Kati ya miaka ya 1970 na 1990 maelfu kwa maelfu ya tembo waliuwawa kwa ajili ya meno yao na kuacha idadi ndogo sana ya tembo inayokadiriwa kuwa 300,000- 600,000. Idadi kubwa ya kupungua kwa kwa idadi yao inatajwa zaidi maeneo ya Magharibu na Mashariki mwa bara la Afrika.
Rafiki yangu unayesoma makala hii jua kuwa makala hii ni matokeo ya uchambuzi wa ripoti inayojulikana kama ELELPHANT IN THE DUST, THE AFRICAN ELEPHANT CRISIS, iliyoandikwa na kuchapishwa mwaka 2013. Taafa zilizopo kwenye makala hii ni uchambuzi wa yale muhimu ambayo yanaweza kutusaidia kama wasomaji na wale wanaohusika na uhifadhi na usimamizi wa maliasili za nchi zetu. Karibu tujifunze pamoja;
Kufuatia kupungua kwa idadi kubwa ya tembo miaka ya 1980 na kitendo cha CITES kuingilia kati hali hiyo na kufunga kabisa masoko na biashara ya meno ya tembo. Idadi ya tembo ilianza kuongezeka kwenye baadhi ya nchi zenye wanyama hawa na ilipofika mwaka 2007, idadi ya tembo ilikadiriwa kuwa 470,000- 690,000.
Tangu wakati huo, hali ya mambo haikuendelea kubaki hivyo kama wengi tulivyotarajia, kwa mujibu wa ripoti za kitafiti kwenye eneo hili zinasema ujangili ulikithiri kwa kasi ya ajabu kuanzaia miaka ya 2006, na kupelekea kushuka sana kwa idadi ya tembo waliopo Afrika ya Kati na baadhi ya maeneo ya Magharibi mwa Afrika. Hata hivyo idadi ya tembo imeendelea kuwa nzuri na kuongezeka kwa baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika.
Wakati hayo yakiwa ni mazuri kwa upande wa Kusini mwa bara hili, idadi ya tembo katika ukanda wa Mashariki na Kusini Mashariki mwa bara la Afrika imekuwa ikididimia kwa kasi kubwa sana kutokana na ujangili uliokithiri sana. Pamoja na hayo kuwa yakiendelea, takwimu za hivi karibuni yani wakati wa kuandika kwa ripoti hii mwaka 2013, jumla ya idadi ya tembo wote inakadiriwa kufkia 419,000- 650,000 hata hivyo idadi kubwa ikiwa imechukuliwa kwa upande wa Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Makadirio ya nusu ya tembo wote wanapatikana katika ukanda wa Kusini mwa Afrika, wakati chini ya asilimia 30 wanapatikana Mashariki mwa Afrika, Magharibi mwa bara hili ndio sehemu yenye idadi ndogo zaidi ya tembo kuliko eneo lolote la Afrika yaani asilimia 2 tu. Hata hivyo ingawa tunajaribu kuweka makisio tu ya taarifa na idadi ya tembo katika maeneo haya, inaweza kuwa sio namba halisi ya uwepo wa tembo, lakini ni namna nzuri ya kujua tuna idadi gani ya tembo katika eneo hili.
Mwenendo wa tembo kwa karne ya 20
Ni ukweli ulio wazi kuwa ujangili ndio umepunguza tembo kwa kiasi kikubwa hasa katika eneo la Magharibi mwa Afrika. Katika kipindi cha miaka ya 1970 na 1990, picha na ripoti nyingi zilionyesha maelfu ya mizoga ya tembo wasiokua na meno yao ikiwa imetapakaa ndani na nje ya hifadhi za wanyama hawa katika bara hili la Afrika.
Kuongezeka kwa uelewa wa dunia kuhusu masuala ya ujangili, ikifuatiwa na kampeni mbali mbali zilizoshika kasi kupitia vyombo vya habari mbali mbali hali hii ilipelekea Shirika la kimataifa linalosimamia Makubaliano ya Kudhibiti na Kuzuia Biashara za Wanyama na Mimea Mwitu ambayo ipo Hatarini Kutoweka yaani CITES, kuingilia kati na kufunga kabisa biashara za kimataifa za meno ya tembo mnamo mwaka 1989.
Hata hivyo, kabla ya mwaka 1989 tembo wa Afrika waliorodheshwa na CITES kuingia katika jedwali namba II yani appendex II, hii ikwa na maana kuwa biashara za nyara za tembo ziliruhusiwa kufanyika kihalali kabisa chini ya uangalizi wa mamlaka husika za nchi wanachama.
Miaka ya 1870 na 1980, kulikuwa na kiwango kikubwa sana cha ujangili katika bara hili, hii ni kutokana na mahitaji ya nyara hizi za meno ya tembo katika masoko makubwa ya nchi za Ulaya, Marekani na Japani. Biashara za meno ya tembo zilifanywa na makampuni halali ya kibiashara ambayo mara kwa mara yaliwausisha maafisa wa serikali.
Baada ya hayo kuendelea kufanyika, jumuiya za kihifadhi ziliingilia kati ikifuatiwa na mashinikizo ya CITES kufunga biashara ya meno ya tembo, hii ni baada ya kuona ujangili unakithiri sana hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa kufanya hayo, baada ya miongo miwili tu hali ikawa nzuri katika uhifadhi wa tembo Mashariki mwa Afrika, mambo akwa mazuri tembo wakaongezeka, kukawa na ahueni kidogo.
Hali ya mambo haikuendelea kama tulivyotarajia, kwani Magharibi mwa Afrika kulikuwa na kilio kikuu cha kushamiri kwa ujangili, hii ni kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni ambazo zinaeleza hali mbaya upande huo wa Afrika, na watabiri wa mambo wanaesma hali hiyo ikiachwa bila kuchukua hatua basi watawapoteza tembo wote kwenye maeneo yao. Hata hivyo si habari nzuri pia kwa upande wa Mashariki ambako kunasifiwa kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo, taarifa za hivi karibuni zimebaini kuongezeka kwa ujangili katika eneo hili.
Katika ukanda huu wa Magharibi mwa Afrika kumekuwa na kushamiri kwa ujangili tangu kuanza kwa karne ya 20, hali ambayo imewapunguza sana tembo katika eneo hili, kwa miaka ya 1980 walikaridiwa kuwa na tembo 4000, .lakini kwa sensa na taarifa za mwaka 2007 ilionekana kuwa kuna idadi ya tembo7500, wakati taarifa za hivi karibuni 2013 zikionyesha ni tembo 7100 walopo katika eneo hili.
Halikadhalika, taarifa za tembo kwa eneo hili la Magharibi mwa Afrika zimekuwa zikitiliwa mashaka kuwa sio sahihi sana, hii ni kutokana na uoto na makazi ya tembo katika eneo hili. Eneo kubwa la upande huu wa Afrika ni misitu minene ambayo sio rahisi kufanya sensa sahihi ya wanyama na tembo wanaoishi humo. Kutokana na hali ya usalama wa nchi za pande hizi inasemekana kwa kiasi kikubwa tembo wameuwawa sana kuliko inavyodhaniwa na wengi.
Kwa upende wa Mashariki mwa bara hili, ambapo ndipo kunadhaniwa kuwa na idadi kubwa sana ya tembo, nako hakujasalimika, ujangili ulitibua kabisa maisha ya wanyamapori na kuancha hifadhi zetu kuwa na mizoga iliyoenea kila mahali, ilikuwa ni hali ya kutisha na isiyo na matumaini katika sehemu hii iliyokuwa kama bustani ya Edeni kwa kuwa makimbilo na sehemu salama ya kuishi kwa wanyama hawa. hali hii inatajwa kutokea katika kipindi cha miaka ya 1970 na 1980.
Kwa hifadhi muhimu kama Tsavo nchini Kenya na Pori la Akiba la Selous nchini Tanzania zilihifadhi maelfu ya tembo na mamilioni ya wanyamapori wengine, nazo zimeingia katika rekodi ya kuhusishwa kwa mambo ya ujangili yaliyokuwa yakiendelea sehemu hizi na kusababisha anguko au kushuka kwa kasi kwa idadi ya tembo katika eneo hili la Afrika Mashariki. Kushamiri kwa mauaji haya ndio kulikopelekea juhudi za kimataifa kufunga biashara ya meno yatembo kwa makubaliano ya CITES.
Ingawa taarifa zilizopo kwenye makala ni za muda kidogo, bado zinaweza kuwa na uhalisia na kutupa picha kubwa namna ujangili unavyomaliza tembo na wanyamapori wengine muhimu. Hivyo naamini kuna ujumbe muhimu ambao jamii itaupata na kufahamu kinachoendelea kwenye sekta ya maliasili za nchi zetu. Hivyo usiache kumshirikisha mwingine makala hii muhimu naye ayafahamu mambo haya.
Ahsante sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho!
Uchambuzi huu umeandaliwa na;
Hillary Mrosso
+255 683 862 481/255 742 092 569