Korongo la Kihansi linapatikana ndani ya hifadhi ya milima ya hifadhi ya Taifa Udzungwa upande wa mashariki . Korongo hili linasifika kwa wembamba na urefu wake kati ya mita 300 hadi 1150m kutoka usawa wa bahari. Kiwango cha mvua kwa mwaka ya pata 1500mm na nyuzi joto 160c hadi 310c.
Mbali na kuwepo kwa aina nyingi za vyura katika nchi hii, chura huyu wa Kihansi ni wa pekee kwa sababu hapatikani sehemu yoyote duniani isipokuwa katika korongo la mto Kihansi. Na Kama ijulikanavyo kwamba vyura wengi hutaga mayai na kuyaacha majini ili kuanguliwa, lakini kwa upande wa chura huyu wa Kihansi ni tofauti kutokana na sifa yake ya kuzaa, chura huyu huzaa watoto kama vile wazaavyo wanyama wanaonyonyesha ‘mammalia’.
Chura wa Kihansi aligundulika mnamo mwaka 1996 katika maporomoko ya maji yaitwayo Mhalala yaliyopo ndani ya milima ya Udzungwa katika wilaya ya Kilombero mkoa wa Morogoro. Anaishi katika mazingira ya maji yanayotiririka na kutoa mvuke mwingi ndio maana kiingereza wanaitwa ‘spray toad’ na kutokana na sehemu wanayopatikana ndio inaleta muunganiko wa jina ‘kihansi spray toad’ kitaalamu anajulikana kama ‘Nectophrynoideis asperginis’.
Huyu ndiye Chura anayezaa; Kihansi Spray toad
Udogo wao yapata inchi tatu au nne kwa chura mkubwa pia hawapitii hatua za ukuaji kama vyura wengine. Chura jike hukutana na chura dume na mayai yanarutubishwa ndani na kuzaa vitoto ambavyo vidogo kati ya 3-15 kwa kila uzazi wakiwa porini. Na wakiwa katika maeneo yaliohifadhiwa na binadamu wana uwezo wa kuzaa vijitoto kati ya 8-30 kama ilivyoripotiwa. Wanakaa na mimba katika muda wa miezi mitatu(3), wastani wa kuishi yapata miaka minne(4).
Vyura hawa wanapendelea kula aina mbalimbali za wadudu na hawana uwezo wa kuwatafuna kwa maana hiyo, mara tu wawakamatapo wadudu hao wanawameza. Wadudu hao wanatakiwa wawe wadogo na sio wakubwa kwa sababu wakiwa wakubwa hushindwa kuwameza, Chura hawa hupendelea zaidi kula minyoo midogo, buibui na aina nyingine ya Wanyama wasio na uti wa mgongo (invertebrate) ambao kitaalamu wanajulikana kama othoziora, isopods nk. Changamoto katika kuwatunza vyura hawa wakiwa wamefugwa (captivity) ni kama zifuatazo; tatizo la kujamiiana kati ya ndugu wanaofanana hivyo kuwafanya wawe na vinasaba au ”gene” dhaifu ambazo huweza kuwafanya wasiweze kustahimili mabadiliko ya mazingira, na pia kuwafanya miili yao kushindwa kuwa na kinga ambazo zaweza kupigana na magonjwa nyemelezi.
Mwaka 1996, timu iliyojumuisha wataalamu wa Elimu ya wanyama na Uhifadhi wa Wanyamapori kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mchakato wa kufanya tathmini ya athari za mazingira (Environmental Impact Assessment) kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa bwawa la uzalishaji wa umeme wa Kihansi. Ndio yalitolewa mapendekezo ya namna ya kuwalinda viumbe hawa. Mwaka huohuo ambao ni 1996 karibu asilimia 90 ya maji ya mto Kihansi yalibadilishwa uelekeo kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kitu kilichosababisha upungufu mkubwa wa maji katika bonde la Kihansi, ambayo ndio hasa makazi ya vyura hawa.
Mradi wa umeme uliyaharibu vibaya kama sio kutaka kuyapoteza makazi ya kivutio hiki muhimu na ya kipekee. Licha ya kubadili mwelekeo wa maji , inaaminika kuwa kulikuwa na upungufu mkubwa wa hewa ya oksijeni ambayo ni muhimu kwa uhai wa viumbe wote, vilevile inaripotiwa kwamba, kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa ‘fangas’ kwa lugha ya kitaalamu unajulikana kama “Chytridomycosis” ulioenezwa na viatu (mabuti) na Wahifadhi wa Mazigira pamoja na wataalamu katika kipindi cha utafiti. Kikubwa kuliko yote hakukuwa tena na uwiano wa kimazingira katika makazi hayo. Yote haya yalipelekea kupungua kwa vyura wa Kihansi kwa idadi inayokadiriwa kutoka vyura 50,000 hadi 12,000.
Ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 2000 ambapo vyura 500 walisafirishwa kutoka bonde la Kihansi,Tanzania kwa ndege maalumu kwenda nchini Marekani katika hifadhi ya Bronx (Bronx Zoo) na baadae kwenye hifadhi ya Taledo (Taledo Zoo) lengo likiwa kuwanusuru vyura hao wasipotee kwa kuwaweka katika mazingira yaliyo na hali karibu sawa na ile ya bonde la Kihansi kabla ya kuharibiwa na mradi wa umeme. Gharama kubwa iliyotumika kukamilisha zoezi la uhamishwaji wa vyura hawa pamoja na uhafadhi wake huko Marekani, hakika linatoa picha ya thamani ya uwepo wa kila kiumbe hapa duniani.
Mwaka 2009 Muungano wa Kimataifa kwa Uhifadhi wa Asili – International Union for the Conservation of Nature (IUCN) ilitangaza rasmi kuwa vyura wa Kihansi kuwa miongoni mwa viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka katika pori ,hivyo kutoa wito kwa jamii ya kimataifa na wanaharakati wa mazingira duniani kuwalinda Vyura hawa ambao ni maliasili adimu duniani. Hata hivyo kumekuwepo na faraja juu ya maisha ya vyura hawa katika kipindi cha maisha yao huko ugeninii. Hii inatokana na ripoti kuwa idadi ya vyura hao iliongezeka inayokadiriwa kufikia vyura 7,000.
Mwaka 2010 vyura 100 walirudishwa Tanzania. Waliifadhiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya kitengo cha wanyamapori kabla ya majaribio ya kuwarudisha katika makazi yao ya awali. Mwaka 2011 walirudishwa kihansi. Mwaka 2012, idadi yao ilionekana kuongezeka hadi kufika 2600 na ndani ya mwaka huo huo idadi hiyo ilionekana kupungua na hivyo kuwafanya wahifadhi waweze kuwahifadhi katika makazi ambayo sio asili yakiwa na hali ya uasilia kwa vyura hao“captivity”. Mitambo mbalimbali ikiwemo uwekaji wa mabomba ulifanywa katika korongo la mto Kihansi ili kuweza kurudisha mazingira asilia ya vyura hao. Hivi sasa mradi wa kuweka mabomba yanayo toa mvuke kwa ajili ya kurudisha uoto asilia na kurudisha mazingira asilia ya vyura hawa umeshakamilika ingawa bado hawajarudishwa katika mazingira yao asilia.
Mabomba yanayotoa mvuke kwa ajili ya kurudisha uoto asilia na kurudisha mazingira asilia ya vyura hawa kama inavyoonekana katika picha hapo juu.
Maadui wa chura huyu;-ukiachilia mbali magonjwa nyemelezi yanayomuathiri chura huyu pia kuna viumbe ambao wanahatarisha maisha yake. Viumbe hivyo ni kama vile nyoka,ndege na chura aina ya A.yakusin kama anavyojulikana kwa kitaalamu. Sifa kubwa ambayo inapelekea jamii yote ya Tanzania hasa wahifadhi wa wanyamapori na serikali kutupia macho yao yote katika viumbe hawa ni kutokana na taarifa kuwa wametoweka katika makazi yao ya asili na hivyo kupatikana katika sehemu maalumu ya kuwatunza.
Vyura hawa kwani wana athiriwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuwaweka wao hatarini zaidi. Kupungua kwa maji katika bonde la Kihansi kutokana na uzalishaji wa umeme ilikua ndio chanzo lakini kwa sasa tunaona dhahiri madadiliko ya hali ya hewa na kuongezeka kwa joto duniani inaweza kuhatarisha zaidi uwepo wao. Athari hizi zinaweza kutokea kutokana na kukata miti bila ya kuipanda hivyo huweza kuathiri zaidi mtiririko wa maji katika bonde hilo pia hata ugonjwa wa fangus kuweza kuenea kwa kasi zaidi.
Mtambo wa kuzalisha umeme uliopo kwenye bonde la mto Kihansi ambao ni moja kati ya sababu zilizosababisha uharibifu wa makazi ya vyura hawa kwa kutumia asilimia tisini(90%) ya maji ambayo yalikuwa yanategemewa kwa ajili ya uhai wa vyura hawa
Ukiachilia mbali mradi wa umeme, mimea vamizi pia inaweza kuwa chanzo cha uharibifu wa makazi ya chura huyu. Mimea hii ni kama vile mitiki ambayo ndiyo changamoto kubwa katika hifadhi ya milima ya Udzungwa kutokana na sifa zifuatazo; inatumia maji mengi hii inasababishwa kuwa na mizizi iliyo na uwezo wa kufika chini sana na kuweza kunyonya maji hivyo kufanya eneo hilo kuwa kavu na kame, pia mimea hiyo vamizi kuwa na sifa ya kuzuia mimea asili kuota na ,pia ina uwezo wa kuvumilia mabadiliko ya hali ya hewa na hivyo kuzaliana kwa haraka.
Vyura hawa wenye umbo dogo wana eneo dogo la kuishi linalokadiriwa kuwa heka tano hivyo uharibifu kidogo wa mazingira unaweza kusababisha kupotea kwao kwa sababu hawawezi kuishi katika mazingira tofauti na makazi yao asili. Pia hawana uwezo wa kuadapt kirahisi katika mazingira mapya hivyo kuwaweka vyura hawa wadogo katika kundi la wanyama ambao wamepotea katika mazingira yao asili.
Kukosa wataalamu ambao wanaweza kuandaa chakula kwa ajili ya hawa vyura pia ni changamoto. Wananchi wanatakiwa kuelewa umuhimu wa hawa vyura katika mazingira yetu. Ni kweli kwamba mradi wa umeme ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa makazi ya rasilimali hii. Pia ukataji wa miti na kusambaa kwa mimea vamizi ambayo inaletwa na wananchi wanao lizunguka eneo hilo bila kujua ina madhara gani katika ardhi kiujumla linatakiwa kuliangalia kwa jicho la tatu.
Umuhimu wa kiuchumi unaotokana na chura huyu wa kihansi;- watu wanaajiriwa kwa ajili ya kuwatunza vyura hawa, kuanzishwa kwa mradi wa kutengeneza mabomba yanayotoa mvuke.
Umuhimu wa kiikolojia;-kuweka uwiano sawa wa kimazingira(ecosystem) katika kitendo cha kula wadudu wengine nayeye kuliwa na viumbe wengine.Wanasaidia katika utunzaji wa mazingira kwa sababu wanapendelea kuishi katika mazingira yasio sumbuliwa.
Umuhimu wa kijamii;-kuweza kutimiza ndoto za kielimu kutokana na kufanya utafiti kuhusu chura huyu na mazingira yake kiujumla, maendeleo ya miundo mbinu kama vile balabala kutoka mrimba ipo katika kiwango cha lami.
Nini kinatakiwa kifanyike? Kwa ajili ya kutunza rasilimali hii kwa faida ya kizazi hiki na kijacho inahitajika jitihada na juhudi kubwa katika kuyarudisha mazingira yao asilia kama inavyoendelea kuwatengenezea mazingira ambayo wanaweza kufanya shughuli zao mbalimbali kama za uzalianaji kutunza watoto wao,kujitafutia chakula nakadhalika. Pia kuwa na wataalamu ambao wanaweza kuwaangalia na kuweza kutibu magonjwa yao.
Kwa maswali, maoni na ushauri unaweza kuwasiliana na mwandishi wa Makala hii kwa mawasiliano yaliyopo mwishi wa Makala hii.
Ahsante sana!
Naomi Mnyali
+255 788 706 476
Barua pepe : naomimnyali@gmail.com