Habari Rafiki yangu mpendwa, karibu katika makala ya leo ambayo imejikita katika kujua na kufahamu utaratibu mpya wa kutembelea hifadhi za wanyamapori. Katika makala hii nitaeleza kwa ujumla utaratibu unaofanana kwa kila hifadhi za taifa.
Kwanza kabisa, niwapongeze wasomaji wa mtandao huu wa wildlife Tanzania ambao wanasoma makala mbali mbali za uhifadhi na utalii katika blogu hii. Kwa wale ambao wemenitumia ujumbe, wengine wameshukuru kwa maarifa wanayoyapata, wengine wameuliza maswali, wengine wanipongeza kwa kazi hii ya uandishi wa makala hizi. Nawashukuru sana kwa kusoma kazi zangu, naamini zinawasaidia kufahamu baadhi ya mambo muhimu kwenye sekta hii ya maliasili na utalii.
Kati ya maswali niliyoulizwa sana na watu wengi wanaosoma makala hizi ni kutaka kufahamu utaratibu wa kuingia hifadhini, au utaratibu wa kutembelea mbuga za wanyama. Nafurahishwa sana na maswali haya kwani yanaonyesha kuwa watanzania wameamka na wanatembelea hifadhi za wanyama, na wengi wanaotaka kufahamu utaratibu huo basi huwa wanatembelea hifadhi hizo.
Tanzania imebarikiwa kuwa na maeneo mengi muhimu kwa vivutio vya utalii, maeneo hayo ni mbuga za wanyama, maeneo ya kihistoria au maeneo ya kale, fukwe za bahari, misitu asilia, milima, maporomoko ya maji na maeneo yenye tamaduni za kipekee zinazovutia watu mbali mbali.
SOMA:Hifadhi Ya Taifa Ya Arusha; Utaratibu Wa Kupanda Mlima Meru
Ukweli ni kwamba Tanzania kuna kila aina ya vivutio vyote vyenye hadhi ya kimataifa, ndio maana wageni hutoka nchi za mbali ili kuja kutembelea maeneo haya yenye vivutio hivi. Wengi wa wageni waliotebelea vivutio mbali mbali vilivyoko Tanzania huwa wanatamani kuja tena na tena, maana ni maajabu tu yaliyopo katika nchi yetu hii nzuri.
Ni vigumu sana kuelezea kila kivutio kilichopo hapa Tanzania kwa ufasaha wake, maana ni vingi na vinashangaza sana. Kuna vitu vingi sana ambavyo ukiviona unaweza kusema hii sio Tanzania. Ndio maana nawahimiza na kuwaandikia watanzania kuwa, njia nzuri ya kufahamu haya yote ni kupanga kutembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine ya vivutio.
Katika makala hii nimejikita kuelezea utaratibu wa kutembelea hifadhi au mbuga za wanyama. Tanzania ina maeneo mengi sana yaliyohifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori. Maeneo haya yametengwa kulingana na vipaumbele katika uhifadhi wake na pia kulingana na kiasi cha rasilimali zilizopo ambazo zinahitaji uhifadhi wa kipekee.
SOMA:Gharama Na Tozo Mbali Mbali Za Kutalii Katika Hifadhi Ya Taifa Ya Arusha
Hivyo basi maeneo mengi yaliyohifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori huwa ndio kivutio kikuu cha wageni kutaka kutembelea maeneo haya. Kwa mfano kuna maeneo yanaitwa hifadhi za taifa, kuna maeneo yanaoitwa mapori ya akiba, kuna maeneo yanaitwa mapori tengefu, kuna maeneo yanaitwa hifadhi ya jamii au WMAs. Maeneo yote haya ni muhimu sana kwa uhifadhi wa wanyamapori, hivyo yapo chini ya usimamizi wa serikali na mamlaka za wanyamapori.
Maeneo ya hifadhi za taifa yanaonekana kuwa na mvuto mkubwa sana kwa wageni, kwasababu ya uhifadhi wake, na usimamizi makini na pia maeneo ya hifadhi za taifa hawaruhusu shughuli zozote za uwindaji wa wanyamapori. Hivyo hali hii hupelekea maeneo haya kuwa na wanyamapori wengi na pia kubakia katika uasili wake.
SOMA :Hifadhi ya taifa ya Arusha
Tanzania kuna hifadhi za taifa 16, ambazo husimamiwa na shirika la uma linaloitwa TANAPA, TANAPA ndio husimamia hifadhi zote za taifa, na ndani ya TANAPA kuna idara nyingi sana ambazo zina majukumu muhimu sana, kwa mfano kuna idara ya ikolojia, idara ya utalii, idara ya ulinzi nk.
SOMA:Hifadhi Ya Taifa Ya Arusha; Utaratibu Wa Kupanda Mlima Meru
Kwa ufahamu zaidi, hizi ndio hifadhi za taifa ambazo husimamiwa na TANAPA;
Hifadhi ya Taifa ya Arusha,
hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara,
hifadhi ya taifa ya Katavi,
Hifadhi ya Taifa ya Saanane,
hifadhi ya Taifa ya Mikumi,
hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro,
hifadhi ya Taifa ya Mkomazi,
hifadhi ya Taifa ya Ziwa Rubondo,
hifadhi ya Taifa ya Tarangire,
hifadhi ya Taifa ya Mlima Uduzungwa,
hifadhi ya Taifa ya Gombe,
hifadhi ya Taifa ya saadani,
hifadhi ya Taifa ya Ruaha,
hifadhi ya Taifa ya Serengeti,
hifadhi ya Taifa ya Kitulo.
Hizo ndio hifadhi za taifa, lakini kwa hivi karibuni waziri wa maliasili na utalii alitangza kuongeza hifadhi nyingine 4 ili kuinua utalii kanda ya ziwa. Pamoja na hayo kuna eneo jingine muhimu sana kwa utalii lakini linatofautiana na hifadhi za taifa, hii ni Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro ambalo ni eneo ambalo husimamiwa na malaka ya Ngorongoro na wanajitegemea kila kitu, eneo hili linavutia sana watalii na linaongoza kwa kuwa na watalii wengi sana.
Sasa tujue utaratibu upoje kuingia hifadhini, au kutembelea hifadhini, na hapa tutaangalia watanzania ambao wanataka kujua utaratibu wa kutembelea hifadhi za taifa au mbuga za wanyama. Ifahamike kwamba huu ni utaratibu mpya kidogo sio sawa na miaka ya nyuma (kabla ya mwaka 2015), mambo yamebadilika ili kuendana na sheria mbali mbali za nchi, hasa za utawala, usimamizi na ukusanyaji wa mapato.
Gharama Na Tozo Mbali Mbali Za Kutalii Katika Hifadhi Ya Taifa Ya Arusha
Gharama za kiingilio!
Kwa hifadhi nyingi za taifa ukiachilia hifadhi za Kaskazini gharama ya kiingilio kwa mtu mmoja ni shilingi 5,000 kwa mtu mzima, watoto ni shilingi 2,000.
Kwa hifadhi za Kaskazini gharama za kiingilio kwa watanzania ni shilingi 10,000 kwa mtu mzima na shilingi 5,000 kwa watoto.
Gharma ya kiingilio cha magari
Gharama ya gari dogo lenye tani 1 hdai 2 ni shilingi 20,000
Kwa ghari yenye tani 3 na kuendelea ni shilingi 35,000
Namna ya ufanya malipo
Utaratibu wa zamani wa malipo ulikuwa ni kupokea fedha taslimu mkononi lakini sasa utaratibu huo haupo. Hakuna atakayepokea fedha mkononi unapofika getini au sehemu ya kufanyia malipo ya kuingia ndani ya hifadhi.
Hivyo basi utaratibu ambao hutumika sasa ni kulipia kwa njia ya kieletronic, ambapo unatakiwa kuwa na kadi ya benki ambayo ni VISA CARD, au MASTER CARD. Hivyo ukifika eneo la malipo hapo gitini unachotakiwa kutoa sio hela, ni kadi ya benk, na hapo watakata gharama zote kisha wanakupa kadi yako na risiti ikionyesha malipo na michanganuo mingine.
Pia ikumbukwe kuwa gharama zote za kiingilio ni pamoja na VAT ambayo ni asilimia 18 kwenye kila malipo hapo juu.
Usafiri
Hapo kwenye gahrama za usafiri zimegawanyika sehemu 2, moja ni kama una gari lako mwenyewe unaweza kuepuka gharama za usafiri na utalipia tu kulingana na uzito wa gari lako. Njia ya pili ni kama umetumia magari ya kukodi au magari ya kitalii nao wanagharama zao watakazo kutoza, hivyo kama utakuja kutalii na gari lako mwenyewe au gari la kukodi inabidi ujipange ili ujue gharama zipoje kwenye kila eneo ili uweze kufurahia safari yako ya kutembelea mbuga za wanyama.
Naamini kati ya mengi haya machache yanaweza kukupa mwanga ili ujue namna ya kujipanga kutembelea hifadhi za wanyamapori. Ukweli ni kwamba unahitaji maandalizi mazuri kama unataka kutembelea mbuga za wanyama. Maandlizi mazuri yaendane na kufahamu maeneo unayotaka kuyatembelea, kama unataka kutembelea hifadhi ya Mikumi au hifadhi nyingine yoyote kitu cha kwanza muhimu kujua ni hifadhi unayotaka kwenda kutembelea, utaratibu, na hapa kwenye utaratibu unapaswa kufahamu gharama halisi kabisa ili usisumbuke kutoa toa hela bila sababu za msingi.
Karibu sana mbugani, karibu tutalii kwenye hifadhi zetu wenyewe. Kwa maoni na ushauri tuwasiliane kwa mawasiliano hapo chini.
Asante sana!
Hillary Mrosso
+255 683 862 481