Habari mpenzi msomaji wa makala hizi za maliasili , Bila shaka ni mzima na buheri wa afya. Matumaini yangu tunaendelea kujifunza mengi kutokana na makala hizi ambazo huandikwa na waandishi wenye umakini na ufahamu wa maliasili zetu ambazo huandikwa kwa lugha yetu pendwa.
Tuzidi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19, Kwani kinga ni bora zaidi.
Karibu sana katika makala yetu ya leo tujifunze machache ambayo yatatuongezea ufahamu zaidi kuhusu wanyama wa mwituni. Asante twende pamoja
Siku ya leo tutajifunza kwa uchache na ufupi kabisa namna ambavyo wanyamapori nikigusa makundi ya wala nyama na wala majani na wengine wadogo kwa wakubwa jinsi wanavyotumia vinyesi vyao, na vya wanyama wengine, mikojo, mizoga , majani ya miti na matunda kwa matumizi mbalimbali katika maisha yao ya kila siku ,
- Katika kuhakikisha usalama wa familia zao
- Kupunguza wadudu ambao ni hatarishi kwa afya zao
- Kutengeneza harufu ambazo huwasaidia katika uwindaji
- Kujitibu vidonda na michubuko mbalimbali katika miili yao
- Kuweka kiwango sawa cha joto katika miili yao
- Kuhakikisha usafi wa mwili na katika kikundi cha familia.
Kama ilivyo kwa binadamu, huwa tunatumia njia, au vitu vya aina fulani ili kuhakikisha mambo yanaenda sawa hususani katika kuhakisha, tuko sawa kiafya, kuhakikisha usalama katika familia zetu, kutumia marashi ya aina tofauti ili kutufanya tuwe nadhifu na watanashati kabisa, pia huwa tunatumia miamvuli ili kujikinga na mvua, kutumia kofia kuweza kujikinga na jua, pia huvaa nguo kulingana na hali ya hewa hususani kipindi cha joto huvaa nguo ambazo ni nyepesi kidogo ukilinganisha na kipindi cha baridi.
Kwa kuanza nianze na wanyama hawa, natumaini kwa kusoma wanyama hawa wachache utapata uelewa mpana na kufahamu wanyama wengine zaidi, na pindi ukipata nafasi ya kutembelea Hifadhi za Taifa, ukitazama filamu mbalimbali zihusuzo wanyama pori na kwa kutazama vipindi mbalimbali ambavyo hutangazwa kwa kupitia channel yetu pendwa Tanzania safari channel, jitaidi usiangalie kwa mazoea jaribu kuwa na jicho la tatu ambalo litakufanya ujue mengi wanayoyafanya hawa wanyama.
Twende pamoja
FARU
Faru hutumia mikojo na vinyesi kutambua uwepo kila faru aliyopo kwenye kundi, pamoja na afya zao, Faru pia hutenga eneo maalumu kwa ajili ya kujisaidia, Hufanya hivyo kwa lengo la kuhakikisha usafi, hivyo faru hawajisaidii kila mahali na pia huwa ni sehemu ya kukutana na kujua hali ya kila mmoja katika kundi. kama binadamu vile tunakua na vyoo kwa ajili ya kutupa taka mwili, vivyo vivyo faru hutenga eneo ilo kwa ajili ya kujisaidia, kukutana kujuana hali, na maendeleo ya kila faru katika eneo husika.
FISI
Fisi hufahamika kama Bwana Afya wa porini, bila Fisi mbuga zetu zingekua zinanuka mizoga, tungekua tunatumia gharama kubwa sana kusafisha masalia ya wanyama wafu. Basi pongezi kubwa kwa huyu kiumbe ambacho ni kiungo muhimu sana kuweka hali sawa ya kiikologia Tabia ya fisi ni hii kabla au baada ya kula, basi hufanya kujiviringisha na ule mzoga wa mnyama na kupata harufu ya ule mzoga.
Pia Fisi wana ishi katika Familia inayojulikana, na huwa wanatumia harufu kali ambayo hutengenezwa na gland ambayo inapatikana katika vinyesi kwa ajili ya kuweka mipaka katika familia yake, wanapaka hiyo harufu katika majani ili kuzuia kundi geni kuingilia eneo lao, hivyo kuwa na eneo la kutosha ambalo hufanya shughuri za uwindaji na shughuri zingine za kila siku, Pia huwa wana eneo maalumu ambapo fisi wote katika familia huwa wanajisaidia hapo “Kinyesi na mikojo” ambapo hujumuishwa kama moja ya eneo la familia, eneo linajulikana kwa lugha ya kiingeleza kama “Latrines”. Binadamu tunaita choo.
SOKWE
Sokwe ni mnyama ambaye ana haiba sawa na binadamu, wanatumia majani katika kufuta Damu sehemu walizoumia na wakati wa hedhi, kufuta vinyesi mara baada ya kujisaidia, Baada ya kujamiiana, mabaki ya chakula, matope, maji, katika miili yao. Pia hutumia majani katika kutengeneza malazi yao. Kama binadamu tunavyotumia vitambaa, madekio kusafisha makazi yetu, kutumia taulo kujifuta maji pindi tukitoka kuoga, kusafisha vidonda kwa kutumia dawa mbali mbali mbali, vivyo hivyo kwa sokwe hutumia majani, matawi ya miti katika kuhakikisha usafi katika Mazingira yanayowazunguka na katika miili yao. Pia binadamu tunavyotumia miamvuli kujikinga na mvua vivyo hivyo na sokwe hutumia matawi ya miti na majani mapana kujikinga dhidi ya mvua
Si ajabu kukuta sokwe anaumia matawi ya miti, mawe, mchanga, kufukuza maadui kama chui, binadamu na wadudu wengine wasumbufu , kama njia ya kujihami. Sokwe hutumia vijiti kwa ajili ya kujitafutia chakula, huingiza miti kwenye mashimo ya mchwa na kutoa, mchwa ambao wametoka pamoja na kijiti huwatumia kama chakula.
WANYAMA WENGINE JAMII YA NYANI
Jamii ya nyani kwa asilimia kubwa, wanatumia vitu kama Majani ya baadhi ya miti , Jongoo na matunda Kujipaka, wanachanganya na mate, ndio hujipaka, Jamii kubwa ya nyani wanajiogesha kujiogesha na mikojo yao, wanachofanya wanaweka kiasi kidogo cha mkojo katika mikono yao na kujipaka katika sehemu mbalimbali za mwili hususani katika miguu yao, Kwa kufanya hivi huwa ni sehemu ya kuhakikisha Usafi katika miili yao, pia kuweka sawa kiwango cha joto mwilini, na kuzuia miwasho ambayo pengine husababishwa na kungatwa na wadudu kama viroboto na wengine wengi, Pia hujipaka mikojo kwa ajili ya kuwasiliana.
SIMBA
Simba ni moja ya mnyama ambaye huweka mipaka ya utawala, kwa kutumia mikojo. Huwa ana weka mikojo kwenye miti, majani na hata mawe na vitu vingine , ili kutambulisha eneo rasmi la utawala katika kundi husika,na hufanya hivyo kila mara anavyozunguka kukagua mipaka yake ya utawala, hili zoezi hufanywa na simba dume , hivyo humsaidia kutambua mipaka ya utawala na kuhakikisha kuna ulinzi wa kutosha kwa familia, na kuwa na eneo la kutosha kwa ajili ya kujitafutia chakula, kuzaliana na kufanya shughuri zingine ambazo huwasaidia katika kuishi maisha yao. Pia hutumia sauti katika kutambulisha mipaka ya utawala, na hufanya hivyo jioni wanapotoka kwenda kuwinda na kabla hawajaamka asubuhi.
WANYAMA WAKUBWA WALA MAJANI
Hapa na jumuisha Nyati na Tembo, wanyama hawa huwa wanatumia mbinu mbalimbali za kuweka kiwango sawa cha joto katika mwili, na kupunguza idadi ya wadudu ambao hatarishi katika ngozi za miili yao, hivyo usishangae ukakuta muda mwingi wanatumia katika madimbwi ya maji na tope wakiogelea, na mara baada ya kutoka kwenye maji au tope, huji mwagia vumbi kudhani kwamba wanajichafua, la hasha wanachofanya , pindi wanapoingia kwenye maji au tope wanapunguza wadudu katika miili yao, na pale wanapo jimwagia vumbi au mchanga wana punguza athari za miaonzi ya jua kuharibu ngozi zao, na kupunguza hatari ya kuathiriwa na wadudu hususani viroboto na kupe na wengine wengi ambao ni hatarishi katika ngozi zao.
HITIMISHO
Kama vile binadamu tunavyohakikisha ulinzi katika familia zetu, usafi katika Mazingira yanayotuzunguka, vivyo hivyo hawa wanayama wa mwituni hutumia mbinu tofauti ili kuhakisha usafi, ili kujikinga na magonjwa, kujitibu na magonjwa, kujitafutia chakula nk, hivyo ni jukumu la kila mtanzania kuhamasisha na kutunza Mazingira ya wanyama hawa wa mwituni, ili tupate kujifunza mengi kutoka kwao, pia kuhakikisha tunahamasishana kwenda kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi na kujifunza mengi zaidi.
Dunia ipo kwenye hamaki kubwa juu ya huu ugonjwa wa COVID-19, basi kwa kipindi hiki cha kujitenga, tutumie huu muda kujifunza mengi kupitia makala hizi za wanyama pori, hivyo ukipata nafasi, baada ya janga hili kupita ukitembelea Hifadhi za Taifa uwe na ufahamu mpana juu ya wanyama hawa adhimu ambao ni zawadi kubwa kwetu
Nichukue nafasi hii kuwasihi na kuwakumbusha tuzidi kuchukua tahadhari juu ya huu ugonjwa wa COVID-19, kama serikali inavyoagiza.
Imeandaliwa na ;
Naomi Mnyali
CONTACT 0788 706 476
Email: naomimnyali@gmail.com