Tanzania imetenga maeneo mengi sana kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa ujumla, kila upande wa nchi yetu imebarikiwa kwa kila maliasili zenye thamani kubwa sana. Kwa uzoefu kidogo nilio nao kwenye sekta hii, nimegundua bado hifadhi za taifa na maeneo mengine yaliyohifadhiwa yanahitaji watu wengi ili kuendelea kuboresha usimamizi wa rasilimali hizi muhumu kwa nchi yetu. Kuna watu wamekata tamaa na kuona nafsi zimeisha kwenye sekta hii ya maliasili. Hii sio kweli kwani kuna maeneo yanahitaji watalaamu ili kuendelea kutunza maliasili hizi.
Kuna wanafunzi wamesoma na kumaliza elimu zao za degrii au diploma au cheti na wapo tu nyumbani hawana kazi na hawataki kufanya kazi nyingine tofauti na kwenye sekta waliyosomea, makala hii inahusu wale wenye nia ya dhati ya kufanya kazi kwenye sekta hii ya wanyamapori na hawajapata fursa hiyo kwa muda mrefu baada ya kumaliza masomo yao. Leo nitakushauri namna ya kufanya ili uende ukafanye kile unachokipenda, ukiwa unasubiri ajira kwenye eneo hilo unalopenda.
- Endelea kusoma
Najua watu wengi baada ya kuhitimu masomo yao ya vyuo, huwa hawana tena utaratibu wa kuendelea kujifunza kupitia njia nyingine kwenye eneo hilo walilosomea, hawasomi tena vitabu, majarida, ripoti au tafiti nyingine zinazo husiana na walichojifunza chuoni. Wengi wakihitimu tu vyuo huanza kuhangaika kutafuta kazi na kusahau kabisa kujinoa na kupata maarifa mbali mbali ya kuwasaidia wanapoipata hiyo kazi; kuna msemo mmoja wa kingereza naupenda sana unasema, “It is better to prepare for an opportunity and not have one, than to have opportunity and not prepared” ikiwa na maana ya kwamba ni bora ukajiandaa kwa fursa ambayo huna kuliko kuwa na fursa ambayo bado hujajiandaa. Hivyo nakushauri ujielimishe na kujifunza kila siku kwenye eneo la kazi unayotaka, soma, fuatilia kwenye mitandao ya kijamii, ulizia na watafute marafiki au watu kwenye sekta hiyo na wakueleweshe na ujifunze zaidi.
- Nenda kajitolee
Nenda kajitolee kwenye kazi unayoitaka, kwa mfano kama unataka kuajiriwa na TANAPA nenda kajitolee huko, au sehemu nyingine inayofanya kazi ambazo zinazofanana na kazi unazotaka, kuna miradi mingi sana kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na maliasili hivyo sio lazima ukajitolee TANAPA ndio upate kazi TANAPA, unaweza kujitolea sehemu nyingine inayofanya kazi kama za TANAPA na ukawa na ujuzi na uzoefu mkubwa utakao kusaidia kwenye kazi ambayo unipenda kuifanya. Wakati unajitolea kufanya kazi unatakiwa ujifunze kwa nguvu na kwa juhudi kubwa sana, jifunze kwa kila unachokutana nacho huko, hata kama hawakulipi endelea kufanya kazi zako kwa uaminifu na kwa maarifa ya hali ya juu sana, uliza maswali mengi jinsi uwezavyo ili ujue mambo mengi usiyoyajua.
Ukizingatia mambo hayo utakuwa umejtengenezea bahati mwenyewe, maana utakuwa unafahamika na kujulikana na watu wengi ambao wanaweza kukuajiri au kukupa kazi ya kufanya na watakulipa kwa ujuzi na uzoefu ulioupata kwa kujitolea na kujifunza kila siku. Miradi mingi huwa wanaajiri mtu baada ya kumwona jinsi anavyofanya kazi na sio jinsi anavyoongea, ndio maana wanapenda watu wenye uzoefu angalau kidogo kwenye jambo ambalo anataka kufanyia kazi.
Nakushauri rafiki yangu unayependa kufanya kazi kwenye sekta hii ya wanyamapori au hata kwa sekta nyingine zingatia haya ili ujitengenezee bahati mwenyewe, watu watakuwa wanasema mwenzetu ana bahati ana kazi na analipwa pesa, lakini hawajui kwamba wewe ndio umejitengenezea hiyo bahati kwa kujiongeza na kufawafanyia watu kazi, wengine hawajakulipa lakini umejifunza kufanya kazi, na sasa una kazi unayoipenda.
Kumbuka hapa nazungumzia wale wenye nia na matamanio ya kufanya kazi kweneye sekta ya wanyamapori, au utalii, nk. Kwa nini nimelenga hawa kwa sababu kuna watu wamesoma kweli mambo ya wanyamapori lakini wanapenda kufanya kazi nyingine tofauti na wanyampori, mimi nazungumzia wale hasa wenye moyo wa kufanya kazi hizi, ndio wachukue hatua hizo mbili nilizoeleza hapo juu, zipo hatua nyingine nyingi lakini muhimu zaidi ni hizo mbili. Jijengee jina kwa kazi unazofanya hata kama hulipwi, jitolee kujifunza mbinu mbalimbali zitzkazosaidia kwenye usimamizi wa maliasili zetu, hasa wanyamapori.
Hivyo kama umehitimu chou na upo nyumbani, chukua maamuzi ya haraka na uondoke uende porini, ukajifunze na kusaidia uhifadhi wa wanyamapori wetu na rasilimali nyingine muhimu. Karibu sana tufanye kazi kwa pamoja, tunakusubiri porini; sisi maisha yetu na ndoto zetu ni kuona wanyamapori wetu wanaendelea kupumua na mazingira ya makazi yao yanaendelea kuwa salama kwa ajili ya sasa na kizazi kijacho. Mwisho, ondoka huko mjini uliko njoo porini, wewe ni muhifadhi!
Asante sana kwa kusoma makala hii iliyoandikwa na kuandaliwa na;
Hillary Mrosso,
Wildlife Conservationist
0742092569