Habari Rafiki unaweza kujiuliza,kulikoni mambo ya ardhi na uhifadhi wa maliasili? Ndio ni muhimu sana tukaangalia sehemu muhimu sana katika uhifadhi wa maliasili zetu kwa jicho la ndani kidogo ili tuweze kuona mbali. Uhifadhi wa wanyamapori au maliasili lazima uendane sambamba na uwepo na uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya ardhi.
Kwa mfano, asasi za kijamii, au maeneo ya hifadhi ya jamii, WMAs ambayo husimamiwa na jamii yanapatikana kutokana na jamii kukubaliana kuyatoa maeneo hayo kwa sababu yanarasilimali ambazo zinahitaji kuhifadhiwa kwa manufaa ya sasa na baadaye.
Hivyo maeneo yote ya vijiji yanatakiwa kujulikana na kufahamika kwa matumizi yake, mfano eneo la Kijiji haliwezi kuwa sawa lote, yani huwezi kukuta eneo lote la Kijiji ni makazi ya wanyamapori, au huwezi kukuta eneo lote la Kijiji ni misitu, au huwezi kukuta eneo lote la Kijiji ni kwa ajili ya kilimo, au huwezi kukuta eneo lote la Kijiji ni kwa ajili ya makazi na makaburi au maeneo ya malisho ya mifugo.
Kwa dhana hii tunatakiwa kufahamu maeneo yote ya Kijiji kuwa hayafanani, na kwa kuwa hayafanani maeneo haya yanatakiwa kuwa na matumizi tofauti tofauti, kama ni eneo lenye kufaa kwa kilimo litumike kwa kilimo na sio vinginevyo, kama ni eneo la malisho ya mifugo litumike kwa ajili hiyo, kama ni eneo la hifadhi ya wanyamapori na misitu basi litumike kwa ajili ya uhifadhi.
Kazi ya kuyaangalia na kupanga maeneo katika matumizi sahihi, inatakiwa kufanywa na watalaamu wa ardhi na udogo wakishirikiana na jamii husika. Utambuzi wa maeneo haya ni muhimu sana kwani endapo jamii itashirikishwa ipasavyo na ikaridhia katka matumizi ya maeneo hayo yaliyopangwa basi itaepusha migogoro mingi sana ambayo inatokea kwenye masuala ya ardhi.
Katika ushiriki wa jamii katika masula ya ardhi, inatakiwa kuzingatia makundi yote muhimu kwenye jamii hiyo, makundi hayo yanaweza kuwa wafugaji, wakulima, wafanyabiashra na watu wengine wote. Kwa ujumla jamii nzima inatakiwa kufahamu na kushirikishwa kikamilifu katika mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Katika utafiti wangu nilioufanya mwaka 2015 katika wilaya ya kilosa, nilibaini changamoto kubwa sana kwenye maeneo yaliyofanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Ingawa kulifanyika mipango ya matumizi bora ya ardhi na maeneo ya shughuli mbali mbali kuainishwa, bado kulikuwa na changamoto kubwa sana, pia migogoro ya chini chini iliendelea kuwepo kwasababu hakuna utekelezaji wa mpango huo wa matumizi ya ardhi.
Kilichosababisha kukosekana kwa utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi, moja ni utekelezaji wa sheria lakini pia kukosekana kwa ushirikishwaji wa makundi yote muhimu kwenye mpango huo. Kama utataka kusoma makala hiyo unaweza kuitafuta kwa kichwa cha habari hiki. Inappropriate village land use plans impede conservation efforts in Kilosa District, Tanzania.
Kwa namna yoyote ile endapo utaratibu wa kuihusisha jamii katika matumizi na mipango muhimu kama ya ardhi haiafanikiwa basi mara zote tutegemee migogoro ya mara kwa mara kwenye ardhi ambayo ina madhara ya moja kwa moja kwa uhifadhi wa maliasili na wanyamapori wetu.
Kwa tafiti nyingi zilizofanyika kuhusu ardhi na migogoro iliyopo, jambo kubwa la kufanya sasa ni kutafuta suluisho kwa maeneo yote yenye migogoro, na kutafuta namna bora kabisa ya kuisulisha migogoro hiyo kwa pamoja, na kwa pamoja jamii nzima ipendekeze njia mbadala na wakubaliane wote kuhusu njia hizo, na pia wakubaliane kuhusu matumizi ya ardhi katika Kijiji chao.
Sio kazi ndogo kufanikisha hayo yote, inahitaji muda, nguvu kazi na fedha za kutosha, lakini ni jambo ambalo linawezekana kabisa tukiamua kulifanya na jamii ikadhamiria kuitikia wito ili kuja kutatua changamoto hizo zilizopo katika ardhi. Elimu ni muhimu sana, hasa elimu ya ardhi, na hapani kuhusu sheria zote za ardhi, sheria ndogo ndogo za ardhi na kanuni zake. Watalaamu wanatakiwa kufanya kazi hiyo kutoa elimu hii kwa jamii. Hii itasaidia sana kukuza fahamu na maarifa muhimu ambayo yatasaidia kuondao au kupuguza migogoro iliyopo, au kuzuia mingine isitokee.
Naamini kwa haya macheche tumepata mwanga has kwenye eneo hili muhimu la ardhi na uifadhi wa maliasili, au uhifadhi wa wanyamapori.
Ahsante sana,
Makala hii imeandikwa na,
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania