Tumbusi ni ndege mkubwa ambaye anavumbua na kula mizoga iliyoachwa na wanyama wanaowinda kama simba, Chui na duma, ni ndege mwenye mnasaba na Tai hivyo hujulikana kama Tai mzoga .Wanapatikana katika Bara Ulaya, Asia, Afrika, Amerika Kaskazini na Kusini. Kuna aina mbalimbali za Tumbusi katika bara Afrika kama Tumbusi mweusi, Tumbusi ngusha, Tumbusi kichwa cheupe ,Tumbusi uso njano Tumbusi mgongo mweupe, Tumbusi kapuchini na kadhalika.
Kimwonekano Tumbusi ni ndege wasio na manyoya kichwani na shingoni ukilinganisha na sehemu nyingine ya mwili . Hii ni muhimu kwani hatochafuka kwa damu pale anapokuwa katika kula na vilevile ni rahisi kujiosha anapokuwa mtoni au ziwani. Tumbusi pia wanamidomo yenye nguvu na iliyojipinda ,hii husaidia katika kupasua mizoga ,ambapo ndege kama Kongoti hawawezi.
FAIDA ZA TUMBUSI /TAI MZOGA
◇Kusafisha mazingira ,Tumbusi pamoja na wanyama wengine kama Fisi ,Mabuu ya kipepeo na Kongoti wamekuwa waondoaji wa mizoga ambayo huleta harufu mbaya inapooza.
◇Kuweka mazingira huru kutoka kwenye magonjwa ambukuzi. Hii ni kutokana na Tumbusi kuwa na tumbo lenye asidi babuzi ambayo inauwezowa kuua bakteriana virusi kutoka kwenye mizoga iliyokufa kwa magonjwa kama Kimeta ,Kichaa cha mbwa na Homa ya nguruwe.
◇Kupunguza Gesijoto ,Tumbusi wanapokula mizoga wanapunguza kuzalishwa kwa gesi chafu inayotokana na kuoza .
◇Tumbusi husaidia mamlaka mbalimbali za Hifadhi kujua kuhusu ujangili ,ndege hawa wanapoona mzoga mahali hujazana na kuanza kusheherekea riziki yao kwa kufwatisha sehemu walipo inasaidia kugundua mizoga ya wanyama kama Tembo na Faru ambao majangili huwawinda kwa ajili ya pembe zao.
◇Huzuia kusambaa kwa magonjwa ya Zoonotic,haya ni magonjwa yanayoweza kumpata binadamu yakitokea kwa wanyama pori mfano Kimeta. Tumbusi hawana mwingiliano mkubwa na binadamu kama walivyo wala mizoga wengine kama Panya ,hivyo magonjwa hayo yanabaki kutunzwa kwao.
Changamoto zinazowakabili Tumbusi.
♧Uadui na Majangili, hii imesababishwa na Tabia yao yakuashiria uwepo wa mzoga hivyo Majangili hutia sumu kwenye mzoga wa Tembo au Faru baada ya kutoa Pembe ili Tumbusi wafe mapema bila taarifa kufikia mamlaka ya Hifadhi.
♧Kuuliwa na wakulima na wafugaji ,ugomvi uliopo kati ya wanyama pori na binadamu unamuweka Tumbusi matatani kwani binadamu hutegesha mizoga yenye sumu ili kuwanasa adui zao kama Simba na Chui wanaovamia vijiji vyao na kuua watu na wanyama kama Ng’ombe na Mbuzi.
HITIMISHO
Tumbusi ni ndege wenye umuhimu kwa binadamu kwa Karne nyingi ambapo Kuna jamii zimekuwa zinawatumia kwa Maziko ya wafu wao, wakiamini marehemu akiliwa na Tumbusi anakuwa amefanya jambo zuri la mwisho . Jamii zingine zimekuwa zikiwaona Tumbusi kama ndege wachafu ,wabaya na wanaochukiza lakini wanasahau Baniani mbaya kiatu chake Dawa.
Ni wajibu wetu kuhakikisha Tumbusi hawatoweki kama Dodo.
“Okoa Tumbusi kwa afya ya mfumo wa ikolojia“
Makala hii imeandikwa na
Maureen FN Daffa
+255 626 331 871