Mpenzi msomaji wa  makala zetu tunashukuru kwa kutenga muda wako na kusoma makala mbalimbali  ambazo zinachapishwa katika blog yetu ya http://wildlifetanzania.home.blog  . Kwa ufupi tu ni kwamba , makala yetu ya mwisho ilihusu wanyama jamii ya swala ambao kwa majina baadhi yao ni pamoja na nyumbu, tandawala, swala tomi, swala paa, nyamera, choroa, pala hala, mbarapi na wengine wengi. Katika makala yetu ya leo tutajifunza kuhusu aina nyingine ya wanyamapori ambao ni ndege. Kundi hili limekuwa halitiliwi maanani sana na waandishi na wasomaji wengi na hivyo kusababisha watu wengi kushindwa kuwajua ndege.

Kwa mujibu wa tafiti ziliwahi kufanyika nchini Marekani zinaonesha kuna takribani aina elfu kumi na nane (18,000) za ndege duniani kote. Hivyo unaweza ukaona ni kwa jinsi gani wanyama hawa walivyo wengi na kwa jinsi tafiti zinavyo zidi kufanyika wanasayansi wanazidi kugundua aina zingine ambazo zilikuwa hazitambuliki.

Ndge ni miongoni mwa viumbe ambao wametawanyika sehemu nyingi duniani. Katika makala ya leo tutamjua ndege mmoja ambaye ni mvivu wa kuatamia na kulea vifaranga vyake. Ndege huyu anaitwa KEKEO ambae kwa lugha ya kiingereza huitwa CUCKOO.

Kekeo ndege ambao wanapatikana maeneo mbalimbali hapa dunia. Ndege hawa ni wasiri sana lakini kama nilivo dokeza kidogo hapo juu ndege hawa huonekana kuwa na asili ya uvivu hasa katika kuatamia mayai na  kulea vifaranga vyao. Tafiti zinaonesha kuna takribani spishi 127 za Kekeo duniani kote ambapo zingine zinapatikana barani Africa tu.

Hivyo katika makala ya leo nitamzungumzia kekeo anae patikana barani Afrika tu na si kwingineko duniani huku na sisi hapa nchini Tanzania tukijivunia uwepo wa ndege huyu. Kekeo huyu hujulikana kama African Cuckoo ambae kwa lugha ya kiswalihi anaitwa KEKEO KIJIVU na yafuatayo ni amaelezo kuhusu ndege huyu.

SIFA NA TABIA ZA KEKEO KIJIVU

  • Ndege hawa wana manyoa yenye rangi ya kijivu na nyeupe na mili yao ina ukubwa wa wastani.
  • Kichwani, mabawa na sehemu ya juu ya miili ya ndege hawa wana rangi ya kijivu iliyo kolea zaidi huku shingoni na kifuani wana rangi ya kijivu iliyo pauka. Sehemu ya tumboni ndege hawa wana manyoa yenye rangi nyeupe na kijivu iliyo kolea.
  • Wana mabawa marefu na mikia mirefu yenye rangi ya kijivu iliyokolea na rangi nyeupe kwenye ncha ya mikia yao
  • Madume wana macho yenye rangi ya njano huku majike wakiwa na macho yenye rangi ya kahawia inayo ng’aa zaidi.
  • Kekeo wa kijivu wote majike na madume wana miguu na vidole vyenye rangi ya njano
  • Wana midomo yenye rangi ya njano hasa sehemu ya shina na kuwafanya karibu nusu ya midomo yao kuwa na rangi ya njano huku sehemu ya ncha ikiwa na rangi nyeusi. Rangi ya njano katika midomo ya kekeo kijivu huwafanya watu wengi kuwachanganya na kekeo wa kawaida kwani hata wao pia wana midomo yenye rangi ya njano.
  • Ndege hawa huishi kwa kujitenga na utafiti zinaonesha kuwa jike na dume wanaweza kuwa na himaya ambayo inakadiriwa kufikia hekari sitini na zaidi. Kiongozi wa himaya katika jamii hii ya kekeo huwa ni dume.
  • Jike hutaga mayai kwenye viota vya ndege wengine na anapo kuta kiota kina mayai basi huyatoa kisha kutaga mayai yake na kuyaacha yaatamiwe na ndege mwenye kiota. Kitendo hiki kwa lugha fasaha tunaita kizazi vimelea ambapo kwa kingereza hujulikana kama brood parasitism
  • Ndege hawa hufanya mawasiliano kwa njia ya sauti na sauti zao husikika sana hasa kipindi wanapotaka kuzaliana. Sauti ya dume hutoka kwa mlio wa “koo-koo-koo” ambao huwa na mfumo wa sauti ya pili ila yenye kusikika zaidi huku sauti ya jike husikika kwa mlio wa ”kwik-kwik-kwik”.
  • Ndege hawa huruka kwa nguvu sana na hasa kufananishwa na ndege jamii ya mwewe. Wana uwezo wa kuruka kwa kasi ya kilometa sitini kwa saa (km60/saa 1).
  • Aina nyingi za kekeo wakiwemo kekeo wa kijivu Mayai yao huatamiwa na ndege wengine na watoto kulelewa na ndege wengine

JE, WAJUA?

1.Baadhi ya jamii huamini kwenye sauti au milio ya kekeo? Baadhi ya jamii hapa nchini Tanzania huamini katika sauti au milio ya baadhi ya jamii za kekeo hasa kwenye suala la misimu ya mvua. Huamini kwamba kekeo wanapolia basi msimu wa mvua una karibia kuanza au mvua inataka kunyesha.

MAZINGIRA

Ndege hawa wanapendelea sana maeneo ya savanna na hasa yaliyo tawaliwa kwa kiasi kikubwa na miti jamii ya michongoma. Huwezi kuwaona ndege hawa maeneo yenye misitu minene. Kwa nchi za Afrika Mashariki ikiwemo hapa Tanzania ndege hawa huonekana sana majira ya msimu wa mvua hasa kuanzia mwezi wa kumi hadi mwezi wa tano.

CHAKULA

Chakula kikubwa cha kekeo wa kijivu ni wadudu na mara nyingi hutafutia chakula chao kwenye miti na hata chini. Wadudu ambao ndege hawa huwapendelea sana ni viwavi wenye vinyweleo na wasio na vinyweleo. Lakini hata baadhi ya wadudu wengine jamii ya mende na kumbikumbi hupendelewa na ndege hawa.

KUZALIANA

Unapofika msimu wa kuzaliana dume na jike kwa pamoja hulia milio ya kuashiria tukio la kupandana na dume ndio huwa ni mtawala wa himaya. Jike huishi na dume kwa muda wote wa kupandana huku wakitafuta kiota mahususi kwa ajili ya kutaga mayai.

Kama nilivo tangulia kusema hapo mwanzoni ndege hawa ni wazazi vimelea (brood parasites). Jike anapo karibia kutaga basi hutafuta kiota cha ndege mwingine mwenye mayai na kisha kuyatoa mayai ya ndege yule nje ya kiota na kutaga mayai yake. Mara nyingi hupendelea kutaga kwenye kiota ambacho mayai ya ndege huyo mwenye kiota yanafanana na mayai yake ili ndege mwenye kiota asiweze kugundua mayai hayo.

Kekeo akisha taga mayai huondoka na kisha mayai hayo huatamiwa na ndege mwenye kiota bila kujua kuwa mayai si yake kwa muda wa siku 12-17 lakini kwa kawaida huwa ni siku 12 kabla ya mayai ya ndege mwenye kiota kutotolewa. Na hii ndio maana kekeo hawa huchagua kiota cha ndege maalumu ambao wanajua siku zao za kutotoa huendana na za kwao. Tafiti zinaonesha kuwa kwa nyingi kekeo wanahupendelea viota vya ndege jamii ya Drongo.

Baada ya kutotolewa watoto wa kekeo huya sukuma nje yakiota mayai au hata kama kuna watoto wa ndege mwenye kiota ambao kwa bahati mbaya mayai yalibaki kwenye kiota wakati kekeo jike ana taga ili tu waweze kubaki wenyewe, na hii ni chembe chembe za urithi ambazo mpaka ukubwani nao hupelekea kuwa wazazi vimelea.

Watoto hufumbua macho kuanzia siku ya 8 na huanza kuruka kuanzia wiki 3 na kuendelea. Kwa kipindi chote hicho watoto wa kekeo hulishwa na kuwa chini ya uangalizi wa ndege mwenye kiota kwani hujua ni watoto wake bila kujali ukubwa wa watoto hao.  Ndege anapo atamia mayai  na kisha kutotoa watoto huwalea tu bila kujali aina au jamii ya watoto alio totoa. Kekeo watoto huendelea kuishi na mama huyo mpaka pale watakapo fikia umri wa kujitegemea na hapo ndipo huachana na mama huyo na kwenda kuanza maisha yao wenyewe bila kuacha asili yao ya uzazi vimelea pale watakapo kuwa tayari kuanza kuzaliana.

UHIFADHI

Ni jambo la kushukuru sana kwa kuwa idadi ya wanyama hawa bado inaridhisha na hakuna taarifa zozote au tafiti zozote ambazo zinaonesha kuwa idadi ya wanyama hawa imepungua katika maeneo wanayopatikana. Shirika la umoja wa mataifa linalo shughulikia na uhifadhi wa maeneo asili  (International Union for Conservation of Nature-IUCN) lime waweka ndege hawa kwenye kundi la viumbe hai ambao bado hawapo katika hatari ya kutoweka duniani.

HITIMISHO

Uhifadhi wa wanyamapori ni jukumu la kila mmoja wetu bila kujali wadhifa wa mtu alionao katika eneo analoishi. Faida zitikanazo na uhifadhi wa wanyamapori nikubwa japo kuna ambao wanaweza wasizione kutokana na kutopata au kushika pesa mkononi moja kwa moja

Faida kubwa itokanayo na uhifadhi wa wanyamapori huonekana kutokana na mambo makubwa yanayo fanywa na mamlaka mbali mbali za uhifadhi wa wanyamapori hasa kwa kusaidia ujenzi wa shule, zahanati, visima vya maji na miradi mingine mingi ya maendeleo. Hii ni dhahiri kabisa mamlaka hizi zinafanya kazi kubwa kuhakikisha tunaendelea kuwa na wanyamapori hapa nchini.

Mwisho kabisa nizipongeze mamlaka husika za hifadhi za wanyamaopri kwa kazi kubwa zinazo endelea kwenye sekta ya uhifadhi Hifadhi za Taifa Tanzania, Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwani jitihada zao zinaonekana katika utekelezaji wa majukumu yao katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao kwa ujumla.

Kwa maswali, maoni na mambo mengine kuhusu wanyamapori au makala hizi basi usisite kuwasiliana nami,

Sadick Omary Hamisi

Simu= 0714116963/0765057969

Email= swideeq.so@gmail.com

Instagram= wildlife_articles_tanzania

Facebook= Sadicq Omary Kashushu

Blog= http://wildlifetanzania.home.blog