekuwa wanaongezeka kama tunavyoongezeka binadamu katika uso wa dunia.

Mambo mengi yalishaandikwa, tafiti nyingi zilishafanyika na zinazidi kufanyika kuhusu tembo, kampeni nyingi zimefanyika na zinaendelea kufanyika kila sehemu ya dunia. Kilio kikubwa ni kusitisha kabisa mauaji ya tembo kwasababu hakuna sababu yoyote ile inayofaa kwa wanyama hawa kuuwawa. Pia dunia imekuwa ikipaza sauti kwa nchi ambazo hufanya biashara ya meno ya tembo kusitisha zoezi hilo kwani ndio chanzo cha kuhitaji meno ya tembo.

Inatia moyo kuona juhudi hizi zikizaa matunda taratibu, sehemu kubwa sana jitihada hizi za serikali na wadau wa uhifadhi wa wanyamapori zimeanza kufanyiwa kazi. Nchi ambazo zilikuwa zinafanya biashara ya meno ya tembo sasa zimedhamiria kuacha na kufunga masoko hayo. Hatua hii imetoa ahueni kwa tembo, hasa tembo wa bara la Afrika.

Tanzania tumebarikiwa kuwa na maeneo mengi na makubwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyama hawa, tuna zaidi ya Hifadhi za Taifa 16 ambazo zina mazingira mazuri kwa wanayama hawa kuishi na kuzaana sana. Tuna Mapori ya Akiba 28 ambayo ni sehemu nyingine muhimu ambayo ina idadi kubwa ya wanyama hawa na wanyamapori wengne, tuna Mapori Tengefu 44 na pia tuna maeneo ya Hifadhi ya Jamii au kama yanavyojulikana na wengi WMAs. Maeneo haya yote ni muhimu sana kwenye uhifadhi na yanasaidia sana kukuza uchumu wa nchi na kuinua maisha ya jamii ambazo zipo kando ya maeneo haya. Kila linalowezekana linatakiwa kufanyika ili kuhakikiasha maeneo haya yanaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa jamii, ili kuboresha maisha ya watu.

Ni wakati sasa wa kufanya maamuzi magumu na sahahi kila mara ili kuhakikisha wanyamapori hawa hawawi tena kwenye hatari, tunatakiwa tuamke na kuchukua hatua, kila mtu anaweza kuchukua hatua kwenye jambo hili ili kuhakikisha ujangili unakomeshwa kabiasa, sehemu yoyote ile ulipo unaweza kusaidi kwenye jambo hili.

Kama watanzania tunaweza kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika zinazoshughulikia usimamizi wa wanyamapori hawa, pia jamii inawza kushirikia katika vita hivi kwa kutembelea hifadhi za wanyamapori mara kwa mara kama watalii, jambo hili litasaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya usimamizi na uboreshaji wa sekta hii katika nchi yetu.

Sitaweza kuandika kila kitu kwa wanyama hawa kwa sasa, lakini kwa uchache tujue kuwa endapo tutaendelea kushuhudia mauaji ya tembo na wanyamapori wengine. Tujue kabisa tutajiweka kwenye hatari mbaya sana, sio tu kwa sababu tutakuwa tumepoteza tembo, lakini pia tutakuwa tumeharibu ule mfumo wa kiikolojia ambao unafanya maisha ya viumbe hai yaendelee kuwepo, endapo tutawaua tembo, wanyama wengine pia watakufa, mimea itakufa, watu watavamia mapori hayo na kuyalima, misitu itatoweka, vyanzo vya maji vitakauka na pia kusababisha mabadiliko mabaya ya tabia nchi. Hivyo basi uwepo wa wanyama hawa sio tu utatuletea maslahi ya kiuchumi, bali kushikilia mfumo wa kiikolojia ambao ni muhimu sana kwa maisha chini ya jua kuendelea.

Nawapongeza serikali zote, mashirika ya umma na yale ya binafsi, wadau na watu wote wanaofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha jamii inaelewa faida za kimazingira na za kiuchumi za wanyama hawa, kipekee nimpongeze mratibu wa kampeni ya OKOA TEMBO WA TANZANIA ndugu Shurbet Mwarabu, anafanya kazi kubwa sana kwenye eneo hili na amekuwa mfano mzuri wa vijana ambao wanafanya kazi kubwa kusaidia uhifadhi wa wanyamapori Tanzania na Afrika.

Asante sana!

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania