Wapendwa wasomaji wa makala za wanyamapori, na maliasili kwa ujumla  awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kunipa uhai na nafasi ya kawaleteeni  makala haya  yamuhusuyo ndege aina ya bundi, lakini pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwenu kwa kuwa na utayari wa kuyapokea na kuyasoma makala haya , aidha nataraji tutajifunza mengi kuhusu ndege huyu lau jamii inavyomtazama na ukweli wake.

   Utangulizi

Makala haya yataangazia mambo mbalimbali yamuhusuyo bundi ikiwamo :utambulisho wa  bundi ,tabia pamoja na sifa zake , mambo yamuwezeshayo bundi kuishi na kuyamudu mazingira yake ,mtazamo wa jamii kuhusu bundi, ukweli  kuhusu bundi ukilinganishwa na mtazamo wa  jamii na mwisho katika tamati yako mapendekezo na maoni yangu kwa jamii. Ningependa kukuomba msomaji wangu ufatane nami katika makala haya ili upate tujifunze mambo mengi na mwonoulimwengu mpya kuhusu bundi.

Bundi ni nani?

Bundi ni miongoni mwa ndege ambae huishi kutegemea nyama kama chakula chake. Bundi hutafuta mawindo yake nyakati za usiku na mara nyigi huutumia mchana kwa mapumziko. Katika uainishaji wa kisayansi, bundi huainiswa kama ifuatavyo: himaya (kingdom) ya wanyama/animalia, faila ( phylum ) ya wanyama wenye uti wa mgongo, ngeli  ( order ) ya ndege na familia  ya bundi. Tafiti zinabainisha uwepo wa aina nyingi za ndege hawa jamii ya bundi diniani, zikiwa ni zaidi ya spishi  200

Sifa  na tabia za bundi

  1. Bundi huwinda wanyama wadogo wadogo kama vile: panya , mijusi, ndege na wadudu, mawindo yake hufanyika majira  ya usiku  ili kuepusha  ushindani dhidi ya ndege wengine walao nyama kama vile: mwewe, na tai, pia hii humsaidia kukamata wanyama hawa kwa urahisi usiku wakiwa wamelala.
  2. Bundi jike huwa na ambo kubwa zaidi, rangi yake imekoza zaidi na huwa mkali kuliko dume.
  3. Bundi jike huwa na uwezo wa kutaga mayai yapatayo 12, lakini kwa mara nyingi hutaga mayai 4 – 8 yakipishana siku moja hadi mbili.
  4. Bundi wana uwezo wa kuishi mabara yote isipokuwa bara la Antaktika, bundi waishio kwenye maeneo yenye baridi huwa na maumbo makubwa zaidi wakilinganishwa na wale wanaoishi kwenye maeneo yenye joto.
  5. Bundi mkubwa ana uwezo wa kumuwinda bundi mwenye umbo mdogo wa aina(spices) nyingine), yaani cannibalism.
  6. Bundi anauono wa mara saba (7) ya uono alionao binadamu, lakini pamoja na sifa hiyo hawezi kuona vitu vilivyo karibu, hivyo bundi hatumii macho kuvamia windo lake, ana uwezo wa kumkata mbuawa(prey) wake akiwa amefumba macho

7. Bundi hupaa kimyakimya bila ya mabawa yake kupiga kelele, hii ni kutokana na umbo la mabawa yake na mfumo wa manyoa, manyoa yaliyopo miguuni mwa bundi hufyonza kelele zitokanazo na upepo, hivyo kuzuia kelele akiwa anapaa.

Namna gani bundi anaweza kuishi na kuyamudu mazingira yake?

  1. Uwindaji wa usiku

Bundi amejitofutisha na ndege wengine walao nyama kama vile tai na mwewe kwa kufanya mawindo yake usiku, hii humpunguza ushindani   wa chakula kati yake na ndege wengine walao nyama, halikadhalika uwindaji wa usiku humsaidia bundi kuotea na kuvamia wawindo yake kwa urahisi kwani muda wa usiku wanyama wengi hupumzika.

  •  Uwezo wa kuruka kimyakimya pasipo kupiga kelele

Mabawa na manyoya na bundi yana muuondo na dizaini ya kipekee ambayo humfanya bundi kupaa kimyakimya hivyo kuweza kumlega na kumkamata mbuawa (prey) wake pasipo kupiga kelele. Hii hufanya uwindaji wa bundi kuwa mwepesi kwani mbuawa wake hawawezi kumsikia bundi akiwa anaenda kuwavamia.

  • Mdomo na kucha  zilizochongoka

Mdomo na kucha za bundi vimechongoka, kielelezo namba 1.0 kimeonesha kucha za bundi katika dizaini imuwezeshayo bundi kukata, kurarua na hatimaye kula mbuawa (prey) wake, picha

Kielelezo namba 1.0; chaonyesha kucha za bundi zilizochongoka ambazo humuwezesha bundi kukamat na kularua mbuawa wake.

  • Usikivu maridadi

Bundi ni ndege mwenye uwezo mkubwa sana wa kusikia, huweza kusika mirindimo ya sauti iliyo ndogo kiasi kwamba binadamu hawezi kuisikia. Hivyo bundi huweza kuwasikia na kuwavamia hata wanyama wadogo na kujipatia chakula.

  • Rangi za manyoya ya bundi hufanana Sana na mazingira yake hivyo kumfanya bundi asionekane kwa urahisi hasa wakati wa mchana, tazama kielelezo mamba 1.1

Kutokana na kufanana sana na mazingira yake, bundi huweza kujikinga dhidi ya maadui au mashambulizi ya wanyama wengine akiwemo binadamu. Siyo rangi tu pia bundi huweza hukaa kwenye tawi la mti au sehemu nyingine bila kutingishika hivyo kuonekana kama kiumbe kisicho na uhai kama vile jani la mti au kisiki. 

Kielelezo mamba 1.1; chaonesha namana bundi anavyofanana na mazingira yake, hivyo kumfanya asionekane kiwepesi.

Mtazamo wa jamii kuhusu bundi

Watu wengi humfahamu bundi  kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo  kichwa cha mviringo na macho yake yenye uwezo wa kuyafumba na kuyafumbua kama binadau, umbo lake na rangi yake, mwonekano wa kichwa chake kinachoweza kugeuka pande zote. Hivyo bundi huchukuliwa kama ndege wa tofauti.

Jamii mbalimbali za ulimwenguni huwa na mitazamo tofauti juu ya bundi, ifuatayo ni baadhi ya mitazamo kutoka jamii mbalimbali duniani;

JAMII MTAZAMO
Wakikuyu (Kenya) Bundi huleta kifo, mikosi na magonjwa.
Japani Huchukuliwa kama ndege anaeleta furaha na bahati.
Marekani Wamarekani wa zamani walimchukulia bundi kama ndege mwenye nguvu za ajabu na ni ndege hatari.
Wanausasa wa Magharibi Bundi anamaanisha busara.

Mtazamo wa Jamii za Kitanzania njuu ya ndege Bundi

Watu wa makabila mbalimbali nchini Tanzania huamini kuwa bundi aonekanapo nyumbani kwa mtu huashiria ama husababisha kifo cha mtu. Hivyo watu wengi huwa na hofu kubwa sana pale wamwonapo bundi katika mazingira yao. Baadhi ya husadiki kuwa bundi ni mchawi au katumwa na mchawi ili kuchukua roho za watu. Watu wasikipo sauti ya bundi hufikri jambo baya litatikea hasa kifo na wengine husema ni mkosi.

Uhalisia kuhusu bundi

Bundi ni ndege kama walivyo ndege wengine, bundi hufanya mawindo yake usiku sio kwa sababu ni mchawi au katumwa na mchawi.  Lengo la kuwinda na kuwa macho usiku  huku mchana akutumia kupumzika ni kupunguza ama kuepuka mapambano ya kugombania chakula na ndege au wanyama walao nyama ambao huwinda mchana. Mlio wa bundi usikikapo usiku sio mkosi kama wasemavyo watu wengi, kama ilivyo kwa ndege wengine bundi hutoa mlio kwa ajili ya mawasiliano baina yao hii inaweza kuwa; kuitana, kuogopa, kumtishia au kumkimbiza adui na sababu nyingine ziwafanyao ndege  wote kutoa milio.

 Je, bundi husababisha au huleta kifo?

Kumekuwa na Imani kwamba bundi anaponekana kwenye nyumba ya mtu ni lazima jambo baya litokee katika nyumba hiyo, hii imepelekea watu wengi kukuhusisha kiumbe hiki na nguvu za giza kuwa ni mchawi au atakuwa katuma na mchawi na kama kuna mgonjwa basi atakufa.

Nipende kuweka bayana ukweli kuhusu jambo hill; bundi ni ndege mwenye uwezo mkubwa sana wa kunusa harufu ya mzoga kutoka mbali, uwezo huu alionao ni wa kipekee, binadamu hana uwezo huo. Hivyo basi itokeapo katika nyumba kuna mgonjwa mahututi ambaye seli za mwili wake zimeshaanza kufa lakini mapigo ya moyo wake bado yanafanya kazi, bundi huweza kunusa harufu ya seli hizo, binadamu hana uwezo wa kuhuhisi wala kuinusa harufu hiyo. Kutokana na hiyo harufu bundi huvutiwa na hufikiri anaweza kupata chakula, hivyo huisogelea nyumba yenye mgonjwa, lakini bundi hawezi kufanya chochote dhidi ya mgonjwa huyo kwa  sababu bundi nae humuogopa binadamu kama walivyo ndege wengi.

Hivyo kuonekana kwa bundi kwenye nyumba yenye mgonjwa inaweza kuashiria kuwa mgonjwa huyo ameshaanza hatua za kufariki na kuna uwezekano wa kufariki katika kipindi hicho.  Inapotokea mgonjwa akafariki ndani ya muda mfupi toka bundi aonekane siyo kwamba kifo kimesababishwa na bundi bali tafsiri sahihi yaweza kuwa mbuni ilizitambua dalili za kifo cha mgonjwa.

Hitimisho

Kidunia idadi ya bundi imekuwa ikipungua, aidha kuna sababu kadha wa kadha zilizopelekea kupungua kwa idadi ya bundi duniani, sababu hizo ni kama; uwindaji wa bundi, ukosefu wa chakuala kutokana kutoweka kwa baadhi ya viumbe kama wadudu na wanyama wadogo wadogo ambao ndio chakula cha bundi  pamoja na magonjwa. Katika Jamii nyingi hususani za kitanzania bundi huwindwa si kwa sababu ya chakula, bali huuliwa kutokana na jamii kuwa mtazamo hasi kwa kiumbe hiki kisicho na hatia. Izingatiwe kiumbe huyu ni muhimu kwani ana mchango mkubwa katika ikolojia ya mazingira kwani ni husidia kudhibiti ongezeko la wanyama waliwao na bundi, baadhi ya wanyama hao ni waharibifu hasa wa mazao ya kilimo kama vile panya na wadudu waharibuo mazao. Kutoweka kwa bundi hutasababisha madhara ambayo yatahathiri ustawi wa viumbe wengi ikiwemo binadamu kutoka na kuathirika kwa mfumo mzima wa kiikolojia.

Mapendekezo

 Kutokana na janga la mtazamo hasi juu ya bundi unaozikumba jamii zetu, kuna haja kubwa ya kutoa elimu katika jamii  ili kuondoa mtazamo hasi uliojengeka miongoni mwa watu wengi, elimu hii inapaswa igusie uhalisia na sababua ya mfumo wa maisha ya ndege huyu, umuhimu wa bundi na faida zake zinapaswa kuwekwa banayana hasahasa kwa wakulima kwani bundi anaweza kutumika kudhibiti wadudu na wanyama waharibifu hivyo kutumika kama mbadala wa dawa za chemikali zinazotumiwa na wakulima.

KWA PAMOJA TUSHIRIKIANE KUUTOKOMEZA MTAZAMO HASI JUU YA BUNDI

Asanteni

Ahsante sana!

Lucy Romward

Lucyromward111@gmail.com