Baada ya kuandikia makala ya jana yenye kichwa cha habari, “Wanafunzi Wanaotaka Kufanya Kazi Kwenye Sekta Ya Wanyamapori Na Hawajapata Hiyo Fursa, Soma Hapa kuna Mambo Muhimu Kwako” kuna baadhi ya watu wamenipigia simu na wengine wamenitumia ujumbe kuniuliza kwamba sio kwamba hawapendi kufanya kazi za wanyamapori bali wanakosa mtu wa kuwashika mkono au kwa lugha ya kingereza tunasema wamekosa “networks”, yani wanakosa mfumo wa kuwasaidia na wenyewe waingie kwenye ajira na kazi wanazozipenda. Kwenye makala hii nimeelezea mambo matano muhimu yatakayokusaidia ili uajiriwe au upate kazi mapema sehemu yoyote ile na kwenye sekta yoyote ile.
1.Tengeneza marafiki
Hapa kwenye kutengeneza marafiki ni lazima ujue na kuchuja sana marafiki unaotaka kuwa nao, kwa mfano wewe umesoma au unasoma mambo ya wanyamapori, na una ndoto za kufanya kazi kwenye sekta hiyo ya wanyamapori au sekta nyingine inayoendana na hiyo kama vile utalii, au kuongoza wageni hifadhini lazima ujifunze na kuwa karibu na watu ambao wana ndoto kama zako za kufanya kazi hizo, angalia kwa makini marafiki zako unaokuwa nao muda mwingi, hasa unapokuwa chuoni au sehemu nyingine kama wana ndoto kama zako mnaweza kuendelea kupeana mawazo jinsi ya kuzifikia ndoto zenu. Epuka kufanya urafiki ambao unakupotezea muda na hauna mchngo wowote kwenye ndoto zako. Mfano unamkuta mtu ni anasomea wanyamapori na muda mwingi unamkuta yupo na watu wanaosomea food nutrition, au food science na hao ndio wanakuwa marafiki zake wakuu. Sio vibaya kuwa na rafiki wa food nutrion au kozi nyinge yoyote ila lenga kujenga mahusiano na urafiki na watu wenye ndoto kama zako. Kwa vyuoni kuna watu wametoka kazini na wapo wanakuja kusoma chuo, jifunze kuwa nao karibu ili ujifunze kutoka kwao na pia kutengeneza hiyo network.
- Jifunze zaidi ya notes za shule
Unapojifunza wakati wote usijifungie na vinotes vya mwalimu wako, nenda nje kajifunze vizuri jinsi kinavyofanyika na kutekelezeka, kama umesoma wanyamapori nenda kwenye mafunzo kwa vitendo, nenda kajifunze uongozi unakuaje kwa wafanyakazi, jifunze wanavyoandika ripoti za kitalaamu, nenda zaidi ya mazoezi ya daraani, mfano mnapofunga chou wenzako wakienda nyumbani wewe tafuta sehemu ya kwenda kujitolea, waulize wale waliotoka kazini watakupa utaratibu jinsi ya kufanya, maana wengi wa wafanyakazi wanaosoma wanapofunga chuo hurudi kazini, omba uende nao wanaporudi kazini, ukajitolee upate maarifa na uzoefu kwenye hiyo kazi unayoitaka kufanya na pia utajenga jina lako kupitia unachokifanya jitengenezee network mapema zaidi na kujifunza mambo mengi na maisha ya kazini yalivyo. Kama unasoma utalii fanya hivyo, inalipa sana
- Kwa wanafunzi
Maisha ya chuo huwa yanakuwa na mambo mengi, na kila mtu anakuja kusoma kwa malengo tofauti tofauti hata kama mnasoma kozi moja, hivyo unapokuwa chuoni, hapa naongea na wanafunzi, jifunze kujua unataka nini, na unaposoma hiyo kozi unategemea nini baada ya kumaliza, jua mapema kabisa unataka nini ili uchukue hatua stahiki za kukupeleka kwenye unachotaka. Usisome some tuu rafiki, uanaamka unaingia darasani na kutoka, jifunze zaidi ya hapo. Angalia sana walimu wanaokufundisha jenga urafiki nao, sio kitu kibaya, waulize maswali ya hatima yako baada ya kusoma kozi yako, waombe ushauri. Na hapa chagua mwalimu mmoja anaweza kuwa profesa, au mwenye shahada ya uzamivu, au mwenye Mastars awe mshauri wako kwenye mambo ya kielimu na ya kimaisha. Hapo napo ni sehemu ya kuchagua vizuri kulingana na jinsi huyo mwalimu anavyofanya kazi zake, fanya kile kinachokuvutia kutoaka kwa mwalimu wako. Unaweza kukuta huyo mwalimu anandika sana makala (articles) za kitalamu, au ana miradi mbali mbali, kaa chini yake ujifunze zaidi, mwambie jinsi unavyoweza kumsadia hata kukusanya taarifa (data) kwenye utafiti anaoufanya, hii itakufanya muwe karibu na utatengeneza network yako mapema kabisa. Usiishi maisha ya chuoni kama mtu ambaye hajitambui, usiishi kivyako vyako tu; yani we wa kusoma kula na kulala, labda na kuangalia series za kikorea. Jiongeze.
- Jiunge na klabu mbali mbali
Popote pale ulipo, lazima utakuta mtu au watu wanafanya kitu kinachofanana au kuendana na kile unachopenda kufanya kwenye maisha yako. Kwa wanafunzi wa chuo hii ipo sana, unakuta chuoni kuna klabu mbali mbali zinaweza kuwa za mazingira, kuzuia rushwa, UKIMWI, afya nk. Sasa kuna watu hasa baadhi ya wanachuo wanadharau sana hizi klabu kwa vile haziwalipi sijui! Ila hawajui kuwa ni sehemu nzuri ya kujenga na kukuza kile wanacho kisomea na network kwenye eneo ambalo ungependa kufanyia kazi. Kwa mfano kwa wale waliosoma au wanaosoma SUA, Sokoine University of Agriculture, au Chuo Kikuu Cha Kilimo Cha Sokoine kuna klabu moja maarufu sana inaitwa WISASUA, haaah, naipenda sana hii klabu, maana inawahusu wanafunzi wote wanaosoma shahada ya usimamizi wa wanyamapori (Wildlife Management). WISASUA ni kifupi cha ” Wildlife Student Association of Sokoine University of Agriculture”. Nakiri mimi nilikuwa ni mwanachama mzuri sana wa klabu hii, na ndio iliyonisaidia kuona mambo mengi ya uhifadhi wa wanyampori kwa jicho la kipekee sana. Kwenye klabu kama hizi kuna fursa nyingi ambazo nimeona zinapatikana, kama vile kutembele hifadhi, kujifunza mafunzo mbali mbali ya uhifadhi wa wanyamapori na hali ilivyo, maswala ya utalii, maswala ya migogoro ya kijamii na watu wanaoishi karibu na hifadhi, ni mengi sana ya kujifunza kupitia klabu hizi, mbali na hayo watalamu kutoka hifadhi za taifa na mashirika mbali mbali huja kutoa mafunzo kwa wanachama wa WSASUA.
Kwa chuo chochote unachosoma, angalia klabu inayoendana na yale unayofanya, ingia huko kwa miguu yote miwili, jifunze kila kitu, hata kama ni uongozi chukua fomu jaza nenda kajifunze. Kaa na watu wenye maono na ndoto kama zako utaona milango mingi ya fursa ikifunguka mbele yako. Lakini wewe ukiendelea kujifanya mjuaji na kukataa kushirikiana na wenzako kwenye mambo ya msingi yanayokuhusu, utashangaa wenzako wakipanda basi, wewe ukiwa huna hata tiketi na unataka kupanda basi, itakuwa ni ngumu sana kwako. Jifunze na wanaojifunza, nenda na wanao enda. Hata kama upo mtaani umemaliza chuo na huja ajiriwa acha kukaa nyumbani peke yako, nenda kaungane na wenzio wanoafanya unachotaka kufanya.
- Fursa kwenye Internet
Kwa ulimwengu tulio nao sasa kila kitu unachotaka kujua kipo kwenye intenet na mitandao ya kijamii. Epuka kabisa kutumia mitandao wa internet na mitandao mingine ya kijamii bila manufaa. Kwenye mitandao hii unaweza kupata taarifa mbali mbali unazohitaji ili kuboresha maisha yako na kazi yako. Hivyo kuwa na vitu unavyotafuta vyenye manufaa kwako, mfano unataka kujua kuhusu kampuni fulani, uncho hitaji hapo ni jina la kampuni au shirika fulani utalikuta lipo kwenye mtandao na taarifa zao zote muhimu unazopaswa kuzijua kuhusu hiyo kampuni, wewe unaingia google unatafuta ili kupata maarifa au nafasi za kazi kwenye kampuni husika. Hivyo jua kwamba makampuni na mashirika yote hupenda kuweka taarifa zao kwenye mitandao ya kijamii. Mfano wa mimi mwenyewe kazi ninayofanya sasa ni kwa sababu nilitafuta hii kazi kwenye internet, nikaona nikaomba kama kujitolea mara tu baada ya kumaliza chuo, sikusubiri watangaze kazi niliomba kabla ya kazi kutangazwa. Kwa mfano mwingine uandishi huu wa makala na blog niliyofungua sikuwahi kuonana ana kwa ana na mtu ndio anipe mafunzo haya jinsi ya kuandika na kuendesha blog, hii yote ni fursa ambazo zipo kwenye mitndao ya kijamii. Unajua kwamba kazi unayoitafuta ipo kwenye kifaa ulichoshka mkononi mwako, simu yako; tumia kwa manufaa yako.
Hivyo rafiki yangu, popote pale ulipo unaweza kutengeneza jina ambalo halitasahaulika kwa ushiriki wako kwenye mambo mbali mbali yanayoendana na kile unachopenda kufanya kwenye maisha yako, hata kama hawakulipi we fanya tu, we nenda tu, jitoe sadaka wewe mwenyewe kwenye kile unachoamini unatakiwa kukifanya. Kwa wanachuo tumieni vizuri muda wenu mnapokuwa chuoni kujenga misingi mizuri ya maisha baada ya chuo. Tumia kila nafasi unayoipata hapo chuoni kuyaweka maisha yako ya baadaye sehemu salama, sehemu ya ndoto zako, sehemu ambayo upo tayari kufanya kazi bila hata kuambiwa. Acha kuiga maisha ya watu wengine, ishi maisha ya ndoto zako ishi maono yako.
Karibuni sana porini!
Asante sana kwa kusoma makala hii iliyoandikwa na kuandaliwa na
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569