Baada ya jana kuandika makala kuhusu hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, na kuelezea kwa undani sababu kumi kwanini ni muhimu kuitembelea hifadhi hii yenye vivutio vingi sana ambavyo vitakuacha mdomo wazi, sasa nimegeukia kwa jirani yake wa karibu kabisa anayepatikana maeneo ya huko huko Kaskazini mwa Tanzania, hii ni hifadhi ya Taifa ya Tarangire.Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ipo upande wa Kusini Mashariki mwa Ziwa Manyara. Hifadhi hii yenye ukubwa wa kilomita za mraba 2,850 inaweza kufikika kwa urahisi kutoka Arusha kupitia barababra nzuri kabisa. Mto Tarangire unaotiririsha maji mwaka mzima kuelekea upande wa Kaskazini mwa hifadhi hii ndio umeipa hifadhii hii jina hilo. Kwa sababu ya uwepo wa mto huu katika kipindi chote cha mwaka, umekuwa msaada mkubwa sana kwa maisha ya wanyamapori ndani na nje ya hifadhii hii.
Kwa kuwa nimepanga kukushirikisha baadhi ya mambo mazuri na ya kuvutia kutoka katika hifadhi hii, naomba ufuatane nami katika kukufahamisha kwa undani na umakini mambo yote muhimu ya hifadhi hii ya Tarangire, hii ni hifadhi niliyotembelea kwa muda mchache sana ukilinganisha na hifadhi nyingine nilizowahi kwenda kutembelea. Nisiwe na maneno mengi ngoja tuangalie vivutio hivi kimoja baada ya kingine, vinavyopatikana kaika hifadhi hii muhimu.
- Mto Tarangire
Mto huu ambao unaingia hifadhini ukitokea katika miinuko ya Kondoa iliyopo upande wa Kusini Magharibi, unatiririsha maji yake kuelekea upande wa Kaskazini mwa hifadhi hii kabla ya kutoka nje ya hifadhi kwa upande wa Kaskazini Magharibi mwa hifadhi hii kubwa. Mto Tarangire unajulikana sana hasa kipindi cha ukame ambapo husaidia sana kutunza maelfu ya wanyamapori na viumbe hai wengine waliopo katika eneo hili la hifadhi. Vile vile kutokana na uwepo wa mto huu kuendelea kuwa na maji mengi hadi kipindi cha ukame, idadi kubwa sana ya wanyama husogea maeneo ya karibu na mto huu, hasa sehemu za Kaskazini mwa hifadhi hii. Hii ndio sehemu nzuri ya kuona wanyama wengi na wa kila aina, kama vile makundi makubwa ya tembo na wanyamapori wengine. Kwa hiyo mto huu ni muhimu sana kwa maisha ya viumbe hai wa hifadhi hii, mimea na wanyama.
- Miti ya Mibuyu
Mibuyu, au miti ya mibuyu ndio miti inayoonekana zaidi katika hifadhi hii ya Tarangire, mibuyu ni miti mikubwa sana kwa umbo, ni miti yenye historia ya kipekee kwa uwezo wake wa kuishi na kuendelea kuwepo kwa zaidi ya miaka 1000, katika hifadhi hii ya Tarangire utajionea miti hii ya ajabu sana, ni miti inayotunza maji sana, na ni miti inayostahimili ukame sana, hivyo mara nyingi miti hii huota au huweza kuonekana zaidi sehemu zenye ukame. Tafiti za masuala ya ikologia ya miti wanasema miti hii ya mibuyu iliyopo Tarangire mingi ina zaidi ya miaka 1000; hivi kwenye maisha yako ulisha wahi kuona kiumbe hai chenye umri zaidi ya miaka 1000. Jibu lako ni hapana. Sasa hapa ndio sehmu pekee unaweza kuona maajabu haya ya miti ya mibuyu.
- Maficho ya majangili
Maficho haya ni kama pango ambalo walitumia miaka ya nyuma sana, kama sehemu ya kujificha na kujihifadhi. Maficho haya yapo ndani ya mti wa mbuyu ambao ni mti mkubwa sana kuliko miti yote ya hifadhi ya Tarangire, pango hili linakadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 300. Uwazi uliopo kwenye mti huu wa mbuyu ni zaidi ya kipenyo cha mita kumi. Ndani ya maficho/pango hili lina uwezo wa kuchukua au kuhifadhi zaidi ya watu 20, ambao wengi waliotumia eneo hili ni wawindaji. Ni sehemu nzuri sana ya kutembelea na kuona ili upige picha na kujionea ukuaba wa pango hili lililopo ndani ya mbuyu.
- Makundi makubwa ya tembo
Hifadhi ya tarangire ina makundi makubwa sana ya tembo, kipindi cha ukame (dry season), hifadhi hii inakadiriwa kuwa na tembo zaidi ya 4000 na 6000, lakini tembo wengi zaidi wanaweza kuonekana kipindi cha mvua. Karibu sana utembelee hifadhi hii nzuri.
- Ndege
Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ina zaidi ya jamii 550 za ndege ambao ndio wamejulikana, na kati ya ndege hao baadhi yao wapo katika tishio la kutoweka. Tafiti zinaonyesha kwamba kipindi cha mvua ndio kipindi kizuri sana kwa aina nyingi za ndege kwenye eneo hili kuzaliana kwa wingi. Mabwawa na mito iliyopo katika hifadhi hii yanakuwa ndio sehemu nzuri zaidi ya kuona ndege wengi sana. Vile vile uoto wa asili katika hifadhi hii ndio unaopelekea wingi wa ndege katika eneo hili.
- Mabwawa
Katika hifadhi ya Tarangire kuna mabwawa makubwa na mapana sana, ambayo ndio sehemu kuu ya vyanzo vya maji kwa sehemu za hifadhi hii, mabwawa haya husaidia kusambaza maji sehemu za Kaskazini za hifadhi hii hadi kwenye ziwa Burunge ambalo ni ziwa la msimu. Mabwawa ni sehemu muhimu sana ya hifadhi yoyote, kwani husaidia wanyama wengi hasa kipindi cha ukame, wanyama kama tembo na nyati hupenda sana maji.
- Vichuguu vya mchwa
Kila kitu ndani ya hifadhi kina maana na kusudi lake, uwepo wa vichuguu hivi imekuwa ndio makazi salama ya wanyama wadogo wanaokula nyama kama vile ng’uchiro, (mongoose), vichuguu hivi vilivyo achwa ndio vinavyo ipendezesha sana hifadhi hii ya Tarangire. Mwonekano wa vichuguu hivi ni muhimu kwa wageni kuweza kuwaona wanyama, pia utawakuta wanyama hawa wadogo wakicheza na kujificha kwenye mashimo madogo madogo yaliyopo ndani ya vichuguu hivi.
Pamoja na haya yote yanayo patiakana ndani ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire, nimejaribu kukupa mwanga ili ujue wapi utapanga kwenda kutembelea hifadhi za wanyama. Pamoja na hayo machache pia kuna vivutio vingine unaweza kuviona ukiwa hata nje ya hifadhi hii ya Tarangire. Hivyo naamini kabisa umepata kitu cha kukusaidia hapa.
Kama una maswali, ushauri na hata maoni, usisite kuwasiliana na mimi, kwa namba za simu hapo chini au kwa email yangu hapo. Au unaweza kuacha comments yako hapo chini. Yote ni mema kwa ajili ya kujengana na kusaidia kukuza utalii na maarifa kwa watanzania wote.
Kila la kheri katika maandalizi yako ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569
hillarymrosso@rocketmail.com