Matumizi yaliyopitiliza ya wanyamapori ndio moja ya kichocheo kikubwa cha kupotea kwa bayoanuai katika nyakati hizi. Na matumizi haya yanajumuisha biashara ya wanyamapori iliyohalali na ile isiyo halali ambayo kwa kiasi kikubwa inasimamiwa na kanuni za Makubaliano ya Kimataifa ya Biashara za Spishi za Wanyama na Mimea Mwitu ambayo ipo hatarini kutoweka, kwa kingereza inajulikana kama, Convention on International Trade in Endangered Species of Wild Fauna and Flora (CITES).

Kwa vyoyote vile biashara haramu ya wanyamapori na mimea ni matumizi yasiyo endelevu ya maliasili na ina madhara mabaya katika uhifadhi wa spishi hizi za wanyama na mimea. Pia inakadiriwa kuwa ni moja ya biashara haramu zenye manufaa na faida kubwa kwa wanaozifanya ikiwa sambamba na biashara nyingine haramu ya madawa ya kulevya, biashara haramu ya binadamu, biashara haramu ya silaha ambazo hufanyika kwa umahiri mkubwa ambao hujumuisha mitandao ya watu wengi ambao ni ngumu kuielewa.

Kakakuona au kama anavyofahamika kwa lugha ya kingereza” pangolin” ni moja ya wanyamapori ambao wanaongoza duniani kwa usafirishaji haramu, inakadiriwa zaidi ya kakakuona milioni moja wameshasafirishwa kutoka katika maeneo yao ya asili katika miaka ya 2000-2013.

Mnyama huyu ameingia katika orodha ya wanyama wenye matumizi makubwa sana kwa baadhi ya nchi duniani,sehemu za mwili wake hutumika katika matumizi mbali mbali, kwa mfano magamba ya mwili wake hutumika kama dawa za asili na pia hutumika kama mapambo, nyama ya kakakuona hutumika kama chakula cha watu wa hadhi ya juu sana yani (luxury food) kwa matajiri na pia kwa watu wa kawaida hutumika kama nyama za kwaida kwa ajili ya kuongeza virutubisho vya protini mwilini, ngozi ya mwili wa kakakuona hutumika kutengenezea nguo na mavazi ya kifahari.

Ilikuwa inaaminika kuwa biashara haramu ya kakakuona imekuwa ikichochewa na mahitaji makubwa kutoka katika mataifa makubwa ya Asia hasa China na Vietnam. Lakini utafiti unaonyesha biashara hii pia imeshamiri kwenye nchi nyingine duniani kama vile Marekani, nchi za Ulaya na Japani.

Kupungua kwa idadi ya kakakuona wa Asia kumepelekea kuwepo kwa ushahidi wa kukua na kuendelea kwa biashara haramu inayovuka mipaka ya kimabara, na sasa macho na nguvu kubwa imeelekezwa katika bara la Afrika ambapo wanyama hawa husafirishwa kutoka katika mataifa ya bara la Afrika kwenda kwenye masoko makuu ya biashara hii katika bara la Asia. Pia taarifa za kitafiti zilizoripotiwa na CITES zinaonyesha kuongezeka kwa biashara halali ya kakakuona baada ya miaka ya 2000, hasa kwa kakakuona wa Afrika.

Rafiki msomaji wa makala hii, kuna mengi ya kujifunza kwa pamoja katika ripoti hii muhimu iliyotoka mwishoni mwa mwaka, yani Desimba  2017 yenye kichwa cha habari THE GLOBAL TRAFFICKING OF PANGOLINS (biashara haramu ya usafirishaji wa kakakuona duniani), hii ni ripoti iliyoandaliwa na jopo la watulaamu makini wa masula haya ya usafirishaji wa wanyampori,  Sarah Heinric na wenzake ndio waandishi wa ripoti hii, katika ripoti hii wameonyesha kwa ufupi (summary) biashara ya kakakuona, njia za zinazotumika katika usafirishaji wake na pia vituo au maeneo ambayo bidhaa au kakakuona hufikia.

Kwa utangulizi hapo juu sasa unaweza kujua tunazungumzia nini katika makala yetu ya leo kwenye uhifadhi wa wanyamapori, bila shaka utakuwa umesikia au umeona au inawezekana pia hufahamu mnyama huyu maarufu anayeitwa KAKAKUONA, kwa kingereza anajulikana kama Pangolin. Ni mnyama ambaye haonekani kwa urahisi, unaweza ukaishi maisha yako yote porini na usifanikiwe kumuona kakakuona, lakini amekuwa anatajwa sana katika biashara haramu za wanyamapori, tumezoea kusikia biashara haramu ya meno ya tembo na pembe za faru, sasa leo mnyama mwingine ameingia kwenye orodha ya wanyama ambao wanasakwa kwa udi na uvumba kutokana na matumizi yake katika baadhi ya mataifa ya Asia na Marekani, pia baadhi ya nchi za Ulaya.

Wakati nasoma ripoti hii nilitamani kuandika kila kitu, kwasababu kuna mengi ya kujifunza na kuyafahamu kama wahifadhi na jamii kwa ujumla. Hivyo uchambuzi huu ni baadhi tu ya mambo niliyoyaona ni muhimu zaidi kuyafahamu ili kwa pamoja tujenge ufahamu wetu na tujue kinachojiri kwenye sekta hii muhimu ya wanyamapori, pia naamini kwa kupata maarifa haya tutakuwa na mipango mizuri ya kuimarisha uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori hawa adimu kaitika hifadhi zetu.

Katika ripoti hii imewataja spishi zote 8 za kakakuona, nne zikitokea katika bara la Asia na nyingine nne zikitoka katika bara la Afrika. Hapa nitazitaja zote pamoja na majina yake ya kisayansi. Pia kakakuona wote wameainishwa na shirika la kimataifa la ICUN kama spishi ambazo zimo katika hatari ya kutoweka kabisa duniani.

Kwa spishi za kakakuona wa Afrika hawapo katika hatari kubwa sana kama kakakuona wa Asia. Kakakuona wa Afrika wapo wane ambao ni;

Giant Pangolin Manis gigantea (Waterman et al., 2014a);

Ground Pangolin M. temminckii (Pietersen et al., 2014a);

Black-bellied Pangolin M. tetradactyla (Waterman et al., 2014b);

White-bellied Pangolin M. tricuspis (Waterman et al., 2014c)),

Kwa kakakuona wa bara la Asia, hawa ndio wapo kwenye hatari kubwa sana ya kutoweka kabisa katika uso wa dunia, hii ni kutokana na kuwindwa sana na kwasababu nchi nyingi za Asia hujuhusisha na matumizi na biashara za kakakuona hao, hivyo hawa ndio spishi za kakakuona wa Asia waliopo katika hatari kubwa ya kutoweka duniani;

Chinese Pangolin M. pentadactyla (Challender et al., 2014b);

Sunda Pangolin, M. javanica (Challender et al., 2014c))

Philippine Pangolin M. culionensis (Lagrada et al., 2014);

Indian Pangolin M. crassicaudata (Baillie et al., 2014)).

Kutokana na hali hiyo kakakuona wamehamishwa na CITES kutoka appendex II na kuwaweka katika Appendex I, hii imefanyika ili kuongeza uhifadhi wa wanyama hawa lakini pia kuzuia biashara za kimataifa za kakakuona. Kwa mujibu wa CITES, spishi za wanayampori na mimea mwitu ambayo imeorodheshwa au ipo kwenye appendexi I, hairuhusiwi kuuzwa kabisa, na hii ni kutokana na makubaliano ya nchi wanachama wote wa CITES ambao walikubaliana na kusaini makubaliano hayo ili kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori na mimea ambayo ipo hatarini kutoweka.

Ili kupata taarifa za kuandika ripoti hii, njia mbali mbali zilitumika kubwa iliyotumika kupata taarifa ilikuwa ni ukamataji wa bidhaa, sehemu za miili ya kakakuona au kukakuona mzima. Taarifa za ukamataji tangu mwaka 2010- 2015 zinaonyesha zaidi ya matukio 1270 ya ukamataji wa nyara za kakakuona. Taarifa kutoka katika ripoti mbali mbali zilizomo katika mitandao, taarifa za wazi zinazopatikana katika website ya CITES, ambapo inaonyesha vituo 179 vya CITES katika maeneo mbali mbali duniani zilitoa taarifa zao.

Taarifa za ukamataji zilionyesha sehemu na tarehe ya kukatama, spishi na vitu vilivyomo na kiasi, pia zilionyesha njia za usafirishaji zilizotumika au zinazotumika, na vile vile vilionyesha taarifa ya njia (trade route information), ikiwa ni pamoja na sehemu ilikotoka, sehemu zitakazopita, na nchi zinakokwenda au zinapoishia.

Ingawa kuna udhaifu kutegemea aina hizi taarifa katika kufanya utafiti, kutokana na ukweli kwamba mamlaka za ukamataji zinaweza zikashawishiwa kwa namna moja ama nyingine kutokana na kuhusishwa kwa rushwa, ukosefu wa uelewa na mambo mengine yanweza kuchangia katika kufanya taarifa zilizopatikana kwa ukamataji kutokuwa za kutegemewa sana. Lakini pamoja na yote hayo, taarifa zilizotumika hapa ni sehemu tu ya taarifa zote za ukamataji wa usafirishaji wa kakakuona kwa njia haramu.

Kazi yote hii ya kandika ripoti imefanyika ikiwa na lengo na makusudi makubwa ikiwa ni pamoja na kubaini njia zote zinazotumiwa kusafirishia nyara hizo, na pia kujua sehemu ambazo kakakuona wanatoka, yani nchi ambazo zimekuwa zikitoa kakakuona na kusafirisha kwenda sehemu nyingine au nchi nyingine. Taarifa hizi ni muhimu sana kwasababu zitatusaidia kujua sehemu ambayo ina mahitaji au uhitaji mkubwa wa wanyama hawa. Kwa kufahamu hayo itakuwa ni moja ya jambo muhimu sana katika kufanya maamuzi, usimamizi na kuchukua hatua stahiki katika juhudi za uhifadhi wa wanyamapori.

Na pia ingawa kumekuwa na ongezeko la kushamiri kwa biashara haramu za wanyamapori na mimea mwitu, hakuna taarifa za kutosha zinazoweza kutupa namna ya kuanza kuchukua hatua muhimu za kukabiliana na changamoto iliyopo katika biashara hii haramu ya wanyamapori hasa kakakuona, hivyo basi ripoti hii ina taarifa ni muhimu sana kwa ajili yetu.

Kwenye ripoti hii mwandishi amechambua namna mbali mbali ambazo kakakuona husafirishwa, anaweza kusafirihwa akiwa mzima au akiwa amekufa, sehemu au viungo mbali mbali vya mwili wake pia husafirishwa kwa mfano, magamba yake, ngozi, kucha, miguu, na bidhaa mbali mbali ambazo hutumika kama dawa, pia viungo au sehemu nyingi za kakakuona hushindwa kujulikana nazo husafirishwa kwenda sehemu zinapo hitajika.

Kumekuwa na njia kadhaa ambazo hutumika kusafirishia biadha za kakakuona, kwa njia ya anga na hapa hutumia ndege, kwa njia ya maji na hapa hutumia meli, boti au mitumbwi, kwa njia ya nchi kavu au ardhini au barabara na hapa hutumia magari, kwa mguu, pikipiki nk.

Ili kuelewa uzito wa mambo haya taarifa zilizopo kwenye ripoti zinaonyesha kiasi kikubwa sana kikikamatwa kwenye maeneo mbali mbali duniani kwa mfano Novemba mwaka 2012 kiasi cha tani 8.5 cha kakakuona waliokufa pamoja na magamba yake yenye uzani wa kilo 350 zilikamatwa katika jiji la Jakarta Idonesia;

September mwaka 2015 kiasi cha tani 11.5 kilikamatwa ambacho kilikuwa ni mizoga ya kakakuona iliyokuwa imefichwa katika maboksi ya kuhifadhia vitu baridi katika jimbo la Gaungdog nchini China.

Pia kuna taarifa za kiasi kinachokadiriwa kuwa ni zaidi ya tani 10 ya kakakuona waliokuwa wamekufa walikamatwa Aprili 2013 ndani ya boti iliyokuwa inapita chini ya matumbawe (corol reefs) katika visiwa vya Palawan nchini Uphilipino, ikiwa ni kiasi kikubwa sana kuwahi kukamatwa na kushikiliwa katika kipindi chote cha utafiti huu.

Hata hivyo taarifa za kina zinaonyesha kukamatwa kwa kiasi cha tani 7.5 ya nyama ya kakakuona pamoja na magamba ya kakakuona yakiwa na uzani wa kilo 64.6 yalishikiliwa yakiwa yanaelekea nchini Vietnam, pia kuna ushahidi unaonyesha kushikiliwa kwa kiasi cha dawa 3000 na kisichojulikana Marekani ikiwa inatokea Vietnam.

Hivyo vyote inaonyesha jinsi ambavyo wanyamapori hawa adimu wanavyovunwa kwa kiwango cha juu sana. Hizi ni taarifa tu zilizobainika kwa kukamatwa na mamlaka mbali mbali zinazosimamia mienendo ya biashara haramu duniani. Lakini kwa vyovyote vile hali hii ni zaidi ya matumizi mabaya sana ya wanyamapori, wanyamapori hawa ambao wamekuwa na matumizi makubwa kwa nchi za Asia na Marekani imepelekea kupungua kabisa kwa wanyama hawa hali ambayo inatishia kabisa kutoweka kwa wanyamapori hawa muhimu katika uso wa dunia.

Katika ripoti hii pia tumeshirikishwa nchi 10 vinara zinazohusika na biashara hii haramu ya kakakuona, hii ni kwa mujibu wa matukio ya ukamataji yaliyotokea kwenye nchi hizo. Hivyo nchi hizi vinara wa biashara hii haramu zimakua zikitokea mara kwa mara kwenye kujihusisha katika biashara hii haramu, hivyo basi idadi ya ukamataji wa nyara hizo ndio unaonyesha ni kwa jinsi gani biashara hii imeshamiri katika nchi hizo, tutaanza na nchi ya kwanza hadi ya mwsho.

China 342, Marekani 127, Vietnam 90, Malasiya 60, Hong Kong RSA 57, Thailand 56, LAO PDR 44, Nigeria 41, Indonesia 40 na Ujerumani 38. Hii ni nchi na namba za matukio ya ukamataji wa usafirishaji haramu wa biadhaa na sehemu za kakakuona.

Kwa utafiti inaonyesha kabisa ni jinsi gani nchi ya China ilivyo juu sana katika matumizi ya wanyamapori hawa ikifuatiwa na Marekani. Hata hivyo hizo ni nchi 10 tu ambazo ni vinara katika biashara hii haramu, ripoti hii inataja pia nchi nyingine kama Uganda, Kameruni, Myanmar, India, Uphilipino, Singapore, Pakistani na Uholanzi zinahusika sana katika biashara hii haramu ya kakakuona.

Utafiti pia unaonyesha kuwa nchi za Afrika zimekuwa ndio sehemu kuu zinapotokea bidhaa za kakakuona, Afrika imekuwa ndio muhusika mkuu wa kutoa malighafi za kakakuona kwenda katika nchi za Asia, nchi za Afrika ambazo ni vinara na zimetajwa kuhusika sana kama kitovu au chanzo cha upatikanaji wa kakakuona ni, Nigeria, Kameruni, Guinea, Liberia, Guinea ya Ikweta, Ivory costi, Kenya, Ethiopia, Mozambique, Uganda na Togo.

Kwa nchi za Asia ambazo zinahusika sana kama chanzo cha kakakuona ni China, Vietnam, Indonesia, Hong Kong SAR, Malaysia, India, Thailand, na Myanmar. Lakini pia kuna nchi ambazo sehemu ambazo malighafi na nyara zote kakakuona hufikia ni China, Viet Nam, Malaysia, and Thailand pia nchi za Lao PDR, Thailand, Viet Nam, and Myanmar zimekuwa na usafirishaji mkubwa wa ndani ya nchi wa nyara hizi za kakakuona.

NJIA ZA USAFIRISHAJI

Zaidi ya njia za kipekee za kimataifa 159 zimegunduliwa na ripoti hii, na kati ya hizo njia 29 zimekuwa zikitumika sana hata katika kipindi cha uandaaji wa ripoti hii

Ulaya imekuwa ndio kitovu cha usafirishaji wa biashara haramu ya kakakuona kutoka kutoka Afrika kwenda sehemu nyingine duniani kama vile China na nchi nyingine za Asia. Nchi ya Uholanzi na Switziland ndizo ambazo hupokea bidhaa za kakakuona na kuziuza katika masoko yake ya ndani, hivyo ni nchi ambazo hazisambazi au kusafirisha nyara za wanyamapori hawa.

Nyara za kakakuona kutoka Afrika husafirishwa hadi nchi za Ulaya, na nchi za Ulaya huzisafirisha hadi nchi za Asia kama vile China na Vietnam. Kwa hiyo Ulaya ndio inapokea shehena kubwa sana ya wanyamapori na nyara kutoka Afrika kwa ajili ya kuzisafirisha kwenda katika nchi zenye uhitaji mkubwa wa nyara hizi za kakakuona.

Pia kuna utabiri unaohusisha nchi za Uarabuni kujihusisha na biashara haramu ya kakakuona, hii ni kwasababu watafiti wanaona kuwa sehemu pekee ambayo itakuwa na malighafi nyingi za kusafirisha wanyamapori hawa kwenda nchi za Ulaya na Asia kupitia Uarabuni ni kubwa. Nchi za Uarabuni zimepakana na nchi za Afrika na pia kwasababu ya njia rahisi za usafiri zilizopo zitasaidia sana katika kushamiri kwa biashara hii haramu kwenye nchi hizi za mashariki ya kati.

Aidha taarifa za kina zinaitaja nchi ya China kuwa ndio kinara na muhusika mkuu wa kushamiri kwa biashara ya kakakuona kutokana na matumizi mbali mbali kama vile chakula, mapambo na kwa matumizi ya dawa. Hali kadhalika kuna ushahidi kuwa matumizi ya kakakuona kama sehemu ya utamaduni wao unaanzia mbali sana kwenye karne ya 16. Hivyo biashara ya kakakuona imeshamiri sana na pia kuna masoko na maduka yanayofanya biashara hii kihalali kwa miaka mingi. Hii ndio hali inayopelekea kuendelea kupugua kwa wanyamapori hawa kila kona ya dunia.

Kwa upande mwingine Marekani imekuwa ikihusika kwa kiasi kikubwa katika biashara hii haramu ya kakakuona, taarifa za matukio ya kukamatwa kwa nyara mbali mbali za kakakuona kama vile, magamba, na viungo vya kakakuona zimeonekana sana, labda hii ni kutokana na nguvu kubwa ya uthibiti na ukaguzi katika sehemu zote zenye njia za uasafirshaji wa nyara za wanyama hawa nchini Marekani.

Hata hivyo kutajwa sana kwa Marekani katika kuhusika na matumizi ya nyara za kakakuona inaweza kuwa ni kwa sababu za kibiashara na za kihistoria ambapo nchi za Asia zilikuwa zinasafirisha kakakuona wa Asia kwenda nchini Marekani kwa ajili ya matumizi ya kutengeneza vitu mbali mbali kama viatu, pochi, mikanda na Mabuti ambayo yaliuzwa kwa gharama kubwa. Hata hivyo bidhaa zilizotengenezwa na sehemu za kakakuona bado zinaendelea kuuzwa sehemu mbali mbali nchini Marekani. Ingawa kuna taarifa zinasema kuwa nchi ya Mexco imekuwa inapeleka malighafi na bidhaa za kakakuona nchini Marekani kwa ajili ya biashara.

Kumekuwa na kukisiwa kuwa, kiasi kikubwa cha kakakuona kinatoka barani Afirka, hii ni kwasababu ya kupungua kwa idadi ya kakakuona wa Asia, hivyo nguvu kubwa na kwa kuwa upatikanaji wake ni rahisi kuliko Asia, Afrika inatoa shehena kubwa sana ya kakakuona. Kutokana na kutofahamika kwa baadhi ya nyara za kakakuona zilizokamatwa zinatoka nchi gani. Watafiti wa mambo haya wanasema inafaa kwa siku za baadaye kukawa na njia ya kufahamu nchi au sehemu walizotoaka kakakuona hao waliokamatwa na hawajulikani nchi walikotoka.

Uwepo wa teknolojia ya utambuzi wa sehemu zilikotoka nyara za kakakuona utasaidia sana katika kuandika ripoti kwa uhaliasia wake kwani taarifa zilizotumika kuandika ripoti hii ni kutokakana na baiashara za kimataifa za kakakuona, lakini inaaminika kuna ukosefu wa taarifa ambazo ni muhimu kwa baadhi ya nchi pia hakuna taarifa za ndani zinazoonyesha mzunguko wa biashara za ndani.

Katika kujumuisha dhumuni la ripoti hii ni kwamba, ni muhimu kufahamu njia zinazotumika, lakini mwisho wa siku tumefahamu kuwa nchi za China na Marekani ndio wahusika wakuu wa baishara hii ya kakakuona. China ikiwa inachukua zaidi magamba ya kakakuona pamoja na kakakuona wazima (sio viungo au sehemu za miili ya kakakuona) wakati Marekani yenyewe imekuwa ikiagiza kuingiza shehena ya sehemu za kakakuona (body parts) kama vile Ngozi, kucha, Ngozi, miguu.

MAPENDEKEZO YA RIPOTI HII, NINI KIFANYIKE

Baada ya kujifunza na kuchambua yale ya muhimu katika ripoti hii, ni vema tukajifunza na mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu katika kukabiliana na changamoto hii ya ujangili wa wanyamapori hawa.

  1. Nchi zote ambazo zimehusishwa na zinajihusisha na biashara haramu ya kakakuona wanatakiwa waangalie tena kwa upya na kubadilisha pale inapobidi sheria na taratibu zao za ndani wanyamapori na makubaliano yao katika biashara za kimataifa za spishi za wanyama na mimea mwitu ambayo ipo hatarini kutoweka duniani, CITES. Lengo la kufanya mapitio ya sheria hizo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na utaratibu wa sheria unaotoa ulinzi na uhifadhi wa spishi zote nane za kakakuona.
  2. Mamlaka za serikali, mamlaka za usimamizi wa wanyamapori, na pia mamlaka za kisheria za Nchi zote ambazo zimetajwa na ripoti hii kujihusisha na biashara haramu zinatakiwa kupewa nguvu ya ziada ili kufanya kazi yao kwa ufanisi. Pia watalamu wamependekeza nguvu kubwa iwekwe kwenye nchi ambazo hazina madhara makubwa ya uhalifu na uasafirshaji wa bidhaa za kakakuona, nchi hizo ni Lao PDR, Nigeria, Myanmar, Cameroon, Guinea, Mexico, the Philippines, Pakistan, Liberia, Equatorial Guinea, Cote d’Ivoire, Ethiopia, Kenya, Singapore, Mozambique, and Togo. Kwa kufanya hivyo itasaidia sana kuhifadhi wanyamapori hawa na mazingira yake.
  3. Mamlaka za usimamizi, na mamlaka za kisheria za nchi zote zilizojihusisha na biashara haramu ya kakakuona zinatakiwa kutumia njia za kiintelijensia na kiupelelezi katika kuchunguza miendendo yote, njia zote na vituo vyote vya usafirishaji ili kubaini na kuweka ulinzi na usimamizi imara ili kuzuia kushamiri kwa biashara ya kakakuona na wanyamapori wengine. Pia kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote waliokiuka sheria zao na sheria za CITES.
  4. Uchunguzi wa kitelijensia unatakiwa kuchunguza sehemu ambako kakakuona hutoka, yani chanzo, njia ambazo hutumiwa zaidi, nchi ambazo hutumika kusambaza na pia nchi ambazo ni masoko ya kakakuona. Hii ni kwa sababu watu wanaofanya biashara hii haramu wana mbinu nyingi ili wasikamatwa na pia kila mwaka wanabuni njia nyingine mpya ya kusafirishia bidhaa zao haramu, hivyo mamlaka za uchunguzi zinzatakiwa kuelewa hilo na kujipanga.
  5. Ushirikiano na mamlaka nyingine ni muhmu sana katika mapambano haya, idara za wanyamapori, mamlaka za kipolisi, masharika ya usimamizi na ulinzi ya nchi mbalimbali yanatakiwa kushirikiana kwa karibu hasa kuweka ulinzi kwenye vituo vya usafirishaji, kama mipakani, viwanja vya ndege, bandarini na sehemu zote ambazo zinaweza kukisiwa kutumika kama njia za kusafirishia biashara haramu. Kwa nchi kushirikiana ni rahisi kukabiliana na tatizo hili na kulimaliza.
  6. Waendesha mashtaka, majaji na mahakama zinazojihusisha na kuendesha kesi za kakakuona zinatakiwa kuwa na taarifa sahihi za wakati katika kufanya maamuzi, wanatakiwa kufahamishwa mabadiliko yoyote ya sheria za usimamizi wa spishi za kakakuona na wanyamapori kwa ujumla ili waweze kutekeleza kazi zao za hukumu kwa wakati na kwa usahihi.
  7. Biashara haramu ya kakakuona inatakiwa kuchukuliwa kwa uzito kama uhalifu wa maliasili na pia utoaji wa adhabu kali kwa wahusika katika uhalifu wa wanyamapori hawa inatakiwa iwe kubwa ili kutoa funzo kwa wengine wenye nia ya kujihusisha na kazi hiyo haramu, Zimbabwe imekuwa mfano mzuri kwenye mampambano haya.
  8. Utafiti wa kiteknolojia unatakwa kuanza kutumika ili kubaini nchi ambazo kakakuona wanatoka, hii itasaidia sana katika kupata taarifa muhimu za nchi ambazo wanyama hawa huvunwa mara kwa mara, pia taarifa hizo zitasaidia sana katika kuweka ulinzi na usimamizi kwa spishi hizi za kakakuona.
  9. Mamlaka za usimamizi na ufuatiliaji za CITES zinatakiwa kushirikiana na kuboresha taarifa zote za kukamatwa au kushikiliwa kwa nyara za kakakuona, hii itasaidia sana kuwa na taarifa za uhakika na za kweli katika usimamizi na uhifadhi wa kakakuona.
  10. Utoaji wa taarifa zinazohusiana na kakakuona unatakiwa uendelee kufanyika na CITES, masharika binafsi, watafiti binafsi na watu binafsi hii itasaidia sana kuwa na taarifa za kutosha kutoka sehemu mbali mbali.
  11. Nguvu ya ziada inatakiwa kutumika katika kutoa elimu na uelewa kwa watumiaji wa kakakuona na wale wanaojihusisha na biashara hii, hii itasaidia kupunguza mahitaji ya kakakuona kwa nchi ambazo zinaagiza au zinawateja wa bidhaa za kakakuona.
  12. Mamlaka za usimamizi wa sheria na ulinzi za nchi ambazo zimepewa kipaumbele katika kupambana na biashara haramu ya kakakuona wanatakiwa kuwapa uelewa maafisa wao kuhusu kakakuona, biashara haramu zinazohusisha kakakuona na mbinu za kukabiliana na changamoto hiyo.
  13. Kwa kuwa inafahamika kuwa nchi za bara la Asia zina mahitaji makubwa ya kakakuona na pia inafahamika pia kuwa mahitaji yao ya kakakuona yanachochewa na nini. Kazi kubwa bado inatakiwa kufanyika kwa nchi ambazo zina uhitaji mkubwa wa kakakuona nchi kama Marekani na Uholanzi, ni nchi ambazo kuna mengi hayafahamiki sana kuhusu kichocheo cha kuhitaji kisi kikubwa cha bidhaa na viungo vya kakakuona. Hivyo katika mapendekezo haya imeshauriwa watafiti kufanya utafiti wa kina ili kubaini vichocheo vikuu vya kushamiri kwa biashara hii haramu ya kakakuona katika mataifa hayo ya Marekani na Uholanzi.

Rafiki yangu, haya ndio macheche kati ya mengi niliyofanikiwa kuyachambua katika ripoti hii nzito, tunatamani sana wanyamapori tunaowaona leo waendelee kuwepo kwa miaka mingi zaidi ijayo, lakini sio kazi nyepesi kufikia lengo hilo. Ndio maana natumia nguvu na muda mwingi kujifunza hali ya mambo inavyokwenda kwenye sekta hii sehemu mbali mbali duniani, nikijua hali hii inaweza kutokea pia kwa wanyamapori wetu. Hivyo kwa kujifunza na kufahamu hayo nimeamua kukushirikisha yale ya muhimu niliyoyachambua katika ripoti hii. Hivyo kwa wote ambao watasoma tutafahamu na kufanya maamuzi mazuri yatakayosaidia uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori wetu.

Nakushukuru kwa kusoma makala hii ndefu ya uchambuzi, naamini utawashirikisha na wengine makala hii kama nilivyofanya mimi.

Shiriki Pamoja Nami Tulinde Maliasili Zetu.

Uchambuzi wa ripoti hii umefanywa na;

Hillary Mrosso

255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com