Habari mpendwa msomaji wetu wa makala za wanyamapori, ni matumaini yangu umzima wa afya na mwenye nguvu nyingi za kupambana na michakato mbalimbali ya maisha. Karibu darasa huru tena ili tuweze kuendelea kujifunza zaidi wanyamaporina uhifadhi wao kwa ujumla. Ni Imani yangu, unaendelea kujifunza na kupata taarifa sahihi za wanyama hawa kama ambavyo leo nimekuandalia makala ya twiga ambaye ndio mnyama wa taifa letu. Karibu sana tuanze pamoja na tumalize tukiwa na kitu kipya.

Utangulizi:

Twiga ndiye mnyama mrefu zaidi duniani kuliko mnyama mwingine yeyote yule aliyejaliwa upole licha ya kwamba haoni karibu. Twiga anapatikana barani Afrika baada ya wale wa bara la Asia kutoweka, hasa katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara katika nchi za Afrika ya kati, kusini na mashariki. Na katika nchi hizo hupendelea zaidi kwenye uoto wa savanna yenye uwazi nyasi fupi na zenye miti mirefu wakati mwingine wenye misitu minene. Twiga huyu yupo kwenye spichi ya “Masai giraffe” ambayo ndio kubwa zaidi ikiambatana na spishi ndogo 9 ambazo zote ni rahisi kuziona kwenye safari za kitalii kwenye nchi za Afrika mashariki, na huishi kwa muda wa miaka 15 porini ila hufikisha miaka 30 akiwa katika ungalizi mkubwa kwenye zoos.undefined

Pia, twiga ni mnyama aliyejitwalia umaarufu sana hasa nchini kwetu Tanzania anapotumika kama miongoni mwa alama za taifa, japokuwa kuna wanyama wengine wanaotumika nchi tofauti tofauti mfano simba kama alama ya taifa nchini Ethiopia, Iran, Kenya, Libya, Singapore na Morocco.

Sifa zake kubwa:

  • Twiga ndiye mnyama mrefu zaidi duniani, twiga mkubwa ana urefu wastani wa 15-19 (4.5-5.7m) wakati huo wastani wa uzito wake ni 2000-2600Ibs (900-1190kg) ambapo dume huwa na uzito wa 1930kg na jike uzito wake hufika 1180kg.  Katika mwili wake vitu vikuu viwili vinavochangia urefu ambavyo ni miguu na shingo yake pia ndivyo vimemwezesha awe na uwezo wa kukimbia 50-60km kwa saa. Wakati huo huo pia mkia wake una urefu wa 1m uliojaa nywele nywele nyeusi mwishoni. Lakini cha kushangaza shingo yake ni fupi sana kwenda chini na hivyo humlazimu kutawanya miguu yake ili aweze kufikia maji yapo.
  • Urefu wa shingo na miguu ya twiga kumemfanya awe na moyo wenye uzito zaidi ambao sawa na 25pounds kwa lugha nyingine ni 11kg. Wakati huo ukifananisha na wa binadamu ni mbali sana wenyewe una uzito wa 0.25kg hivyo, kutokana na uzito huo kumeufanya moyo huo kuwa na nguvu nyingi ili uweze kusukuma damu na hewa ya oksigeni nyingi iweze kufika umbali wa 2m kuufikia ubongo ulipo.
  • Kila twiga ana madoa yake na yamepangika tofauti katikati yao kama ilivyo kwa alama za pundamilia na alama za vidole kwa binadamu. Hivyo, kutokana na hayo madoa kuwa tofauti kwa kila mnyama kumechangia zaidi kufanikisha tafiti mbali mbali za mnyama mmoja mmoja.
  • Twiga ni mnyama anayelala kwa masaa machache zaidi makadirio dakika 30 au ikiwa zaidi ni masaa 4, hufanya hivyo akiwa amesimama au wakati mwingine hulala chini shingo ikiwa juu ya mwili. Pia, ni mnyama anayetumia maisha yake akiwa amesimama hasa muda mwingi akiwa anakula (ambapo kiasi cha chakula kwa siku ni sawa na 34kg) imepelekea hata wakati mwingine kuzaa akiwa amesimama. Na ndama huo husimama baada ya nusu saa na baada ya masaa 10 hukimbia pamoja na mama yake.

Mfumo wa uzalianaji wao:

Dume moja kuwa na majike mengi, hivyo madume hulazimika kuingia kwenye ugomvi wakati wa kutafuta wake na mara nyingi hutumia zaidi shingo kupigana na mwenye shingo ndefu na imara hupata majike mengi. Pia, wakati huo huo dume hutambua jike ambaye yupo tayari kupandwa kwa kunusa mkojo ambao hutoa harufu tofauti. Jike hukaa na mimba kwa muda wa siku 400-460 ambapo hujakuzaa ndama mmoja mwenye wastani wa urefu 1.7-2m japokuwa mara chache inatokea kuzaa mapacha.

Mfanano na binadamu:

Twiga anafanana na binadamu kwa upande wa idadi ya meno ambayo idadi yake ni 32 ila tofauti kubwa ipo kwenye jinsi yalivyopangika. Pia wanafanana na binadamu kwa idadi ya mifupa ya uti wa mgongo ambayo ipo 7 kote, utofauti upo kwenye ukubwa na urefu ambapo twiga mifupa hiyo imerefuka zaidi na yenye ukubwa hivyo kumfanya aonekane mwenye shingo ndefu sana.

Maadui wa twiga:

 anakabiliana na maadui mbalimbali ikiwemo binadamu ambaye mara nyingi huwawinda kwa ajili ya ngozi, mikia pamoja na kitoweo, pia akiwa mbugani huwindwa zaidi na simba, fisi, chui na mamba hasa kipindi cha kunywa maji na hasa akiwa kwenye umri mdogo. Lakini pmashirika mengine ya uhifadhi ikiwemo shirika la kimataifa la uhifadhi wa mimea na wanyama pori (IUCN) wameongeza na kutaja kuwa twiga wanapungua kwa kasi zaidi kutokana na kupungua kwa eneo la makazi yao inayosababishwa na kilimo na makazi ya watu iliyotokana na ongezeko kubwa la watu, mapambano ya kisiasa, ujangili na mabadiliko ya kiikolojia pamoja na usimamizi mbovu wa maeneo wanayohifadhiwa.

Athari za mabadiliko ya nchi na idadi yao:

Mabadiliko ya tabia ya nchi yamechangia kwa kiasi kikubwa kutoweka kwa twiga wa Asia wakati kwa upande wa twiga Afrika wao walibadilika na kuzaliwa spishi nyingine mpya kwa upande wa Afrika mashariki yapata miaka millioni moja iliyopita. Na idadi yao kwa kipindi cha mwaka 2010 haikuwa ya kutisha ambapo idadi ya 1600 walikuwa kwenye hifadhi zilizotengenezwa na binadamu (zoos), mwaka 2016 idadi ya twiga 97500 waliokuwa wamebakia porini (mbugani) na kufikia mwaka 2020 mwezi wa tatu idadi ya twiga wakubwa jumla ni 68293 (takwimu kutoka Africa Wildlife Foundation AWF) hivyo kuingizwa kwenye kundi la wanyama waliohatarini kutoweka pasipofanyika njia yoyote ya kuwaokoa (Vulnerable species).

Asanteni kwa usomaji wenu, naamini umepokea na kuongeza kitu kipya kuhusu mnyama huyu twiga. Tuungane kwa pamoja tuwe walimu na wawakilishi bora wa utunza na uhifadhi wa mazingira kwa sababu madhara yake hayaishii kwetu wenyewe.

Makala hii imeandikwa na; Leena Lulandala

 Mwanafunzi mwaka wa tatu, UDSM.

Mawasiliano;0755369684

lulandalaleena@gmail.com.