Wapendwa wasomaji wa makala za wanyamapori na maliasili kiujumla, ninayo furaha isiyokifani kuwashirikisha hisia nilizonazo kuhusu uhifadhi wanyamapori zinazonipelekea kusema “NISIPOHIFADHI WANYAMAPORI SIONI UTU WANGU”. Kabla sijaeleza maana ya kauli hii, nitoe pongezi kwa mashirika, taasisi na miradi yote inayojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori.
Mpendwa msomaji, uhifadhi wa wanyamapori ni kitendo la kutunza ama kulinda mimea na wanyama pori pamoja na makazi yao, kwa kutambua uthamani wa tendo hili nimejawa na hisia kali za kupenda uhifadhi hivyo kusema, nisipo hifadhi wanyamaporo sioni utu wangu”
Kwanini nashindwa kuona utu wangu nisipohifadhi wanyamapori? Wanyamapori ni zawadi pekee tuliyopewa na Mola katika mazingira yetu na viumbe hivi vina maslahi makubwa sana kwetu na mazingira kwa ujumla, kushindwa kutunza zawadi hii ya kipekee hakika ni kukosa utu. Bila shaka kilia mtu atambuaye thamani ya viumbe hawa bila shaka ataniunga mkono kuwa utu wangu ni pale nitakapowatunza wanyamapori au viumbe hawa wa porini.
Tendo la kuhifadhi wanyamapori limesheheni faida kedekede kwa binadamu, viumbe wengngine na mazingira kiujumla, faida hizo ni kama;
Kutunza uoto wa asili, maeneo yaliyohifadhiwa kama vile mbuga za wanyama pamoja na mapori ya akiba, ndio maeneo yaliyofanikiwa kuhifadhi uoto wa asili na kudhibiti shughuli za kibinadamu, uoto huu ni muhimu katika mfumo mzima wa maisha ya viumbe hai, pia katika kujikinga na majanga hatarishi yanayoweza kutokea kwasababu ya kukosekana kwa uoto wa asili.
Kudumisha urithi wetu, uhifadhi unahakikisha wanyamapori wanaendelea kuwepo kizazi baada ya vizazi, hivyo husaidia kuacha urithi huu kwa vizazi vingine, ikumbukwe kuwa wanyamapori tunao waona leo ni kwasababu wazee wetu au vizazi vilivyopita viliwajibika katika kuwahifadhi wanyama hawa ambao leo tunawaona, hivyo ni jukumu letu kufanya hivyo kwa vizazi vijavyo.
Kutatua changamoto za kuharibiwa kwa mazingira ya wanaymapori, uhifadhi husaidia sana katika kulinda mazingira muhimu ya wanyamapori hasa wale walio katika hatari ya kutoweka kama vile faru, mbwa mwitu na sokwe na wengneo.
Uhifadhi ndio msingi mkuu wa utalii,watalii huvutiwa na wanyamapori na makazi yao, hivyo utalii unategemea uhifadhi wa wanyamapori, ikumbukwe pia nchi hupata mapato ya fedha nyingi za kigeni kupitia utalii.
Hutunza mazingira na kuleta usawa wa kiikolojia, kwa kuthibiti shughuli za uharibifu wa mazingira kama ukataji miti, uchomaji wa miti hovyo, uhifdhi husaidia sana kutunza mazingira na kuleta usawa mzuri kiikolojiaa.
Kuhifadhi wanyamapori na mazingira yake ni kipimo cha utu nani zawadi ya kipekee tunayoweza kutoa kwenye mazingira yetu, kwani mazingira hututunza lakini sisi tumeshindwa kurudisha fadhila kwa kuyaharibu.
Mpendwa msomanji wa makala hii nakushukuru kwa kusoma makala hii, ni Imani yangu kwa sasa tutakuwa bege kwa bega kuhifadhi wanyamapri.
Makala hii imeandaliwa na Lucy Romward, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Dar es salam (UDSM), akisoma shahada yake ya kwanza ya Sayansi ya Uhifadhi wa Wanyamapori. Lucy anapenda sana kujifunza na pia ana mapenzi ya dhati katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Kama alivyotangulia kutuambia hisia zake na matamanio yake katika uhifadhi, sisi hatuna budi kuungana na Lucy katika kulinda na kuhifadhi wanyamapori kwa vizazi vya sasa na vizazi vingi vijavyo.
Ahsante sana!
Lucy Romward