Je! Wajua, binadamu yupo hatarini kutoweka kuliko hata faru? Katika kipindi hiki kigumu cha tukio kubwa la sita la utowekaji wa viumbe (sixth mass extinction) binadamu bado ananafasi na fursa ya kufanya maamuzi madogo ya kujiokoa na kuwaokoa viumbe wengine.
Ni matumaini yangu msomaji wetu wa makala hizi umzima wa afya na mwenye nguvu. Nipende kukukaribisha tena kwenye darasa letu huru kabisa la uhifadhi na wanyamapori kwa ujumla katika somo la leo ambalo naamini litakubadilisha na kukujenga mahali, somo ambalo linahusu jinsi shughuli za kibinadamu zinachangia kwa kiasi kikubwa tulio la sita la utowekaji wa viumbe (sixth mass extinction) mbalimbali.
Utangulizi
Tukio la kutoweka kwa mimea na wanyama (mass extinctions) ni tukio ambalo nusu ya spishi zilizopo duniani kutoweka kwa muda mfupi. Ikumbukwe kila spishi iwe ya mimea au ya wanyama ina muda wake wa kutoweka kiasilia, lakini inapotokea ndivo sivyo kwamba spishi nyingi zenye uwezo wa kukaa duaniani tofauti tofauti vikalazimika kutoweka kwa muda mfupi hiyo huingizwa kwenye matukio makubwa ya kutoweka kwa viumbe duniani. Kuna matukio makubwa matano ambayo yamewahi kutokea na kusababisha nusu ya spishi duniani kutoweka pasipo kusahau tukio kubwa la sita ambalo dunia inapitia sasa. Matukio hayo ni pamoja na
- Miaka 440 milioni iliopita (Ordovician-Siluvian extinction). Tukio hili lilihusisha kutoweka kwa wanyama wadogo wadogo wa majini, na inasemekana ilisababishwa na mabadiliko ya ghafla ya mawimbi ya bahari yaliyoambatana na hali ya baridi kali hasa maenano ya kiikweta.
- Miaka ya milioni 365 (Devonian extinction). Tukio hili lilihusisha wanyama wa majini pia hasa maeneo ya kitropiki na sababu kubwa kwa kipindi hiki ilikuwa mlipuko wa volkano Siberia iliyopelekea kupungua kwa wingi hewa ya oksigeni katika bahari.
- Miaka milioni 250 (Permian-triassic extinction). Tukio hili linasemekana ndio kubwa kwa upotevu mwingi wa spishi kuliko yote matano ambayo yaliwahi kutokea pia ilipoteza spishi nyingi tofauti tofauti za wanyama wenye uti wa mgongo. Tukio hili lilisababishwa na mlipuko wa volkano Siberia iliyopelekea kusambaa kwa hewa chafu iliyoungana na tindikali na kuharibu maji ya bahari, hewa chafu hiyo inasemekana ilitoboa ‘ozone layer’ kuruhusu miale mikali ya jua kuifikia duniani moja kwa moja.
- Miaka 210 (Triassic-Jurassic exntiction). Tukio hili lilitokana na mlipuko wa volkano kwenye bahari ya Antlantic ambayo ilipelekea mabadiliko makubwa ya tabia ya nchi na hivyo wanyama wengi wa nchi kavu kutoweka na kupisha uzalianaji wa mijusi mikubwa (dinosaurs).
- Miaka 65 (Cretaceous-tertiary extinction). Tukio hili la kutoweka kwa viumbe pia lilisababishwa na mlipuko wa volkano kwenye bahari ya India ambapo uliongeza utengenezaji wa hewa chafu ya Cabonidioksaidi (CO2) na kuingia kwenye maji ya bahari, hivyo kupunguza hewa ya Oksijeni na kutengenezeka kwa baridi kali. Na hali hiyo ikapelekea mijusi wengi wakubwa kutoweka na walioweza kubakia walitengenezeka tofauti wengine wakawa ndege na wengine kama wanyama wanyonyeshao.
- Miaka milioni 0.01 (Holocene extinction/ Anthropocene extinction). Tukio hili limetajwa kuwa linaweza kusababisha upoteaji wa viumbe wakubwa kutokea unaosababiswa na shughuli za binadamu. Je, wajua sis indo kizazi pekee tunaoshuhudia tukio hili? na wenye kulazimika kufanya maamuzi ili kuokoa na kupunguza kasi utowekaji au kuacha na tuje kujionea madhara yake!!
Hayo ndiyo matukio makubwa ya kihistoria yaliyowahi kutokea katika utowekaji wa aina tofauti tofauti za viumbe kabla hata ya umri wake wa kutoweka. Je? wajua sisi ndo kizazi pekee cha kufanya mabadiliko katika utunzaji wa viumbe wote? Makazi yao? Pamoja na dunia kwa ujumla? ili kupunguza kasi ya utokeaji wa tukio la sita. Labda nikufumbue macho kwa sasa dunia inapitia tukio kubwa na gumu la sita la utowekaji wa aina mbalimbali za viumbe. Chaguo sahihi lipo vichwani mwetu, kusimama imara kutetea dunia yetu au kuiacha iende vile inavyoenda na mwisho wa siku tujekutumiua sentensi zenye neno ‘nge’. Kuna kitu kingine kidogo cha kukitazama tuu kawaida, angalia idadi ya spishi za wanyama ambao wapo kwenye orodha ya wanyama ambao wapo hatarini kutoweka duniani (IUCN Red List) ni 116,000 sawa inawezekana wapo ambao muda wake umeisha duniani hivyo ni lazima watatoweka tu, lakini ndio ziwe spishi zote hizi kwa wakati mmoja? Ni kitu ambacho hakiwezekani.
Utawala wa binadamu katika dunia ambao hauzidi hata miaka milioni moja umechangia maafa makubwa na uharibifu mkubwa sana majini, nchi kavu na hata angani unaosababishwa na shughuli mbalimbali za kila siku kama uchomaji wa mafuta ya mabaki ya vitu vya zamani (fossil fuels), uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa hasa na wakulima pamoja na wafugaji katika kutafuta riziki zao, uwindaji huria usiofuata taratibu na mpangilio wa kiikolojia, biashara haramu za wanyamapori pasipokujali kazi kubwa zinazofanywa na wanyama hao katika makazi yao kusaidia wanyama wengine, utanuzi wa makazi ya watu kwenye maeneo yaliyotengwa kama hifadhi pamoja na shorobo za wanyamapori, utupaji taka ovyo, ukataji miti na misitu, kilimo kisichofata kanuni na taratibu zenye muongozi wa kilimo bora chenye tija katika kuilinda ikolojia, pia matumizi ya kupita kiasi kwenye kutumia dawa mbalimbali za kuua wadudu na mimea sumbufu mashambani.
Hivyo shughuli zote hizo zinapeleka ikolojia ya dunia nzima kushindwa kufanya kazi vizuri. Na badala yake kufungua milango ya majanga mengi yanayoitikisa dunia mfano kubadilika kwa kasi sana kwenye tabia ya nchi yenye kuambatana na ongezeko kubwa la joto, mvua zisizo endana na majira ya mwaka, ongezeko la ukame baadhi ya maeneo, vita juu ya siasa na mali asilia.
Majanga haya yote yanaathari kubwa sana kwa binadamu (ambapo sisi ni tegemezi kwenye mimea na wanyama wengine) pia na kwenye ukuaji na uzalianaji wa viumbe pasipokujali ni mimea au wanyama na hivyo kuongeza kasi ya kutoweka mfano wanyama ambao wapohatarini sana kutoweka ni pamoja na faru, tembo (japokuwa idadi imeanza kuongezeka), wanyama wakubwa walao nyama pasipokumsahau mbwa mwitu, sokwe mtu, n.k.
Ikumbukwe kuna vitu ambavyo mara nyingi tunazaliwa tumevikuta hivyo hasa kwenye jamii zinazotuzunguka na kwa namna moja havina mchango mkubwa sana kwenye kuhifadhi ikolojia ya maenao hayo zaidi sana ni kudidimiza na kuharibu. Hapo jua unahitajika wewe uwe badiliko kwa lile eneo au ile jamii, usione aibu kuwa badiliko zuri kwa jamii hasa katika kutunza, kulinda na kuhifadhi mazingira yetu kwa sababu madhara yake hayampati mmoja bali wote wanaozunguka jamii hio. Mfano mdogo, matumizi ya dawa za wadudu kwenye mashamba yetu yasiyofuata maelekezo na kanuni za kisayansi zinauwa wadudu ambao dawa haikutengenezwa kwa ajili yao na hivyo kupunguza uchavushaji wa mimea na mwisho wake ni mapato madogo yenye kuleta janga la njaa. Yapo mambo mengi yenye kuendana na hili hivyo tujitahidi kuwa mabalozi wazuri wa mazingira.
Katika kipindi hiki cha tukio la sita la utowekaji wa aina mbalimbali za viumbe, je shughuli za binadamu ndizo zilaumiwe au ongezeko la watu ndilo lilaumiwe?, hakuna chaguo sahihi hapo kwani lawama haibadilishi kitu. Badala yake ni kuchukua hatua zozote tuwezavyo katika kuitetea dunia na kupunguza kasi ya utowekaji wa spishi pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi. Mtu mmoja mmoja kuchukua hatua za awali inawezekana kama kutenga maeneo maalumu ya kutupa taka, upandaji wa miti, kufata kanuni na taratibu elekezi za kilimo bora na chenye tija kiikolojia, kutokana na kwamba inaweza kuwa ngumu kufanywa na kila mtu kwa kuamua mwenyewe kutokana na ufinyu wa akili na viburi.
Hivyo basi, wizara husika zenye mamlaka na zenye kushikilia utunzaji, ulinzi na uhifadhi wa mazingira na mali asilia, taasisi za kiserikali na za binafsi, vyama na club mbalimbali mashuleni na mitaani kuandaa baadhi ya hatua na miongozo katika kupiga vita janga hili la utowekaji wa viumbe. Hatua baadhi kama mwangaza kwa taasisi zinazohusika pamoja na wizara ni kama
- Utoaji wa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira na viumbe asilia pamoja na umuhimu wake. Elimu hii ikitolewa izingatie sana umri, kazi za wanajamii, shughuli wanazofanya pamoja na asili yake na tamaduni hii tasaidia sana kujenga uelewa wa haraka katika fikra zao. (elimu ya hivi ili iweze kueleweka kwa haraka na ufasaha ni vizuri zaidi mtoaji mada au muelimishaji awe wa ile jamii lengwa, hata pale lugha inayoeleweka kwa wote isipojitosheleza lugha mama inaweza tumika na pia iwafikie watu wote kupitia vyombo vya habari,mikutano, makongamano pamoja na semina). Pia, umuhimu wake wa mazingira na viumbe asilia sio lazima utajwe upande wa fedha ambazo kwa naman moja au nyingine ni ngumu kumfikia kila raia bali upande wa faida za moja kwa moja kama kutusafishia hewa nzuri, kututunzia vyanzo vya maji n.k.
- Kupunguza uhitaji wa malighafi zitokanazo na viumbe pori na zenye kuutoa uhai wa kiumbe huyo. Mfano mdogo, tembo wengi na faru wamekuwa wakipotea kwa kasi sana barani Afrika kwa sababu ya meno na pembe zao yani kuua mnyama mwenye uzito wa kilo 4000/7000 kwa sababu tu ya jino/ pembe lake lenye uzito usiozidi hata kilo 100, ni zaidi ya uonevu na ubinafsi uliopitiliza, wauwaji wakilenga kutengeneza dawa au urembo. Yani urembo wako wewe mtu mmoja ambapo hauzidi hata uzito wa kilo 150 ndo umuue mnyama mwenye kilo 4000/7000, si sahihi hivyo ni lazima kupunguza uhitaji wa maligfhafi hizo kwenye masoko yake barani Asia hasa nchini China na Vietnam. Na, kama kuna dawa mbadala au urembo mwingine ni bora kutumia hivyo kuliko kuua wanyama hawa, ambao kupata mtoto mmoja tu kuna mgharimu miezi isiyopungua 22 ambayo takribani miaka miwili.
- Uhifadhi shirikishi wa mazingira na viumbe pori kwa jamii husika. Katika kila sehemu haijalishi ipo karibu na eneo tengefu la uhifadhi au liko mbali na maeneo hayo, kuna sughuli nyingi za kiuhifadhi zinaweza ratibiwa na kushirikisha wanajamii hivyo kutunza na kulinza mazingira kwa ujumla. Mfano upandaji miti, utunzaji wa vyanzo vya maji, kujiwekea sharia zenye makali kwa watu watakao kuwa wanaenda kunyume na makubaliano katika utekelezaji huo. Kwa jamii zilizopo karibu na maeneo maalumu ya hifadhi mbalimbali za mazingira, misitu na viumbe pori ni vyema zaidi wakishirikishwa kwenye tafiti mbalimbali zinazofanyika, watumike kama waongoza watalii pia wapewe ajira ndogo ndogo itasaidia kuwajenga kiakili katika swala zima la uhifadhi na kuwa wakali pale ambapo watu wengine wanaenda kinyume na taratibu za utunzaji wa,mzingira na hifadhi hizo kwa ujumla.
- Utekelezaji wa sera, kanuni, miongozo, na taratibu elekezi za utunzaji, ulinzi na uhifadhi wa viumbe pori na mazingira kwa taasisi husika. Kuna taasisi mbalimbali za kitaifa na za kimataifa zenye kusimamia utunzaji na ulinzi wa mazingira na viumbe pori zinazofata sharia za kwenye makubaliano pamoja na taratibu a utekelezaji hivyo zifate makubaliano na zitekeleze kazi zake ipasavyo ili kupunguza kasi ya utowekaji wa viumbe pori. Kama CITES taasisi ya kimataifa inayohusika na biashara za wanyamapori na mimea iliyopo hatarini kutoweka ni vyema zaidi izidi kutekeleza na shughuli zake kulingana na makubaliano pasipo kujali aliyekamatwa kinyume na sharia ni ndugu wa mtu fulani mwenye pesa, cheo au jina kwa sababu madhara yake tunapata wote, na hivi ikawe kwa kila taasisi na vyamba husika na kupewa adhabu kulingana na kosa.
- Kuboresha mbinu zote na vifaa vote vya ulinzi. Kwa wanyamapori waliopo kwenye mazingira ya kutengenezwa kama zoo, aquariums na captive breeding ni vyema wakalindwa pasipo kuwafanya wajisikie kunyanyasika na kusononeka kwani inatawawia wao vigumu kuendelea na ukuaji na uzalianaji. Pia, kwa wanyamapori walioko kwenye maeneo yao asilia mfano hifadhi za taifa na mapori ya akiba ni vyema kuzidi kuimarisha ulinzi na vifaa vyake ili kupunguza uwindaji haramu wa wanyama hao, uchomaji misitu na pia uvamizi wa mifugo na wakulima katika mazingira tengevu. Na wakati mwingine kuongeza nguvu za ulinzi ni pamoja na kushirikisha jamii jirani ambazo kwa haraka zinakuwa zinatoa taarifa kwa ofisi Fulani pale inapotokea majangili na shughuli zingine zilizozuiliwa kufanyika katika maeneo hayo, lakini pia ni njia nzuri kwa ulinzi na utunzaji wa mazingira.
- Uhamishaji na utambulishaji wa wanyama sehemu nyingine kwenye usalama zaidi. Pia hatua nyingine katika kupigana vita na janga hili la sita la utowekaji wa wanyama na viumbe vya aina zote kwa ujumla, inatakiwa mamlaka husika kufatilia ongezeko au upungufu wa viumbe katika eneo lililohifadhiwa na kama idadi inapungua ni vyema ziadi kufanya utambulishaji (translocation) katika maeneo mengine ambayo kwa namna moja yatasaidia ongezeko lao na pia lenye uwanja mpana na nafasi kubwa hivyo kurahisisha ulinzi na uendeshaji wa shughuli nyingine.
Inawezekana hatua tajwa hapo juu zinafanyika katika maeneo yetu lakini bado hazijajitosheleza au hazifanyiki ipasavyo, hivyo ni jukumu letu sote kukumbushana na kuzifanya kila tuwezapo ili kujiokoa, kupunguza utoekaji wa viumbe na pia kuifanya dunia kuwa sehemu bora kwa kila chenye uhai ikiwa tu ikolojia yake itakuwa kwenye mstari.
Asante kwa muda wako ulioutoa katika kusoma makala hii, lakini pia nipende kukushukuru zaidi kama utakuwa miongoni mwa watu wafanyao mabadiliko mazuri kwa ajili ya kupunguza janga hili.
Ahsanteni sana.
Makala hii imeandaliwa nakuandikwa;