Mandhari ya hifadhi ya Ruaha ni sehemu muhimu sana inayopewa kipaumbele kimataifa kwa ajili ya uwepo wa kanivora wakubwa, katika sehemu hii muhimu inakadiriwa kuwa inazaidi ya asilimia 10 ya simba wote waliopo duniani, na pia ni sehemu muhimu sana yenye idadi nzuri ya chui na fisi.
Ukosefu wa taarifa muhimu za kiikolojia zinazoonyesha mtawanyiko na makazi ya kanivora hawa wakubwa imekuwa ndio changamoto kubwa sana inayozuia kusiwepo na mipango na mikakati imara ya uhifadhi wa wanyama hawa.
Hata hivyo makala hii imeandikwa kutokana na taarifa chache zilizopatikana kwa njia mbali mbali ambazo ndio zilizosaidia kuwepo kwa makala hii. Makala tunayoichambua leo imeandikwa kitalaamu sana na ina maneno mengi ya kisayansi na kitalaamu, hivyo kwa kuwa nataka kila mtu aelewe dhima na maudhui ya makala hii, nimeamua kuchambua makala hii na nitakushirikisha yale yaliyo muhimu zaidi.
Makala tunayoichambua inajulikana kwa jina la “Using Landscape and Bioclimatic Features to Predict the Distribution of Lions, Leopards and Spotted Hyaenas in Tanzania’s Ruaha Landscape” kwa Kiswahili kisicho rasmi sana anamaanisha kutumia mandhara na mabadiliko hai ya tabia nchi katika kubashiri mtawanyiko wa simba, chui na fisi madoa katika mandhari ya hifadhi ya Ruaha Tanzania, makala hii iliyoandikwa na Leandro Abade na wenzake.
Kwa ufafanuzi kidogo ni kwamba, hapo mwanzo umeona nimetumia neno “kanivora” neno hili kanivora lina maana ya wanyama wanaokula nyama, hivyo nikisema kanivora wakubwa nitakuwa namaanisha wanyama wanaokula nyama wakubwa, mfano simba, chui, fisi, mbwa mwitu, duma, nk. Katika uchambuzi wa makala ya leo utaona nikilitumia sana neno hili kanivora ili kuelezea dhima ya makala hii.
Makala hii tunayoichambua ina mambo mengi sana ya kitalaamu na kisayansi na pia imeandikwa na watu waliobobea kwenye mambo ya utafiti wa wanyamapori hasa, wanyamapori wanao kula nyama, yani kanivoras, hivyo ndugu yangu naomba twende pamoja kujua yaliyopo katika eneo hili muhimu la hifadhi ya Ruaha kama ilivyoelezwa kwenye makala tunayoichambua.
Kanivora wakubwa kama vile simba, chui, na fisi madoa ni muhimu sana katika mfumo mzima wa ikolojia, wanyama hawa wakiwa ndio kanivora wakuu wanasaidia sana kusawazisha na kuwepo kwa usawa katika mfumo wa ikolojia ya wanyama na mazingira, ili hifadhi za asili ziendele kuwa katika afya na hali nzuri kanivora hawa ni muhimu sana katika kuhakikisha hilo linafanyika.
Kiasili wanyama na mimiea hutegemeana katika mazingira, mimea na wanyama vyote hutegemeana, sasa kanivora wakubwa wanaweza kusaidia utunzaji wa mazingira asilia ya wanyama na kuepusha majangwa na ukame kwa kuwala au kuwapunguza wale wanyama wakubwa wanaokula sana nyasi au mimea, hivyo katika kuwapunguza husaidia katika kuweka mazingira na makazi yao kubakia katika hali nzuri na endelevu. Hata hivyo, huweza kuwapunguza wale kanivora wakubwa wa kati ambao ni wengi ili wasiendelee kuwaua wanyama wanaokula nyasi.
Watafiti na waandishi wa makala hii wanatuambia endapo wanyama hawa wakubwa wanaokula nyama wataondolewa au watatoweka katika mfumo wa ikolojia, hali itakuwa mbaya sana kwenye hifadhi zetu na pia kutakuwa hakuna uhifadhi endelevu katika kuwahifadhi wanyamapori na mimea.
Pamoja na umuhimu wote huo wa kiikolojia wa kanivora wakubwa, bado kuna janga kubwa sana linalowakabili wanyama hawa muhimu sehemu mbali mbali duniani hasa Afrika, idadi ya wanyama hawa imeshuka kwa kasi sana, makazi ya wanyama hawa yanaendelea kutoweka na kupotea kabisa, migogoro ya watu na wanyama hawa imeongezeka na hivyo kutishia sana uwepo wa wanyama hawa katika makazi yao.
Katika sehemu kubwa ya bara la Afrika, migogoro ya watu na kanivora ni mikubwa sana na imechangia kuuwawa kwa kanivora wengi sana. Mfano mzuri ni maeneo yanayozunguka hifadhi ya Taifa ya Ruaha, jamii zinazoishi kando kando ya maeneo haya wamekuwa na vita na migogoro isiyoisha baina yao na wanyama hawa wanaokula nyama. Migogoro ambayo kama juhudi za makusudi za kuitatua hazitachukuliwa tutakuwa katika hatari kubwa ya kuwapoteza kabisa wanyama hawa.
Kwa kuwa changamoto kubwa ipo kwa maeneo yaliyo karibu na hifadhi za wanyamapori, mwandishi anapendekeza kuwepo kwa mpango mkakati wa makusudi kabisa wa kuwahifadhi kanivora hawa nje ya maeneo ya mipaka ya hifadhi, yani kuwepo na mipango itakayohifadhi wanyamapori hata katika maeneo ya vijiji ambavyo vipo karibu na hifadhi za taifa.
Ingawa kubuni mipango na mbinu za kuhifadhi kanivora nje ya maeneo ya hifadhi ya Ruaha au hifadhi nyingine yoyote inahitajika uelewa mzuri wa maeneo hayo, kuelewa sehemu ambazo hupendelea kufika na kupita, kujua sababu za wanyama hao kufanya uharibifu kwenye maeneo ya vijiji na pia uelewa wa makazi yao nje ya maeneo ya hifdhi za wanyamapori.
Kwa ujumla ni kwamba mtawanyiko au mgawanyiko wa kanivora wa kubwa na uchaguzi wa makazi yao mara zote husababishwa na uwepo wa chakula chao, yani uwepo wa wale wanyama wanao liwa na kanivora. Hivyo kanivora wakubwa hupendelea kuwa na makazi yao sehemu ambazo zina chakula cha uhakika, kama vile wanyama ambao wanaweza kuwala.
Kwasababu hiyo, wanayama wanaoliwa na kanivora mara nyingi nao hupenda kuwepo sehemu ambazo kuna chakula chao kama vile majani, nyasi na maji. Hivyo tunaweza kusema uwepo wa uoto na mazingira mazuri yenye chakula cha kutosha kwa wanyama wanaokula nyasi huvutia sana uwepo wa kanivora kwenye maeneo hayo. Hivyo basi, mimea ni sehemu muhimu sana kwa uhifadhi wa kanivora wakubwa na pia wanyamapori kwa ujumla.
Hata hivyo watafiti wanadai kuwa kukosekana kwa taarifa za kitafiti za kina kwenye maeneo muhimu ya uhifadhi wa wanyamapori, kumechangia sana kutokuwepo kwa mipango ya kiuhifadhi kwa kanivora wakubwa, taarifa nyingi zilizopatikana ni kwa njia ya kuona moja kwa moja (opportunistic), hivyo kuna taarifa nyingi za makazi na mtawanyiko wa kanivora wakubwa tunazikosa kutoka katika maeneo mengi ambayo yametengwa maalumu kwa ajili ya uhifadhi wa wanyama hawa.
Aidha, taarifa katika makala hii zinaonyesha hali ilivyo katika mandhari ya hifadhi ya Ruaha, au katika hifadhi ya Ruaha hapa Tanzania. Kama ilivyotajwa kuwa hifadhi ya Ruaha ni muhimu sana duniani kwa uhifadhi wa kanivora wakubwa, inakadiriwa kuwa na zaidi ya asilimia 10 ya simba wote waliopo duniani, pia inatambuliwa kuwa ni sehemu yenye ya nne kwa Afrika Mashariki kwa na idadi kubwa sana ya duma, ambayo inakadiriwa kuwa 200 au zaidi, uwepo wa mbwa mwitu ambao wapo katika hatari kubwa ya kutoweka duniani, hifadhi hii inajulikana kuwa ya tatu duniani kwa idadi kubwa ya mbwa mwitu. Hata hivyo ni sehemu yenye idadi ya kuridhisha ya kanivora wengine kama vile chui na fisi madoa.
Pamoja na umuhimu huo wa kitaifa na kimataifa, hifadhi ya Ruaha na mandhari yake bado ndio eneo ambalo halijafanyiwa tafiti za kutosha kuhusu kanivora wakubwa. Kwa kukosa taarifa muhimu za kanivora waliopo katika eneo la Ruaha inapelekea kutokuwa na mikakati ya kuchukua hatua sahihi za kuhifadhi kanivora hawa. makala tunayoichambua inaonyesha wazi kabisa kutokuwepo kwa tafiti au taarifa za uwepo wa kanivora hawa kwenye maeneo hayo, hakuna taarifa za makazi yao, hakuna taarifa za mitawanyiko yao, jambo ambalo litatupa wakati mgumu wa kuchukua hatua na kupanga mipango ya uhifadhi.
Hata hivyo, mradi wa Ruaha Carnivore Project, ambao umejikita katika kufanya utafiti wa kanivora hawa waliopo kwenye eneo hili la Ruaha kwa kushirikiana na serikali, hifadhi ya taifa ya Ruaha na wadau wengine wamesaidi sana na kutoa mwanga kwenye kuchukua hatua katika kuweka mipango ya kiuhifadhi kwa kuishirikisha jamii kwa kiasi kikubwa kushiriki kwenye utafiti huo. Utafiti ambao kwa kiasi kikubwa umelenga maeneo ya vijijini, ardhi ya Kijiji ambako ndio kuna changamoto kubwa ya umavizi wa mifugo kutokana na kanivora.
Nikiwa naelekea mwishoni mwa makala hii, lazima tujue kwa uhalisia wake eneo la Ruaha kuwa na uwepo wa kanivora wengi kwenye baadhi ya maeneo kunasababishwa na vitu vingi sana. Lakini makala tuliyoichambua inaonyesha kuna kitu mihimu sana ambacho kwa upande wa Ruaha ndio husababisha kuwepo kwa mtawanyiko mkubwa wa kanivora wakubwa, uwepo wa mto Ruaha Mkuu na sehemu nyingine zenye maji ya uhakika karibu na hifadhi ya Ruaha ndio kigezo kikuuu cha uwepo wa kanivora wakubwa kwenye maeneo hayo.
Wanyama wanapenda maji na wanapenda kuishi sehemu ambazo zina upatikanaji wa maji, hivyo maeneo ya mto Ruaha ndio yana wanyama wengi kulingana na taarifa zilizopo. Na kwasababu mto upo karibu na maeneo ya hifadhi ya jamii yani WMA na ardhi ya Kijiji kutoka katika hifadhi ya taifa ya Ruaha, inakuwa haimpi shida simba na wanyama wengine kutembea umbali huo kutafuta maji na chakkula chake. Na pale wanapovuka mto tu, uwezekano wa kuingia katika maeneo ya Kijiji ni mkubwa na hapo ndipo ilipo changamoto na migogoro huanzia.
Hivyo ndivyo pia kwa kanivora wengine na hata wanyamapori wengine. Licha ya uwepo wa mto kama kivutio kikuu cha kanivora katika maeneo ya vijiji, pia hata uwepo wa mvua nao umetajwa kuwa ni sababu ya kuwepo kwa kanivora katika maeneo ya vijiji. Pia makala hii inamalizia kwa kuonyesha kuwa upande wa mashariki wa hifadhi ya taifa ya Ruaha ndio huathirika zaidi na changamoto za uwepo wa kanivora kwenye maeneo ya vijiji vyao.
Kwa kutambua hilo, au kwa kupata ufahamu huu kidogo kuhusu hali halisi ilivyo katika hifadhi ya Ruaha na mandhari yake, bado kazi kubwa ya kufanya inahitajika katika uhifadhi wa wanyamapori hawa. Kwa kuwa kanivora husababisha hasara pindi wanapoingia kwenye maeneo ya vijiji na kuua mifugo na hata maisha ya watu kuwa hatarini, tunatakiwa sasa kuweka mipango na mikakati ya uhifadhi wa wanyama hawa.
Pia ikumbukwe kuwa kanivora wanaposababisha hasara kwa jamii hasa wafugaji hali ya kutaka kulipiza kisasi ni kubwa sana kwa jamii hizi, kuna matukio ya uuaji wa kanivora katika eneo hili la Ruaha kutokana na kanivora kuua mifugo ya wafugaji, kuna matukio ya uwekaji sumu ili kuua kanivora katika eneo hili, yote hayo huchangia sana katika kupungua kwa kanivora katika eneo hili muhimu duniani kwa uhifadhi wa kanivora.
Kwa kutambua hili, naiomba serikali ya Tanzania, wadau wa uhifadhi, watafiti, na pia mashirika ya uhifadhi na yale yanayopenda uhifadhi wa maliasili kushirikiana kwa pamoja katika kuweka mipango ya kudumu katika uhifadhi wa kanovora wakubwa. Pia kwasababu eneo hili la Ruaha linatajwa sana kuwa ndio eneo muhimu zaidi duniani kwa kuwa na kanivora wakubwa na pia wanyamapori wengine, hii itupe hamasa na dhamira ya dhati ya kuwekeza katika kufanya utafiti wa wanyama hawa na kuweka mipango ya kuwahifadhi kanivora hawa na makazi yao.
Naamini kabisa kufikia hapa umepata kitu kikubwa cha kukusaidia, na pia ni vizuri ukaisoma makala hii niliyoichambua na kukushirisha yale muhimu. Nimetumia muda mwingi kusoma na kuainisha yale ambayo tunatakiwa kuyajua na kuchukua hatua pale inapobidi.
Asante sana kwa kusoma makala hii,
Mchambuzi wa makala hii ni
Hillary Mrosso
+255 683 862 481