Uhifadhi wa wanyamapori na mazingira asilia, unagusa mambo mengi na maeneo mengi, hata hivyo serikali ya Tanzania imejitahidi sana kutenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli za uhifadhi wa mazingira asilia na makzi ya wanyamapori. Maeneo yote ya hifadhi za taifa, hifadhi ya mamlaka ya eneo la Ngorongoro, mapori ya akiba, mapori tengefu, maeneo ya hifadhi ya jamii, WMA, maeneo ya wazi nk. nchi kavu na maeneo ya bahari, maeneo ya hifadhi ya ardhi oevu, misitu nk. Yote yanatambuliwa kisheria na yanasimamiwa na mamlaka za uhifadhi wa malisili Tanzania. Leo muhifadhi Leena amatuandalia makala hii yenye kichwa cha habari. “Kwanini Tuhifadhi Wanyamapori Na Mazingira Yake Asilia”?

 

 Inawezekana neno “uhifadhi” kwako likawa rahisi sana na unaweza kulielezea, lakini kwa baadhi yetu ni neno gumu sana kama kurudisha siku nyuma kitu ambacho hakiwezekani!

“Uhifadhi” ni kitendo endelevu chenye mikakati yake inayohakikisha kutunza, kulinda, na kuendeleza uwepo wa wanyamapori na mazingira yake asilia. Na neno  “Wanyamapori” ni viumbe visivyofugwa na binadamu na vinakaa kwenye uasilia wake mfano makundi ya wanyama mbugani kama tembo, nyati, nyumbu, swala na ndege pia. Na neno “Mazingira asilia” ni mazingira ambayo hayajaharibiwa na shughuli zozote za kibinadamu pia ni mazingira yaliyoundwa na uoto wake bila kupandwa na binadamu kama miombo, mibuyu, na miningo.

Historia inaweza kutusaidia kufanya mabadiliko hasi au chanya, na uhifadhi una historia yake.Tukirudi nyuma kabisa miaka ya 1891 wakati Sheria za Uhifadhi  Tanzania zilianzishwa kwa lengo la kudhibiti uwindaji holela.

Pia Azimio la Arusha la Mwaka 1961 chini ya Mwal.Nyerere, Raisi wa kwanza Tanzania, linatumika kutoa mwongozo wa Uhifadhi wa wanyamapori hapa Tanzania hadi leo.

Inawezekana wanatumia vibaya (japo kwao wanaona wapo sahihi) uwepo wa fahari kubwa ya viumbe pori nchini pasipo kujua Kwanini Serikali inatumia nguvu nyingi kimawazo, kimtazamo, kiuongozi, na hata nguvu kazi katika kuhimiza uhifadhi. Usijali! Nipo ili tujifunze na tuungane katika Uhifadhi,  zifuatazo ni faida za uwepo wa wanyamapori na mazingira yake.

1)Faida za kiuchumi

Kwa mfano Tanzania imekuwa ikijiongezea kipato chake kikubwa na kukua kiuchumi kutokana na viumbe hawa

-Kupitia  Utalii, ambapo watalii wengi duniani wamekuwa wanatembelea mbuga zetu kujionea fahari ya wanyamapori na kupata hewa nzuri ya misitu asilia, na kupitia pesa zao za viingilio vimechangia ongezeko la kukua kiuchumi nchini.

-Uwindaji Halali, na kupitia uhifadhi bora, nchi yetu imeweza kutoa vibali halali vya uwindaji wa wanyamapori katika mapori ya akiba ambako nako imesaidia ongezeko kubwa la kipato ajira na fedha za kigeni.

-Upigaji picha na utengenezaji filamu za wanyamapori, kupitia uwepo maliasili hizi za wanyamapori na mimea, uchumi unakua kila siku kutokana na vibali ambavyo wageni na watalii wanalipia kwa ajili ya shughuli za kupiga picha wanyamapori na utengenezaji wa filamu za wanyama na maliasili kwa ujumla ambapo pamoja na mambo mengine zinauzwa na kuongeza kipato na zaidi kuitangaza nchi yetu duniani.

-Maendeleo makubwa ya miundombinu ikiwemo barabara  nyingi zimeimarishwa kutokana na mapato yanayotokana na utalii na ili kuweza kuwavuta wageni wengi kwa sababu ya kupitika kwake, Viwanja vya ndege pia vimeongezwa na kuimarishwa ili watalii waweze kufika kwenye mbuga zetu kwa urahisi.

-Kukuwa kwa miji mingi kuwa majiji pamoja na ongezeko kubwa la masoko ya vitu asilia, kupitia uwepo wa wanyamapori na utalii unaokua kila siku, miji mingi imekua kiuchumi kwa mfano jiji la Arusha ambalo limekua jiji la Utalii na la katikati ya upande wa Kaskazini kwenye mbuga nne zilizokaribiana ambazo ni  Ngorongoro, Manyara, Serengeti, na Tarangire pia hifadhi ya mlima Kilimanjaro ambao pia ni makazi ya ndege, uoto wa asilia na vyanzo vya maji, na masoko mengi ya vitu vya kitamaduni kama vile  vya kimasai kupata dau duniani kote.

2) Faida za kibaologia

-Kuboresha hali ya hewa, kupitia misitu ya asili ambayo ipo nchini inatusaidia kufyonza gesi chafu mbalimbali kutoka viwandani na shughuli nyingine za kimaendeleo, mfano cabonidioksaidi.

-Kutunza ardhi na vyanzo vya maji, uwepo wa viumbe pori imesaidia Serikali katika maamuzi sahihi ya mgawanyo wa ardhi na kuvipa kipaumbele vyanzo vya maji mfano chanzo cha maji cha mto Ruaha, chanzo cha maji cha bonde  la Usangu, na chanzo cha maji mlima Kilimanjaro nk.

-Wanyamapori kuzaliana kwa wingi katika mazingira yake, kutokana na mazingira mazuri yanayofanya hali za wanyama kuwa nzuri na afya, wao pia wana haki ya kuishi na kuzaliana katika mazingira yake ambapo ongezeko lao ni faida kwetu mfano mbuga moja ikawa na simba wengi itasaidia kuwasafirisha na kuwahifadhi kwenye mbuga nyingine kitu ambacho kitasaidia mgawanyo wa watalii na sio mbuga moja tu iwe inapokea watalii wengi.

3) Faida za kiafya

-Chakula na matunda, kupitia uwepo wao na ongezeko lao tunaweza kupata chakula kama nyama kutoka kwa nyati ambapo tunaimarisha afya zetu kupitia protini tunayopata na matunda kutoka kwenye misitu yetu (ingawa kwa sasa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, hairuhusu kabisa uwindaji kwa ajili ya nyama bila kibali kutoka kwa mamlaka husika za usimamizi wa wanyamapori Tanzania).

-Dawa za magonjwa, pia kupitia uhifadhi wa viumbe pori tunapata dawa kutoka kwenye misitu na uoto wa asilia mfano alovera. Kwa maeneo yaliyohifadhiwa kisheria uvunaji wa nyama na matunda, dawa nk. hufanyika kwa kufuata taratbu za kisheria na kibali cha uvunaji hutolewa.

4)Faida katika kupunguza ongezeko la majangwa, ukame,mafuriko na vimbunga, kupitia uwepo wa misitu na juhudi kubwa za uhifadhi inasaidia kuzuia majangwa kutokea, ukame kutokea pia kupitia misitu mafuriko imekuwa nadra sana kutokea kwani miti hiyo imekuwa kama kizuizi au kingo hivyo hata vimbunga na upepo mkali vimepungua.

5)Umahiri na Ushujaa wetu kwa vazazi vijavyo, ni tuzo kubwa sana kwetu kwa vizazi vijavyo kuja kuona wanyamapori na makazi yao asilia, naamini watatupongeza sana, kama sasa tulivoweza kupokea tuzo ya mahali pazuri duniani kutalii ikiwa ni tuzo ya tatu kwa miaka saba mfululizo, ila yote yatatokea ikiwa tu tutawatunza vizuri viumbe hao leo kama ambavyo mpaka leo sisi tunawaenzi wale wote waliopigania uwepo wa wanyama pori kipindi cha nyuma.

6) Upatikanaji wa Nishati, kupitia wanyamapori  na mazingira yao tunapata nishati ya kuni kutoka kwenye misitu ambapo husaidia kupika kama njia mojawapo ya kuzalisha joto.

Uhifadhi wa wanyamapori na mazingira asilia, unagusa mambo mengi na maeneo mengi, hata hivyo serikali ya Tanzania imejitahidi sana kutenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli za uhifadhi wa mazingira asilia na makzi ya wanyamapori. Maeneo yote ya hifadhi za taifa, hifadhi ya mamlaka ya eneo la Ngorongoro, mapori ya akiba, mapori tengefu, maeneo ya hifadhi ya jamii, WMA, maeneo ya wazi nk. nchi kavu na maeneo ya bahari, maeneo ya hifadhi ya ardhi oevu, misitu nk. Yote yanatambuliwa kisheria na yanasimamiwa na mamlaka za uhifadhi wa malisili Tanzania.

Mpaka hapo! Nachukua fursa hii kukushukuru kwa muda wako uliotenga kuisoma makala hii na ninaimani pia umeongeza kitu kikubwa sana na umevutiwa na uhifadhi kwa kiasi, zipo faida nyingi ila kubwa ndo hizo.

Tupaze sauti zaidi katika kushawishi na kuelimisha watu wengine katika uhifadhi ili tupate nguvu kazi zaidi.

Ahsanteni sanaa      

  Leena Lulandala

Mwanafunzi-UDSM

0755369684

  lulandalaleena@gmail.com