Migogoro kati ya wanyamapori na jamii zinazo zizunguka hifadhi nyingi katika nchi yetu na maeneo mengi ya hifadhi kote ulimwenguni ni moja ya changamoto katika uhifadhi wa wanyamapori kwa maendeleo endelevu, ambapo gharama( Fedha, Muda na nguvu) nyingi hutumika kupunguza migogoro hii ili kuleta ustawi mzuri kwa maliasili hizi hasa wanyamapori.
Wanyama pori ni urithi wa asili na wakipekee na wenye umuhimu mkubwa katika taifa letu na uhai wa binadamu kwani vitu hivi hutegemeana kwa kiasi kikubwa. Migogoro kati ya wanyamapori na binadamu ni muingiliano kati ya hizi pande mbili ambayo huweza kuleta mahusiano hasi kati yao.Wanyama ambao huleta mgongano na migogoro hii kwa asilimia kubwa ni wale wakubwa na hatari kama Simba, Tembo, Fisi, Chui na wengine wadogo kama nyani , ngedere na ndege. Migogoro mingi husababishwa na mambo kadhaa ikiwemo ongezeko la makazi na idadi ya watu, hupelekea kufanya shughuli za kilimo kwenye shoroba au mapito ya wanyama, kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi, mabadiliko ya hali ya hewa.
Migogoro hii hutokea pale uharibifu wa mazao, mifugo kuuawa, watu kuuawa au hata kujeruhiwa hali hii huleta chuki ndani ya watu na kufanya mauaji ya hawa wanyama kwa kulipa kisasi ikiwa hii sio njia sahihi yakupunguza au kuondoa hii migogoro katika kurasa zinazoendelea tutaongelea kwa undani zaidi sababu za migogoro, vyanzo vya migogoro, njia ya kupunguza hii migogoro ili kujenga jamii inayoishi uzuri na wanyamapori
MIGOGORO INAYOSABABISHWA NA WANYAMAPORI KWA BINADAMU
UHARIBIFU WA MAZAO
Inasadikika Tembo ndiye mnyama ambaye anafanya uharibifu mkubwa wa mazao ya binadamu ambao huweza kuchangia kuongezeka kwa umaskini, ikiwa kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa , ingawa kuna wanyama wengi kama pundamilia, nyani pia husababisha uharibifu huo, lakini Tembo amejikuta ndio mnyama ambaye yuko kwenye vita kubwa sana dhidi ya uharibifu huu, swali la kujiuliza ni kwamba kati ya tembo na binadamu ni nani chanzo cha mgogoro?
Je ni nani wa kuumaliza huu mgogoro, tuwaachie wahifadhi, au serikali?. Ongezeko la watu na makazi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi hubadilisha mazingira kuwa mashamba na kuchukua njia za jadi za mapito ya wanyamapori( Shoroba) shughuli hizi huzua migogoro baina ya binadamu na wanyamapori inayopelekea matokeo hasi na mtazamo hasi dhidi ya wanyamapori. Jambo la kukumbuka na kutafakari ni kwamba wanyamapori hawatambui mipaka, kwakusema hivyo, inatupasa sisi viumbe wenye akili na utashi kutafuta mbinu sahihi ya kupunguza uharibifu wa mazao katika mashamba yetu tukishirikiana na wadau wa uhifadhi na serikali.
VIFO KWA MIFUGO
Wanyama ikiwemo Simba, Chui na wengine wala nyama, husababisha vifo vya mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, ikiwa nje ya hifadhi au hata ndani ya maeneo yaliyo hifadhiwa, jamii za watu wanaojihusisha na shughuli za ufugaji ndio waathirika wakubwa, hivyo hujenga chuki dhidi ya wanyama wala nyama na kuwaua kwa visasi. Nani wakuumaliza huu mgogoro kuwanusuru wanyama hawa ambao wako hatarini kutoweka?
Kuwaua kwa visasi haimalizi tatizo kwa hawa wanyama ambao wako katika hatari kubwa ya kutoweka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujangili, mabadiliko ya hali ya hewa , madiliko ya matumizi ya ardhi pia kuuawa kwaajili ya visasi, jitihada nyingi zinaitajika kwa kubuni njia mbadala yakupunguzu na kuondoa kabisa tatizo hili.
MAJERUHI NA VIFO KWA BINADAMU
Wanyama wala nyama na wala majani husababisha majeruhi pia hata vifo kwa binadamu, mara nyingi inakua ni kwakujihami mfano Nyati, mara nyingi uwajeruhi au pengine kuwaua binadamu kwa sababu ya kujihami, nyati inasemekana ndio mnyama hatari na mwenye hasira zaidi porini, haswa wale waliotengwa na waliojeruhiwa huwa wakali zaidi inapotokea binadamu amekutana ana kwa ana na huyu mnyama ni nini kinatokea?.
Mamba pia, binadamu wanapofanya shughuli zao katika maji kama uvuvi, kuchota maji huweza kukutana na mnyama huyu hatari na kumjeruhi,au pengine kuuawa kabisa. Chuki hujengeka na hivyo hupelekea wanyama hawa kuwindwa na kuuawa. Nani wakutatua tatizo hili wahifadhi wanahitajika kutoa elimu kwa jamii jinsi yakujihami na kujilinda pindi wakutanapo na hawa wanyama hatarishi. Tutatue, tupunguze na sio kuwaua hawa wanyama ambao ni rasilimali adhimu tuliyotunukiwa kuwa nayo katika nchi yetu.
MIGOGORO INAYOSABABISHWA NA BINADAMU KWA WANYAMAPORI
MABADILIKO YA TABIA YA NCHI (UKAME)
Ni tatizo la Dunia ongezeko la joto ambalo husababishwa na uharibifu wa mazingira kama ukataji miti, kwaajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, makazi, viwanda, nk. Shughuli hizi huleta ukame ambao husababisha ukosefu wa chakula na vyanzo vingi vya maji kukauka katika maeneo yetu, inatokea wafugaji wanaswaga mifugo yao kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ili wapate chakula kwa mifugo yao, jambo hili huongeza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori kwa kuwa ng’ombe au mifugo ambayo ni dhaifu hujikuta wakishambuliwa na Simba pamoja na wanyama wengine walao nyama.
Upande mwingine inaweza tokea vyanzo vya maji na chakula kupungua katika maeneo yaliyoifadhiwa hiyo hupelekea wanyamapori kutoka katika maeneo yao na kwenda maeneo ya binadamu kutafuta chakula na maji ndipo inatokea wanyamapori kuua mifugo, uharibifu wa mazao,
Swali je ni nani chanzo cha huu ukame, jibu ni binadamu, wengine wanaweza kuhoji na kusema kuna sababu za kiasili husababisha mabadiliko ya tabia ya nchi lakini madhara yatokanayo na ukataji wa miti na uharibifu wamazingira inachangia kwa kiasi kikubwa katika utokeaji wa migogoro hii.
ONGEZEKO LA WATU
Kuongezeka kwa makazi ya binadamu husababisha kuvamia maeneo ya hifadhi kuwa mashamba na huchukua njia za jadi za mapito ya wanyamapori (Shoroba), shughuli hizi za binadamu huzua migogoro baina ya binadamu na wanyamapori inayopelekea matokeo hasi kwa binadamu na kwa wanyampori.
UPANDAJI WA MAZAO AMBAYO HUWAVUTIA WANYAMAPORI
Shughuli ya kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu na ndio tegemeo la watanzania wengi kujikimu kimaisha. Jamii hizi zinazoishi pembezoni mwa hifadhi hufanya shughuli za kilimo na mara nyingi kwasababu ya uelewa mdogo kwamba ni mazao ya aina gani wanyama hasa tembo hupendelea hujikuta wanaingia katika mgogoro huu, mfano upandaji wa mazao kama tikiti maji, mahindi, mihogo nk huwavutia wanyama wajamii ya Tembo ambapo hupelekea uharibifu mkubwa na huleta migogoro mikubwa zaidi, ukiangalia mtu umepoteza nguvu na pesa nyingi kwaajili ya kilimo, hivyo huzua migogoro na mtazamo hasi juu ya hawa wanyama.
SHERIA NA SERA ZILIZOANDALIWA NA SERIKALI ZA AFRIKA MASHARIKI Binadamu na wanyamapori wamekuwa wakiishi pamoja bila ya migogoro kwa karne nyingi ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki mpaka hapo uamuzi wa kutenga maeneo ya hifadhi, uamuzi huo umechangia pia mgogoro wa kugombania ardhi kati ya Wanajamii wanaoishi pembezoni mwa maeneo yaliyohifadhiwa na wanyama pori.
NJIA YA KUPUNGUZA MIGOGORO HII
FIDIA KWA MALI ZILIZO HARIBIWA
Kulipa fidia au kifuta machozi kwa wafugaji na kwa wakulima walioaribiwa mali zao hii inaweza saidia na kuleta suluhu iliyo dhahiri, ni mbinu nzuri kutumika hasa wakati wa migogoro kama vile baa la njaa ambapo matukio ya simba kuua mifugo kuongezeka.
Kwa upande mwingine ulipaji wa fidia huwa hausaidii kupunguza uharibifu wa mifugo na unaweza kuchangia katika mbinu mbovu za ufugaji na kuondosha umuhimu wa kulinda vyema mifugo. Pia hakuna anaeweza kulipa fidia ikitokea mtu kauawa ni ngumu, zaidi tunatoa kifuta machozi ili kuondoa dhana mbaya, kwa Tanzania, fidia hulipwa kwa mashamba yaliyohalibiwa na wanyama kama Tembo kwa shamba lenye ukubwa wa kuanzia hekari tano kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi wanatakiwa kulifahamu ili, kwa mtu akijeruhiwa kuuwawa pia fidia hizo hutolewa na waziri mwenye dhamana ndio muhusika mkuu wakushughulikia ili. Fidia huongea uvumilivu kwa jamii hizi dhidi ya wanyamapori waharibifu katika kuchukua jukumu la kuwaangamiza kwa visasi.
ELIMU KWA JAMII
Kuwajengea jamii uelewa na uwezo wa kulinda mali zao ikiwapo mifugo na mashamba kwakutumia mbinu na vifaa mbalimbali. Kuna miradi mbalimbali ilifanikiwa kupunguza hii migogoro huko Namibia wadau wa mradi wa wanyama wala nyama (carnivore project) kwa lengo lakupunguza mauaji kwaajili ya visasi.
Kwa kushirikiana na jamii mradi umejenga mabanda makubwa na yaliyo salama ili kuipa mifugo sehemu salama ya kukaa, hiyo huwawia vigumu kwa wanyama hatari kama simba kuchukua mifugo kwa urahisi, jambo ambalo hapo awali lilikua la kawaida mno katika mabanda legelege. Na kuripotiwa kupungua kwa idadi ya simba waliouawa imepungua kutoka 20 kwa mwaka 2013, kabla mabanda salama hayajajengwa hadi 1 kwa mwaka 2015 na kufikia vifo sifuri kwa mwaka 2016.
Kwa Tanzania jitihada nyingi hufanyika kupunguza migogoro hii kwakutoa miongozo mbalimbali inayosaidia kuzilinda jamii na mali zao dhidi ya wanyama kama tembo kwenye uharibifu wa mazao katika mashamba ikiwemo njia mbalimbali zinazotumika kwa mtiririko ikiwemo utumiaji wa Tochi yenye mwanga mkali wakati wa usiku, Honi yenye kelele inayokera, Baruti za pilipili, flashi flashi, mizinga ya nyuki katika kutengeneza uzio kwenye mashamba au mpakani mwa hifadhi. Kuwaelimisha wasipande mazao ambayo huwavutia wanyama hawa waaribifu.
WITO KWA WATAFITI, WAHIFADHI NA SERIKALI
- Tuishilikishe jamii katika kutatua hii migogoro kwani wanaweza kusaidia kubuni njia mbalimbali hasa za kijadi kupunguza migogoro hii, umuhimu wa kuishirikisha jamii katika majadiliano na maamuzi juu ya hii migogoro ni kwamba inasaidia kujenga ushirikiano na ushiriki wa moja kwa moja katika kujilinda wao na mali zao na kutoa ushirikiano wa kutosha pindi matukio ya uharibifu yakitokea. Inaipa jamii umiliki wa maliasili na kuona kuwa nao ni sehemu ya uhifadhi na wanamchango katika kuhakikisha migogoro kati ya wanyamapori na binadamu haitokei
- Jamii inahitajika ipewe elimu juu ya umuhimu wa hawa wanyama kimazingira, hasa kiikologia, katika uingizaji wa mapato hivyo husaidia kuongeza pato la taifa,wafundishwe jinsi yakujilinda wao na mali zao, kwa upande wa wahifadhi na wenye dhamana ya kuhifadhi hawa wanyamapori wanatakiwa wajitahidi kuwashilikisha jamii zinazozingukuka hifadhi mbalimbali katika mstakabadhi mzima wa kuandaa miongozo na suluhu kuhusiana na migogoro hii,
- Kipindi cha kiangazi ambapo vyanzo vya maji vingi hukauka wahifadhi wanatakiwa ,kutumia njia mbadala kama kuvuna maji wakati wa masika na kuchimba mabwawa ambayo wataweza wasaidia hawa wanyama wasitoke nje ya hifadhi kutafuta maji na chakula itasidia kupunguza hii migogoro kwa asilimia kubwa.
- Watafiti pia wanatakiwa kufanya tafiti zaidi kuhusiana na migogoro hii na kuja na njia mbadala ambazo zitawasaidia wahifadhi kutatua hii migogoro.
HITIMISHO
Nani hasa wakusuluhisha hii migogoro na kuimaliza kabisa?
Jamii yote kushirikiana na kila mtu achukue nafasi yake ili kuleta mbadala wa hii migogoro na kuisha kabisa, kuna nchi zimefanikiwa kuhakikisha migogoro hii imeisha ikiwamo Scandinavia kwanini sisi tusiweze maamuzi jitihada zinahitajika licha ya changamoto nyingi kuwako. Pamoja tunaweza kuondoa changamoto hizi ili kuleta uhifadhi kwa maendeleo endelevu.
Makala hii imeandikwa;
Naomi Mnyali
0788 706 476