Mafanikio yoyote ya binadamu yamejengwa kwenye misingi ya kujifunza, kujifunza ndio msingi wa maendeleo kwenye nyanja zote za maisha, pia lazima tukubaliane kujifunza kokote lazima kuendane na vitendo, yani kufanyia kazi kile ulichojifunza au kukisoma au kukisikia. Leo nimekaa chini kuandika makala hii ili kukufahamisha baadhi ya mambo muhimu sana yatakayokufanya kuwa na ufanisi kwa kile unachokifanya. Lakini nimelenga kwa wanafunzi, hasa wale wanaosomea maswala ya wanyamapori. Kwa sababu naandika makala hii kwa uzoefu wangu mwenyewe kwenye mafunzo kwa vitendo. Kuna baadhi ya vitu wanafunzi wengi hawafahamu, au wanavipuuzia au wanajua lakini hawafanyi, makala hii lengo lake ni kukukumbusha cha kufanya ili usiachwe nyuma. Hivyo karibu sana kwenye safari yetu ya kupata ufahamu na maarifa.

Nitaanza na mambo yote muhimu unayopaswa kuyajua na kuyafanya ili unapojiandaa au unapokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo baada ya kumaliza masomo yako kwa nadharia basi ujue nini cha muhimu zaidi ili ufurahiye na kuelewa vizuri majukumu yako.

  1. Ielewe vizuri kozi unayosoma

Kitu cha kwanza unapokuwa chuoni, shuleni au kwenye mafunzo yoyote, elewa kwa undani kabisa kozi unayoisoma, elewa lengo la kusoma hiyo kozi ni nini, elewa malengo ya hiyo kozi baada ya kumaliza kuisoma ni nini, elewa mambo yote ya msingi kabisa unayoopaswa kwenye hiyo kozi yako. Ili uelewe yote hayo inatakiwa ufanye kazi, fuatilia mtaala wa masomo yako, fuatilia ukubwa na pointi za hiyo kozi, elewa kabisa kama hiyo kozi baada ya kuisoma kama ina mafunzo kwa vitendo au haina. Ichimbe ifahamu sana hiyo kozi/masomo yako, uelewa wako kwenye hiyo kozi utakupa hamasa sana kwenye kuuliza maswali, kuifuatilia zaidi. Na pia hata unapokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo utaelewa nini kinaendelea na pia utashiriki kikamilifu kwenye kila kinachoendelea unapokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo (field practical). Ukiwa mvivu utakuwa huelewi mambo yanavyokwenda, kuna wanafunzi wengine hawaingii darasani kujifunza, unakuta mwalimu/ mhadhiri yupo darasani lakini yeye yupo sehemu nyingine mbali kabisa na hashiriki vipindi muhimu vinavyo muhusu, na pia hata hafuatilii ni nini cha msingi kimefundishwa, hivyo huwa na uelewa mdogo sana kwenye somo husika. Na mara nyingi watu wa aina hii ndio wanaokuwa wasumbufu hasa wanapokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo, kwa sababu hawaelewi nini kinaendelea. Hivyo basi kwa mwanafunzi au mtu yeyote unayesoma, zingatia masomo yako uyaelewe vizuri ili utakapo kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo usipate shida.

  1. Jiandae kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo (field practical)

Kwa uzoefu nilio nao wengi huwa hawajiandai, inapofika kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo, ukiona maandalizi ujue ni kwa ajili ya usafiri, chakula, malazi, nk. Hali hii nimeiona sana nilipokuwa chuoni, hasa kwa wanafunzi wanaosoma maswala ya usimamizi wa wanyamapori. Ni wachache sana au hakuna kabisa wanaojiandaa kitaaluma zaidi wanapokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo. Hapa kwenye kujiandaa namaanisha wewe mwenyewe umejipangaje kwenda kupata maarifa na ujuzi zaidi kwenye yale uliyojifunza? Unajua ni maswali gani utakayo kwenda kuuliza? Unajua ni kwa nini mnaenda kufanyia mafunzo kwenye eneo hilo? Unao mwongozo wako binafsi kwenye mafunzo? Je, unavyo vifaa vyote muhimu kwa ajili ya kufanya mafunzo? Hapa namaanisha ujiandae kiakili zaidi, akili yako inatakiwa iandaliwe mapema ijue cha kufanya. Andaa vifaa vyako binafsi, angalia nini unahitaji kuwa nacho ili masomo yako uyaelewe vizuri, beba vifaa vyako binafsi, kalamu za kukutosha, daftari, kitabu, kamera na hadubini kama unayo. Unapojiandaa kwenda field nenda kama unakwenda kuifanya wewe mwenyewe binafsi ( hasa kwa wanafunzi wanaosoma usimamizi wa wanymapori ). Unajua kwa baadhi ya kozi za vyou mbali mbali, kwa mfano wanafunzi wanaosoma masuala ya wanyamapori mara nyingi huwa wanaenda kwenye mafunzo kwa vitendo wote, yani wote wanaenda sehemu moja na kukaa hapo hadi wamalize, hivyo baadhi ya wanfunzi hujisahau sana na kutengeneza utegemezi wa vifaa na hata kwenye ufanyaji wa kazi, wanawategemea wanafunzi wengine. Hii sio nzuri hata kidogo, unatakiwa kuwajibika na kufanyia kazi elimu yako, usipende mwingine ndio akufanyie kazi zako binafsi, au majukumu yako ya msingi, pambana mwenyewe kwenye elimu yako upate unachokitaka, acha kuwatwisha wengine wajibu wako wa msingi.

  1. Ukiwa kwenye mafunzo

Tumesha angailia mambo muhimu mawili, kuielewa kozi yako au masomo yako vizuri na kujiandaa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, sasa hapa tuangalie kwenye kiini chenyewe cha makala hii, ukiwa kwenye mafunzo, umeilewea kozi yako, umeshajianda wewe mwenyewe kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo sasa twenda ndani kabisa. Na nikwambie tu mapema endapo hatua mbili za mwanzo hukuzifanya, au hujazielewa unapofika sehemu ya mafunzo kwa vitendo utaishia kuwa mtazamaji tu. Hii ndio sababu nimekuandikia makala hii muhimu rafika yangu, kwasababu najua na nimeona makosa makubwa sana wanayoyafanya wanafunzi wanapotaka kwenda kwenye mafunzo. Hivyo kwa kupata ufahamu huu utakusaidia kuchukua hatua muhimu kwenye kuboresha maisha yako ya kielimu popote pale unaposoma. Sasa ngoja nianze kuelezea kipengele hiki muhimu. Unapofika sehmu ya mafunzo, cha kwanza elewa vizuri mazingira yako, au mazingira mliyofikia, kama mmeenda darasa zima unatakiwa kuwa mwepesi kuelewa haraka mazingira yako, pangilia ratiba yako na vitu vyako, angalia mnaanza na jambo gani kufanyia mafunzo,halafu angalia kwenye jambo hilo mnalotaka kufanyia mafunzo kwa vitendo linataka uelewe kitu gani, ili ikusaidie uulize maswali gani au kama hukuelewa vizuri uanzie wapi.

Unapokuwa kwenye mafunzo au mkisha anza mafunzo, acha kushanga shangaa, fanya yaliyokupeleka kweye mafunzo. Pia zingatia hili, endapo mtapangwa kwenye makundi makundi angalia sana kundi lako ni la watu wa aina gani, kisha mjiwekee utaratibu wa kufanya kazi kwa pamoja asiwepo mtu wa kutegea au anayekimbia majukumu yake, gawinaneni majukumu manapokuwa kwenye makundi yenu, mtu mwenye mizaha na hataki kufanya kazi mtoeni mara moja, wekeni misimamo yenu, wekeni malengo yenu, kiongozi wa kundi anatakiwa kuwa muwajibikaji, ili kila mtu afanya kila alichopangiwa, wekeni muda wa kutosha wa kujadili kazi yenu na maswali mliyopewa, mnatakiwa kuwepo wote wakati wa majadilianao na wakati wa kuwasilisha mpangiane kila mtu awasilishe sehemu yake, na wakati wa kuandka ripoti kila mtu ashirki. Jijengeeni nidhamu kwenye kile mnachokifanya hata kama ni kidogo namna gani. Wekeni utaratibu kila mnapotembelea na kufanya utafiti au kujifunza jambo lolote kila mmoja wenu awe na kitu alichojifunza ili mfanye kazi zenu kwa wakati. Muda wa kazi kuwa kwenye kazi, heshimu kila hatua na nafasi ya kujifunza inayotokea mbele yako.

Jambo jingine muhimu unapokuwa kwenye kituo au sehemu ya mafunzo, mtumie vizuri mwalimu/ mhadhiri unayekuwa naye, kumbuka yeye anafahamu mambo na vitu vingi kuliko wewe, muulize maswali mengi, kila kitu unachokiona huko kielewa kama huelewi uliza kwa wahusika. Kwa wanafunzi wanaofanyia mafunzo kwa vitendo porini, kuna mambo mengi mlioyosoma yanayoendana na mnachokikuta huko, hivyo kuwa mtulivu na jifunze kwa kila unachokiona na kwa watu unaokutana nao huko.

Onyesha nidhamu na hamasa kwenye ufanyaji wako wa kazi mnapokuwa sehemu ya kituo, kumbuka watu wanakuona, mwalimu wako anakuona, na pia hata wanafunzi wenzako wanakuona, usikubali kuonyesha uzembe au uvivu kwenye kazi uliyopewa. Wajibika, watu ni fursa, watu watakupa fursa watu watakusaidia. Amua kuwa mwanafunzi mzuri, wajibika kwa elimu yako mwenyewe, usikubali kumpa mtu majukumu yako ya kielimu, fanyia kazi elimu yako upate haki yako kweli, maana kuna wengine ni wavivu na wazembe sana mazoezi na kazi wanazopewa na walimu wanasubiria wengine wafanye na wao ndio waangalizie, wengine wanakopi na kuchukua kazi za watu. Wewe ni muhifadhi, achana na njia za mkato kwenye elimu yako. Ipiganie na kifanya kazi yako mwenyewe, mwisho wa siku unakuwa na elimu na cheti chako kweli ulichokifanyia kazi kweli na sio njia za mkato na uongo uongo. Heshima  yako ipo kwenye kazi ulizofanya kwa mikono yako mwenyewe.

Kuna mengi sana ya kuandika ili kupeana mwanga kwenye kila tunacho kifanya, kama mnavyojua blog hii inahusu mambo ya wanyamapori, wildlife Tanzania, nimeandika makala hii nikilenga wanafunzi wanaosomea wanyamapori ili wawe na msingi mzuri kwenye kazi na uelewa wao wa mambo, na pia ni kwasababu ya makossa niliyoyaona yakifanywa sana na wanafunzi wengi kwenye eneo hili. Lakini pia hata kama ni mtu mwingine na wanafunzi wengine inaweza kuwa msaada hii makala. Hivyo kama umesoma usisite kumshirikisha mwenzio maarifa haya.

Kila la kheri kwenye maisha yao ya kielimu.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569

hillarymrosso@rocketmail.com