Heloo wadau wangu katika sekta ya wanyamapori. Natumai muwazima wa afya na mnaendelea kupambana na majukumu ya kila siku ili kujenga taifa letu na basi kama haupo vzuri kiafya Mwenyezimungu akuponye maradhi yako. Kama kawaida leo tena tunaingia darasani kuendeleza mfululizo wa makala zetu kuhusu wanyamapori na uhifadhi wao bila kusahau hadhi ya wanyama hawa hapa nchini na duniani kote.

Basi nikusihi uendelee kuwa nami katika mfululizo wa makala hizi na kufuatilia kwa kina ili uweze kujifunza mambo mengi kuhusu wanyamapori na faida zao. Bila kujali zinakufikia moja kwa moja au kupitia mikono ya watu wengine kwaani siku zote faida zitokanazo na uhifadhi wa wanyamapori zinabaki kuwa ni chachu ya maendeleo kwa taifa zima.

undefined

Huyu ndio Mondo

UTANGULIZI

Katika makala ya leo nakuletea mnyama mwingine jamii ya paka ambae wengi kwa haraka haraka wanaweza kusema ni chui au duma hasa kwa ambao hawawafahamu wanyamapori vizuri. Mnyama ambae nitamzungumzia katika makala yetu ya leo anaitwa “MONDO” ambae kwa lugha yakiingereza hujulikana kama “SERVAL”

Mondo ni wanyama wenye umbo la saizi ya kati kwenye kundi la wanyama jamii ya paka. Kundi hili la wanyama jamii ya paka kuna aina mbali mbali/ nyingi za wanyama kama lilivo kundi la wanyama jamii ya swala ambao nimewazungumzia kwa upana sana katika makala mbali mbali zilizopita nah ii naweza kusema kundi la swala ndiyo kundi lililo chukua sehemu kubwa sana ya makala hizi.

Mondo wana sifa kemkem ambazo wengi hawazifahamu, lakini sio tu kuto zifahamu sifa za mnyama huyu bali wengi hawajawahi kumuona kwani ni mnyama ambae hazungumziwi sana. Kupitia makala hizi za wanyamapori basi nitakuwa nakujuza mambo mengi sana kuhusu wanyama ambao huwafahamu au hawazungumziwi sana midomoni mwa watu. Mondo wamegawanyika katika jamii/ nusu-spishi mbali mbali na tafiti zinaonyesha kuna takribani nusu-spishi 3.

 Endelea kutiririka nami mwanzo mpaka mwisho wa makala hii ili uweze kumjua mondo sifa zake na mambo mengine mengi kuhusu mnyama huyu.

SIFA NA TABIA ZA MONDO

Miili ya mondo ina mchanganyiko wa madoa na mistari sifa ambayo wengi huwachanganya wanyama hawa na chui, duma, simbamangu.

Sehemu ya tumboni kwa chini huwa na madoa pia lakini huonekana kupauka tofauti na mgongoni au maeneo mengine ya mwili. Mikia yao huwa na miduara myeusi na sehemu ya ncha ya mkia huwa pia na rangi nyeusi.

Rangi ya manyoya yao hasa sehemu ya juu huwa na rangi ya lulu ambayo hufanana na rangi ya dhahabu manjano huku sehemu ya chini ikionekana kupauka tofauti na ilivyo sehemu ya juu. Lakini kwa mondo ambao wanapatikana maeneo ya Kenya na Ethiopia huwa na rangi nyeusi kwa asilimia kubwa.

Ukiangalia kwa umakini viini macho vya wanyama hawa huwa vina umbo linalo shabihiana na mviriongo wama walivyo simbamangu na paka wafugwao majumbani. Sifa hii ina watofautisha wanyama hawa na jamii nyingine za paka kama simba, duma, puma na tiger kwani wao wana viini macho ambavyo vinaweza kujiminya na kuwa kama nukta ya duara.

Wana masikio makubwa yenye umbo la duara ambayo huwasaidia sana kusikia sauti ya vitoweo au mawindo yao hasa wanapokuwa sehemu yenye majani marefu.

Sehemu ya nyuma ya masikio huwa na rangi nyeusi huku yakiwa na mistari myeupe ya kipekee iliyo katiza sehemu ya kati kati ya sikio kwa upande huo wa nyuma.

Mondo wana miili myembamba, miguu mirefu na mikia mifupi. Mondo ndio wanyama wenye miguu mirefu kwenye kundi la wanyama jamii ya paka hasa ukilingalisha urefu wa miguu na maumbo ya miili yao.

Mondo ni wanyama ambao wanaishi kwa kujitenga. Hii inamaanisha kwamba wanyama hawa ni nadra sana kuwaona wakiwa wawili au zaid. Maranyingi hukutana kipindi wanapotaka kuzaliana tu.

Wanyama hawa wana uwezo mkubwa sana wa kuruka angani. Asilimia kubwa ya chakula hupata kwa kutumia njia ya kuruka angani na kutua kwa kutumia mikono kisha kuvamia mawindo huku mawindo yakiwa bado yana shangaa.

Mondo hutumia pia mikono yao mirefu kutafutia mawindo yao kwenye mashimo na wakati mwingi huonekana wakitumia njia hiyo hiyo kukamata samaki kwenye maji.

Mondo ni wanyama wenye uwezo mkubwa sana kwenye kuwinda sifa ambayo imefanya wanyama hawa kuitwa wawindaji wenye mafanikio makubwa.

Mondo wana uwezo wa kuona zaidi nyakati za usiku kuliko mchana hivyo shughuli zao nyingi hasa za uwindaji hufanya nyakati za usiku.

Dume huweka mipaka kwenye himaya kwa kutumia mkojo na maranyingi hufanya doria katika himaya yake ili kuzuiya wavamizi au madume mengine yasiingie kwenye himaya hiyo. Japo jike pia huwa na tabia hiyo ya kuweka mkojo katika mipaka ya himaya yake ila huwa ni mara chache sana ukilinganisha na dume.

JE, WAJUA THAMANI YA MONDO? MUHIMU NIKUJUZE

Mondo alikuwa ni kiashiria au ishara ya familia ya kifalme ya bwana Tomasi huko nchini Italia hasa kwa mwana mfalme wa kisiwa cha Lampedusa. Mwana mfalme huyo alijulikana kama “Giuseppe Tomasi di Lampedusa” ambae aliandika riwaya maarufu sana huko nchini Italia iliyo pewa jina la kiitaliano “IlGattopadro” ikiwa na maana ya chui. Mbali na kujulikana kama ni chui kwa kingereza, lakini kichwa cha nchi ya Italia kina maanisha MONDO. Hii ni kwasababu katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika wanyama hawa wameenea hadi karibu na maeneo ya Lampedusa.

KIMO, UREFU NA UZITO WA MONDO

Kimo= Wote madume na majike huwa na kimo sawa ambapo huwa na kimo cha futi 2.

Urefu= Kuanzia kichwani hadi mwisho wa kiwiliwili mondo huwa na urefu wa sm 59-sm 92 na mkia huwa na urefu wa sm 20-sm 38.

Uzito= Uzito kati ya dume na jike huwa tofauti kidogo kwani dume huwa na uzito mkubwa kidogo kuliko jike. Dume huwa na uzito wa wastani kati ya kg 9-kg 18 huku jike wakiwa na uzito wa kg 9-kg 12.

MAZINGIRA

Mondo ni wanyama wanao patikana bara la Afrika tu na si kwingineko duniani huku Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi ambayo inajivunia kuwa na wanyama hawa kwa idadi kubwa tu na inayo ridhisha.

Mazingira wanayo pendelea wanyama hawa kuishi ni yale ambayo sehemu kubwa ya eneo hilo limetawaliwa na majani. Japo kuna wakati mwingine wanyama hawa huonekana sehemu zenye miti iliyo tawanyika lakini hata siku moja huwezi kuwaona maeneo yenye misitu minene.

CHAKULA

Mondo ni miongoni mwa jamii ya wanyama walao nyama hivyo zaidi ya 99% ya chakula chao hutokana na viumbe wengine. Wanyama hawa wana uwezo wa kula wanyama wadogo wadogo ambao wapo kwenye makundi kama mamalia, tambaaji, amfibia, ndege na wadudu.

Kama nilivo tangulia kudokeza hapo juu, mondo hukamata mawindo yao kwa njia ya kuruka juu kisha kutua kwa kutumia mikono yao juu ya windo na kumfanya mnyama wanae muwinda kubaki anashangaa kisha humuuwa.  Kuna wakati mwingine huruka juu na kumkamata mnyama huko huko juu hasa pale wanapokuwa wanawinda ndege.

Miongoni mwa wanyama ambao mondo hupendelea kuwawinda na kufanikiwa sana ni sungura, panya, baadhi ya jamii za nyoka hasa wa kwenye mchanga na majani, mijusi, vyura, ndege jamii ya flamingo, samaki, panzi na baadhi ya swala wadogo kama digidigi. Kuna wakati mwingine wanyama hawa wameonekana wakila vyakula ambavyo siojamii ya nyama kama ndizi na maparachichi.

KUZALIANA

Hapo mwanzo nilidokeza kuwa wanyama hawa huishi kwa kujitenga hivyo maranyingi hukutana na kuwa pamoja kipindi au msimu wa kuzaliana. Mondo huweza kuzaa mara 2 kwa mwaka.

Jike anapokuwa katika kipindi cha kuhitaji kubeba mimba hutoa mlio ambao humvutia dume na kisha anapo kutana na dume huanza kujisogeza na kuuburuza mwili wake kwenye mwili wa dume. Kwa kawaida jike huwa katika kipindi hiki kwa takribani siku 1-4 hivyo dume hulazimika kuwa pamoja na jike kwa siku zote hizo. Mara baada ya kupandana jike huondoka hali kadhalika pia dume huondoka na kila mmoja huendelea na shughuli yake mwenyewe. Hali hii imepelekea wanyama hawa hasa majike kuitwa au kupewa jina la mlezi mmoja.

Jike hubeba mimba kwa muda wa siku 65-75 (sawa na miezi miwili na siku tano mpaka kumi na tano) na baada ya hapo huzaa watoto kati ya 1-3. Lakini kwa mara chache sana mondo huweza kuzaa watoto hadi watano. Watoto huzaliwa wakiwa hawaoni, masikio yamejikunja ambayo hukunjuka baada ya muda mfupi tu, miili yenye rangi ya kijivu na huwa na uzito wa gramu 250. Watoto huanza kufumbua macho kati ya siku 9-13. Mama hulazimika kuwinda mara kwa mara ili kuzalisha maziwa yakutosha kwaajili ya watoto kunyonya nawatoto wafikishapo miezi 5-6 huanza kula nyama. Kwa kipindi chote chini ya miezi 3 mama hulazimika kuwahamisha watoto sehemu tofauti tofauti zilizo jificha ili kuwakinga dhidi ya maadui.

Watoto wanapokuwa wakubwa mama hulazimika kuwafukuza watoto wa kiume kabla ya watoto wa kike. Watoto wa kiume huanza kupanda wafishapo miezi 17-26 wakati watoto wa kike huwa na uwezo wa kubeba mimba wafikishapo miezi 15-16 na kwa kipindi hiki wote huwa tayari wana jitegemea tofauti na kumtegemea mama kwani wanakuwa washa fukuzwa na mama katika himaya.

Mondo wawapo katika mazingira yao asilia wanawezakuishi na kufikia miaka 10-11 ila kma wanafugwa katika mabustani ya wanyama basi huweza kufikisha myaka 20-22.

UHIFADHI

Hiki ndio kipengele muhimu sana katika makala hizi kwani kipengele hiki kitakupa mwangaza kujua hadhi ya mnyama husika hapa nchini kwetu na duniani kwa ujumla. Hivyo nakusihi ufikapo kwenye kipengele hiki kisome kwa umakini na utulivu wa hali ya juu.

Idadi ya wanyama hawa bado ni ya kuridhisha hapa barani Afrika na hii ni kwasababu wanyama hawa wamekua wakionekana maeneo mengi sana hususani hapa nchini Tanzania. Tafiti hizi zimefanywa na shirika la umoja wa mataifa linalo simamia uhifadhi wa maumbikle asili (IUCN-International Union for Conservation of Nature) mwaka 2014.

Japo idadi ya wanyama hawa bado ni ya kuridhisha lakini kuna baadhi ya nchi wanyma hwa wamekuwa wakionekana kwa nadra sana. Mfano mzuri kuna baadhi ya maeneo nchini Afrika Kusini wanyama hawa wametoweka kabisa. Idadi kubwa ya mondo wanapatikana katika hifadhi za taifa na maeneo mengine tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori lakini kwa mondo ambao wapo nje ya maeneo haya idadi yao imekuwa ni ngumu kujua hasa kwa upande wa Afrika kaskazini. Kuna baadhi ya nchi za Afrika kaskazini wanyama hawa wamekuwa tishio kutoweka baadhi ya maeneo katika nchi hizo ambazo ni Morocco, Algeria na Tunisia. Idadi ya wanyama wakubwa katika maeneo haya inaonekana kuwa chini ya mondo 250.

Hapa nchini tafiti ilifanyika katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na matokeo yalionesha kuwa kwa kila kilometa moja ya mraba kuna 0.42 ya mondo. Hivyo japo tunasema idadi ya wanyama hawa bado inadhirisha lakini tafiti za IUCN zinaonesha kuwa idadi ya wanyama hawa inapungua japo sio kwa kasi kubwa sana. Na hii ni kwasababu wanyama hawa wamekuwa hawa fuatiliwi kwa ukaribu zaidi kama baadhi ya wanyama wengine jamii ya paka.

TISHIO NA CHANGAMOTO KWA MONDO

Uharibifu wa maeneo yenye ardhi oevu, maeneo oevu yana changia kwa kiasi kikubwa cha mazalia ya panya kuliko maeneo mengine yoyote yaliypo baki hali ambayo inapelekea mondo kupatikana katika maeneo hayo kutokana na upatikanaji wa chakula kwaurahisi hivyo kuyaaribu maeneo haya ni tishio kubwa sana kwa wanyama hawa.

Uharibifu wa maeneo yenye nyasi hasa kwa kuchoma moto maeneo hayo. Hali hii imepelekea kwa kiasi kibwa kwa mondo kuyakimbia makazi yao na kutowekea sehemu nyingine.  Hii haisababishi ni kuharibu mazingira ya wanyama hawa bali pia kupunguza idadi ya mawindo yao.

Idadi kubwa ya mifugo inayo chungwa karibu na maeneo ya mazalia au mawindo ya mondo pia imekuwa ni tishio kubwa kwa wanyama hawa. Mifugo huaribu mazingira yao lakini pia kula nyasi au majani kwa kiasi kikubwa sana kitu kinacho pelekea kutoweka kwa wanyama hawa katika maeneo hayo kutokana na upungufu wa chakula unao tokana na kupungua kwa wanyama wadogo wadogo ambao ni mawindo yao.

Biashara haramu ya wanyama hawa imeripotiwa kuwa ni changamoto nyingine kwa baadhi ya nchi hapa barani Afrika. Japokuwa kipimo halisi cha uvunwaji wa wanyama hawa bado ni vigumu kukizungumzia lakini inaonesha kwa asilimia kubwa hufanyika ndani ya nchi hasa kwa shughuli kama sherehe za kitamaduni na matumizi ya dawa kuliko wanavyouzwa nje ya nchi kwa dhumuni la kibiashara.

Kuna baadhi ya nchi manyoa ya wanyama hawa yamekua yakiuzwa sana kwa watalii na wengine kufikia kudanganya kama ni manyoa ya chui kwasababu tu yanafanana na ya chui. Kati ya nchi ambayo inakumbwa na changamoto hii kwa kiasi kikubwa ni Nigeria.

Changamoto nyingine kubwa kwa mondo ni mauwaji ya kisasi toka kwa binaadamu. Watu wamekuwa wakiwauwa wanyama hawa kwa kulipizakisasi kutokana na wanyama hawa kula mifugo yao kama kuku. Mondo wanaopatikana karibu na maeneo ya makazi wamekuwa wakila kuku na kusababisha kuuwawa kutokana na kula mifugo.

NINI KIFANYIKE KUWANUSURU MONDO HASA HAPA NCHINI KWETU TANZANIA

Usimamizi na utekelezaji wa sheria zinazo simamia uhifadhi wa maeneo oevu. Hii itasaidia sana kupambana na wale wote waao haribu maeneo haya kwa makusudi kwani tumeona athari zake kwa mondo, na si mondo tu bali hata kwa viumbe hai wengine ambao maisha yao kwa asilimia kubwa hutegemea maeneo oevu.

Kuzuia uvamizi wa watu katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori. Hii itasaidia kuepukana na matatizo kama ya uchomaji moto hovyo kwa ajili ya upanuzi wa mashamba lakini pia mauwaji ya wanyama hawa kutokana na kulipiza kisasi kwa ajili ya kuliwa kwa mifugo yao.

Wizara ya maliasili kwa kushirikiana na wizara ya mifugo wasimamie changamoto ya uingizwaji wa mifugo katoka maeneo wapatikanayo mondo. Hii itasaidia kupunguza athari zitokanazo na idadi kubwa ya mifugo kuvamia maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

Kudhibiti biashara haramu ya mondo ambayo inasababishwa na kigezo cha utalii. Hali hii itasaidia kupunguza kuuwawa kwa wanya hawa kwani kuna watu wasio na huruma na maliasili zetu wenye ufisadi na kujali matumbo yao wenyewe kuliko kmbele maslahi ya taifa.

Kudhibiti matumizi ya mondo kwenye sherehe za kitamaduni au kwa matumizi ya dawa bila kuwa na vibali maalumu vya uwindaji wa wanyama hawa. Kigezo cha dawa kinaweza kuwa sababu kubwa sana ya kuuwawa kwa wanyama hawa na wakati mwingine wasitumike kwa kusudi maalumu la dawa bali kama biashara.

HITIMISHO

Hakun jambo zuri kama ifike siku na wewe uwaambie wajukuu zako kuwa ulishiriki kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha mondo wanaendelea kuwepo hapa nchini na kuwakuta kwao basi kumetokana na jitihada zenu wakati huo. Hii ita saidia sana kwa vijana hao kukuwa huku wakiwa na hamasa ya uhifadhi wa wanyamapori kwani watakuwaa wamejifunza mengi kupitia wewe kama babu au bibi yaao

Pongezi kubwa kwa mamlaka zinazo simamia uhifadhi wa wanyamapori na zile zinazo fanya tafiti mbali mbali hapa nchini na duniani kote kuhakikisha wanyamapori wanaendelea kuwepo kwa faida ya vizazi vijavyo. Kazi kubwa sana inafanywa na mamlaka hizi kwani wanajitoa kwa hali na mali mbali na kukutana na changamoto nyingi lakini hawakati tama. Hongereni sana TANAPA, TAWA, Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yenu.

Sisi wananchi pia tuna jukumu kubwa sana la kuhakikisha tuna shirikiana na mamlaka hizi hata kama hatupo kwenye mifumo yao kwa kutoa taarifa kuhusu wale wote wanao fisidi maliasili zetu kwani wamekuwa wakinufaikawao tu bila kujali maendeleo yaw engine. Majangili ni watu wenye roho zisizo na imani hivyo tukiweza kuwafichua tutakuwa tume zisaidia mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori kwa kiasi kikubwa sana.

…………………….MWISHO………………

Mwisho wa makala hi indo mwanzo wa makala nyingine, hivyo nikusihi uendelee kufuatilia mfululizo wa makala hizi ili uweze kujifunza mambo mengi sana kuhusu wanyamapori.

Kwa mawasiliano, maswali na ushauri kuhusu makala hizi basi usisite kuwasiliana nami kupitia;

Sadick Omary Hamisi

Simu= 0714116963 na 0765057969

Email; swideeq.so@gmail.com

Instagram; wildlife_articles_tanzania

Au tembelea tovuti yetu; www.wildlifetanzania.home.blog

…………..I’M THE METALLIC LEGEND……….