Heloo ndugu zangu watanzania, habari za siku nyingi kidogo. Ni matumaini yangu mu wazima wa afya kwani tumepotezana kwa muda kidogo hasa kwenye darasa letu huli huru kuhusu wanyamapori na kujuzana mambo yenye faida kubwa sana kuhusu uhifadhi wa wanyama hawa. Ilikua ni sababu ambazo zipo nje ya uwezo wangu zilizo nifanya kuwa kimya kwa muda kidogo ila kwa sasa nimerudi tena kwa hari kubwa sana.

Basi kama kawaida leo tena tutaingia darasani tuweze kujifunza machache kuhusu wanyamapori na kwa hakika nimekuandalia makala nzuri sana kwa hakika utafurahia kumfahamu mnyama huyu ambae naamini waliyo wengi hamumfahamu.

Basi bila kupoteza muda leo nakuletea makala kuhusu mnyama jamii ya paka ambae wengi hawamfahamu lakini kupitia makala hii naamini utajifunza mengi sana kuhusu mnyama huyu na utakuwa miongoni wa wadau wakubwa ambao wana tumia jitihada kubwa sana katika kuhakikisha wanyamapori wetu wanaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo. Mnyama wa leo katika makala yetu anaitwa “KANU” ambae kwa lugha ya kiingereza anaitwa “GENET”.

Aina za kanu zina changanya sana kwasababu zipo aina ambazo zinafanana kwa vinasaba lakini pia baadhi ya sifa nyingi sana. Kutokana na tafiti iliyo fanyika mwaka 2005, spishi za kanu zilizo ainishwa ni 17. Hivyo kwa leo hapa tutamzungumzia kanu wa kawaida ambae kwa kingereza anajulikana kama common genet. Mara nyingi sifa za spishi za kanu hufanana sana na utofauti wake ni mdogo sana hasa kutokana na maeneo wanayoishi na muonekano kwa kuwatazama.

UTANGULIZI

Kama nilivo tangulia kudokeza hapo juu kuwa Kanu ni mnyama jamii ya paka ambae waliyo wengi hawa mfahamu mnyama huyu ila ana umuhimu mkubwa sana katika mazingira ya kila siku ya viumbe hai wengine. Mnyama huyu ana sifa kemkem ambazo zina vutia sana hasa kutokana na umbo lake zuri, nakshi nakshi za mpangilio wa rangi katika mwili wake ambazo kusema kweli zinamfanya mnyama huyu huwa ni mwenye kuvutia sana.

Hivyo basi twende pamoja mwanzo hadi mwisho wa makala hii ili uweze kupata sifa zote kuhusu mnyama huyu bila kusahau tutaangalia pia kuhusu uhifadhi na uelekeo wa wanyama hawa hapa nchini kwetu.

SIFA NA TABIA ZA KANU

Wana alama nyeusi usoni ambazo alama hizi ukiwaangalia kwa haraka haraka unaweza sema wamevaa kinyago usoni.

Wana madoa madoa katika migongo yao ambayo imejipanga kwa umbo la mistari sambamba na inazidi kuongezeka kadiri unavyo elekea mkiani ambayo inatengeneza umbo la maduara yenye rangi nyeusi.

Kanu wana kucha zenye uwezo wa kuingia ndani na kutoka kama walivyo wanyama wengine jamii yap aka. Sifa ya kucha zao huwasaidia wanyama hawa kuweza kupanda miti kwa wepesi zaidi.

Kanu ni wanyama wenye maumbo madogo na kama nilivyo sema hapo juu wana matezi kama yale ya paka.

Kanu wana manyoa mengi eneo la shingoni ambayo kipindi wanapo hisi hatari ya adui huyasimamisha manyoa haya ili miili yao ionekane mikubwa na kuwa tishio kwa adui yao.

Wana mikia minene yenye manyoa mengi ambayo huufanya mkia wake uonekane kama brashi huku masikio yao yakiwa yamesimama ambayo kwa haraka haraka yanafanana na masikio ya fisi.

Wanyama hawa huwasiliana kwa kutumia sauti hasa baina ya mama na watoto na sauti hii hutoka mfano wa kwikwi. Lakini wakati mwingine hata kati ya jike na dume hasa inapofika msimu wa kuzaliana.

Kanu ni wanyama ambao wana uwezo wa kuona sana usiku kuliko mchana na ni wanyama wenye aibu sana. Wanyama hawa ni miongoni mwa wanyama wenye aibu sana na wenye usiri mkubwa sana hivyo huwa wana jificha sana hasa pale wamuonapo binaadamu.

Mbali na uwezo wa wanyama hawa kupanda miti, muda wao mwingi huutumia wakiwa aridhini hasa wanapokua kwenye mawindo na maranyingi malazi yao huwa kwenye miamba.

Kanu ni wanyama ambao wana uwezo wa kubana miili yao kwa kiasi kikubwa sana. Sifa hii huwafanya wanyama hawa kuweza kupita katika maeneo madogo sana kuliko hata miili yao.

Madume huwa na miili mikubwa kidogo kuliko majike. Kanu wakubwa huishi kwa kujitenga na mara nyingi hukutana kipindi cha kuzaliana au wakati kanu jike anaongozana na watoto wake.

Wana uwezo wa kutoa matezi ambayo hutumika katika kuweka mipaka kwenye himaya. Wanyama hawa wanapo jeruhiwa au kuwa na hasira huzalisha maji maji toka kwenye matezi ambayo hutoa harufu mbaya yenye kumfanya adui ashindwe kuendelea kuwashambulia.

UREFU NA UZITO WA KANU

Urefu= miili yao huwa na urefu wa sentimita 40-60 huku mikia yao mirefu ikiwa na urefu wa sentimita 40-55.

Uzito= kanu huwa na uzito wa wastani wa kati ya kilogramu 1-3. Kama nilivo tangulia kusema hapo juu, dume huwa na mwili mkubwa kidogo kuliko jike.

MAZINGIRA

Wanyama hawa wameenea karibu bara zima la Afrika na wana uwezo wa kuishi mazingira mbali mbali yenye mimea mingi. Mazingira ambayo huishi wanyama hawa huwa na miti mingi, savanna, misitu na wakati mwingine huonekana hata karibu na makazi ya watu hasa maeneo ya vijijini.

Baadhi ya jamii za wanyama hawa zilisafirishwa kutoka barani Afrika na kupelekwa bara la Ulaya hasa nchi za kusini magharibi mwa bara hilo. Mfano wan chi ambazo wanyama hawa walipelekwa toka barani Afrika ni Uhispania, Ufaransa na Ureno.

CHAKULA

Wanyama hawa wamewekwa kwenye tabaka la jamii ya wanyama walao nyama, lakini kuna tafiti zinaonyesha wanyama hawa hawategemei nyama pekee tu kama chakula chao bali kuna wakati hula hata aina mbali mbali za matunda na sifa hii kuwafanya wanyama hawa kuwa kwenye kundi la wanyama walao vuakula aina mbali mbali.

Miongoni mwa vyakula ambavyo kanu hupendelea kula sana ni ndege na mayai, mamalia wadogo kama panya na popo, pia hula wanyama jamii ya tambaaji kama mijusi. Mbali na hawa kanu pia hula viumbe wadogo wadogo kama jongoo, tandu, vyura lakini hata baadhi ya matunda pia ni chakula kwa wanyama hawa.

KUZALIANA

Ni mambo machache sana yanayo julikana kuhusu kuzaliana kwa wanyama hawa. Pamoja na uchache huo kuna vitu muhimu sana vimeweza kufuatiliwa na wana sayansi na kugundua machache kuhusu mfumo wa kuzaliana kwa wanyama hawa. Msimu wa kuzaliana kwa wanyama hawa hutegemeana na maeneo. Mashariki, magharibi na kusinu mwa Afrika wanyama hawa huzaliana sana kipindi cha majira ya mvua huku kaskazini mwa Afrika wanyama hawa huzaliana sana majira ya kipupwe.

Mara tu baada ya kupandana jike hubeba mimba kwa muda wa wiki 10-11 (sawa na siku 70-80) na baada ya hapo huzaa watoto kati ya 1-4. Watoto wanapo zaliwa huwa hawaoni na hawana manyoa hivyo kwa wakati huu huwa hawawezi kufanya chochote hivyo huhitaji uangalizi makini wa mama kwa muda wote na hutegemea maziwa ya mama tu kama chakula.

Watoto wa kanu huanza kula nyama wafikishapo wiki saba na baada ya miezi minne huwa wapo tayari kuanza kuongozana na mama yao. Wafikishapo miezi 5 watoto huwa na uwezo wa kuwinda wenyewe kwani wanakua tayari wamesha pata ujuzi toka kwa mama. Wafikishapo miezi 19 watoto huweza kuzaliana na hapo huanza kuanzisha himaya zao wenyewe.

Maisha ya kanu ni kati ya myaka 8 wawapo katika mazingira yao asilia lakini kama wanafugwa katika bustani za wanyamapori basi wanyama hawa hufikisha myaka 13-34.

UHIFADHI

Idadi ya wanyama hawa kwa sasa inaonekana ipo vizuri yaani hawapungui na wanaonekana kuongezeka kidogo. Hii ni kutokana na utafiti uliofanywa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile asili (International Union for Conservation of Nature-IUCN). Ni jambo la kujivunia sana kwani moja kati ya tafiti hizo ilifanyika katika moja ya hifadhi ya taifa ipatikanayo hapa nchini kwetu na hifadhi hiyo ni Serengeti mnamo mwaka 1980.

Japo idadi ya wanyama hawa inaonekana kuridhisha hususan hapa nchini Tanzania, bado kuna baadhi ya nchi idadi ya wanyama hawa inaonekana kupungua kidogo kidogo siku hadi siku. Hii inatokana na changamoto mbali mbali zinazo wakumba wanyama hawa hivyo jitihada za dhati inabidi ziongezwe kuwanusuru wanyama hawa.

Wanyama hawa wana umuhimu sana kwani husaidia kupunguza baadhi ya wanyama hatari kama vicheche ambao wana sababisha hasara sana kwa wafugaji wa kuku.

MAADUI NA CHANGAMOTO KWA KANU

Kama ilivyo kwa wanyamapori wengine basi wanyama hawa pia wana maadui asilia ambao ni muhimu sana katika ikolojia ya viumbe hai. Uwepo wa maadui asilia ni muhimu sana kwani husaidia kuleta usawa katika ikolojia ya maeneo yao. Maadui wakuu wa kanu ni bundi, chui, chatu, nyegere na binaadamu.

Mbali na maadui nilio waorodhesha hapo juu, kuna changamoto nyingine ambazo ni tishio kwa kanu. Changamoto hizo ni kama zifuatazo;

Kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kilimo, wanyama hawa wamelazimika kuhama maeneo yao asilia na kuzoea maeneo ya mashamba hasa wakifuata mifugo kama kuku na kula kuku hao. Hali hii inapelekea sana wanyama hawa kuuwawa sanana binaadamu kwani wamekuwa ni tatizo kwa mifugo yao. Mfano mzuri wa kutambua kwamba wanyama hawa wana uwawa sana ni kwa kuangalia nguo nyingi za kitamaduni utakuta watu wamevaa mikia ya wanyama hawa.

Wanyama hawa wamekuwa wakiwindwa sana katika nchi nyingi hasa kutokana na manyoa yao yanayo vutia. Kuna baadhi ya makabila wanyama hawa hutumika kama dawa za kitamaduni na baadhi ya jamii huwinda kanu kwaajili ya kitoweo.

Uchomaji wa misitu kwa ajili ya maandalizi ya mashamba hupelekea uharibifu mkubwa wa mazingira ya wanyama hawa na hivyo kusababisha kanu kuyahama mazingira yao lakini wengine wanakufa hasa watoto kutokana na ukosefu wa chakula lakini pia maeneo ya kujificha. Kuna tafiti zinaonyesha kuwa hata mbwa wafugwao wamekuwa wakiwauwa sana wanyama hawa.

Kuna baadhi ya nchi wanyama hawa wamekuwa wakigongwa na magari sana na kusababisha idadi yao kupungua kwa kiasi kikubwa sana. Mfano nchini Ureno, idadi kubwa ya wanyama hawa wanapoteza maisha kutokana na kugongwa na magari ambapo kanu 12 huuwawa kwa kugongwa na magari kila mwaka.

Kuna baadhi ya maeneo wanyama hawa wanatoweka kutokana na kuongezeka kwa miji, utengenezaji wa miundombinu pamoja na maendeleo ya shughuli za kitalii.

NINI KIFANYIKE ILI IDADI YA WANYAMA HAWA IENDELEE KURIDHISHA HAPA NCHINI KAMA ILIVYO SASA

Kudhibiti uanzishwaji wa makazi au upanuzi wa mashamba karibu na maeneo ambayo ni makazi ya kanu hasa maeneo muhimu kama ya kuzaliana. Kwa kufanya hivi itasaidia kwa kiasi kikubwa sana kupunguza mauwaji ya wanyama hawa yatokanayo na ulipizaji wa kisasi kwa kula kuku wa wafugaji.

Jamii hazina budi kupewa elimu juu ya umuhimu wa wanyama hawa ili kupunguza kasi ya uwindaji kwani tumeona hapo juu wanyama hawa huwindwa kama kiweo lakini pia kama dawa za kitamaduni na wengine kama mapambo ya kutengenezea nguo.

Usimamizi mzuri wa sheria za uhifadhi wa wanyamapori kwani kuna baadhi ya wanyama inaonekana kama wamesahaulika sana na kupelekea wanyama hawa kupata changamoto kubwa sana katika maisha yao ya kila siku. Mfano mzuri ni kwa mnyama huyu kanu, waliyo wengi hawamfahamu lakini pia hata mamlaka mbalimbali za wanyamapori hazimchukulii kama mnyama muhimu kwenye ikolojia na hatimae kumsahau sana. Hivyo inabidi sheria zisimamiwe kwa ukamilifu zaidi ili kunusuru maisha ya kila mnyamapori bila kujali kujulikana kwake au kutojulikana sana na jamii.

Usimamizi mzuri wa kasi za magari barabarani kwani hili nalo ni tatizo kwa wanyama wengi sana na sio kwa kanu pekee tu. Mfano mzuri tumeona hapo juu nchini Ureno, idadi kubwa ya wanyama hawa hupoteza maisha kutokana na kugongwa na magari. Ili na sisi hapa nchini lisijitokeze hilo kwani tumeona hata katika hifadhi ya taifa Mikumi wanyama wengi wanagongwa kutokana na mwendo kasi wa magari yapitayo hifadhini hapo.

Serikali isimamie utoaji wa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori. Hili huwa nalisema karibu kwenye kila makala kwani ni nguzo muhimu sana ya kustawisha uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini. Serikali kupitia ushirikiano baina ya wizara ya elimu na wizara ya maliasili ni lazima kuandaa mitaala ya somo la uhifadhi wa wanyamapori kuanzia ngazi ya elimu ya msingi mpaka sekondari. Kwa kufanya hivi niwazi kwamba tutazalisha wahifadhi wengi sana hapa nchini kwani watakuwa huku wakitambua thamani na umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini pia uchumi wan chi yetu.

HITIMISHO

Kwasababu idadi ya wanyama hawa bado inaridhisha basi sote kwa pamoja hatuna budi kuendelea kuwatunza wanyama hawa ili waweze kutuletea faida hasa zitokanazo na pesa za kigeni kwani watalii wanapokuja nchini basi taifa linaingiza pesa nyingi kupitia sekta ya utalii. Jamii pia inabidi kujitoa kwa hali na mali ili kuzisaidia mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori ili kupunguza wimbi la ujangili kwa kuwafichua wale wote wanao jihusisha na ujangili wa wanyamapori.

Pongezi zangu za dhati ziende kwa wizara ya maliasili na utalii kwa jitihada kubwa sana wanazofanya kupambana na changamoto ya ujangili kwani kwa myaka ya hivi karibuni wizara hii chini ya Dr. Hamisi Kigwangala imepunguza kasi ya ujangili kwa zaidi ya 85%. Hali hii inazidi kutoa ari kwa jamii na mamlaka za wanyamapori kuzidi kufanya kazi kwa weledi mkubwa sana ili kuendeleza gurudumu la uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini.

Nizipongeze pia mamlaka za usimamizi wa uhifadhi wanyamapori hapa nchini kama TANAPA, TAWA na NCCA kwa kazi kubwa sana na kujitoa kwa dhati kusimamia uhifadhi na ustawi wa wanyamapori kwa maslahi ya taifa na kwa vizazi vijavyo. Kiukweli wanafanya kazi kubwa sana na wapo wengine wanapata ajali na kujeruhiwa na majangili lakini hawajawahi kukata tama ili kunusuru wanyamapori wetu hapa nchini.

………MWISHO………..

Mwisho wa makala hii ndoo mwanzo wa makala nyingine. Hivyo nikusihi endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi kwani utajifunza mambo mengi sana kuhusu wanyamapori na uelekeo wa wanyama hawa hapa nchini na duniani kote kwa ujumla.

Kwa maswali, ushauri na mengineyo kuhusu wanyamapori basi usisite kuwasiliana nami kupitia;

Sadick Omary Hamisi

Simu; 0714116963 au 0765057969

Email; swideeq.so@gmail.com

Instagram; wildlife_articles_tanzania

Au tembelea tovuti yetu; www.wildlifetanzaniahome.blog

………………”I’M THE METALLIC LEGEND”……………