Habari ndugu msomaji wa makala za uhifadhi wa wanyamapori na utalii, karibu tena leo kwenye makala muhimu sana ambayo nimepanga kukuandikia mambo muhimu yatakayokufanya uchukue hatua katika kutimiza moja ya ndoto zako za miaka mingi.
Wakati nafikiria nini ambacho naweza kuwashirikisha marafiki zangu na wasomaji wenzangu wa makala za Wildlife Tanzania, nimekumbuka na kuamua kuwaandikia makala hii muhimu. Ili kama unaweza kuchukua hatua, uchukue na uache alama katika mwaka huu 2018.
Kama ilivyo ada, leo sitaandika kuhusu uhifadhi na ujangili wa wanyamapori; nitaandika kuhusu kutembelea hifadhi za wanyamapori na sehemu nyingine zenye vivutio vya kitalii. Tanzania tumebarikiwa kuwa na sehemu nyingi sana zenye maeneo yenye mvuto sana, ambayo yametapakaa kila kona ya nchi yetu, ukienda Kaskazini utakutana na mambo ya kushangaza, ukienda Kusini utakutana na mambo mazuri ambayo ulikuwa hujui kama yapo, ukienda Mashariki utaona maajabu ya Mungu, ukienda Magharibu ndio utakaa na kufikiria kama kuna vivutio vya aina hiyo katika nchi yetu ya Tanzania.
Vivutio na ufahari wote uliopo Tanzania sio kwa ajili ya kikundi cha watu fulani tu, au kwa ajili ya wazungu tu, au kwa ajili ya matajiri tu; vivutio na ufahari uliopo hapa Tanzania ni kwa ajili ya kila mtanzania, ni haki yako ya msingi kabisa kuwa mtalii na kutembelea vivutio vilivyopo nchini Tanzania, ni haki yako ya kuzaliwa kutembelea na kufurahia uzuri na maajabu ya nchi yako.
Kufikiri kuwa utalii ni kwa ajili ya wazungu au wageni kutoka nchi za nje, ni mawazo potofu kabisa, utalii ni kwa ajili yetu, ni kwa ajili yako mtanzania mwenzangu, utalii unaanza na sisi wenyewe kabla ya kwenda kuwanufaisha watu wengine. WEWE PIA UNAWEZA KUWA MTALII NA UKAPEWA HESHIMA ZOTE.
Na hapa simaanishi watalii kutoka nje ya nchi hawafai, la hasha, watalii na wageni kutoka nje ya nchi ni muhimu sana, katika sekta hii muhimu hapa Tanzania, tunatakiwa kuijenga sekta ya maliasili na utalii ili iweze kuwa kivutio kikubwa kwa wazawa na wageni kutoka nje.
Ndio maana nimesukumwa kuandika makala hii, ni ili kuweka mitazamo yetu sawa kuhusu suala la kutalii, watu wengi linapokuja suala la kutalii huwa wanajitoa haraka sana na kuona wao hawastali kuitwa watalii wala kufanya utalii. Huu ni utamaduni wa ajabu na wa kizamani sana, tunatakiwa kuchangamkia fursa hizi kwa ajili yetuna watoto wetu.
Hivyo basi, nakushauri, nakusihi kabla ya mwaka huu kuisha chagua kuwa mtalii, najua mwisho wa mwaka watu wengi wanaenda kwenye mapumziko, hivyo wanakuwa na muda mzuri wa kufikiria kuhusu kutembelea ndugu, kutembelea sehemu mbali mbali nk,
Hivyo ni wakati wako kutafuta sehemu ya kwenda kutembelea, unaweza kutembelea mbuga za wanyama, sehemu za kihistoria kama vila makumbusho, miji mikongwe kama Zanzibar, Bagamoyo, Kilwa na sehemu nyingine nyingi. Pia unaweza kutembelea fukwe za bahari na kupata hewa safi na upepo mzuri, kwa kweli maeneo ya kutembelea yapo mengi sana.
Panga kutembelea vivutio, hifadhii za wanyama na sehemu nyingine ambazo hujawahi kufika, nenda na Watoto wako, mwenzi wako, Rafiki yako, familia yako, au unaweza kwenda kutalii mwenyewe. Jiandikie kwenye kijitabu chako, kwamba nitamaliza mwaka huu 2018 kwa kutembelea sehemu hii, au ile.
Naamini, utapanga kutembelea sehemu yoyote unayotamani. Sehemu nyingi za kutalii kwa watanzania ni gharama nafuu sana, acha alama mwaka huu, timiza malengo na ndoto yako ya siku nyingi ya kuwa mtalii, tenga bajeti kuanzia sasa ili kutimiza malengo yako.
Endapo utapata changamoto yoyote, unataka kujua zaidi kuhusu gharama, utaratibu na mambo mengine kuhusiana na kutalii sehemu yoyote usisite kuwasiliana nami, mawasiliano yapo hapo chini. Wote tunaweza kuwa watalii, uzalendo ni kufanya jambo kama hili ndani ya nchi yako mwenyewe.
Karibu sana tutalii na tufurahie uzuri na uumbaji wa Mungu katika nchi yetu ya Tanzania.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania