Habari ndugu msomaji wa makala hizi za kila siku kuhusu wanyamapori, naamini unaendelea kupambana na kuboresha maisha yako kila siku. Siku ya leo ni siku ya tofauti sana kwa sababu nataka nikushirikishe mambo ya kipekee sana kutoka katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Kuna siku nilikuwa naangalia filamu ya wanyamapori, hasa wanyama wanao kula nyama, nililchokiona humo ni cha ajabu sana kuliko filamu zote nilizowahi kuona. Hii filamu niliyokuwa naangalia ilikuwa inaitwa “Ruaha Lion Battle Zone”. Ni filamu ambayo inaelezea sana amkundi ya simba yaliyopo kwenye hifadhi hii, pamoja na idadi ya simba waliopo kwenye makundi hayo. Kwa kweli ni filamu iliyonisisimua sana na kunifanya niiangalia mara kwa mara.

Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni moja ya  maeneo yaliyobaki hapa duniani kwa kuwa na idadi kubwa sana ya simba. Tafiti nyingi za wanyama wanaokula nyama zinonyesha kwamba idadi ya simba duniani imeporomoka kutoka milioni moja hadi sasa ni chini ya elfu thelethini, kati ya hao elfu thelethini asilimia kumi yake ipo Ruaha. Yaani asilimia kumi ya simba wote waliopo duniani, wapo katika hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Pamoja na kwamba Hifadhi hii inayo wanyamapori wengine wengi, bado kuna idadi kubwa sana ya wanyama hawa wanaokula nyama katika hifadhi hii. Pia ijulikane kuwa sio simba tu ndio wanaopatikana kwa wingi katika eneo hili, kuna kanivora wote wakubwa na wadogo katika hifadhi hii, kanovira (kanivora ni wanyama wanao kula nyama tu ) wakubwa ni simba, chui, duma, mbwa mwitu, na fisi, lakini pia kuna idadi kubwa ya kanivora wadogo.

Sasa kwenye filamu hii ya wanyama niliyokuwa naangalia ilikuwa inaelezea tu maisha ya simba wa Ruaha na jinsi wanavyotumia mbinu mbali mbali kuwinda wanyama wakubwa kama nyati, twiga. Baada ya kuangalia na kumsikiliza yule jamaa anayelezea filamu hii nikaona na kujua kwamba makundi ya simba yanatofautiana katika uwindaji, kila kundi lina mbinu zake za kuwinda,  katika hifadhi hii yenye zaidi ya makundi 17 ya simba, yaliwinda kwa mbinu mbali mbali kulingana na aina ya mnyama.

Katika filamu niliyokuwa naangalia ameelezea sana makundi haya ya simba yanayo tambulikana kama, baobab pride, Kumi pride, Njaa pride, brushback pride. Makundi haya ya simba hupenda sana kukaa karibu na mto mkuu wa Ruaha, hivyo wanyama kama nyati au wanyama wengine wanapokuja kunywa maji kwenye mto huu mara nyingi hupita katika njia au kwenye himaya ya makundi hatari ya simba na hapo ndipo huliwa na simba bila huruma.

Makundi haya ya simba yemepewa majina kulingana na sehemu yalipo, au idadi au tabia za makundi hayo, mfano kundi linaitwa Njaa , hili ni kundi la simba hatari sana ambalo linawinda hadi ndege, hadi wale wanyama wengine kama kuro ambao sio mara zote huwindwa na simba, kundi hili linakula kila mnyama aliyetokea mbele yake, hahaah, nilicheka sana baada ya kuona jinsi wanavyogombania kamnyama kadogo walichowinda, kuna kundi jingine linaitwa Kumi, hili ni kundi ambalo mara zote wapo kumi tuu, hawaongezeki, na mara nyingi unapowaona wanaonekana kuwa na idadi hiyo tu, hili kundi jingine linaloitwa baobab, ni kundi ambalo linapatikana sana maeneo yenye mibuyu, ndio asili ya kundi hili, ambalo ni kundi linalowinda sana nyati pamoja na kundi la bushback haya ni makundi hatari sana yanayowinda nyati.

Kama tunvyojua mara nyingi kwenye makundi ya simba, simba jike ndio huwinda na simba dume hulinda familia na mipaka ya eneo wanaloishi familia yake, na pia dume ana wajibu wa kulinda familia yake isivamiwe na wanyama wengine kama fisi, maana fisi hupenda kuua watoto wa simba na hata simba wengine madume, hivyo kwa mara nyingi sana wanaowinda ni simba jike tu, mara chache sana utaona dume akiwinda. Kuna sababu nyingi sana kwa nini majike ndio hodari zaidi kwenye uwindaji kuliko madume, kwenye makala zijazo nitaandaa kuhusu simba na tabia zake ili tupate uelewa mzuri wa wanyama hawa wanaovutia sana.

Ni filamu inayochekesha na kufundisha pia, mfano simba mmoja jike anauwa nayati akiwa peke yake, lakini hapo hapo simba kumi walishindwa kumuua na hata kuwangusha twiga mmoja. Haya ndio maajabu ya hifadhi hii iliyobarikiwa kuwa na simba wengi sana. Kama hajawahi kumwona simba, basi njoo tembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha utawaona wa kutoasha hasa kipindi cha kuanzia mwezi mai hadi desemba.

Kwa leo nimeona nikushirikishe hayo machache, endelea kutembelea mtandano wako wa wildlife Tanzania, na kuwashirikisha wengine haya unayojifunza. Karibu sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683248681

hillarymrosso@rocketmail.com