Habari za siku wadau wangu katika uhifadhi wa wanyamapori. Ni siku nyingine tena tunakutana katika mfululizo wetu wa makala za wanyamapori ili kujuzana machache lakini yenye faida kubwa sana kuhusu wanyama hao. Kupitia makala hizi niwazi kwamba unajifunza mambo mengi sana kuhusu wanyamapori huku ukibaki na mshangao kwa baadhi ya mambo ambayo hapo awali hukuyafahamu kuhusu wanyamapori.
Katika mfululizo wa makala hizi leo tutaendelea tena kuwachambua wanyama jamii ya swala kwani kundi hili kama nilivokwisha kusema katika makala mbalimbali zilizopita lina wanyama wengi sana na tutajitahidi kuwachambua kwa kadri ya uwezo wetu ili tu ndugu msomaji uweze kuwafahamu wanyama hawa. Makala ya leo ningependa kumleta darasani swala ajulikanae kama “Swala Granti” au kwa lugha ya kiingereza hujulikana kama “Grant’s Gazelle”.
Hivyo nikusihi ndugu msomaji wa makala hii uwe nami mwanzo mpaka mwisho wa maka hii kwani utapata kujua mambo mengi sana kuhusu mnyama huyu na mengi ya kushangaza hasa tukitazamia mambo kama sifa na tabia za mnyama huyu, mazingira anayoishi, jinsi wanyama hawa wanavyo zaliana na mambo mengine mengi tu.
UTANGULIZI
Swala Granti ni wanyama ambao wanapatikana katika kundi la wanyama jamii ya swala. Swala hawa wanafanana kwa ukaribu sana na swala wajulikanao kama “Swala tomi” ambao kwa kiingereza wanaitwa “Thomson’s Gazelle”. Kama sio mzoefu vizuri wa wanyama hawa basi ni dhahiri kwamba hutoweza kuwatofautisha pale unapowaona katika mazingira mbali mbali katika maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori au mabustani maalumu ya ufugaji wa wanyamapori.
Lakini ukweli ni kwamba wanyama hawa wana tofauti nyingi sana na kupitia makala hii utaweza kujua tofauti zilizopo baina ya swala hawa na wengineo. Swala Granti wanapatikana maeneo mengi sana hapa nchini hasa katika hifadhi za taifa na mapori mengine ya akiba. Kitu cha kujivunia nikwamba wanyama hawa bado hawajawa hatarini sana kutoweka duniani na Tanzania ni miongoni mwa chi chache duniani ambayo wanyama hawa wanapatikana kwa wingi nakuweza kuonekana kwa urahisi.
Sasa bila kupoteza muda tuangalizie sifa na tabia za Swala Granti.
SIFA NA TABIA ZA SWALA GRANTI
Wana alama ya mstari mnene wenye rangi nyeupe unaoanzia maeneo ya kiunoni na kuelekea hadi semu ndogo ya mgongoni. Hii ni miongoni mwa tofauti kubwa kati yao na swala tomi kwani kwa swala tomi mstari huu huishia mkiani.
Baadhi ya jamii nyingine za swala granti wana mistari myeusi pande zote mbili za mwili kama walivo swala tomi. Kwa jamii nyingine mistari hii huwa inang” aa na wengine hawana kabisa. Kwa wale wenye mistari myeusi ukiwachunguza utagundua wana mistari mingine ambayo imejichora sambamba na mapaja yao.
Wana miili mikubwa kuliko swala tomi, rangi za miili yao zikiwa za kupauka na miguu mirefu.
Pembe zao zina umbo la vinubi, nene sehemu ya chini na zina miduara. Pembe za wanyama hawa hurefuka na kufikia urefu wa inchi 18 hadi 32.
Wana umbo la kipekee la pembe tatu ya rangi nyeupe sehemu ya juu ya miguu ya nyuma na alama ya mstari mweusi unaolekea sehemu ya mapajani.
Madume wana miili mikubwa kuliko majike na pembe zao hurefuka zaidi kuliko zile za majike.
Majike wana ngozi nyeusi iloyo zunguka maziwa na manyoa meupe kwenye kiwele. Rangi hizi humsaidia mtoto kujua maziwa yalipo kipindi anapokuwa na umri wa kuongozana na mama wakati wa malisho.
Macho yao yamezungukwa na alama nyeusi huku wakiwa na alama ya manyoa yenye rangi nyeupe yanayo anzia sehemu za machoni na kuelekea sehemu ya mdomoni.
Swala grani ni wanyama ambao huishi kwenye makundi na wanauwezo wakuona zaidi majira ya mchana.
Dume aliye pevuka huanzisha himaya yake na huweza kuiongoza himaya hiyo hadi miezi 8. Hutumia kinyesi na mkojo kuweka alama katika himaya yake. Katika himaya hii dume huweza kumiliki majike 10 hadi 25 na huwa na jukumu kubwa la kuhakikisha majike hawa hawatoki katika himaya yake kwa kuwafukuza madume wengine ambao wavamia himaya yake.
Kwa baadhi ya misimu wanyama hawa huwa wanahama kutoka eneo moja kwenda eneo linguine na kuhama huku huzingatia wadhifa katika kundi. Endapo sehemu waliyopo kipindi hicho ina chakula cha kutosha basi wanyama hawa wanaweza kubaki eneo hilo kwa mwaka mzima. Wanapo hama kundi huwa na dume mtawala, majike na baadhi ya madume makapera.
Kuhama kwa wanyama hawa ni tofauti na swala wengine kama nyumbu, swala tomi na wengineo. Wakati swala wengine wanahama ili kutafuta chakula na maji, swala granti wao huja kwenye maeneo walohama wenzao kwasababu changamoto ya chakula inakuwa ni ndogo na pia wanauwezo wakuishi muda mrefu bila kunywa maji.
KIMO, UREFU NA UZITO WA SWALA GRANTI
Kimo= swala granti hufikia kimo cha inchi 30 mpaka 36
Urefu= hufikia urefu wa inchi 55.12 mpaka 65.35
Uzito= swala granti hufikia uzito wa kilogramu 45 mpaka 65.
MAZINGIRA
Wanyama hawa hupendelea mazingira ya savana ya wazi, maeneo ya nusu jangwa na nyika ambazo hazina miti. Swala granti huepuka sana maeneo yenye misitu labda tu kama wanatumia maeneo hayo kama njia wakati wanahama toka eneo moja kwenda eneo linguine.
Swala granti wanapatikana maeneo ya Mashariki mwa Afrika tu ambapo hutawanyika mpaka kufikia muinuko wa mita 2,000 toka usawa wa bahari. Kama nilivokwisha dokezea hapo juu, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo tunajivunia kuwa na wanyama hawa tena kwa wingi zaidi.
CHAKULA
Swala granti ni miongoni mwa wanyama walao majani na hupendelea sana sehemu za majani na mashina kwenye mimea. Wanyama hawa wanauwezo wakuishi kwa muda mrefu bila kunywa maji na hii inatokana na uwezo wa miili yao kutunza maji mengi na uwezo pia wa kupandisha jotoridi la miili yao kulingana na jotoridi la mazingira.
KUZALIANA
Swala granti huzaliana majira yoyote ya mwaka japo kuzaliana huku huathiriwa na mabadiliko ya mazingira na tabia ya nchi. Dume mwenye kumiliki himaya ndiye mwenye mamlaka yakupanda majike wote wapatikanao ndani ya himaya yake. Majike wanafikia msimu wa kubeba mimba hukojoa mkojo ambao humfanya dume kutambua kuwa majike hawa sasa wanahitaji kupandwa ili wabebe mimba.
Mara baada ya kupandana jike hubeba mimba kwa muda wa miezi saba na baadae huzaa mtoto mmoja. Majike huakikisha wana zaa watoto katika mazingira salama dhidi ya maadui zao. Baada tu yakuzaa mama hulazimika kula kiwambo cha mimba na dakika chache tu mtoto anapokuwa na uwezo wa kunyonya na kutembea mama hulazimika kuhama eneo hilo na kutafuta eneo salama zaidi kwa ajili yake yeye na mtoto. Mtoto huanza kula majani mara tu afikishapo mwezi mmoja japo huendelea kunyonya na kuwa chini ya uangalizi wa mama kwa muda wa miezi 6.
Watoto wa swala granti hupevuka mara tu wafikishapo miezi 18 (sawa na mwaka mmoja na nusu). Wafikishapo umri huu watoto wakike hubaki kwenye kundi la kina mama huku watoto wa kiume hufukuzwa kundini na kwenda kujiunga na kundi la madume wengine ambao hawana himaya. Japo kwa wakati huu watoto wakiume wanakuwa hawana uwezo wa kuanzisha himaya kwasababu hawana uwezo wa kupigana na madume wakubwa ili kuwa watawala.
Swala granti wakadiriwa kuwa na uwezo wakuishi miaka 12 hasa wawapo katika mazingira yao asili. Japo umri huo unawezakuzidi kama wanyama hawa wanafugwa katika mabustani maalumu kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori.
UHIFADHI
Ni jambo la kushukuru kuwa wanyama hawa bado hawajawa hatarini kutoweka duiani. Kutokana na takwimu za shirika la umoja wa mataifa linalo simamia uhifadhi wa maumbile asilii (International Union for Conservation of Nature-IUCN) za mwaka 2016, idadi ya wanyama hawa inakadiriwa kuwa ni 140,000 japo bado ilionekana kuwa huenda walikuwa zaidi ya hao kwani sensa ilifanyika kwa kutumia ndege hivyo kuna baadhi ya maeneo hawakuweza huhesabu vizuri.
Kutokana na takwimu hizo nifuraha kubwa kuona kwamba Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ndio inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama hao ambapo wanakadiriwa kufikia swala granti 35,000-55,000 huku ikifuatiwa na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ambayo inakadiriwa kuwa na swala granti 4,300. Hifadhi zote hizi mbili zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama hawa zinapatikana hapa nchini Tanzania, nijambo la furaha sana na kujivunia kwa ufahari huu.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa asilimia 30 ya wanyama hawa ndio wanapatikana maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Swala granti wanaonekana kulindwa sana na ndio maana wameendelea kuwa na idadi kubwa hasa kama tulivoona idadi yao katika hifadhi ya taifa ya Serengeti japo inasemekana kuwa idadi kubwa ya wanyama hawa wanapatikana nje ya mipaka ya hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Halikadhalika takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wanyama hawa inapungua kidogo kidogo kutokana na changamoto mbalimbali ambazo tutaziona kwenye kipengele kinacho fuata.
MAADUI NA TISHIO KWA SWALA GRANTI
Nikianza kwa upande wa maadui hapa nazungumzia maadui asilia wa wanyama hawa katika mazingira yao asilia. Madui hawa ni simba, chui, duma, fisi na mbwa mwitu. Maadui hawa asilia ni muhimu sana kwani husaidia kuweka sawa mahitaji ya kiikolojia kwa wanyama hawa na viumbe wengine katika mazingira yao.
Nikirudi kwa upande wa tishio kwa wanyama hawa, hapa nazungumzia changamoto ambazo zinawakumba wanyama hawa tofauti na zile asilia katika mazingira yao. Nazo ni kama ifuatavyo,
Ujangili unaoendelea katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori umekuwa ni tishio kubwa sana kwa uwepo wa swala granti. Wanyama hawa wamekuwa wakiwindwa sana kutokana na mahitaji ya malighafi zao kitu ambacho kinapelekea wapungue siku hadi siku. Ngozi, nyama pamoja na baadhi ya sehemu za wanyama hawa zimekuwa zikitumika kwa matumizi mbalimbali hali ambayo inazidi kusababisha biashara haramu ya wanyamapori kushamiri kila siku.
Uharibifu wa mazingira hasa kutokana na upanuzi wa mashamba kwa ajili ya kilimo. Baadhi ya jamii ambazo zinapakana na maeneo ya hifadhi za wanyamapori zimekuwa zikiharibu mazingira sana kwa uchomaji moto holela ili tu kupata maeneo makubwa kwa ajili ya kilimo. Hali hii imepelekea uharibifu wa mazingira ya wanyama hawa kitu ambacho kinapelekea wanyama hawa kuhama baadhi ya maeneo kutokana na upatikanaji hafifu wa mahitaji yao hasa maficho, chakula na maji.
Ongezeko na uingizwaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Wimbi la ongezeko la mifugo ni tatizo kubwa sana kwa sasa hasa kwa upande wa uhifadhi wa wanyamapori. Idadi kubwa ya mifugo inapelekea kuwepo kwa uhaba wa chakula kwa swala granti na hata wanyama wengine walao majani kwani sehemu kubwa ya chakula chao hutumiwa na mifugo. Baadhi ya jamii zimekuwa zikikiuka sheria za hifadhi za taifa na maeneo mengine ya hifadhi za wanyamapori kitu ambacho kinapelekea kupungua kwa idadi ya swala granti katika maeneo hayo.
NINI KIFANYIKE ILI KUWALINDA SWALA GRANTI HASA HAPA NCHINI TANZANIA
Mapambano dhidi ya ujangili unaokithiri katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Mamlaka mbali mbali kama TANAPA, TAWA na Ngorongoro zihakikishe zinaimarisha doria za mara kwa mara ili kubaini wahusika wakuu wa ujangili nakuwachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine ambao wana dhamira ya kuendeleza ujangili dhidi ya wanyamapori. Kuongeza idadi ya askari waadilifu katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori kutasaidia ufanisi wa kazi ya ulinzi wa wanyama dhidi ya majangi kitu ambacho kinarudisha nyuma sana shughuli za uhifadhi wa wanyamapori.
Wanao haribu mazingira wachukuliwe hatuakali zakisheria ili iwe fundisho kwa wengine. Jamii zote zinazo pakana na hifadhi za taifa pamoja na mapori ya akiba zifuatiliwe kwa ukaribu zaidi hasa kwa suala la utunzaji wa mazingira kwani shughuli za kilimo zimekuwa zikisababisha uharibifu mkubwa sana wa mazingira kitu ambacho kinawafanya wanyama kukosa mahitaji yao na kulazimika kuyahama maeneo hayo. Hivyo mamlaka mbalimbali za hifadhi za wanyamapori kwa kushirikiana na wizara husika zijitahidi kufuatilia suala la uharibifu wa mazingira nakutoa adhabu kali kwa wahusika ili kutokomeza kabisa changamoto hii kwa swala granti.
Utaifishaji wa mifugo au faini kubwa zitolewe kwa yeyote atakaekamatwa kaingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Hii itasaidia wafugaji kuwa makini zaidi na kuepika kusogeza au kulisha mifugo yao katika maeneo hayo. Lakini pia serikali ijitahihidi kuweka idadi maalumu ya mifugo kwa jamii zinazo zunguka maeneo ya hifadhi za wanyamapori na atakayekiuka sheria na kuzidisha idadi ya mifugo hiyo basi hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake ili iwe fundisho kwa wafugaji wengune wenye tabia kama hizo.
Kuhamasisha utalii wa ndani ili kila mmoja aweze kutambua umuhimu wa kuwa na wanyama hawa kwani kupitia utalii huu nidhahiri kwamba watu watajifunza mambo mengi sana kuhusu wanyama hawa na umuhimu wao katika pato la taifa kwani moja kati ya vitu vinavyo liingizia taifa pesa nyingi hasa za kigeni kupitia wizara ya maliasili na utalii ni utalii hasa kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori.
Serikali kupitia wizara ya elemu, sayansi na mafunzo ya ufundi ijitahidi kuingiza mtaala wa elimu ya uhifadhi mashuleni hasa kuanzia ngali ya shule ya msingi ili kuwafanya watoto waweze kujua mapema umuhimu wa rasilimali hizi za wanyamapori. Kwa kufanya hivyo ni dhahiri kwamba watoto hawa watakuwa na moyo wa uadilifu huku wakkitambua umuhimu wa uwepo wa wanyama hawa na hatimae tutakuwa na mabalozi wazuri sana ambao watasaidia kuliendeleza gurudumu la uhifadhi wa wanyamapori hawa nchini.
HITIMISHO
Thamani ya kitu huonekana pale kinapo toweka machoni mwako. Kwa sasa idadi ya swala granti niyakuridhisha hapa nchini Tanzania hivyo hatuna budi kuingeza jitihada ili kuhakikisha idadi ya wanyama hawa inaendelea kuwa hidhi na ikiwezekana kuongezeka. Jitihada za dhati zikifanyika hakuna kitakacho tukwamisha kufikia malengo yetu kama taifa kwenye sualala uhifadhi wa wanyamapori.
Pongezi zangu za kipekee kwa shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA kwa kazi kubwa sana wanayo ifanya ili kunusuru uwepo wa wanyama hawa kwanini tumeona hapo juu kuwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ndio inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya swala granti ikifuatiwa na Hifadhi ya Taifa ya Trangire huku hifadhi zote hizi zikiwa chini ya usimamizi wa TANAPA, hongereni sana. Bila kuzisahau mamlaka nyingine kama TAWA NA NGORONGORO kwa kazi kubwa sana yakusaidia uwepo wa wanyama hawa hapa nchini. Ni kweli kwamba mnafanya kazi kubwa sana na yakipekee ili tu kunusuru wanyamapori waendelee kuwepo hapa nchini mana bila nyie tusingekuwa na wayama hawa kabisa.
Shukrani zangu za dhati pia ziende wizara ya maliasili na utalii chini ya Daktari Hamiss Kigwangalla kwa kazi kubwa sana anayoifanya katika kuiongoza wizara hiyo na ufuatiliaji wa utekelezaji majukumu katika wizara ya maliasili na utalii. Ushirikiano mkubwa uliopo baina ya wizara na mamlaka zake umesaidia sana kuhakikisha suala la uhifadhi wa wanyamapori linatiliwa kipaumbele sana kwani ni moja kati ya sekta zinazo liingizia taifa fedha nyingi sana. Kila la kheri kwa ushirikiano huu baina ya wizana na mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori.
Nasi wananchi kwa namna moja ama nyingine na kwa uwezo tulojaaliwa hatuna budi kuziunga mkono mamlaka husika pamoja na wizara ya maliasili na utalii katika mapambano dhidi ya ijangili na kuhamasisha uhifadhi wa wanyamapori ili taifa letu liendelee kuwa kinara kwenye suala la uhifadhi na tuzidi kuingiza fedha nyingi za kigeni kupitia utalii ambao hasa hulenga zaidi kwa upande wa wanyama.
MWISHO
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori, maswali na ushauri kuhusu makala hizi usisite kuwasiliana nami kupitia,
Sadick Omary Hamisi
Simu= 0714116963 au 0765057969
Email= swideeq.so@gmail.com
Facebook/Messenger= Sadicq Omary Kashushu
Au tembelea= www.mtaalam.net/wildlifetanzania
”I’M THE METALLIC LEGEND”